Saturday, January 26, 2013

SERIKALI :SIMBA HAWANA ADABU BAADA YA KUCHEZESHA KIKOSI CHA SIMBA B



 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhxNhRWqQLHTYmdrWi42_YmUFoQblVMd8uzQQ0nJBLkauhmy6Mpjc7_fN8dr1FC5jxdy1973Wx3jsrO6QXyYTHR1wEc0CS5hgjiL2jyBXprHgKjrymwZUYyOuZDtBIfx50pCX0WlMo16eY/s400/moro13.jpg 

Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla amekosoa kitendo cha mabingwa wa Bara, Simba kuchezesha kikosi B katika mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya Black Leopards ya Afrika Kusini juzi kwa kuwa kitendo hicho kiliwanyima raha wapenzi wa soka.

Mechi hiyo ilimalizika kwa wageni hao waliofungwa mara mbili mfululizo na Yanga Dar es Salaam na Mwanza, kushinda 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini.


 Makalla amesema Simba haikuwatendea haki mashabiki walioingia uwanjani kushuhudia mechi hiyo kwa kuwa walitegemea kuona kikosi cha kwanza cha 'Wekundu wa Msimbazi'.


"Mechi hiyo ilitangazwa sana, nilikuwapo uwanjani , Kwa kweli sikutegemea kuona Simba wanaingiza kikosi chao cha vijana katika mechi hiyo. Mashabiki walinunua tiketi kushuhudia Simba yenyewe na siyo kikosi cha pili," alisema Makalla.


"Katika hali kama hii tunapunguza utamu wa mpira. Watu wataacha kuingia viwanjani kwa sababu ya vitu kama hivi," alisema kwa sababu "leo unawaambia kuna mechi kubwa, wanaingia uwanjani wanakutana na timu tofauti.


"Kesho hawataingia watasita kuingia uwanjani wakihofia kudanganywa."

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' amesema kuwa waliamua kuingiza kikosi B katika mechi hiyo ili kuwapa 'yosso' wao uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa.

"Watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wachezaji wenye umri mdogo hawapewi nafasi za kutosha katika timu zetu. Sisi tumewapa nafasi vijana wetu, kwanini tunalalamikiwa?" alihoji Kaburu akionyesha dhahiri kushindwa kuona ama kuelewa wasiwasi wa Makalla.

No comments:

Post a Comment