Wednesday, October 17, 2012

MANJI AENDA KUFANYA IBADA YA HIJJA


Yussuf Mehboob Manji, Alhaj mtarajiwa 
MWENYEKITI wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Yussuf Mehboob Manji kesho anatarajiwa kwenda Makka, Saudia Arabia kufanya ibada ya Hijja.
Habari ambazo nimezipata  kutoka kwa mtu aliye karibu na Manji zimesema kwamba, Manji ameamua kwenda kufanya ibada hiyo ya Hijja kufuata asili ya ukoo wao, wote waislamu safi.
Ibada ya Hijja inatararajiwa kufanyika wiki ijayo Makka na kundi la mwisho la waumini wa dini ya Kiislamu litakalokwenda huko, linatarajiwa kuondoka kesho.
Akikamilisha ibada ya Hijja, Manji atakuwa sawa na Mwenyekiti wa wapinzani wake wa jadi, Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alikwenda kufanya ibada hiyo mwaka 1999 kwa ofa wakati huo akiwa bado Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (TFF), sasa shirikisho (TFF).
Manji amekuwa mfadhili wa Yanga tangu mwaka 2006, wakati klabu hiyo ikiwa chini ya Mwenyekiti, Francis Mponjoli Kifukwe na baada ya kuona jitihada zake za kuifanya Yanga iwe ya hadhi ya juu zinakwamishwa na viongozi, Julai 14, mwaka huu akaamua kujitosa kugombea Uenyekiti wa klabu hiyo, katika uchaguzi mdogo.
Ni miongoni mwa wafanyabiashara vijana wenye mafanikio makubwa, ambaye amerithi na kuendeleza vema utajiri wa baba yake, marehemu Mehboob Manji. 
Ibada ya Hijja ipo katika nguzo ya tano ya Uislamu; inayomtaka muumini wa dini ya Kiislamu mwenye uwezo kwenda kuitekeleza ibada hiyo na kuna imani kwamba baada ya ibada hiyo, muumini huyo hufutiwa dhambi zake za awali ila baada ya hapo, hatakiwi tena kurudia kufanya yaliyokatazwa na mafundisho ya dini hiyo na akifanya hivyo 'atajipalilia makaa ya moto' siku ya hukumu.

YANGA WAENDELEA VIZURI NA MAANDALIZI YA KUIUA RUVU SHOOTING JUMAMOSI

Yanga SC
KIKOSI cha Yanga kilichoingia kambini jana katika hoteli ya Uppland, Changanyikeni, Dar es Salaam kinaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pamoja na kuweka kambi Changanyikeni, lakini Yanga inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Beki Kevin Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu, anaendelea vizuri na mazoezi mepesi sawa na mshambuliaji Said Bahanuzi aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Jumatatu wiki iliyopita.
Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba iliyocheza mechi saba pia, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 17, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, iliyocheza mechi sita.

SIMBA KUENDELEZA UBABE TAIFA LEO, AZAM INA KAZI KWA PRISONS SOKOINE

Simba SC
LIGI Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara, leo inaingia katika mzunguko wake wa nane kwa nyasi za viwanja vitano kuwaka moto, huku macho na masikio ya wengi yakielekezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako mabingwa watetezi Simba watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar kutoka Bukoba mkoani Kagera.
Mechi hiyo namba 52 itachezeshwa na refa Ronald Swai kutoka Arusha, akisaidiwa na Julius Kasitu na Methusela Musebula, wote kutoka Shinyanga na refa wa akiba atakuwa Ephrony Ndisa wa Dar es Salaam.
Kagera Sugar inayofundishwa na kocha na mchezaji wa zamani wa Simba SC, Abdallah Kibadeni mara nyingi imekuwa timu ambayo inaonyesha upinzani mkali inapokutana na Simba SC, iwe Dar es Salaam au Bukoba na leo inatarajiwa kuwa hivyo pia.
Katika mchezo wa leo, huenda Simba ikaendelea kumkosa kiungo wake hodari, Mrisho Khalfan Ngassa ambaye pamoja na kuanza mazoeozi juzi na timu yake Simba SC, lakini amesema bado hayuko sawa sawa.
Akizungumza nami juzi kwa njia ya simu , Ngassa ambaye aliugua Malaria baada ya mechi dhidi ya Yanga, Oktoba 3, mwaka huu alisema kwamba bado anahisi hana nguvu.
“Nimeanza mazoezi na timu, lakini hata hivyo bado hali yangu haiko sawa sawa kwa kweli, najisikia mwili hauna nguvu, hii Malaria ilinipelekesha sana, ila najikongoza hivyo hivyo,”alisema Ngassa.
Lakini kuna uhakika kwa kiungo mwingine wa Simba SC aliyekuwa anaumwa Malaria pia, Ramadhani Chombo ‘Redondo’  akacheza leo, kwa kuwa yeye yuko fiti asilimia 100.  
Mbali na Redondo, katika mchezo huo, Simba inatarajiwa kuwapokea wachezaji wake wengine watatu iliyowakosa kwenye mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana, Emmanuel Okwi aliyekuwa kwao Uganda kuichezea timu yake ya taifa, Komabil Keita, Haruna Shamte na Kiggi Makasy waliokuwa majeruhi.
Mechi nyingine za leo Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Tanzania Prisons inayofundishwa na Jumanne Chale na Azam iliyo chini ya kocha Boris Bunjak kutoka Serbia. Nayo Polisi Morogoro iliyopanda msimu huu itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Mgambo Shooting ambayo imepata ushindi mara mbili mfululizo itakuwa nyumbani Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga ikiikaribisha Toto Africans katika mechi itakayochezeshwa na Geofrey Tumaini wa Dar es Salaam. Oljoro JKT inayonolewa na Mbwana Makata itakuwa nyumbani Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha dhidi ya African Lyon.
Simba bado ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 17, baada ya kucheza mechi saba, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, ambayo hata hivyo imecheza mechi sita, wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza mechi saba pia.
REKODI YA SIMBA NA KAGERA:
Machi 3, 2012
Simba 3-1 Kagera Sugar
Septemba 18, 2011
Kagera Sugar 1-1 Simba
Machi 29, 2011
Simba 0-0 Kagera Sugar
Oktoba 27, 2010
Kagera Sugar 0-2 Simba
Februari 3, 2010
Kagera Sugar 1-1 Simba     
Septemba 10, 2009
Simba 2-0 Kagera Sugar
Aprili 5, 2009
Kagera Sugar 0-2 Simba 
Oktoba 14, 2008
Simba 1-0 Kagera Sugar  
Aprili 19, 2008
Kagera Sugar 0-1 Simba
Oktoba 13, 2007
Simba 2-1 Kagera Sugar
Oktoba 18, 2006
Simba 2-1 Kagera Sugar
Juni 3, 2006
Kagera Sugar 1-0 Simba
(Kagera wakapewa ushindi wa mezani
2-0, kwa Simba kumchezesha Mussa
Mgosi akiwa ana kadi tatu za njano)
Septemba 28, 2005
Kagera Sugar 0-2 Simba    
Mei 25, 2005
Simba 0-1 Kagera Sugar


KOMBE la DUNIA=ULAYA: Poland v England yaenda na maji!!

>>GERMANY waongoza 4-0 na kutoka sare na Sweden 4-4!!
>>MABINGWA SPAIN 1-1 na FRANCE!
BRAZIL_2014_BESTMechi ya Poland na England iliyokuwa ichezwe huko Warsaw hapo jana ililazimika kuahirishwa kwa sababu ya mvua kubwa na Uwanja kujaa maji licha ya Uwanja huo wa kisasa kuwa na Paa ambalo huweza kufungwa na kufunguliwa lakini, katika hali ya utata, iliamuliwa lisifungwe kabla ya Mechi wakati utabiri ulikuwa ni wa Mvua kubwa.
Mechi hiyo imepangwa kufanyika leo.


Germany 4 Sweden 4
Germany wameivua ile rekodi yao ya ushindi kwa Asilimia Mia moja kwenye Kundi lao baada ya jana kuongoza kwa Bao 4-0 lakini Sweden wakapigana kiume na kulazimisha sare ya bao 4-4 katika Mechi iliyochezwa Uwanja wa Olimpiki huko Munich, Germany.
Germany waliongoza kwa bao 2 ndani ya Robo Saa kwa bao za Moroslav Klose na Sentahafu Per Mertesacker kupiga bao la 3.
Katika Dakika ya 56, Mersut Ozil akafunga bao la 4 na kuifanya Germany iwe mbele kwa bao 4-0.
Ndipo katika Dakika ya 62, Sweden, wakiongozwa na Nahodha wao Zlatan Ibrahimovic, wakaanza kurudisha mabao kwa bao la kichwa la Ibrahimovic kufuatia pasi ndefu ya Kim Kallstrom.
Mikael Lustig akapiga bao moja na Johan Elmander akapiga bao la 3 na kuifanya ngoma iwe 4—3 katika Dakika ya 76.
Rasmus Elm akafunga bao la 4 na la kusawazisha Dakika za mwisho.
Germany bado wanaongoza Kundi C wakiwa na Pointi 10 kwa Mechi 4 wakifuatiwa na Sweden wenye Pointi 7 kwa Mechi 3.
 
 
Spain 1 France 1
Mchezaji wa France, ambae ni Straika wa Arsenal, Olivier Giroud, alitoka Benchi na kuifungia bao la kusawazisha katika dakika za mwisho na kuwafanya kutoka sare na Mabingwa wa Dunia na Ulaya, Spain, ya bao 1-1 katika Mechi ya Kundi I iliyochezwa huko Madrid.
Sergio Ramos ndie aliefunga bao la Spain katika Dakika ya 25 na baadae Kipa wa France Hugo Lloris, anaedakia Tottenham, aliokoa Penati iliyopigwa na Cesc Fabregas.
Spain, ambao watarudiana na France Machi Mwakani huko Ufaransa, bado wanaongoza Kundi hili kwa ubora wa magoli wakiwa na Pointi 7 sawa na France kwa Mechi 3 kila mmoja.


MATOKEO:
Jumanne Oktoba 16
Russia 1 Azerbaijan 0
Israel 3 Luxembourg 0
Belarus 2 Georgia 0
Andorra 0 Estonia 1
Latvia 2 Liechtenstein 0
Bosnia-Hercegovina 3 Lithuania 0
Czech Republic 0 Bulgaria 0
Romania 1 Netherlands 4
Ukraine 0 Montenegro 1
Cyprus 1 Norway 3
Faroe Islands 1 Rep of Ireland 4
Croatia 2 Wales 0
Hungary 3 Turkey 1
Iceland 0 Switzerland 2
Macedonia 1 Serbia 0
San Marino 0 Moldova 2
Slovakia 0 Greece 1
Austria 4 Kazakhstan 0
Belgium 2 Scotland 0
Germany 4 Sweden 4
Italy 3 Denmark 1
Albania 1 Slovenia 0
Spain 1 France 1
Poland v England [IMEAHIRISHWA KUCHEZWA LEO]
Portugal 1 Northern Ireland 1
FAHAMU:
-ULAYA yapo Makundi 9
-Washindi 9 wa kila Kundi wataingia Fainali moja kwa moja na Washindi wa Pili 8 bora wenye rekodi nzuri dhidi ya Timu zilizomaliza nafasi za Kwanza, Tatu, Nne na Tano kwenye Kundi lao watapelekwa kwenye Droo kupanga Mechi 4 za Mchujo, zitakazochezwa nyumbani na ugenini, ili kupata Timu nne zitakazoingia Fainali.
 

KOMBE la DUNIA-Marekani ya Kusini: Argentina bado juu!!

MATOKEO:
Jumatano Oktoba 17
Bolivia 4 Uruguay 1
Venezuela 1 Ecuador 1
Paraguay 1 Peru 0
Chile 1 Argentina 2
++++++++++++++++++++++++++++++
BRAZIL_2014_BESTKatika Mechi za mwisho kwa Mwaka huu za Kanda ya Nchi za Marekani ya Kusini kuwania kutinga Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014 huko Brazil Vinara wa Kundi hili Argentina wamezidi kujikita kileleni baada ya leo Alfajiri kushinda ugenini bao 2-1 kwa kuifunga Chile.


Bao za Argentina zilifungwa na Lionel Messi, Dakika ya 28, na Gonzalo Higuain, Dakika ya 31.


Bao la Chile lilifungwa na Guterrez katika Dakika ya 90.


Nayo Bolivia iliichapa Uruguay Bao 4-0 kwa Bao za Saucedo, hetitriki, na Mojica, na Bao la Uruguay kufungwa na Luis Suarez.
++++++++++++++++++++++++++++++





MSIMAMO KANDA ya NCHI za MAREKANI ya KUSINI:
Timu zote zimecheza Mechi 8
1 Argentina Mechi 9 Pointi 20
2 Ecuador Mechi 9 Pointi 17
3 Colombia Mechi 8 Pointi 16
4 Venezuela Mechi 9 Pointi 12
5 Uruguay Mechi 9 Pointi 12
6 Chile Mechi 9 Pointi 12
7 Peru Mechi 9 Pointi 8
8 Bolivia Mechi 9 Pointi 8
9 Paraguay Mechi 9 Pointi 7
FAHAMU: Timu 4 za juu zinatinga Fainali Brazil moja kwa moja na ile ya 5 itaenda Mechi ya Mchujo.
++++++++++++++++++++++++++++++
RATIBA MECHI ZIJAZO:
Ijumaa Machi 22, 2013
Colombia v Bolivia
Argentina v Venezuela
Peru v Chile
Uruguay v Paraguay
Jumanne Machi 26, 2013
Bolivia v Argentina
Chile v Uruguay
Ecuador v Paraguay
Venezuela v Colombia