Friday, October 12, 2012

REDONDO APONA, AENDA KUONGEZA NGUVU SIMBA NA COASTAL KESHO MKWAKWANI

Chombo Redondo


KIUNGO Ramadhani Chombo ‘Redondo’ ameondoka Dar es Salaam leo kwenda Tanga, kuungana na timu yake, Simba SC kwa ajili ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Coastal Union.
 
Redondo hakuondoka na wenzake juzi kutokana na kusumbuliwa na Malaria, lakini baada ya kupata nafuu amepanda basi mchana wa leo kwenda Tanga, ingawa uwezekano wa kuhusishwa kwenye programu ya mechi hiyo ni mdogo.
 
Simba inaendelea vizuri kwa maandalizi yake ya mchezo huo wa kesho dhidi ya wenyeji Coastal Union mjini Tanga na wachezaji wote 22 waliokwenda huko wana morali ya kutosha ya ushindi.
 
Vigogo wa Friends Of Simba (F.O.S) wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Zacharia Hans Poppe wamekodi ndege kwenda Tanga kuwaongezea morali washinde mechi ya kesho, ambayo inatarajiwa kuwa ngumu kutokana wenyeji kupania kuwa timu ya kwanza kuifunga Simba msimu huu.
 
Ikumbukwe Simba imetoa sare moja ya kufungana 1-1 na Yanga, Oktoba 3, mwaka huu katika mechi zake sita ilizocheza sasa na nyingine zote tano imeshinda, jambo ambalo linawafanya waendelee kuwa kileleni mwa Ligi Kuu.
 
Simba, ambayo kwenye mechi hiyo itawakosa nyota wake saba, Emanuel Okwi ambaye amekwenda kujiunga na timu yake ya taifa, Uganda, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Mrisho Khalfan Ngassa wanaosumbuliwa na Malaria, Haruna Shamte, Kiggi Makassy Kiggi, Hamadi Waziri na Komabil Keita ambao ni majeruhi ipo Tanga tangu juzi.
 
Wachezaji 22 walio na timu Tanga ni makipa Juma Kaseja, Wilbert Mweta, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma Nyoso, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Hassan Khatib, Paulo Ngalema, Komabil Keita, viungo Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Salim Kinje, Ramadhani Singano, Uhuru Suleiman, Haruna Moshi ‘Boban’ na washambuliaji Felix Sunzu, Edward Christopher, Haroun Chanongo, Daniel Akuffo na Abdallah Juma.
 
 
Katika kujiandaa na mechi ya Tanga, Simba Jumanne ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
 
Mabao ya Simba siku hiyo yalifungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
 
Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
 
Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.     
 
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.

AZIM DEWJI AWAPA MANENO YA HEKIMA NA MAANA SIMBA, YANGA ILI ZIJITAMBUE

Azim Dewji


WAKATI klabu za Yanga na African Lyon zikiendelea kusuguana na mdhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kampuni ya simu ya mkononi ya Vodacom, klabu za soka nchini zimeaswa kuanza kujitambua ili ziweze kunufaika kwa mambo mengi zaidi, badala ya kutumia muda mrefu kulumbana kwa mambo madogo, akitolea mfano wa nembo ya Vodacom katika
jezi za klabu.
 
 
Ushauri huo umetolewa na mfadhili wa zamani wa Simba, mfanyabiashara Azim Dewji aliyesema kuwa, kama klabu za Tanzania zingekuwa zinajitambua, kamwe zisingepoteza muda kwa malumbano ya nembo, bali maslahi.
 
 
Akizungumza na tano juma kwa njia ya simu hii  leo, alisema klabu kubwa kama Simba na Yanga, zinapaswa kujenga hoja nzito kwa wadhamini, ilin ziweze kunufaika zaidi kwa kuwa zina thamani kubwa kutokana na ukongwe wake na utajiri wa wafuasi kote ndani na nje ya Tanzania.
 
“Sawa wana haki, lakini klabu zetu ifike mahali zijitambue.
Wavuke hapo, mfano Simba na Yanga si zijenge hoja za kupata fedha zaidi kwa wadhamini kwamba ili zivae jezi na nembo, zilipwe vizuri kulingana na hadhi halisi ya klabu hizi.
 
“Haiingii akilini kuona zimeshindwa kujenga ushawishi hata baada ya kuwekwa kundi moja na timu ambazo hazina wanachama wala ofisi, lakini kwa mujibu wa mkataba zote zinalipwa sh milioni 7 kwa mwezi.
 
“Jamani, hivi Yanga yenye utitiri wa wanachama na wafuasi, utajiri wa majengo mfano jingo lake lina thamani ya bilioni 2, inalipwaje sawa na African Lyon ambayo haina wanachama wala ofisi? “Si kama naidharau Lyon, la hasha, bali ndio uhalisia kwa sababu kama
ni kunufaika, Vodacom itanufaika zaidi kwa Yanga kutokana na wafuasi wake wengi kuliko Lyon, kwanini wasitumie mwanya huo kujenga hoja?”
 
alihoji Dewji na kuongeza kuwa, hadhi ya klabu za Simba na Yanga ni angalau kila moja iambulie sh milioni 250 kwa mwaka, na jezi za hadhi ya juu kulingana na hadhi ya klabu zenyewe.
 
Aidha, alisema udhamini mnono wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ni uthibitisho tosha kuwa thamani ya Simba na Yanga. 
 
TBL kupitia bia ya Kilimanjaro, inazidhamini Simba na Yanga kila moja kwa wastani wa sh bilioni 1.5 kwa mwaka, udhamini ukigusa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi, mabasi, vifaa vya michezo, gharama za mikutano ya
kila mwaka na kadhalika.
 
“Una sasa, TBL si wadhamini wakuu wa soka ya nchi hii, lakini klabu hizi zinanufaika, kama ukweli ndio huo kwa nini wasimbane mdhamini wa ligi ili wanufaike zaidi na badala yake wanabaki na malumbano ya nembo pekee? Ni wakati wa klabu zetu kubadilika kwa sababu kote ulimwenguni, soka ni biashara kubwa mno,” alisema.
 
Kauli ya Dewji imekuja huku klabu za Yanga na Lyon zikiwa katika mgogoro juu ya kutovaa jezi zenye nembo ya Vodacom, Yanga ikisema haiko tayari kuvaa jezi zenye nembo nyekundu ya mdhamini huku Lyon ikitaka iruhusiwe kuvaa jezi za mdhamini wake binafsi, kampuni nyingine ya simu za mkononi ya Zantel.
 
Kutokana na mvutano huo, klabu hizo zimejiingiza katika hatari ya kuadhibiwa, kwani Shirikisho la Soka nchini (TFF) limetishia kuchukua hatua dhidi ya klabu zinazokwenda kinyume na matakwa ya mkataba wa udhamini wa Ligi Kuu ambao hata hivyo klabu zinalalamikia kuwa hauko wazi.

KIM POULSEN AENDEA KUANGALIA VIPAJI ZANZIBAR

Kim Poulsen


KOCHA Mkuu wa timu ya soka taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen anatarijia kuwasili visiwani Zanzibar kwa ziara maalum kwa ajili ya kuangalia mechi za Ligi Kuu ya Zanzibar inayoendelea, ili kupata wachezaji ambao atawateua katika kikosi cha Taifa Stars.
 
Akizungumza kwa njia ya simu, mjumbe wa Kamati tendaji wa Zfa Taifa, Masoud Atai, amesema kuwa wamepokea taarifa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) ya ujio wa kocha huyo.
 
"Tumepokea taaifa kutoka kwa wenzetu TFF, na barua wametuletea kwamba kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars atakuja Zanzibar kwa lengo la kuangalia mechi za ligi kuu ya Zanzibar na kutizama wachezaji ambao watamfaa katika timu yake ya Taifa Stars". Alisema Atai.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya mjumbe huyo ni kuwa Kim Poulsen anatarajiwa kuwasili visiwani Zanzibar tarehe 18 ya mwezi huu na anatarajiwa kwenda kisiwani Pemba tarehe 19 ya mwezi huu na kukaa huko kwa muda wa siku 3 kwa ajili ya kuangalia mechi za ligi kuu zitakazochezwa katika kiwanja cha Gombani.
 

Kim Poulsen atarejea kisiwani Unguja siku ya tarehe 22 ya mwezi huu kwa ajili ya kuangalia mechi za ligi kuu katika uwanja wa Amaan. na anatarajiwa kuondoka visiwani Zanzibar tarehe 26 ya mwezi huu.




VPL: Kuendelea Jumamosi, Simba wako kwa ‘Wapwa’ Tanga!


VPL_LOGO>>AZAM yaomba Mechi zao na Yanga, Simba zichezwe COMPLEX!!
>>Ruvu Shooting wataka yao na Yanga ihame COMPLEX ije TAIFA!!
Ligi Kuu Vodacom, VPL, itaendelea Jumamosi kwa Mechi 5 na Mabingwa watetezi ambao pia ni vinara watakuwa ugenini kwa ‘Wapwa’ zao Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
RATIBA:
Jumamosi Oktoba 13
Polisi Moro v Azam FC [Uwanja wa Jamhuri, Morogoro]
Tanzania Prisons v Oljoro JKT [Uwanja wa Sokoine, Mbeya]
Coastal Union v Simba [Mkwakwani, Tanga]
Ruvu Shooting v African Lyon [Mabatini, Mlandizi, Pwani]
Mtibwa Sugar v Mgambo Shooting [Manungu, Turiani, Morogoro]


TAARIFA KAMILI ya TFF:
Release No. 167
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 12, 2012
VPL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI KESHO
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea kesho (Oktoba 13 mwaka huu) kwa timu kumi kupambana kwenye viwanja vitano tofauti katika raundi ya saba ya ligi hiyo yenye timu 14.

Polisi Morogoro itaikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati mwamuzi wa FIFA, Oden Mbaga atakuwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuchezesha mechi kati ya wenyeji Tanzania Prisons na Oljoro JKT.

Jijini Tanga, Simba itakuwa mgeni wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Abdallah Uhako wote kutoka Arusha.
Mechi nyingine za kesho ni Ruvu Shooting dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi, na Mtibwa Sugar watacheza na Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.


Wakati huo huo, Azam imeomba mechi zake za nyumbani dhidi ya Yanga na Simba zichezwe kwenye uwanja wake wa Azam Complex ulioko Chamazi badala ya Uwanja wa Taifa.
Nayo Ruvu Shooting imeomba mechi yake ya ugenini dhidi ya Yanga ya Oktoba 20 mwaka huu ichezwe 

Uwanja wa Taifa badala ya Uwanja wa Azam Complex.
Maombi hayo yatawasilishwa kwenye kikao cha Kamati ya Ligi ya TFF kinachotarajiwa kufanyika kesho (Oktoba 13 mwaka huu) kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
 

AFCON 2013: Kimbembe Vigogo Afrika, Cameroun Mguu nje…….!!


AFCON_2013-NORMALNI WIKIENDI ya kujua Timu zipi 15 zitaungana na Wenyeji Afrika Kusini Mwezi Januari 2013 Nchini humo kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada Mechi 15 za marudiano kuchezwaCAMEROUN-SONGJumamosi na Jumapili huku baadhi ya Vigogo wakiwa kwenye hali tete, na hasa Cameroun ambao walipigwa 2-0 katika Mechi ya kwanza na Kisiwa kidogo Cape Verde na Jumapili watarudiana huko Yaounde, Cameroun huku Viongozi wa Nchi hiyo ‘wakimpigia magoti’ Samuel Eto’o kurudi kuokoa jahazi baada ya kususa kuichezea.

>>DROGBA, TOURE, GERVINHO v PAPISS CISSE, DEMBA BA=Nani kidedea???
Lakini Cape Verde, baada ya kuimarishwa na Wachezaji wengi waliozaliwa Ureno na wanachezea Klabu zao huko huko Ureno, si goigoi na bila shaka huu utakuwa mtanange mkali hapo Jumapili.
Mabingwa watetezi, Zambia, watatua Kampala kucheza na Uganda wakiwa na uongozi wa bao 1-0 walilopata huko kwao huku wakijua kutetea Taji lao si kazi rahisi na hilo lilimlazimu Kocha wao Herve Renard kuamua kupiga Kambi ya mazoezi huko Afrika Kusini.
Renard, ambae amekiri kuwa licha ya Uganda kuwa chini kwenye Listi ya Ubora Duniani ya FIFA, Mechi hiyo kwao ni ngumu mno na DEMBA_BAmambo ni magumu kwao hasa baada ya kumkosa Kiungo wao mahiri Rainford Kalaba alieumia akiichezea Klabu yake TP Mazembe kwenye Nusu Fainali ya CAF CHAMPIONZ LIGI ilipotoka sare 0-0 na Mabingwa wa Afrika Esperance.
Ukiondoa Mechi za marudiano za Congo DR ambao waliifunga Equatorial Guinea 4-0 katika Mechi ya kwanza na ile ya Mali, walioifunga Botswana 3-0, Mechi nyingine zote zitachezwa huku mazingira yakiwa magumu kufuatia matokeo ya Mechi za kwanza.
Nigeria, waliotoka 2-2 na Liberia, wako kwao kusaka ushindi au sare ya 1-1 dhidi ya Liberia iliyoahidiwa Dola 300,000 wakipita na Tunisia nao, waliotoka 2-2 na Sierra Leone, wako kwao wakisaka mbinu za kusonga.
Ghana, wakiwa na ushindi wa 2-0, wako ugenini kuutetea dhidi ya Malawi lakini Morocco, ambao wako nyumbani, inabidi wakipiku kichapo cha 2-0 walichopewa na Mozambique.
Mechi iliyosheheni Masupastaa ni ile ya Ivory Coast na Senegal itakayochezwa ndani ya Stade Leopold Senghor huko Dakar, Senegal huku Ivory Coast ya kina Didier Drogba, Ndugu wawili Toure, Kolo na Yaya, wa Manchester City na Gervinho wa Arsenal, wakitinga kwenye marudiano wakiwa bao 4-2 mbele kupambana na Senegal inayoongozwa na Mastraika hatari wa Newcastle, Papiss Cisse na Demba Ba.
++++++++++++++++++++++++++++++
 AFCON 2013=RATIBA: 
[Kwenye Mabano Matokeo Mechi za kwanza]
[SAA za BONGO]
Jumamosi Oktoba 13
1530 Malawi v Ghana [0-2]
1600 Botswana v Mali [0-3]
1600 Nigeria v Liberia [2-2]
1600 Uganda v Zambia [0-1]
2130 Senegal v Cote d'Ivoire [2-4]
2115 Tunisia v Sierra Leone [2-2]
2200 Morocco v Mozambique [0-2]
Jumapili Oktoba 14
2000 Algeria v Libya [1-0]
1700 Cameroon v Cape Verde [0-2]
1830 Togo v Gabon [1-1]
1800 Angola v Zimbabwe [1-3]
1800 Niger v Guinea [0-1]
1600 Ethiopia v Sudan [3-5]
2100 Burkina Faso v Central African Republic [0-1]
2100 E.Guinea v Congo DR [0-4]
FAHAMU: Washindi 15 wa Mechi hizi watajumuika na Wenyeji Afrika Kusini kwenye Fainali zitakazochezwa Afrika Kusini Januari 2013.
++++++++++++++++++++++++++++++

 

MASKINI LIVERPOOL, UHABA MASTRAIKA: Borini avunjika Mguu!


>>’’Mhadaaji’’ Suarez atetewa na UAF, yaiandikia FIFA kulalamika!!
BORINIBaada ya kumtoa Straika wao Andy Carrol kwa mkopo huko West Ham, Liverpool sasa imejikuta imebakiwa na Straika mmoja tu wa Timu ya Kwanza, Luis Suarez, kufuatia kuumia kwa Fabio Borini akiwa na Timu ya Taifa ya Vijana ya Italy ya chini ya Miaka 21 hivi juzi.
Borini alinunuliwa Mwezi Agosti kwa kitita cha Pauni Milioni 11 hasa kwa ajili ya kuichezea Timu hiyo kwenye michuano ya Makombe, hasa CAPITAL ONE CUP na EUROPA LIGI, lakini sasa itabidi Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers, achukue Chipukizi kutoka Timu za Akiba na zile za Vijana za Klabu hiyo baada ya Straika huyo kuvunjika Mguu.
Borini anatarajiwa kurudi Liverpool kutoka Italy ili kufanyiwa uchunguzi zaidi Mguu aliovunjika wakati wa mazoezi wa Timu ya Italy.
Wakati huo huo, Chama cha Soka cha Uruguay, UAF, kimeamua kuiandikia barua FIFA kulalamikiaSUAREZ-KUJIRUSHAkauli ya Makamu wa Rais wa FIFA, Jim Boyce, ambae alimtaja Luis Suarez wakati akiponda ile tabia ya Wachezaji kujidondosha kusudi ili kuhadaa Marefa wapewe Penati ambayo aliita ni ‘kansa’ katika gemu.
UFA imeandika Barua kwa FIFA ikisema haikuwa haki kwa Jim Boyce, ambae pia ni Mwakilishi wa Uingereza kwenye FIFA, kumtaja Suarez kwa jina kwenye kauli zake.
Katika Barua hiyo aliyopelekewa Sepp Blatter, Rais wa FIFA, UAF imetaka Kamati ya Maadili ya FIFA imchunguze Boyce kwa kukiuka Maadili ya Uongozi.
Kwa sasa Suarez yuko huko Marekani ya Kusini na Timu ya Taifa ya Uruguay ambayo leo inacheza na Argentina huko Buenos Aires Mechi ya Kundi la Nchi za Marekani ya Kusini kuwania kutinga Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014 huko Brazil.
Hivi majuzi, Bosi wa Stoke City Tony Pulis aliitaka FA imuadhibu Straika wa Liverpool Luis Suarez kwa tabia yake ya kutaka kuwahadaa Marefa kwa kujidondosha makusudi ndani ya boksi ili apate Penati kufuatia tukio la kwenye Mechi ya Ligi ya Jumapili ambayo Stoke City ilitoka 0-0 na Liverpool  na katika Kipindi cha Pili Luis Suarez ‘alijidondosha’ kutaka Penati ambayo Tony Pulis anaamini ulikuwa ni udanganyifu.
Hata hivyo kwa Sheria za sasa, madamu Refa anampa Mchezaji aliejaribu kuhadaa kwa kujidondosha Kadi ya Njano, FA haiwezi tena kuchukua hatua yeyote ya ziada kwa kosa hilo hilo.
Pia kwa vile kosa la kuhadaa adhabu yake ni Kadi ya Njano tu, FA haiwezi baadae kumchukulia hatua Mchezaji yeyote hata kama Refa hakuliona kosa hilo kwa vile Sheria zinawapa haki ya kuadhibu baadae kwa makosa tu yanayostahili Kadi Nyekundu.
Lakini Jim Boyce ametaka Sheria zibadilishwe ili FA zipate nguvu ya kuwaadhibu Wachezaji kwa makosa ya udanganyifu.
Boyce amesema: “Nimeona matukio kadhaa hivi karibuni na nimeliona hili la Suarez na kulitazama mara mbili au tatu na kwangu mimi huu ni udanganyifu. Hii ni kama Kansa ndani ya gemu na naamini ikiwa wazi kwa kila Mtu kwamba kujidondosha ni udanganyifu ni lazima wapewe adhabu!”
Aliongeza: “Kuna wakati Marefa wanapata ugumu kuamua kama ni faulo au sio na kama Wachezaji wanahadaa basi kazi yao inakuwa ngumu zaidi!”
 

Poulsen kutua Zenji!!


TAIFA_STARS-FRAMED>>RIPOTI na Ally Mohammed, COCONUT FM 88.2, Zenji

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen anatarijiwa kuwasili Visiwani Zanzibar kwa ziara maalum kwa ajili ya kuangalia mechi za Ligi Kuu ya Zanzibar inayoendelea ili kupata Wachezaji ambao atawateua katika Kikosi cha Taifa Stars.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mjumbe wa Kamati Utendaji wa ZFA Taifa, Masoud Atai, amesema kuwa wamepokea taarifa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini, TFF, ya ujio wa Kocha huyo.
"Tumepokea taaifa kutoka kwa wenzetu TFF, na barua wametuletea kwamba Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars atakuja Zanzibar kwa lengo la kuangalia mechi za Ligi Kuu ya Zanzibar na kutizama Wachezaji ambao watamfaa katika Timu yake ya Taifa Stars" Alisema Atai.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mjumbe huyo ni kuwa Kim Poulsen anatarajiwa kuwasili visiwani Zanzibar tarehe 18 ya mwezi huu na anatarajiwa kwenda kisiwani Pemba tarehe 19 ya mwezi huu na kukaa huko kwa muda wa siku 3 kwa ajili ya kuangalia mechi za Ligi Kuu zitakazochezwa katika Kiwanja cha Gombani.
Kim Poulsen atarejea Kisiwani Unguja siku ya tarehe 22 ya mwezi huu kwa ajili ya kuangalia mechi za Ligi Kuu katika Uwanja wa Amaan na anatarajiwa kuondoka Visiwani Zanzibar tarehe 26 ya mwezi huu.