Wednesday, December 5, 2012

NGASSA ATUA MERREIKH KWA DOLA 75,000 NA MSHAHARA MNONO WA DOLA 4,000 YEYE MWENYEWE AKATIWA DOLA 50,000 ZA WINO

 

Ngssa; Sasa mutu ya fweza

BIASHARA imeisha. Azam FC imemuuza Mrisho Khalfan Ngassa kwa dola za Kimarekani 75,000 kwenda El Merreikh ya Sudan ambako amesaini mkataba wa miaka miwili, utakaomuwezesha kulipwa mshahara wa dola za Kimarekani 4,000 kwa mwezi huku naye akilipwa dola 50,000 za kusaini.
Awali, Merreikh walitaka kumpa mkataba wa miaka mitatu Ngassa wenye thamani ya dola 100,000, lakini wakala wake Alhaj Yussuf Said Bakhresa akakataa akisema utambana mchezaji wake aking’ara na kutakiwa na klabu nyingine.
Sasa Ngassa baada ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwishoni mwa wiki hii, atakwenda Sudan kufanyiwa vipimo tayari kujiunga na klabu hiyo, ambayo ni jambo la kawaida kucheza hatua ya makundi ya michuano ya klabu Afrika.
Azam FC imesema imeweka mbele maslahi ya mchezaji na taifa kwa ujumla katika maamuzi ya kumuuza Sudan, kutoka Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo. “Hii timu (Merreikh) kila mwaka inacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, maana yake huyu mchezaji atakwenda kupata maendeleo na kuja kuisaidia zaidi Tanzania katika mashindano ya kimataifa,”alisema kiongozi mmoja wa Azam.  
Alipoulizwa kuhusu Simba SC aliyokuwa anaichezea klabu hiyo, kiongozi huyo alisema wao walimtoa kwa mkopo Ngassa kwenda kwa Wekundu wa Msimbazi hadi Mei 31, mwakani na mkataba wao ndio unasema hivyo.
“Sisi tuliwapa Simba huyu mchezaji kwa mkopo hadi Mei 31 na wakatupa Sh. Milioni 25, ila tuko tayari kuwarudishia fedha zao walizota, lakini huyu mchezaji ni mali yetu  na hata TFF wanatambua hilo, na tumekwishamuuza Merreikh,”alisema.
Alipoulizwa kuhusu Simba kusaini mkataba mpya na Ngassa, alisema; “We uliona wapi dunia nzima timu inapewa mchezaji kwa mkopo halafu inamsainisha mkataba? Simba lazima ifike wakati waache kurudia makosa, haya ndio mambo ya Mbuyu Twite sasa,”alisema kiongozi huyo wa Azam.
Katika kukamilisha mauzo ya mchezaji huyo, kiongozi wa Marreikh akiwa Dar es Salaam mbele ya viongozi wa TFF na Azam, alipigiwa simu Ngassa aliye hapa Kampala, Uganda na kuhusishwa katika dili hilo, naye akakubali ndipo mambo yakamalizwa.
Aidha, Azam wameomba TFF ihakikishe kunakuwa na ulinzi katika kambi ya timu ya taifa mjini hapa, ili Simba wasimfanyie vurugu Ngassa na kumvuruga kisaIkolojia, wakati ndiyE tegemeo la timu katika kampeni ya kutwaa Kombe la Challenge mwaka huu mjiini hapa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe akizungumza kutoka Dar es Salaam, alisema kwamba watawapeleka mahakamani Azam kwa kitendo cha kumuuza mchezaji wao kinyume cha sheria.   
“Haiwezekani wamuuze wao, wakati wao walituuzia huyu mchezaji na sisi tuna mkataba ambao tulisaini nao, hii ni kinyume cha sheria na sisi tutawapeleka mahakamani,”alisema Hans Poppe ambaye anatua kesho mjini hapa.
Azam walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.

HAKUNA MAJERUHI STARS, VIJANA WAKO TAYARI KUCHINJA KORONGO

Kikosi cha Stars

KOCHA wa timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesema hana majeruhi hata mmoja kikosini mwake kuelekea mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kesho, Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
Akizungumza leo mjini hapa baada ya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu Kyambogo, Poulsen alisema kwamba timu iko tayari kwa mchezo huo wa kesho unaotarajiwa kuwa wa kukata na shoka.
“Vijana wamejiandaa vizuri kabisa na wote wako katika hali nzuri ya kucheza ila tunachoomba ni fair play kutoka kwa muamuzi maana tunacheza na wenyeji ambao wana watazamaji wengi,” alisema.
Alisema timu zote mbili ni nzuri na iwapo muamuzi atachezesha vizuri basi utakuwa ni mchuano mkali. “Vijana wana ari na mchezo huu na tukipewa fair play tutacheza vizuri kama tulivyofanya katika michezo  dhidi ya Rwanda,” alisema Poulsen.
Refa wa mechi ya Cranes na Stars anatarajiwa kuwa Mohamed El Fadil kutoka Sudan ambaye pia alichezesha mechi ya Stars dhidi ya Rwanda Robo Fainali.
Alisema ana furaha kwa kuwa hakuna majeruhi hata mmoja na pia aliwasifu wachezaji wake kwa kuonyesha umoja na nidahmmu ya hali ya juu. “Hawa wanakaa kama familia si unawaona walivyo pamoja?” alisema Poulsen na kuongeza kuwa hilo ni muhimu sana kwa mchezaji.
Naye kocha msaidizi, Sylvester Mash alisema Stars ina nafasi kubwa sana ya kushinda mechi hii kwa sababu wenyeji wao, The Cranes watakuwa wanacheza kwa wasiwasi kwa kuwa wako nyumbani .
“Timu yetu ina hamasa kabisa na ukizingatia Uganda wako nyumbani, wao ndio wana tension kubwa zaidi,” alisema na kuongeza kuwa mchezo huu utakuwa wa kusisimua sana.
Akizungumza kutoka Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, wadhaminiwa Stars, George Kavishe alisema Stars ina kila sababu ya kutinga fainali na kunyanyua kombe kwa mara ya nne.
“Sisi kama wadhamini tunasubiri ushindi maana tuna imani na Stars na hatua waliyofikia ni nzuri nay a kutia moyo kwa hivyo watanzania wajitokeze kwa wingi na kuufuatilia mchezo huu kesho,” alisema Kavishe.
Mchezo wa Stars na Cranes utatanguliwa na semi fainali ya kwanza kati ya Zanzibar na Kenya ambao pia ni mchezo wa kusisimua kwani timu zote mbili zimeshaonyesha uwezo mkubwa.
Kocha wa Zanzibar Salum Nassor ameshatangaza mara mbili akiwa Zanzibar na hapa Kampala kuwa iwapo hataondoka na kombe basi atabwaga manyanga.

TFF WAITAFUTIA USHINDI WA MEZANI SERENGETI BOYS

Kikosi cha U17 ya Kongo kilichoitoa Serengeti

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limewasilisha barua ya malalamiko yake dhidi ya matumizi ya wachezaji wenye umri mkubwa na unyanyasaji uliofanyuwa kwa maofisa wa timu ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17 wa Serengeti Boys wakati wa mechi ya marudiano ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana dhidi ya Congo.
Serengteti Boys iliondolewa kwenye mashindano hayo kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyofanyika Novemba 18, 2012 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es salaam na baadaye kukubali kipigo cha mabao 2-0 kwenye mechi ya marudiano jijini Brazaville Jumapili iliyopita.
Hata hivyo, mechi hizo mbili zilizingirwa na matukio tata, hasa kuhusu umri wa wachezaji wa Congo ambao kimaumbile walionekanakuwa ni umri mkubwa zaidi na kusababisha TFF kuwasiliana na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuhusu njia zinazowezekana kupata uthibitisho wa umri wa wachezaji hao, lakini ilishindikana na ndipo TFF ilipocheza mechi hiyo ikiwa na imeweka pingamnizi.
Katika barua iliyotumwa CAF jana, TFF imerejea barua ya pingamizi aliyokabidhiwa kamisaa wa mechi ya kwanza jijini Dar Es salaam, Bw. Chayu Kabalamula na malalamiko yaliyowasilishwa kwa kamisaa wa mechi ya marudiano kuhusu vurugu walizofanyiwa maofisa wa timu.
Katika barua hiyo, TFF imeomba CAF iagize kuwa wachezaji wote wa Congo waliocheza mechi hizo mbili wapimwe tena kwa kutumia kipimo cha M.R.I na gharama za zoezi hilo zilipiwe na TFF; na pili Shirikisho limeomba kuwa CAF ikubali kuipa Tanzania wiki tatu za kukusanya ushahidi na kuuwasilisha Cairo kwa ajili ya maamuzi.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, nchi shiriki zinatakiwa kuwapima wachezaji wake kwa kutumia kipimo cha M.R.I ambacho kinaweza kutambua umri wa vijana walio chini ya miaka 17 na kwamba matokeo yake yanatumwa CAF, ambayo itahifadhi matokeo hayo hadi hapo kutakapotokea pingamizi na ndipo itafanyia kazi kwsa kutoa matokeo ya vipimo hivyo.
 “Ni matumaini yetu kuwa suala letu litafanyiwa kazi na kutolwewa ufumbuzi ili kulinda soka la vijana barani Afrika dhidi ya vitendo vilivyokomaa vya udanganyifu wa umri,” alisema katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jana, kocha Jacob Michelsen alisema alishangaa kuona wachezaji wenye umri mkubwa zaidi wakichezeshwa kwenye mechi ya marudiano, lakini akaisifu TFF kuwa inafuata njia sahihi ya maendeleo na haina budi kuendelea na programu yake ya soka la vijana.
"Najivunia vijana wangu kwa kuwa walijituma kwa muda wote pamoja na kwamba wenyeji waliongeza wachezaji wenye umri mkubwa zaidi kuliko waliokuja huku," alisema kocha huyo kutoka Denmark.
"Kitu cha msingi ni kufuata njia sahihi ya kuendeleza soka na natumaini TFF iko kwenye njia sahihi na itaendelea na programu yake ya vijana. Hakuna njia ya mkato kama mnataka maendeleo. Ni lazima tufuate njia sahihi na matunda yake tutayaona baadaye.
"Kila mara nasema mambo (ya vijana) huchukua muda mrefu (Things Take Time) na hivyo hatuna budi kuwa wavumilivu.
"Wenzetu walitumia njia za ajabu na hata hiyo penati ya bao la kwanza haikuwa faulo. Ilitokea nje kabisa ya eneo la penati. Refa
alimuangalia kibendera akaona ametulia, akamuangalia beki mchezaji akamuona amesimama, mara akaangalia juu na kupuliza filimbi kuonyesha kuwa ni penati."
Naye kocha msaidizi, Jamhuri Kihwelo alishindwa kujizuia na kujikuta akibubujika machozi wakati alipoelezea jinsi alivyoshambuliwa na askari kabla ya mchezo huo.

ROLLING STONE YAANDAA KOZI YA MAKOCHA DARAJA C


KITUO cha Kukuza Vipaji cha Rolling Stone kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kimeandaa kozi ya leseni C ya walimu wa mpira wa miguu itakayofanyika kuanzia Desemba 10, 2012 hadi Desemba 23, 2012 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Kozi hiyo itahusisha makocha walio na Cheti cha Kumaliza Elimu ya Sekondari au wale waliohitimu kozi ya ualimu wa mpira wa miguu ya ngazi ya kati (intermediate).
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni alisema kuwa washiriki wa kozi hiyo wanatakiwa kuwa wamewasili Arusha ifikapo Desemba 9, 2012 na wanatakiwa kwenda na vyeti vyao halisi vya elimu. Alisema tayari Rolling Stone wameshasajili walimu 25 ambao watashiriki kozi hiyo na hivyo kuwataka watu wengine wanye sifa kutoka mkoa wa Arusha na mikoa mingine kujitokeza kushiriki mafunzo hayo muhimu.
Kayuni alisema kuwa kadri taifa litakavyozalisha walimu wengi, ndivyo taifa litakavyokuwa na uwezo wa kuandaa watoto na vijana wengi katika misingi sahihi ya mpira wa miguu na hivyo kuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
Kozi hiyo itaendeshwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Kayuni kwa kushirikiana na mkufunzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF), Bw. Dominic Niyonzima kutoka Rwanda.
Kwa mujibu wa Rolling Stone, kila mshiriki atajigharimia nauli ya kwenda Arusha na atatakiwa kwenda na ada ya fedha zinazolingana na Dola 100 za Kimarekani (dola moja ni sawa na Sh1,580 za Tanzania). 

SITA TU WAPITISHWA KUGOMBEA TAFCA



KAMATI ya Uchaguzi ya Chama cha Waliku wa Mpira wa Miguu (TAFCA) imetangaza matokeo ya usaili wa wagombea uongozi chama hicho, ikiwa imepitisha wagombea sita sita na kuwaengua wagombea watano kwenye nafasi tofauti.
Baada ya usaili wa wagombea hao, Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA iliwaengua wagombea hao watano kwa kutokidhimasharti ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya TAFCA na Kanuni ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na pia kutokidhi utashi wa masharti ya 11 (1) ya kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Katika nafasi ya mwenyekiti Oscar Don Korosso alipitishwa kuwa mgombea pekee baada ya Kenedy Mwaisabula na Jamhuri Kihwelo kuenguliwa kwa kutokidhi masharti ya ibara ya 26 (2) ya Katiba ya TAFCA na kanuni ya tisa ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Katika nafasi ya makamu mwenhyekiti, Kamati imempitisha Lister J. Manyara kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo huku Marco Bundara akipitishwa kuwa mgombea pekee wa nafasi ya katibu mkuu wa TAFCA.
Hali kadhalika wagombea wawili wa nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF, Wilfred Kidau na Magoma Rugora wamekidhi masharti ya Katiba ya TAFCA na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na hivyo watachuana kuwania kura za wajumbe wa mkutano mkuu,  huku Ally A Mtumwa akienguliwa kwa kutokidhi masharti ya kanuni ya 11 (1) ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Katika nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji, wagombea wote wawili, Abubakar Balingula na Aboubakar Salum wameenguliwa kwa kutokidhi masharti ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya TAFCA na Kanuni ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.



MBWANA SAMATTA KINARA WA KUFUMANIA NYAVU TP MAZEMBE MSIMU HUU.


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayechezea klabu ya TP Mazembe Mbwana Samatta amekuwa wa kwanza katika orodha ya wafungaji bora wa klabu hiyo iliyotolewa jana.

Taarifa hiyo ambayo ipo kwenye mtandao wa klabu hiyo inasema TP Mazembe msimu wa 2012 imefunga jumla ya mabao 112 na Mbwana Samatta amefunga mabao 23.

Mtanzania Mbwana Samatta ambaye huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)humwita jina la utani  Samagoal amemaliza akiwa mfungaji bora kwa kufunga mbao 23 katika mashindano yote, mabao 6 akiyafunga katika mashindano ya klabu bingwa ya Afrika ambapo alishika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora wa msimu wa mashindano hayo.

Mtanzania mwingine Thomas Ulimwengu ameshika nafasi ya nne akiwa amefunga mabao 9 katika msimu mzima sawa na Given Singuluma.

Ifuatayo ni orodha kamili iliyotolewa na TP Mazembe kwenye mtandao wake

1.Samatta mabao 23, 2. Mputu mabao 16, 3. Lungu mabaon 13, 4.Ulimwengu na Singuluma mabao tisa, 6. Kanda na Traore mabao sita, Salakiaku mabao  matano, 8. Bokanga na Kalaba mabao manne, 10.Lusadisu na Sinkala TUSILU mabao matatu, 13. Ilongo, Kasongo, Nkulukuta, Kabangu mabao mawili, 17. Hichani, Kasusula, Kanteng, Lofo, Sunzu na sundry.

Katika ligi ya mabingwa wa Afrika wanaongoza kwa mabao ni
Emmanuel CLOTTEY wa Berekum Chelsea ambaye amefunga mabao 12 matatu kwa Penati

Mbwana Samatta alifunga mabao sita ya kawaida sawa na mshambuliaji mwenzake wa TP Mazembe Treasury Mputu lakini yeye moja ni kwa njia ya penalti na Mohamed  Aboutrika wa Al Ahly lakini yeye mabao mawili ni kwanjia ya penalti.

  UHAI CUP KUANZA KUTIMUA VUMBI DESEMBA 7 MWAKA HUU

 
Michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu B za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom inatarajia kuanza Desemba 7 mwaka huu na kumalizika Desemba 22 mwaka huu.
 

Mashindano haya ambayo yamedhaniwa na kampuni ya Azam kupitia maji ya Uhai yatashiriki  wachezaji  ambao usajili wao ulifanyika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kupata leseni. Hakutakuwa na usajili mwingine wowote mbali na ule uliofanyika sambamba na wa Ligi Kuu.
Taratibu zote za michuano hiyo zitafahamishwa kwa klabu husika ikiwemo ratiba ya michuano hii

 

MWAKALEBELA AJA NA UHURU DAR CORPORATE BONANZA

TIMU ya soka ya waandishi wa habari za michezo nchini ni miongoni mwa timu nane zitakazoshiriki bonanza la kusheherekea miaka 51 ya uhuru wa Tanganyika litakalofanyika kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam Desemba 9 mwaka huu kuanzia saa mbili asubuhi.

Mwenyekiti wa TASWA Majuto Omary alisema kuwa walipata barua toka Mkurugenzi wa kampuni ya Vennedrick (T) Limited kupitia Mkurugenzi wake Fredrick Mwakalebela na wameshathibitisha kuwa watashiriki.

Bonanza hili linameandaliwa na kampuni ya Vennedrick (T) Limited na litachezwa kwa mtindo wa ligi na timu mbili toka kila kundi zitafuzu hatua ya nusu fainali na limedhaminiwa na NMB banki na sasa wachezaji wa TASWA wapo kwenye maandalizi.

Timu za Barrick, NMB, DSTV na Radio Times zipo kundi A na TASWA FC, Jubilee, Azam Group na wenyeji Gymkhana wapo kundi B

Mwakalebela amesema kuwa mshindi wa kwanza, wa pili na watatu watapata zawadi na lengo la mashindano haya mbali na kuadhimisha miaka 51 ni kutumia fursa kujadili masuala mbalimbali ya michezo, matatizo na maendeleo na nini kifanyike.
 


TIMU za taifa za Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars na Visiwani, Zanzibar Heroes kesho zinatarajia kujitupa uwanjani kwa nyakati tofauti kuwania nafasi ya kucheza fainali ya michuano ya Cecafa Tusker Cup inayofanyika jijini Kampala, Uganda. Zanzibar Heroes ambao wametinga hatua hiyo baada ya kuindoa Burundi kwa changamoto ya mikwaju ya penati 6-5 katika mchezo wa robo fainali itaingia uwanjani kuchuana na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars ambayo iliiondosha Malawi kwa bao 1-0 lililofungwa na mchezaji wa zamani wa Yanga Mike Baraza. Kwa upande wa Kilimanjaro Stars wao wataingia uwanjani huku wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuiondosha Rwanda katika michuano hiyo baada ya kuifunga mabao 2-0 yaliyofungwa na nyota wake machachari Amri Kiemba na John Bocco ambaye anashikilia usukani wa kufunga mabao mengi sambamba na Mrisho Ngassa wote wakiwa na mabao matano. Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Uganda wametinga katika hatua hiyo baada ya kuifunga timu ngumu ya Ethiopia ambayo itashiriki michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani kwa mabao 2-0 hivyo Stars haitakuwa na kazi rahisi katika mchezo wa leo. Kocha wa Stars Kim Poulsen amesema kuwa wamejiandaa vyema kwa ajili ya kuikabili Uganda na wana matumaini ya kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo ingawa alikiri hautakuwa mchezo rahisi. Mchezo wa kwanza utakaoanza unatarajiwa kuwa kati ya Zanzibar Heroes na Harambee Stars majira ya saa 10 za jioni wakati mchezo utakaofuata utachezwa majira ya saa moja usiku.

 

 

WALEVI, WAZINZI HARAMBEE STARS WAPANDISHWA NDEGE KUJA KUIVAA ZANZIBAR HEROES KESHO

Paul Wer
KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni mchecheto wa mechi dhidi ya Zanzibar, Kenya imeongeza wachezaji wawili Paul Were na Kevin Omondi kwa ajili ya mechi hiyo ya Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge inayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
Wawili hao waliondoka jana usiku Nairobi, mara tu baada ya Harambee Stars kuvuzu Fainali, wakiifunga 1-0 kwa mbinde Malawi na tayari wapo Kampala, Uganda kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Zanzibar Stars.
Baada ya kuifunga 1-0 Sudan Kusini katika mchezo wa pili wa Kundi A, wachezaji hao walikwenda kujirusha kwenye klabu ya usiku na kurejea kambini na wanawake, jambo ambalo lilifanya asubuhi yake waoandishwe ndege wote kurejea Nairobi, lakini kutokana na mchecheto wa mechi ya kesho, wamerejeshwa.
Kocha wa Harambee Stars, James Nandwa aliliomba Shirikisho la Soka Kenya (FKF) liliwarejeshe wachezaji hao kwa ajili ya Nusu Fainali.
Kocha wa Fisa FC, Charles ‘Korea’ Omondi, ambaye amekuwa akifanya mazoezi na wachezaji hao tangu warejeshwe nyumbani, amethibitisha wamebadilika kinidhamu na wako vizuri kimchezo.
Were na Omondi wapo kwa mkopo AFC Leopards na Gor Mahia kutoka timu inayoshiriki Ligi ya Jimbo la Nairobi, Fisa FC.
Mchezo kati ya Zanzibar Heroes na Kenya utaanza kesho saa 10:00 jioni, ukifuatiwa na Nusu Fainali ya pili, kati ya Uganda na Tanzania Bara Kilimanjaro Stars.

 

 

HANS POPPE AJA KAMPALA KWA MAMBO MAWILI MAKUBWA, WANAOSEMA SIMBA IMEFULIA WANAJIDANGANYA

Hans Poppe 
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe anatarajiwa kutua mjini hapa kesho, kwa ajili ya mambo mawili makubwa, usajili wa wachezaji na kocha mpya, atakayerithi mikoba ya Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick.
Akizungumza  jana kwa simu kutoka Dar es Salaam, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) anakuja Kampala kufanya kazi za Simba SC.
Ingawa Hans Poppe hakutaka kuzugumzia kwa undani ujio wake hapa, lakini  tunatambua amekuja kufanya mazungumzo na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri na wachezaji kadhaa waliowavutia katika mashindano haya, akiwemo mshambuliaji Mganda Brian Umony.
Lakini pia, Hans Poppe anakuja kumalizana na mshambuliaji wao Mganda, Emmnanuel Okwi ambaye amemaliza mkataba wake.
Vyombo vya habari Dar es Salaam vimeripoti kuwa, Okwi atasaini mkataba wa mwaka mmoja zaidi Simba SC kwa dau la dola za Kimarekani 40,000 pamoja na nyongeza ya mshahara.      
Okwi amekuwa akihusishwa na habari za kuhamia Yanga na Azam FC baada ya kumaliza mkataba wake Simba SC, lakini wakati huo huo inaelezwa amekwishafikia makubaliano na Wekundu wa Msimbazi kuongeza mkataba.
Kwa upande wa kocha wa timu ya taifa ya Malawi, iliyotolewa katika Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kwa kufungwa na Kenya 1-0 jana, tayari Phiri amekwishasema yupo tayari kufanya kazi Simba SC na inaelezwa mazungumzo ya awali yamekwishafanyika.

 

 

POULSEN AFICHUA SIRI YA KUMPIGA BENCHI MSUVA

Kim Poulsen kulia na Msaidizi wake Marsh kushoto
KOCHA wa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amesema kwamba anamuweka benchi kwa sasa kiungo mshambuliaji Simon Msuva, katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, kwa sababu Amri Kiemba anafanya kazi nzuri katika kikosi cha kwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalum jana, Uwanja wa Mandela, Namboole, alisema kwamba alipompa nafasi ya Kiemba amefanya kazi nzuri ambayo imemvutia na kuamua kuendelea kumtumia kwenye kikosi cha kwanza.
“Najua Msuva ni winga mzuri, ana kasi na anashambulia sana, lakini hata Kiemba anafanya kazi nzuri, tena kama jana (juzi) amefunga hadi bao, kwa kweli ananivutia na anafanya kazi yake vizuri,”alisema.
Msuva alianza katika mechi mbili za mwanzoni za Kundi B kwenye michuano hii, dhidi ya Sudan na Burundi, lakini baada ya hapo amemalizia benchi dakika zote 180 katika mechi kwenye mechi mbili zilizofuata dhidi ya Somalia na Rwanda. 
Hata hivyo, Kim alisema bado Msuva anaweza akatokea benchi wakati wowote na kwenda kuongeza nguvu katika kikosi cha Kilimanjaro Stars hasa katika hatua ngumu ambayo michuano hii imefikia.
Stars imefika Nusu Fainali na kesho itamenyana na wenyeji Uganda, Uwanja wa Mandela, Namboole, kuanzia saa 12: jioni, mchezo ambao utatanguliwa na Nusu Fainali nyingine kati ya Kenya na Zanzibar, itakayoanza saa 10:00 jioni.
Stars ilitinga Nusu Fainali, baada ya kuifunga Rwanda mabao 2-0 juzi kwenye Uwanja wa Lugogo mjini hapa, ambayo yalitiwa kimiani na Amri Kiemba na John Bocco.
Awali ya hapo, Stars ilifuzu Robo Fainali kama mshindi wa pili kwenye kundi lake, nyuma ya Burundi baada ya kujikusanyia pointi sita, yaani ikishinda mechi mbili 2-0 na Sudan na 7-0 na Somalia, wakati yenyewe ilifungwa 1-0 Mbayuwayu wa Bujumbura. 

 

 

INJINI YA THE CRANES YAOMBA JEZI YA NIYONZIMA YANGA HARAKA

Oloya
KIUNGO wa Uganda, Moses Oloya amesema kwamba yupo tayari kuachana na klabu yake, Saigon Xuan Thanh ya Vietnam na kujiunga na Yanga SC ya Dar es Salaam, ambao watampa maslahi mazuri.
Yanga SC inamfuatilia mchezaji huyo katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kwa ajili ya kumsajili, akazibe pengo la kiungo wake Mnyarwanda, Haruna Niyonzima anayetakiwa na El Merreikh ya Sudan.
Akizungumza  jana, Uwanja wa Mandela, Namboole baada ya kuiongoza nchi yake, kuifunga Ethiopia mabao 2-0, Oloya alisema kwamba kama Yanga watafika Kampala na kuzungumza naye, wakiafikiana atahamishia maisha yake Dar es Salaam.
“Nimebakiza mkataba wa mwaka mmoja katika klabu yangu, lakini tukikubaliana naweza kuondoka Vietnam bila masharti magumu, Yanga waje tu tuzungumze,”alisema.
Kiongozi mmoja wa Yanga, jana alisema kwa njia ya  simu jana kutoka Dar es Salaam kwamba, wanafuatilia maendeleo ya Oloya katika michuano hiyo na iwapo ataendelea kufanya vizuri watakuwa tayari kumsajili.
“Unajua Haruna ana asilimia kubwa ya kuondoka, sasa lazima tupate kiungo mbadala mzuri kama yeye na mzoefu, tumefuatilia kwa haraka haraka tumemuona huyu Oloya, ngoja tuendelee kumuangalia,”alisema kiongozi huyo.  
Oloya alizaliwa Oktoba 22, mwaka 1992 na kabla ya kujiunga na Saigon Xuan Thanh mwaka 2010, aliichezea KCC ya nyumbani kwao tangu mwaka 2009. Kiungo huyo alianza kuichezea Uganda mwaka jana na sasa amekuwa tegemeo la timu hiyo. 

 

 

SSENTONGO SASA AITAKA MWENYEWE SIMBA SC

Ssentongo

MSHAMBULIAJI wa Uganda, Robert Ssentongo amesema kwamba atakuwa tayari kujiunga na Simba SC ya Dar es Salaam, wakiafikiana naye dau.


Ssentongo anayeng’ara katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, amewahi kuchezea Simba kwa muda tu katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, mwaka juzi mjini Kigali, Rwanda.


Lakini baada ya michuano hiyo, akatemwa na badala yake akasajiliwa kiungo Mganda mwenzake, Patrick Ochan ambaye baada ya msimu mmoja aliuzwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).


“Mimi nipo tayari Simba wakinitaka, wao wafike bei tu, ile ni timu kubwa na ninaamini nikijiunga nayo nitapata mafanikio,”alisema.

Ssentongo amewahi kucheza African Lyon ya Dar es Salaam na alipomaliza mkataba wake akachezea Simba kwa muda kabla ya kurejea Uganda.
Awali Ssentongo aliwahi kuchukua fedha za Simba, lakini hakuja kujiunga nayo hadi alipokuja Lyon.  

 

NGASSA, BOCCO WAMNYIMA USINGIZI UMONY


Umony
MSHAMBULIAJI wa Uganda, Brian Umony amesema kwamba katika mechi mbili zilizobaki za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge atajitahidi awapiku wachezaji wa Tanzania, John Bocco na Mrisho Ngassa katika ufungaji wa mabao kwenye michuano hiyo.
“Mimi nina mabao matatu, wao kila mmoja ana mabao matano, sijakata tamaa, nitajitahidi niwapiku, najua ni kazi ngumu, lakini nitajitahidi sana,”alisema mchezaji huyo ambaye ameonyesha nia ya kujiunga na Simba SC ya Dar es Salaam.
Akiizungumzia mechi ya Nusu Fainali dhidi yao na Tanzania Bara kesho, Umony alisema anaamini itakuwa ngumu sana, lakini watapambana kushinda.
“Tanzania wana timu nzuri sana, ina wazoefu ambao mimi nawajua kama Mrisho Ngassa na Juma Kaseja, kwa kweli mchezo utakuwa mgumu, itakuwa mechi nzuri sana yenye hadhi ya fainali,”alisema Umony.
Brian amerejea nyumbani Uganda na kujiunga na Express baada ya kumaliza mkataba wake, Becamex Binh Duong F.C. ya Vietnam.
Mwaka 2009, baada ya Simba kuzidiwa kete na SuperSport United ya Afrika Kusini kwa Umony, ikamsajili Emmanuel Okwi aliyekuwa SC Villa wakati huo.
Umony aliichezea Supersport United hadi 2010 alipohamia University of Pretoria ya Afrika Kusini pia hadi mwaka 2011 alipohamia Portland Timbers ya Marekani kwa mkopo na mwaka huu akatua Becamex Binh Duong F.C.
Tayari Umony amesema anaweza kujiunga na Simba wakiafikiana naye dau.
WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE 2012
John Bocco                    Tanzania  5
Mrisho Ngassa               Tanzania  5
Brian Umony                  Uganda    3
Suleiman Ndikumana     Burundi    3 (1 penalti)
Chris Nduwarugira         Burundi    3
Geoffrey Kizito               Uganda    2
Robert Ssentongo          Uganda    2
Khamis Mcha                 Zanzibar   2
David Ochieng               Kenya       2
Clifton Miheso                Kenya       2
Dadi Birori                      Rwanda    2

 

 

CANNAVARO: KENYA WAUPE, TUTAWANG'OA WATAKE WASITAKE

Cannavaro

NAHODHA wa Zanzibar, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alikuwapo jana Uwanja wa Mandela, Namboole akiishuhudia Kenya ikiichapa Malawi 2-0 na kutinga Fainali, lakini amesema Harambee Stars ‘weupe tu kwao’.
Akizungumza jana baada ya mechi hiyo, Cannavaro alisema kwamba kulingana na kiwango kiliochoonyeshwa na Kenya katika mechi hiyo dhidi ya Malawi, wanaamini watawafunga.
“Yaani jamaa weupe sana, hata bao walilopata la kibahati bahati sana, mimi nakuambia sisi hawa tunawafunga, timu yetu nzuri sana,”alisema beki huyo wa kati wa Yanga SC ya Dar es Salaam.
Nahodha huyo wa Yanga SC, alisema kwamba baada ya kuitoa Burundi juzi sasa anaamini Kombe la Challenge litakwenda Zanzibar, kwani haoni timu nyingine ya kuwasumbua wao katika mashindano haya.
Zanzibar juzi ilikata tiketi ya kutinga Nusu Fainali baada ya kuichapa Burundi kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 na sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
Shujaa wa Zanzibar juzi alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya kipa Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
Manahodha wa timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa Burundi walipoteza penalti zao juzi.
Ndikumana alikuwa wa kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya lango, wakati wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo, Amisi Tambwe, Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
Upande wa Zanzibar Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya Zanzibar, Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu, kabla ya Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa Burundi, Samir Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na Othman kutumbukiza nyavuni ya ushindi.

 

 

BEKI STARS YAMVUNJA NGUVU OKWI

Okwi
EMANUEL Okwi, mshambuliaji tegemeo wa Uganda, amesema kwamba ukuta wa Tanzania Bara ni mzuri na kuupita ni kazi, lakini akaapa kesho watafanya kila wawezalo kuhakikisha wanaupenya na kufunga.
Akizungumza  jana, Okwi alisema kwamba wachezaji wote wa safu ya ulinzi ya Stars wana akili na nguvu za kupambana na mshambuliaji wa aina yeyote, hivyo keso itakuwa kazi sana.
“Inahitaji maarifa sana kuweza kupenya pale, Shomary (Kapombe) ni mchezaji mwenye akili sana na anajituma, Yondan (Kevin), pia ana akili sana, uzoefu na anajituma. Mimi nimemkuta pale Simba hadi anahamia Yanga (msimu huu).
Na tangu nakuja Simba yeye ni mchezaji wa timu ya taifa, wana Kaseja (Juma) kipa mzuri na mzoefu, tena sana, kwa hivyo ukuta wao ni mzuri sana, ila na sisi tuna safu kali sana ya ushambuliaji, Diego (Hamisi Kiiza), Brian (Umony), Ssentongo (Robert), Kizito (Geoffrey) na mimi, wote nadhani unajua cheche zetu.
Kwa hivyo hiyo mechi itakuwa sana, lakini sisi kwa sababu tunacheza nyumbani, inatupa nafasi nzuri zaidi ya kusonga mbele, yote kwa yote, mchezo utakuwa mgumu, ila kushinda sisi lazima,”alisema Okwi.
Wakati ukuta wa Cranes haujaruhusu hata bao moja, ukuta wa Stars umeruhusu bao moja tu katika mechi nne, dhidi ya Burundi, tena la penalti lilofungwa na Nahodha wao, Suleiman Ndikumana, Kilimanjaro Stars ikilala 1-0.         

 

KIIZA: BOCCO ATAKUTANA NA UKUTA WA ZEGE

Kiiza
MSHAMBULIAJI wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ amesema John Raphael Bocco ‘Adebayor’ wa Tanzania Bara ni mkali, lakini ajue The Cranes ina ukuta ambao haujaruhusu hata bao moja, hivyo asitarajie kufunga bao kesho katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge.
Akizungumza  jana, katika Uwanja wa Mandela, Namboole, Kiiza alisema kwamba anamfahamu Bocco na kwenye Challenge ya mwaka huu anang’ara sana, lakini kesho atakutana na ukuta wa wanaume wa shoka.
“Tunaiheshimu Tanzania ni timu nzuri, na zaidi mfumo wao wanaocheza hivi sasa ni mzuri sana, lakini hata sisi ni wazuri, hiyo mechi itakuwa kali sana,”alisema mshambuliaji huyo wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam.
Kiiza alisema mbali na Bocco, Tanzania Bara ina mchezaji mwingine hatari, Mrisho Ngassa lakini wote wajue kwamba watakutana na ukuta wa Uganda, ambao katika mechi nne haujaruhusu hata bao moja.
Uganda jana ilifuzu kuingia Nusu Fainali ya Challenge, baada ya kuifunga Ethiopia mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Geoffrey Kizito dakika ya nne na Robert Ssentongo dakika ya 60.
Kwa ushindi huo, Uganda itamenyana na Tanzania Bara katika Nusu Fainali Alhamisi usiku, mchezo ambao utatanguliwa na Nusu Fainali nyingine kati ya Kenya na Zanzibar, itakayoanza saa 10:00 jioni.
Kenya ilifuzu Nusu Fainali jana, baada ya kuifunga Malawi 1-0, bao pekee la Mike Barasa dakika ya 56.


 

SENEGAL YAKUBALI YAISHE.

SHIRIKISHO la Soka nchini Senegal-FSF limetangaza jijini Dakar jana kuwa hawatakata rufani kufuatia adhabu waliyopewa na Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kufuatia tukio la mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2013. Maofisa wa FSF wamesema ingawa wamepewa nafasi ya kukata rufani kuhusiana na uamuzi wa shirikisho hilo kuufungia Uwanja wa Leopold Sedar Senghor kwa kipindi cha mwaka mmoja wameamua kutokupinga adhabu hiyo. Kamati ya Nidhamu ya CAF pia imelitoza shirikisho hilo faini ya dola 100,000 ambayo inatakiwa kulipwa katika kipindi cha miaka miwili. Adhabu hiyo imekuja kufuatia mashabiki wan chi hiyo kuvuruga mchezo wa marudiano wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika baina ya Senegal na Ivory Coast Octoba 13 mwaka huu katika kipindi cha pili wa Ivory wakiwa wanaongoza kwa mabao 2-0. Tukio lilisababisha mchezo huo kusimamishwa huku baadae CAF ikiamua kuiengua Senegal na kuipa nafasi Ivory Coast kufuzu.

 

SIJAHUZUNISHWA NA UAMUZI WA FIFA - DROGBA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Ivory Coast, Didier Drogba amesema kuwa hajakasirishwa na uamuzi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kumkatalia ombi lake la kuondoka Shanghai Shenhua kwa mkopo kwenda katika klabu yake ya zamani Chelsea kabla ya kipindi cha dirisha la usajili kufunguliwa. Drogba amesema hakutegemea kukubaliwa kwa ombi lake kutoka kwa shirikisho hilo kwasababu ni kitu kisicho cha kawaida na hakukuwa na dhamana kwamba kitakubalika. Nyota huyo ambaye kwasasa anafanya mazoezi katika klabu yake hiyo ya zamani kwa ajili ya kujiwenda na michuano ya Mataifa ya Afrika yakayoanza Januari 19 mwakani amesema kukataliwa huko hakuwezi kumkosesha usingizi kwakuwa alikuwa anajaribu. Katika taarifa yake FIFA imesema kuwa ombi la mchezaji huyo lingewezekana kama mkataba wake ungekuwa umeisha wakati wa dirisha la usajili bado halijafunguliwa lakini Drogba bado ana mkataba na Shenhua mpaka 2015.

 

MSHINDI WA BALLON D'OR TAYARI AMESHAJULIKANA.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid, Jose Mourinho amedai kuwa mshidi wa tuzo ya Ballon d’Or tayari ameshaamuliwa kwa kuwatuhumu Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kumpigia debe nyota wa Barcelona Lionel Messi. Messi ndio anayepewa nafasi kubwa ya kunyakuwa tuzo hiyo ya mchezaji bora duniani kwa mara ya tatu mfululizo lakini anakabiliwa na upinzani kutoka kwa mchezaji mwenzake kutoka Barcelona Andres Uniesta na mshambuliaji nyota wa Madrid Cristiano Ronaldo. Kauli hiyo ya Mourinho ilikuja wakati akiulizwa kama Ronaldo ana nafasi ya kunyakuwa Ballon d’Or baada ya ushindi wa mabao 4-1 iliyopata Madrid dhidi ya Ajax jana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akijibu swali hilo Mourinho amesema kuwa wakati FIFA wakiongea na kufanya kampeni hakuna unaloweza kufanya hivyo anadhani tuzo ya Ballon d’Or tayari imeshatolewa. 

 

MESSI KUVUNJA REKODI YA MULLER KATIKA MCHEZO DHIDI YA BENFICA.

MSHAMBULIAJI nyota wa Barcelona Lionel Messi amepata nafasi nyingine ya kufikia rekodi ya mabao 85 ambayo yalifungwa na Gerd Muller katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya kocha wa timu hiyo Tito Vilanova kumjumuisha katika kikosi chake kitakachopambana na Benfica katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Messi mwenye mabao 84 hivi sasa amebakisha bao moja kufikia rekodi ya miaka 40 ambayo iliwekwa na Muller ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Ujerumani na klabu ya Bayern Munich. Vilanova amesema kuwa ameamua kumtumia Messi na kuwapumzisha nyota wengine kwasababu mchezaji huyo alipumzika katika mchezo wa Kombe la Mfalme wiki iliyopita. Nyota wa klabu hiyo waliopumzishwa ni pamoja na Andres Iniesta, Xavi Hernandez, Javier Mascherano, Pedro, Jordi Alba na Cesc Fabregas ambapo nafasi zitachukuliwa na wachezaji vijana kutoka katika akademi ya klabu hiyo.


 

USIKU WA ULAYA MANCHESTER CITY WAAGA KWA AIBU ILHALI ARSENAL NAO WAKISHIKISHWA ADABU NA OLYMPIAKOS.HABARI NA MATUKIO KATIKA PICHA .

Olympiakos iliyotokea nyuma imefanikiwa kuichapa Arsenal mjini Piraeus, na kuwafanya washika mitutu hao kumaliza katika nafasi ya pili katika kundi B nyuma ya Schalke.
Tomas Rosicky alianza kufunga bao la uongozi kwa Arsenal kabla ya bao la kipindi cha pili la Giannis Maniatis lililokuwa la kusawazisha na baadaye Kostas Mitroglou kuandika bao la pili na la ushindi kwa wagiriki.
Kocha wa Schalke Leonardo Jardim aliwatumia wachezaji wake ambao ni wafungaji wakubwa katika ligi ya Ugiriki  Rafik Djebbour na Djamel Abdoun sehemu ya kiungo.
Akiwa ni mwenye matumaini ya kufuzu, Wenger alikifanyia mabadiliko kikosi chake kilichopoteza dhidi ya Swansea mabao 2-0 mwishoni mwa juma akimrejesha Rosicky kiungoni pamoja na kinda wa miaka 20 Jernande Meade akicheza dakika zote za mchezo.
MANCHESTER CITY 0 VS DOTMUND 1
Manchester City imemaliza kampeni ya michuano ya ligi ya mabingwa ulaya kwa kichapo kingine cha bao 1-0 toka  Borussia Dortmund.
Bao la kipindi cha pili la Julian Schieber kunako dakika ya 57 lilitosha kuwaondosha katika harakati za kusonga mbele na michuano hiyo huku wajerumani wakifurahia mchezo ambapo walitengeneza nafasi nyingi karibu sehemu kubwa ya mchezo.
Matokeo hayo yana maanisha kuwa kikosi cha Roberto Mancini kimemaliza michezo yake ya kundi D kikiwa mkiani bila ushindi hata mmoja na Dortmund wakifanikiwa kusonga mbele katika hatua ya mtoano ya michuano hiyo.
 
  •   MATOKEO MENGINE
  • Din Zagreb     1 - 1     Dynamo Kiev FT
  • Malaga       2 - 2     Anderlecht FT
  • Montpellier      1 - 1           Schalke 04 FT
  • Paris SG      2 - 1         FC Porto FT
  • Real Madrid   4 - 1               Ajax FT
AC Milan      0 - 1   Zenit St P'sbg

 

UEFA CHAMPIONZ LIGI: Man City waikosa hata EUROPA LIGI!

>>TIMU 13 zipo Mtoano, Bado 3 kupatikana Mechi za LEO!
>>CHELSEA nini LEO??
UEFA_CHAMPIONZ_LIGI_LOGO-BOMBAZMabingwa wa England, Manchester City, jana walichapwa Bao 1-0 na Borussia Dortmund katika Mechi ya mwisho ya Kundi D na kutupwa nje ya Ulaya huku wenzao Arsenal wakifungwa 2-1 huko Ugiriki na Olympiacos lakini Arsenal walikuwa tayari wameshafuzu kutoka Kundi lao kabla ya Mechi hiyo.
+++++++++++++++++++++++++++++++
MATOKEO:
Jumanne Desemba 4
GNK Dinamo 1 FC Dynamo Kyiv 1
Paris SaintvGermain 2 FC Porto 1
Montpellier Hérault 1 FC Schalke 1
Olympiacos FC 2 Arsenal 1
Málaga 2 RSC Anderlecht 2
AC Milan 0 FC Zenit St. Petersburg 1
Borussia Dortmund 1 Manchester City 0
Real Madrid 4 AFC Ajax 1
+++++++++++++++++++++++++++++++
Wakihitaji ushindi, hasa wakati Real Madrid, wakiicharaza Ajax Bao 4-1 katika Mechi nyingine ya Kundi D kwa msaada mkubwa wa Nyota wao Cristiano Ronaldo, Man City walijikuta wakitunguliwa Bao katika Dakika ya 57 na Julian Schieber.
+++++++++++++++++++++++++++++++
TIMU ZILIZOFUZU KUCHEZA RAUNDI YA MTOANO YA TIMU 16:
-KUNDI A: PSG, Porto
-KUNDI B: Schalke, Arsenal
-KUNDI C: Malaga, AC Milan
-KUNDI D: Dortmund, Real Madrid
-KUNDI E: Shakhtar Donetsk
-KUNDI F: Bayern Munich, Valencia
-KUNDI G: Barcelona
-KUNDI H: Manchester United
+++++++++++++++++++++++++++++++
Man City sasa wapo nje kabisa ya Mashindano ya Ulaya kwani nafasi ya 3 imechukuliwa na Ajax ambao watacheza Raundi ya Mtoano ya Timu 32 za EUROPA LIGI.
Mechi nyingine za mwisho za Makundi E mpaka H zinachezwa leo ambazo ndizo zitatoa Timu 3 zilizobaki kukamilisha jumla ya Timu 16 zitakazocheza Raundi ya Mtoano ya Timu 16.
+++++++++++++++++++++++++++++++
RATIBA MECHI ZA MWISHO ZA MAKUNDI:
[Mechi zote kuanza Saa 4 Dak 45 Usiku]
Jumatano Desemba 5
FC Shakhtar Donetsk v Juventus
Chelsea FC v FC Nordsjælland
LOSC Lille v Valencia CF
FC Bayern München v FC BATE Borisov
FC Barcelona v SL Benfica
Celtic FC v FC Spartak Moskva
Manchester United FC v CFR 1907 Cluj
SC Braga v Galatasaray A.S.
++++++++++++++++++++++++++++++++