Tuesday, December 4, 2012

 

HAKUNA HILA KATIKA KUBADILI KATIBA - TENGA.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema hakuna hila yoyote katika nia ya Shirikisho kutaka marekebisho matatu kwenye katiba kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu na kuwataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia mabadiliko hayo kwa maslahi ya maendeleo ya mchezo huo. Tenga alisema hayo jana wakati akiongea na waandishi wa habari kufafanua juu ya waraka wa kuomba ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kuridhia mapendekezo matatu ya mabadiliko ya katiba yanayohusu uingizaji wa kipengele cha utoaji leseni kwa klabu (Club Licensing); kuundwa kwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wa TFF na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF. Hatua ya kutuma waraka wa kuomba ridhaa ya mabadiliko hayo imetafsiriwa tofauti na baadhi ya wadau, wengine wakisema ni mbinu za uongozi wa sasa kutaka uendelee kukaa madarakani wakati wengine wakitaka ufafanuzi wa vipengele hivyo. “Hakuna hila hata kidogo. Yote ni mambo ya maendeleo na nia yetu ni kufanikisha ili mambo yaendelee,” alisema Rais Tenga kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF jana. “Tusifikie sehemu tukaanza kulaumu kwa nini mtu ametaka maelezo. Lakini sikutarajia kuwa mtu wa mpira akiambiwa hili ni agizo la FIFA (Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu), atasita; akiambiwa hili ni agizo la CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika), atasita, au akaambiwa haya ni maamuzi yenu wenyewe, akasita.” Tenga alisema kuwa nia ya Kamati ya Utendaji ilikuwa ni kuitisha mkutano mkuu kwa ajili ya mabadiliko hayo ya katiba, lakini akasema baada ya kutafakari kwa kina na kuangaliwa uwezo wa Shirikisho, Kamati iliona haiwezi kuitisha mikutano miwili kwa sasa kwa kuwa TFF haina fedha. “Tumetoa maelezo kuwa tunafahamu kuwa katika mazingira ya kawaida tungeitisha mkutano mkuu; tuje tuzungumze na baadaye siku ya pili watu waondoke halafu tuwaite tena kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi,” alisema Tenga ambaye alibainisha kuwa gharama za chini za mkutano mkuu wsa TFF ni kati ya Sh milioni 90 na Sh milioni 110. “Lakini tumeeleza bayana kuwa uwezo huo hatuna, tungelikuwa nao wala tusingefika mahali hapa; vijana wetu wanahangaika hadi tunatafuta watu watusaidie. Kwa hiyo tukasema kuna dhambi gani kuwa wa kweli. Katiba inasema mkitaka kufanya mabadiliko ya katiba, itisheni mkutano mkuu. Unaita Mkutano Mkuu kwa sababu gani, ili mlete wajumbe wa mkutano mkuu ambao ndio watakaopitisha mabadiliko hayo na ndio maana tumeona dhana hiyo ya kutuma waraka.” Kuhusu mabadiliko hayo, Tenga alifafanua kuwa maagizo kuhusu utoaji leseni kwa klabu (Club Licensing) na kuundwa kwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wa TFF yalitolewa mwishoni mwa mwezi Julai, ikiwa ni baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji cha Julai na hivyo suala hilo kulazimika kuzungumzwa kwenye kikao cha Septemba. Alisema: ”Pamoja na kwamba Tanzania ilishaingiza kwenye kanuni za ligi masharti ya utoaji leseni, CAF imekuja na maagizo kwamba ni lazima itamkwe kwenye katiba kuwa TFF itatoa leseni kwa klabu kwa mujibu wa maagizo ya CAF na msipofanya hivyo klabu zenu hazitaruhusiwa kushiriki mashindano ya klabu ya Afrika ya mwakani,” Simba na Azam FC zitaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika na Kombe la Shirikisho na hivyo kutopitishwa kwa mabadiliko hayo mapema kutasababisha wawakilishi wa Tanzania wazuiwe kushiriki michuano hiyo. Kuhusu kuundwa kwa Kamati ya Rufaa, Tenga alisema kuwa baada ya kuomba ufafanuzi wa utata uliojitokeza katika vyombo vya maamuzi vya TFF, FIFA ilisema kuwa ili kuondoa mgongano wa kimaslahi, ni muhimu ikaundwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wa TFF badala ya mfumo wa sasa ambao Kamati ya Rufaa hujigeuza kuwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi inapofikia wakati wa uchaguzi mkuu wa TFF. “Kwa hiyo tunachoomba hapa ni ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kwamba iwepo Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wa TFF ili kama mtu hatatendewa haki na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, basi akate rufaa kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi badala ya chombo kimoja kushughulikia mambo mawili,” alisema Tenga. Kuhusu kuiondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, kiongozi huyo alisema kuwa suala hilo lilitokana na maamuzi ya Mkutano Mkuu uliopita kuwa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza ziendeshwe na chombo huru. “Baada ya hapo Kamati ya Utendaji iliziambia klabu kuwa tunaunda Kanuni za Kuendesha chombo huru cha ligi, tunaomba mapendekezo yenu. Na ndipo walipotuletea mapendekezo yao kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Ligi atoke kwenye klabu sita za juu na kwamba kiwango cha chini cha elimu kiwe Cheti cha Kumaliza Elimu ya Kidato cha Nne kama ilivyo kwenye katiba,” alisema. “Maana yake ni kwamba sifa hizo hazikidhi utashi wa kikatiba wa sifa za mgombea wa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa TFF ambazo ni Elimu ya Chuo Kikuu, lakini klabu zikasema hazina haja na nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais na ndio maana tunaomba ridhaa sasa ya kuondoa nafasi hiyo.” “Napenda kusema jambo hili ni la maendeleo na hakuna hata moja ambalo si la maendeleo. Tumepata barua kutoka Kagera ikieleza kuwa utaratibu huu haufai, Katibu Mkuu amepata na atawajibu. Pwani nao wameomba ufafanuzi na tutatoa waraka wa ufafanuzi kwa wote. “Watu wana haki ya kuhoji na sisi ni wajibu wetu kuwaelimisha. Ombi langu ni tushirikiane ili twende kwenye mkutano mkuu wetu unaokuja ili tuchaguane. Tukichaguana tutakuwa tumetimiza jambo muhimu kweli kweli.” Tenga pia aliwasihi wajuimbe wa Kamati ya Utendaji kuendelea na jitihada za kuelimisha wajumbe ili waridhie mabadiliko hayo na shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu ziendelee kama kawaida.

CHALENJI CUP: Wachezaji 17 na Daktari wa Eritrea waingia mitini Kampala!!

>>WACHEZAJI 5, MAAFISA 2 TU, wapanda Ndege kurudi kwao!!
>>2010 WALIYEYUKA BONGO, wakabambwa na kuomba Hifadhi ya Kisiasa!
Vyombo vya Dola Nchini Uganda na FUFA, Chama cha Soka cha Uganda, vinafanya msako mkali kuwatafuta Wachezaji 17 na Daktari wa Timu ya Taifa ya Eritrea ambao wameyayuka toka Hotelini kwao na kuwaacha Wachezaji watano tu na Maofisa wawili kupanda Ndege kurudi kwao mara baada ya kutupwa nje ya CHALENJI CUP inayoendelea huko Kampala, Uganda.
Akithibitisha kuyeyuka kwa wenzao, Kocha wa Eritrea, Teklit Negash, amesema: “Hatujui Ndugu zetu wako wapi!”
Eritrea ilitolewa kwenye Michuano ya CHALENJI CUP ambako walikuwa Kundi C baada ya kutoka sare 0-0 na Zanzibar, kufungwa 3-2 na Malawi na 2-0 na Rwanda.
Mwaka 2010, kwenye Michuano ya CECAFA Nchini Tanzania, Wachezaji 13 wa Eritrea waliyeyuka na hatimae kubambwa na kuomba Hifadhi ya Kisiasa na baadae kupelekwa huko Houston, Marekani chini ya Programu ya Wakimbizi
 

KLABU BINGWA DUNIANI kumnusuru Benitez CHELSEA?

>>UEFA CHAMPIONZ LIGI HATIHATI, KUFUZU KWAO SI MIKONONI MWAO!!!
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
RATIBA Mechi za Chelsea chini ya Benitez:
Nov 25 Chelsea 0 City 0 [BPL]
Nov 28 Chelsea 0 F’ham 0 [BPL]
Des 1 West Ham 3 Chelsea 1 [BPL]
Des 5 Chelsea FC v FC Nordsjælland [UEFA CHAMPIONZ LIGI]
Des 8 Sunderland v Chelsea [BPL]
Des 13 Usain Hyundai/Monterrey v Chelsea [Klabu Bingwa Duniani]
Des 19 Leeds United v Chelsea [CAPITAL ONE CUP-Robo Fainali]
Des 23 Chelsea v Villa [BPL]
Des 26 Norwich v Chelsea [BPL]
Des 30 Everton v Chelsea [BPL]
Jan 2 Chelsea v QPR [BPL]
FAHAMU: BPL ni Barclays Premier League=Ligi Kuu England
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

BENITEZChelsea, chini ya Meneja aliesakamwa, Rafael Benitez, mara baada ya kucheza Mechi yao ya Ligi Kuu England ugenini na Sunderland Jumamosi Desemba 8, ikiwa ni Mechi ya 5 kwa Meneja huyo ambae ametoka sare mbili na kubondwa Bao 3-1 na West Ham, ataenda na Kikosi chake huko Japan kuwania Taji la FIFA la Klabu Bingwa Duniani lakini hii pia haimpi kumbukumbu nzuri kwani Siku 5 tu baada ya kuiongoza Inter Milan kuwa Mabingwa wa Dunia Mwaka 2010 alifukuzwa kazi.
Kwenye Michuano hiyo huko Japan, Chelsea, wataanza kucheza hatua ya Nusu Fainali dhidi ya Mshindi kati ya Bingwa wa Barani Asia, Usain Hyundai kutoka Korea na Monterrey, ambao wanatoka Mexico na ni Mabingwa wa Marekani ya Kati na Kaskazini.
Lakini, kabla hawajacheza na Sunderland kwenye Mechi ya Ligi Kuu England, huenda Jumatano Desemba 5 wakajikuta wamebwagwa nje ya UEFA CHAMIPONZ LIGI kwani nafasi yao ya kufuzu kutoka Kundi E haipo moja kwa moja mikononi mwao.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
UEFA CHAMPION LIGI
KUNDI E
Uwezo wa Chelsea kutinga Raundi ya Mtoano ya Timu 16 haupo mikononi mwao pekee.
Chelsea wapo nafasi ya 3 wakiwa Pointi 2 nyuma ya Juventus na 3 nyuma ya vinara
Shakhtar Donetsk ambao tayari wamefuzu Raundi ya Mtoano ya Timu 16.
Ikiwa Shakhtar watatoka sare na Juventus katika Mechi ya mwisho ya Kundi hili, Chelsea wapo nje hata wakiifunga Nordsjaelland Bao Milioni Uwanjani Stamford Bridge.
Usalama wao pekee ni kwa Juventus kufungwa na wao kuifunga Nordsjaelland.
MSIMAMO:
[Kila Timu imecheza Mechi 5]
1 Shakhtar Donetsk Pointi 10
2 Juventus 9
3 Chelsea 7
4 Nordsjaelland 1
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Kwa safari ya Japan, Benitez ameshatangaza Kikosi imara ambacho ni:
KIKOSI KAMILI:
Makipa: Petr Cech, Ross Turnbull, Hilario
Mabeki: Branislav Ivanovic, Ashley Cole, David Luiz, Paulo Ferreira, Gary Cahill, John Terry, Cesar Azpilicueta, Ryan Bertrand
Viungo: Oriol Romeu, Ramires, Frank Lampard, Oscar, John Obi Mikel, Eden Hazard, Marko Marin, Lucas Piazon
Mafowadi: Fernando Torres, Juan Mata, Victor Moses, Daniel Sturridge
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
2012FIFA_CLUB_WORLD_CUPKLABU BINGWA DUNIANI
TIMU ZITAKAZOSHIRIKI:
Chelsea-BINGWA ULAYA
Corinthians-BINGWA MAREKANI ya KUSINI
Monterrey-BINGWA MAREKANI ya KATI NA KASKAZINI
Auckland City-BINGWA KANDA ya OCEANIA
Usain Hyundai-BINGWA-Barani Asia
Al Ahly-BINGWA-Barani Afrika
Sanfrecce Hiroshima-BINGWA-Japan J-LIGI
RATIBA:
Raundi ya Mchujo - Desemba 6, Yokohama
1 Sanfrecce Hiroshima v Auckland City
ROBO FAINALI - Desembar 9, Toyota
2 Usain Hyundai  v Monterrey
3 MSHINDI Mechi Na 1 v Al Ahly
MSHINDI wa 5- Desemba 12, Toyota
Aliefungwa Robo Fainali 1 v Aliefungwa Robo Fainali 2
NUSU FAINALI
Desemba 12, Toyota
5 Mshindi Mechi Na 3 v Corinthians
Desemba 13, Yokohama
6 Mshindi Mechi Na 2  v Chelsea
MSHINDI wa 3 - Desemba 16, Yokohama
FAINALI - Desemba 16, Yokohama

KAMA KAWA, WACHEZAJI WOTE ERITREA WAINGIA MTAANI KAMPALA, FUFA WAHAHA KUWASAKA


WACHEZAJI 14 wa Eritrea wametoweka kambini kwao, baada ya kutolewa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mjini hapa Jumamosi.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA), waandaaji wa mashindano ya mwaka huu, Rogers Mulindwa amesema  leo kwamba, hawakufanikiwa kuwapata wachezaji hao wakati wanatakiwa kuondoka leo mara tu baada ya kutolewa.
Mulindwa alisema kambini wamebaki kocha Ngash Teklit na viongozi wengine wanne tu, lakini wachezaji wote hawapo.
“Wachezaji 14 wametoweka kambini na hatujui walipo kwa sasa. Ndege yao inatarajiwa kuondoka leo, lakini tunaendelea na jitihada za kuwasaka kwa kushirikiana na Polisi,”alisema.
Eritrea ilikuwa kundi moja na Rwanda, Zanzibar na Malawi na wakashika mkia katika kundi hilo, wakifungwa mechi zote na kutoa sare moja tu Zanzibar katika mechi ya kwanza.
Sasa hii inakuwa desturi sugu ya nchi hiyo kuzamia nchi za watu wanapokwenda kwenye mashindano, kwani awali wachezaji wanne walizamia walipokwenda kucheza na Tusker nchini Kenya kwenye Ligi ya Mabingwa mwaka 2006 mjini Nairobi na wengine zaidi ya 10 walizamia kwenye michuano kama hii mwaka 2007 mjini Dar es Salaam.
Waliwahi kuzamia pia walipokwenda Angola mwaka 2007 kucheza mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.
Timu hiyo ilifanya hivyo hivyo mwaka 2009 nchini Kenya na katika kambi nzima alibaki kocha na mchezaji mmoja tu. Kutokana na mfululizo wa matukio hayo, walijitoa kwenye mashindano ya kimataifa mwaka 2010 na mashindano ya mwaka huu ya Challenge ndio ya kwanza kushiriki baada ya kurudi.
Serikali ya Eritrea ilisema ili kudhibiti tabia hiyo, kila mchezaji atatakiwa kuweka bondi fedha za nchi hiyo 100,000 kabla ya kusafiri kwenda kuiwakilisha nchi, lakini hiyo nayo inaonekana bado haijawa tiba.

KOMBE LA UHAI KUANZA DESEMBA 7 KARUME

Rais wa TFF, Leodegar Tenga
MICHUANO ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za U20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Michuano hiyo, ambayo hudhaminiwa na Azam, watengenezaji na wasambazaji wa maji ya Uhai, inatarajiwa kufikia tamati Desemba 22 mwaka huu.
Ofrisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo amesema leo   kwamba, wachezaji watakaoshiriki michuano hiyo ni wale tu ambao usajili wao umefanyika TFF na kupatiwa leseni.
“Hakutakuwa na usajili mwingine wowote mbali na ule uliofanyika sambamba na wa Ligi Kuu. Taratibu zote za michuano hiyo zitafahamishwa kwa klabu husika ikiwemo ratiba ya michuano hiyo,”alisema ‘Big Bon’.

REFA AMPUNGUZIA MABAO BOCCO, LAKINI BADO YUPO MATAWI YA JUU

Bocco akiwawajibisha mabeki wa Rwanda juana
KAMA si refa kukataa bao lake safi tu alilofunga katika mechi ya Kundi B dhidi ya Burundi, leo Bocco angekuwa kileleni kwenye msimamo wa wafungaji wa mabao katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kwa mabao sita, lakini kufanyiwa dhuluma hiyo ana mabao matano.
Hata hivyo, jambo moja tu ameonyesha Bocco mjini hapa, yeye ni mfungaji wa uhakika anapocheza kwenye mazingira mazuri pasipo kuzomewa zomewa na mashabiki anapokosea kidogo kibinadamu.
Hiyo inatokana na Bocco kufunga katika mechi aliyocheza kuanzia hatua ya makundi, dhidi ya Sudan mabao mawili, Burundi moja lililokataliwa, Somalia mawili na jana mojas dhidi ya Rwanda.
Bocco sasa ina idadi sawa ya mabao na Mrisho Ngassa wa Tanzania Bara pia, ambaye yeye alifunga mabao yote katika mechi moja dhidi ya vibonde Somalia.
Bocco na Ngassa wanafuatiwa kwa mbali na Brian Umony wa Uganda mwenye mabao matatu, sawa na Warundi wawili, Suleiman Ndikumana na Christopher Nduwarugira katika mbio za kiatu cha dhahabu cha mashindano haya.
Khamis Mcha ‘Vialli’ wa Zanzibar, David Ochieng, Clifton Miheso wote wa Kenya na Dadi Birori au Taddy Etikiama wa Rwanda, wote wana mabao mawili kila mmoja.
WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE 2012
John Bocco                     Tanzania 5
Mrisho Ngassa               Tanzania 5
Brian Umony                  Uganda    3
Suleiman Ndikumana Burundi   3 (1 penalti)
Chris Nduwarugira        Burundi   3
Khamis Mcha                 Zanzibar  3
David Ochieng               Kenya       2
Clifton Miheso               Kenya       2
Dadi Birori                      Rwanda   2

KAMA SI MWADINI, NILIKUWA NIMEKWISHA, ASEMA CANNAVARO

Cannavaro baada ya kukosa penalti jana
NAHODHA wa Zanzibar, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema kwamba anamshukuru sana kipa wao, Mwadini Ally kwa kucheza penalti ya Abdul Fiston wa Burundi jana, kwani vinginevyo walikuwa wamekwishatolewa kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge.
“Mimi nilipokosa tu penalti kwa kweli mwili ulikufa ganzi na kuamini sasa safari ya kurudi Zanzibar imeiva na mimi ndiye nimewaangusha wenzangu. Sikuwa na raha tena, lakini nguvu ziliniijia baada ya Mwadini kucheza penalti,”alisema Cannavaro alipozungumza na waandishi wa habari  jana Uwanja wa Lugogo.
Nahodha huyo wa Yanga SC ya Dar es Salaam, alisema kwamba baada ya kuitoa Burundi sasa anaamini Kombe la Challenge litakwenda Zanzibar, kwani haoni timu nyingine ya kuwasumbua wao katika mashindano haya.
Zanzibar jana ilikata tiketi ya kutinga Nusu Fainali baada ya kuichapa Burundi kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 na sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
Shujaa wa Zanzibar jana alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya kipa Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
Manahodha wa timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa Burundi walipoteza penalti zao jana.
Ndikumana alikuwa wa kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya lango, wakati wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo, Amisi Tambwe, Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
Upande wa Zanzibar Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya Zanzibar, Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu, kabla ya Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa Burundi, Samir Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na Othman kutumbukiza nyavuni ya ushindi.

NIYONZIMA AWAPA UBINGWA STARS

Niyonzima akibadilishana kibendera na kaseja
NAHODHA wa Rwanda, Haruna Niyonzima amewatabiria Tanzania Bara kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwaka huu.
Kiungo huyo wa Yanga SC ya Dar es Salaam aliyasema hayo baada ya mechi ya Robo Fainali jana Uwanja wa Lugogo baina ya nchi hizo mbili, ambayo Bara walishinda mabao 2-0.
“Tumekubaliana na matokeo, sisi tulishindwa kutumia nafasi, wenzetu walicheza vizuri na walitumia nafasi, tunakubali huo ndio mpira sisi tumetolewa,”alisema.
Niyonzima aliisifu Bara kucheza vizuri na kwa nidhamu ya hali ya juu na akasema kama wataendelea hivyo, basi watarejea na Kombe Dar es Salaam. “Kila mtu alikuwa anatekeleza majukumu yake vizuri uwanjani na kwa kweli mimi nawapongeza,”alisema.
Bara ilifanikiwa kuingia Nusu baada ya kuilaza Rwanda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Lugogo mjini hapa.
Hadi mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba, dakika mya 33 akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza wachezaji wawili wa Rwanda kabla ya kutoa pasi maridadi.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na aliwafanya waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.
Katika hicho kipindi cha kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya Jean Claude Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19 Jean Baptiste Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.
Stars pamoja na kufunga bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha na ikawapita wote.
Ngassa tena, katika dakika ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda nje sentimita chache.
Kipindi cha pili Stars walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na Rwanda nao waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.
Hata hivyo, walikuwa ni Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili dakika ya 53 baada ya John Bocco kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti kali la Mwinyi Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.

SIMBA NA YANGA KAMA MNA JEURI ILETENI KWA KIFAA HIKI


Image
SIMBA SC, Azam na Yanga, kama wana jeuri wailete hapa Kampala, Uganda kugombea saini ya mchezaji aliyekuwa anakipiga Ulaya.
Huyo si mwingine zaidi ya kiungo wa kimataifa wa Uganda, David Obua ambaye amemaliza mkataba wake katika klabu ya Hearts ya Ligi Kuu ya Scotland na hataki kuongeza, ingawa pia amekuwa mgumu kuelezea mikakati yake mipya.
Akizungumza , Obua alisema kwamba amemaliza mkataba wake Hearts na kwa sasa yupo tu nyumbani Kampala. Alipoulizwa kuhusu mikakati yake mipya, Obua alisema; “Sina cha kusema,”.
David amekuwa akifuatilia mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mjini hapa tangu yameanza Novemba 24 na jana alikuwapo Uwanja wa Lugogo kushuhudia Zanzibar na Bara zinazotengeneza Muungano wa Tanzania zikitinga Nusu Fainali.
David ni mtoto marehemu Denis Obua, ambaye aliichezea Uganda katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1978 na ana mdogo wake, Eric Obua ambaye pia anachezea The Cranes.
Mjomba wake, John Akii-Bua aliweka rekodi ya kuwa bingwa wa kwanza Mganda wa Olimpiki kwa kushinda mita 400 huku akiweka rekodi ya dunia ya kutumia muda wa dakika 47 na sekunde 82 mwaka 1972  mjini Munich, Ujerumani.
David Obua, alizaliwa Aprili 10 mwaka 1984 mjini Kampala, Uganda na kisoka aliibukia katika klabu ya Polisi mwaka 1999, kabla ya mwaka 2001 kusajiliwa Express ‘Red Eagles’ alikocheza hadi mwaka 2002      alipohamia AS Port-Louis ya Mauritius ambako alicheza msimu mmoja na kurejea Express alikocheza hadi 2005 alipohamia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Lakini pia, David wakati anasoma Marekani, alizichezea kwa muda klabu za Raleigh na Wilmington Hammerheads za nchini humo.
Mwaka 2008, David alitua Ulaya katika klabu ya Hearts ambako hadi anamaliza mkataba wake amecheza jumla ya mechi 91 na kuifungia mabao sita.
Tangu mwaka 2003, Obua amekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda    na katika kipindi chote hicho, ameichezea Cranes mechi 27 na kuifungia mabao 14.

KIIZA, OKWI KUJILENGESHA AU KUJIKWEPESHA KWA STARS LEO?


ROBO Fainali za mwisho za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge zinatarajiwa kupigwa leo kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
Kenya, mabingwa mara tano wa Kombe hilo katika miaka ya 1975, 1981, 1982, 1983 na 2002, watamenyana na Malawi walioalikwa tu kuongeza changamoto ya mashindano kuanzia saa 10:00 jioni.
Wenyeji, mabingwa watetezi na mabingwa wa kihistoria wa mashindano haya, Uganda The Cranes waliotwaa Kombe hilo katika miaka ya 1973, 1976, 1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003, 2008, 2009 na 2011, watamenyana na Ethiopia.
Ethiopia ni timu pekee kati ya wanachama wa CECAFA, iliyofuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Afrika Kusini.
Mchezo kati ya Kenya na Malawi unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua hata kama mashabiki hawatakuwa wengi uwanjani.
Kenya na Malawi ni vigumu kuutabiri kulingana na viwango vilivyoonyeshwa na timu zote katika mashindano haya kutopishana sana.
Lakini Uganda wanapewa nafasi kubwa ya kuwafunga Ethiopia, ambao katika michuano hii hawajaonyesha kiwango cha kutisha kama ilivyo kawaida yao licha ya kufuzu AFCON.
Brian Umony, Hamisi Kiiza, Rpbert Ssentongo na Emmanuel Okwi- hizi zinatarajiwa kuwa silaha za Korongo wa Kampala katika mchezo wa leo, lakini pia yupo kiungo mmoja hodari sana Joseph Oyola.  
Katika Robo Fainali za kwanza jana Uwanja wa Lugogo, Zanzibar iliichapa Burundi kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90. Kwa matokeo hayo, Zanzibar sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
Shujaa wa Zanzibar jana alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya kipa Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
Manahodha wa timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa Burundin walipoteza penalti zao jana.
Ndikumana alikuwa wa kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya lango, wakati wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo, Amisi Tambwe, Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
Upande wa Zanzibar Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya Zanzibar, Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu, kabla ya Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa Burundi, Samir Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na Othman kutumbukiza nyavuni ya ushindi.
Mapema katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali, Bara ilifanikiwa pia kuingia Nusu baada ya kuilaza Rwanda mabao 2-0 kwenye Uwanja huo huo wa Lugogo mjini hapa.
Hadi mapumziko, Stars walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba, dakika mya 33 akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza wachezaji wawili wa Rwanda kabla ya kutoa pasi maridadi.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na aliwafanya waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.
Katika hicho kipindi cha kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya Jean Claude Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19 Jean Baptiste Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.
Stars pamoja na kufunga bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha na ikawapita wote.
Ngassa tena, katika dakika ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda nje sentimita chache.
Kipindi cha pili Stars walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na Rwanda nao waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.
Hata hivyo, walikuwa ni Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili dakika ya 53 baada ya John Bocco kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti kali la Mwinyi Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.

MESSI ANASTAHILI BALLON D'OR - NEYMAR.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Santos ya Brazil, Neymar anaamini kuwa Lionel Messi atashinda Ballon d’Or mbele ya mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo kutokana na kiwango bora alichokionyesha msimu huu. Kwa mwaka huu pekee Messi amefunga mabao 84 katika mechi za kimataifa na klabu na Neymar mwenye umri wa miaka 20 anaamini kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Argentina anastahili tuzo hiyo kutokana na kiwango alichokionyesha. Neymar amesema kuwa ingawa anadhani mshindi atakuwa Messi lakini hata Ronaldo naye amekuwa msimu mzuri hivyo kitakuwa kinyang’anyiro cha kuvutia katika tuzo hizo za Ballon d’Or. Nyota huyo pia aliendelea na msimamo wake wa kubakia Santos mpaka mkataba wake utakapoisha mwaka 2014 ndipo atafikiria kama aende Ulaya au aendelee kubakia Brazil kwa kipindi kingine. Amesema anazo ndoto za kwenda kucheza soka Ulaya lakini kwasasa anafurahia kuwepo Santos kwakuwa anakuwa karibu na familia yake pamoja na marafiki.

QUIT SMOKING WITH BARCA CAMPAIN.

KLABU ya Barcelona ya Hispania imeungana na Tume ya Ulaya kusaidia mashabiki wa soka kuacha kuvuta sigara. Baadhi ya wachezaji nyota wa klabu hiyo wakiwemo Andres Iniesta, Xavi Hernandez na Carles Puyol wako katika kampeni hiyo wakitaka mashabiki kusema hapama kuvuta sigara na wamejitolea kutoa mwongozo na msaada kwa mashabiki ambao wanataka kuachana na suala la kuvuta sigara. Kampeni hiyo iliyoanzishwa na klabu hiyo ambayo inaitwa Quit Smoking with Barca pia iko katika mitandao ya internet na simu za mkononi ambapo mashabiki wa klabu hiyo watakuwa wakipata maelezo ya jinsi gani ya kuacha kuvuta sigara na kupewa hamasa kutoka kwa wachezaji, kocha Tito Vilanova pamoja na rais wa klabu hiyo Sandro Rosell. Katika kampeni hiyo ya mtandao ambayo inaitwa FCB iCoach mvutaji sigara atahitajika kuingia na kujibu maswali rahisi kabla ya kuanza kupata maelezo mbalimbali ya kukabiliana au kuachana kabisa na tabia hiyo ya kuvuta sigara. Kukiwa na zaidi wavutaji sigara milioni 140 kuzunguka bara la Ulaya, Tume ya Ulaya inaamini kuwa muonekano wa klabu hiyo ambayo ni kubwa duniani utasaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na suala hilo.

UEFA YAMFUNGIA MAISHA SAMMUT.

SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA limemuongezea adhabu beki wa kimataifa wa Malta Kevin Sammut kutoka miaka 10 mpaka kumfungia maisha kujishughulisha na masuala ya soka baada ya kukutwa na hatia ya kupanga matokeo. Mchezaji huyo alikutwa na hatia ya kupanga matokeo katika mchezo wa kufuzu michuano ya Euro 2008 kati ya Norway na Malta ambapo katika mchezo huo nchi yake ilipoteza kwa kufungwa mabao 4-0. Agosti mwaka huu kamati ya nidhamu ya UEFA ilimfungia miaka 10 lakini mchezaji huyo na mkaguzi wa kamati hiyo walikata rufani kutaka adhabu hiyo iangaliwe upya ndipo adhabu ya kufungiwa maisha ilipotolewa. Sammut amepewa siku 10 za kukata rufani katika Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS kupinga adhabu hiyo aliyopewa. 

MSHIRA KIBENDERA AFARIKI BAADA YA KIPIGO.

MSHIKA kibendera Richard Nieuwenhuizen raia wa Uholanzi amefariki dunia baada ya kupigwa na wachezaji wakati akichezesha mechi ya vijana ambayo mwanae wa kiume naye alikuwa akicheza. Mwamuzi huyo alianguka na kukimbizwa hospitali masaa machache baada ya wachezaji wa klabu ya Nieuw Sloten ya Amsterdam kumshambulia kwa ngumi na mateke katika mchezo huo. Klabu ya Buitenboys ambayo walikuwa wakicheza na Sloten wamesema kuwa mshika kibendera huyo mwenye umri wa miaka 41 alifariki Jumatatu jioni lakini hawakuweka wazi kilichosababisha kifo chake. Mwenyekiti wa Buitenboys, Marcel Oost alionyesha kushangazwa na kilichotokea haswa ukizingatia vijana wenyewe waliokuwa wakicheza walikuwa na umri kati ya miaka 15 na 16. Wachezaji watatu ambao miaka yao ni kati 15 na 16 walikamatwa mapema Jumatatu wakituhumiwa kuwa vinara wa kuanzisha vurugu hiyo ya kumpiga Nieuwenhuizen na kumsababishia umauti.

WENGER AWEKA WANNE KATIKA RADA ZAKE JANUARI.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anajipanga kumsajili mpachika mabao wa klabu ya Schalke 04 ya Ujerumani Klaas-Jan Huntelaar mwezi ujao katika kipindi cha dirisha dogo la usajili kwa ada ya paundi milioni sita. 

 Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi amekuwa akitazamwa kwa karibu na maskauti wa klabu hiyo wakati wa wiki za ufunguzi wa msimu mpya. 

 Wenger amekuwa akimhitaji nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 kwa kipindi kirefu na baada ya kushauriana na mkuu wa maskauti wa klabu hiyo kocha huyo ameamua kumfukuzia nyota huyo mara dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa.

 Mbali na mchezaji huyo Wenger pia anapanga kumchukua tena kwa mkopo Thierry Henry na kumtengea kitita cha paundi milioni tisa kinda lenye maajabu la Crystal Palace, Wilfried Zaha. Arsenal pia iko sokoni ikitafuta golikipa mpya huku Pepe Reina akitajwa kuwa chaguo la kwanza la Wenger.

Scolari ambebesha Neymar da Silva Santos Júnior zigo la taji kombe la dunia 2014. Man United waonywa kuachana na mpango wa Lewandowski.


 Neymar da Silva Santos Júnior si mdogo kuibeba wa kushindwa kubeba matumaini ya Brazil kushinda kombe la dunia. Hii ni kauli ya kocha mpya wa timu ya taifa ya Brazil Luiz Felipe Scolari.
Mshambuliaji huyo wa klabu ya Santos ambaye kwasasa ana umri wa miaka 20, amekuwa akitazamwa na baadhi ya watu kama bado kinda kuweza kubebeshwa matumaini ya Brazil, lakini Scolari ana matumaini kuwa uwezo wa mchezaji huyo ni chachu ya mafanikio wakati Brazil itakapokuwa mwenyeji wa michuano mikubwa ya kombe la dunia 2014.
Scolari  ametolea mfano kwa mkongwe Edison Arantes do Nascimento 'Pele', kuwa alikuwa kijana mdogo wakati nchi hiyo ilipochukua taji mwaka 1958, kama ilivyokuwa kwa Ronaldo Luís Nazário de Lima
Alipoulizwa juu ya umri Neymar na matumaini ya mchezaji huyo kwenye kikosi amesema mbona Ronaldo alitumiwa kuiongoza Seleção, na alifanya hivyo akiwa na umri wa miaka 19 na 20.
"Pele pia alikuwa na umri wa miaka 17 tu , licha ya kwamba hakuwa na jina kubwa wakati huo na alifanikiwa kutengeneza jina wakati na baada ya kombe la dunia 1958.
Man United waonywa kuachana na mpango wa Lewandowski.
 Matumaini ya Manchester United kumsajili Robert Lewandowski katika usajili wa mwezi januari yameanza kutiwa mashaka baada ya klabu yake ya Borussia Dortmund kuthibitisha kuwa mshambuliaji huyo atasalia Bundesliga.
Lewandowski mwenye umri wa miaka 24, amekuwa akihusishwa kuelekea katika ligi kuu ya nchini England “Premier League” katika klabu ya Manchester.
Bosi wa Dortmund Jurgen Klopp amesisitiza kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Poland bado hajatoa ombi la kutaka kuondoka nchini Ujerumani licha ya kwamba mpango huo uko ndani ya maamuzi yake.
Akikaririwa Klopp amesema
"sina wasiwasi kuwa ataondoka, Manchester United ni moja miongoni mwa timu sinazo mkodolea macho lakini ukweli ni kwamba atasalia na sisi.
"Ahsante mungu, wakati wa klabu kubwa tajiri ya England kujaribu kuchukua wachezaji wetu sasa umekwisha. Wakati wa mzunguko wa pili wa msimu ataendelea kukaa nasi"
Klopp anaamini kuwa Bundesliga kwasasa ni ligi kubwa kuliko Premier League, licha ya kwamba Shinji Kagawa aliondoka Dortmund kiangazi.
Mabingwa hao wa ujerumani hii leo watakuwa wenyeji wa Manchester City katika mchezo wa vilabu bingwa Ulaya ambapo licha ya kuwa tayari klabu hiyo imeshapata nafasi katika hatua ya mtoano, Klopp atashusha kikosi cha nguvu kusaka uongozi wa kundi D.