Tuesday, October 16, 2012

HAKUNA UFISADI KATIKA USAJILI SIMBA, HANS POPPE AKANUSHA MADAI YA MRWANDA

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe kushoto akimkabidhi jezi ya Simba Daniel Akuffo baada ya kusajiliwa. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu'


SIMBA SC imesema kwamba hakuna ‘ufisadi’ wa aina yoyote katika zoezi la usajili katika klabu hiyo kutokana na utaratibu mzuri uliowekwa na mshambuliaji Danny Mrwanda aliachwa kwa sababu ya dau kubwa alilotaka.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amekanusha kwa nguvu zote madai kwamba wachezaji huombwa ‘twenty percent’ ili kusajiliwa na kusistiza kwamba Mrwanda alishindana na klabu hiyo ndiyo maana akaachwa.
“Alitaka dau kubwa, baadaye akakubali dau tulilotaka kumpa, baadaye tena ajaka anatutajia timu nyingine inamtaka, sisi tukamuambia basi nenda kwenye hiyo timu nyingine, ndivyo tulivyoachana naye huyo bwana,”alisema Hans Poppe.
Mrwanda alijiunga tena na Simba na Juni mwaka huu, akitokea Vietnam alipokuwa anacheza soka ya kulipwa, lakini baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu akatemwa.
Baada ya kutemwa Mrwanda, akasajiliwa mshambuliaji Daniel Akuffo kutoka Ghana ambaye hata hivyo, kocha Mserbia Milovan Cirkovick haridhishwi na uwezo wake.
Mrwanda aliwahi kumzungumzia Akuffo na kusema tatizo ni twenty percent, jambo ambalo sasa Hans Poppe anakanusha.  


LIGI DARAJA LA KWANZA YAANZA OKTOBA 24, MAJIMAJI, ASHANTI ZARUDI KIVINGINE



LIGI Daraja la Kwanza Tanzania Bara inatarajiwa kuanza rasmi Oktoba 24, mwaka huu kwa timu 18 kati ya 24 kujitupa kwenye viwanja tisa tofauti katika ligi hiyo inayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema leo kwamba Mechi za raundi ya kwanza za kundi A zitakazochezwa Oktoba 24 mwaka huu ni Burkina Faso dhidi ya Mbeya City (Jamhuri, Morogoro), Mlale JKT na Small Kids (Majimaji, Songea) na Kurugenzi Mufindi dhidi ya Majimaji (Uwanja wa Wambi, Mufindi mkoani Iringa).
Amesema Mkamba Rangers na Polisi Iringa zitakamilisha raundi ya kwanza kwa kundi hilo Oktoba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wakati mechi za raundi ya pili kwa kundi hilo zitachezwa Oktoba 27 mwaka huu kwa Polisi Iringa vs Mbeya City (Samora, Iringa), Majimaji vs Small Kids (Majimaji, Songea), Burkina Faso vs Mkamba Rangers (Jamhuri, Morogoro) na Kurugenzi Mufindi vs Mlale JKT (Wambi, Mufindi).
Amesema raundi ya tatu ni Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Mbeya City vs Mlale JKT (Sokoine, Mbeya), Small Kids vs Mkamba Rangers (Nelson Mandela, Sumbawanga), Majimaji vs Burkina Faso (Majimaji, Songea) na Polisi Iringa vs Kurugenzi Mufindi (Samora, Iringa).
Amezitaja timu za Kundi B ambazo zitamenyana Oktoba 24, mwaka huu ni Ndanda vs Transit Camp (Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara), Villa Squad vs Moro United (Mabatini, Pwani) wakati Oktoba 25 mwaka huu ni Green Warriors vs Tessema (Mabatini, Pwani) na Polisi Dar es Salaam vs Ashanti United (Chamazi, Dar es Salaam).
Amesema raundi ya pili kwa kundi hilo ni Oktoba 27, mwaka huu Ndanda vs Green Warriors (Nangwanda Sijaona, Mtwara), Villa Squad vs Tessema (Mabatini, Pwani) wakati Oktoba 28 mwaka huu ni Ashanti United vs Transit Camp (Mabatini, Pwani) na Oktoba 29 mwaka huu ni Moro United vs Polisi Dar es Salaam (Chamazi, Dar es Salaam).
Amesema Novemba 1, mwaka huu Green Warriors itamenyana na Ashanti United (Mabatini, Pwani), Novemba 2 mwaka huu ni Polisi Dar es Salaam vs Villa Squad (Chamazi, Dar es Salaam), Novemba 4 mwaka huu ni Tessema vs Ndanda (Chamazi, Dar es Salaam) na Transit Camp vs Moro United (Mabatini, Pwani).
Amesema Kundi C nalo ambalo mechi zake zitachezwa Oktoba 24, mwaka huu ni kati ya Kanembwa FC vs Polisi Dodoma (Lake Tanganyika, Kigoma), Mwadui vs Morani (Kambarage, Shinyanga), Pamba vs Polisi Mara (Kirumba, Mwanza) na Rhino Rangers vs Polisi Tabora (Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Amesema Raundi ya pili ni Oktoba 27 mwaka huu; Polisi Tabora vs Polisi Dodoma (Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mwadui vs Polisi Mara (Kambarage, Shinyanga), Kanembwa FC vs Morani (Lake Tanganyika, Kigoma) na Pamba vs Rhino Rangers (Kirumba, Mwanza), wakati Oktoba 31 mwaka huu ni raundi ya tatu; Polisi Mara vs Rhino Rangers (Karume, Musoma), Morani vs Polisi Tabora (Kiteto, Manyara), Polisi Dodoma vs Pamba (Jamhuri, Dodoma) na Kanembwa FC vs Mwadui (Lake Tanganyika, Kigoma).

MBAGA AZICHEZESHA KENYA, BAFANA BAFANA

Oden Mbaga kulia akimuonya Haruna Moshi 'Boban' wakati wa mechi kati ya Taifa Stars na Malawi, Mei 26, mwaka huu. Kulia ni kiungo wa The Flames, James Sangala aliyechezewa rafu na Haruna.

REFA Oden Mbaga wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ndiye anayechezesha mechi ya kirafiki kati ya Kenya (Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana Bafana).
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema leo kwamba mechi hiyo inachezwa leo Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Nairobi na Mbaga atasaidiwa na marefa wasaidizi wa FIFA, John Kanyenye kutoka Mbeya na Erasmo Jesse wa Morogoro.
Amesema TFF imeteua marefa hao baada ya kupata maombi kutoka kwa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) ambao ndiyo waandaaji wa mechi hiyo ambayo ni moja ya vipimo kwa kocha mpya wa Harambee Stars, Henry Michel kutoka Ufaransa.
Wakati huo huo: Wambura Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Soka Tanzania (TAFCA) imeongeza muda kwa wagombea kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa chama hicho ambao sasa utafanyika Novemba 25 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, jana ndiyo ilikuwa mwisho wa kuchukua fomu lakini mwitikio wa wagombea bado umekuwa mdogo ambapo ni watano tu waliojitokeza.
Hivyo, amesema wameongeza muda wa kuchukua na kurudisha fomu ambapo mwisho itakuwa ni Oktoba 19 mwaka huu saa 10 kamili alasiri. Fomu zinapatikana ofisi za TAFCA ambazo ziko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Mhazini na wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji.

NGASSA AANZA KUJIFUA NA SIMBA, LAKINI ASEMA HALI YAKE BADO TETE

Ngassa
MRISHO Khalfan Ngassa ameanza mazoeizi jana timu yake Simba SC kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam, lakini amesema bado hayuko sawa sawa, maana yake uwezekano wa kucheza mechi ya kesho dhidi ya timu yake ya zamani, Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni mdogo.
Akizungumzajana, Ngassa ambaye aliugua Malaria baada ya mechi dhidi ya Yanga, Oktoba 3, mwaka huu alisema kwamba bado anahisi hana nguvu.
“Nimeanza mazoezi na timu, lakini hata hivyo bado hali yangu haiko sawa sawa kwa kweli, najisikia mwili hauna nguvu, hii Malaria ilinipelekesha sana, ila najikongoza hivyo hivyo,”alisema Ngassa.
Kiungo mwingine wa Simba SC aliyekuwa anaumwa Malaria, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ naye ameanza mazoezi na timu na anaweza kucheza kesho.  
Mbali na Redondo, katika mchezo huo, Simba inatarajiwa kuwapokea wachezaji wake wengine watatu iliyowakosa kwenye mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana, Emmanuel Okwi aliyekuwa kwao Uganda kuichezea timu yake ya taifa, Komabil Keita, Haruna Shamte na Kiggi Makasy waliokuwa majeruhi.
Mechi nyingine za kesho zitakuwa kati ya Prisons na Azam FC kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Polisi Morogoro na JKT Ruvu Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Mgambo JKT na Toto Africans Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na JKT Oljoro dhidi ya African Lyon Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Simba bado ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 17, baada ya kucheza mechi saba, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, ambayo hata hivyo imecheza mechi sita, wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza mechi saba pia. 

YANGA SC SASA KUINGIA KAMBINI LEO BAADA YA KUKWAMA JANA

Wachezaji wa Yanga wakipasha

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kuingia kambini leo katika hoteli ya Uppland, Changanyikeni, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga ilikwama kuingia kambini jana ilivyopanga na badala yake sasa wataingia leo Changanyikeni, ili kuziweka fikra za wachezaji pamoja kuelekea mechi hiyo ya Jumamosi.
Habari njema ni kwamba, beki Kevin Yondan jana alianza mazoezi mepesi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza tangu agongwe na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu.
Pamoja na Yondan, mshambuliaji Said Bahanuzi aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja naye alianza pia mazoezi mepesi jana kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam.
Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Jumatatu wiki iliyopita.
Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba iliyocheza mechi saba pia, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 17, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, iliyocheza mechi sita.

AZAM FC KUIONJA SOKOINE LEO

Azam FC


AZAM FC leo jioni watafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, ili kuuzoea kabla ya mechi ya kesho dhidi ya wenyeji, Prisons katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na washindi wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame wapo mjini Mbeya tangu juzi saa 1:00 usiku na jana walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Iyunga mjini humo.
Kikosi kizima cha Azam kipo vizuri kuelekea mchezo unaitarajiwa kuwa mgumu kwao na wachezaji wa morali ya ushindi, ili kuweka vizuri mazingira ya kutwaa taji la kwanza la ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara.
Azam waliondoka Morogoro juzi asubuhi baada ya mechi yao na Polisi kwenye Uwanja, Jamhuri Jumamosi ambayo walishinda 1-0, bao pekee la mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche.
Mbeya ni kati ya vituo ambavyo vinawaogopesha vigogo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam, Simba na Yanga kutokana na imani kwamba Prisons haifungiki kwenye Uwanja wake.
Sababu kubwa ni ubovu wa Uwanja wa Sokoine, ambao wenyewe Prisons wameuzoea na wanaujulia, wakati timu nyingine hupata tabu mno.
Kati ya vigogo hao watatu, ambao wanafukuzana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu, Azam inakuwa timu ya pili kwenda Mbeya, baada ya Yanga iliyolazimishwa sare ya bila kufungana na Wajelajela hao kwenye mechi yao ya kwanza ya ligi hiyo.
Simba imeanzia Dar es Salaam kucheza na Prisons, Septemba 29, mwaka huu katika mechi ambayo walishinda kwa taabu mabao 2-1 na sasa watarudiana na Wajelajela hao mjini Mbeya katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo.   
Mikoa mingine tishio ni Kanda ya Ziwa, ambako Azam tayari imekwishamaliza na kukusanya pointi nne baa ya kuifunga 1-0 Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Yanga pia imemaliza deni la Kanda ya Ziwa, ikiambulia pointi tatu, baada ya kufungwa 1-0 na Kagera na kushinda 3-1 dhidi ya Toto.


KATIBU MKUU Osiah atoa Taarifa kuhusu Chaguzi za Wanachama wa TFF

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana Oktoba 11, 2012 kujadili michakato ya chaguzi mbalimbali za wanachama wa Shirikisho. Katika kikao chake, Kamati ilijadili michakato ya chaguzi za viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu (FRAT), Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Dar es salaam (DRFA),.
Pia Kamati ilijadili mchakato wa chaguzi za Chama cha Madaktari wa Michezo (TASMA) na kupokea mchakato wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Mbeya (MRFA).
Baada ya kujadili chaguzi hizo kwa kina, Kamati ilifikia uamuzi ufuatao:

1.       FRAT
Uchaguzi wa FRAT haukufanyika baada ya wajumbe kugoma wakipinga kuondolewa kwa baadhi ya wagombea. Kamati ilikubaliana kuiagiza Kamati ya Uchaguzi ya FRAT kuhakikisha uchaguzi unafanyika Novemba 17, 2012 na kufanya maandalizi yote muhimu ikiwa ni pamoja na sehemu ambako uchaguzi huo utafanyika. Mkutano utatakiwa kuwapigia kura wajumbe waliopitishwa kugombea uongozi tu.
 
2.       RUREFA
Baada ya kufuta uchaguzi wa viongozi wa RUREFA na kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitaka Kamati ya Utendaji ya RUREFA kuteua kamati mpya ya uchaguzi ya chama hicho kabla ya Oktoba 20, 2012 na kuiagiza kamati mpya kuwa imeshatangaza mchakato wa uchaguzi ifikapo Oktoba 24, 2012.

3.       SHIREFA
Kamati ilipokea pingamizi dhidi ya baadhi ya wagombea uongozi wa SHIREFA na hivyo kuagiza walioweka pingamizi na waliowekewa pingamizi pamoja na mwakilishi wa Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA kuhudhuria kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Alhamisi ya Oktoba 18, 2012 kwa ajili ya maamuzi ya mwisho.

4.       MRFA
Kamati ilipokea rufaa na pingamizi kutoka kwa baadhi ya wagombea walioenguliwa kuwania uongozi wa chama hicho na hivyo imewataka walioweka pingamizi na waliokata rufaa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Oktoba 18, 2012 jijini Dar es salaam.

5.       TASMA
Kamati iliona mapungufu katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa TASMA na kuamua chama hicho kifanye uchaguzi ifikapo Desemba mosi badala ya uchaguzi kufanyika  Oktoba 27, 2012 kama ilivyokuwa imepangwa awali. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaiagiza Kamati ya Uchaguzi ya TASMA kuhakikisha kasoro zilizojitokeza zinarekebishwa ili uchaguzi ufanyike kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na Kanuni za Uchaguzi.

6.       DRFA
Awali, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilitangaza kuwa hatma ya uchaguzi wa DRFA itajulikana baada ya kikao cha leo, lakini kutokana na wajumbe kutoweza kuhudhuria kwa sababu tofauti, mustakabali wa suala hilo sasa utajulikana baada ya kikao cha Oktoba 18, 2012.
Wagombea na wadau wanaotakiwa kuhudhuria kikao cha Oktoba 18, 2012 wanataarifiwa kuwa kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za TFF kuanzia saa 08:2012.
Kamati inawaomba wajumbe wote kuhudhuria bila ya kukosa.
Angetile Osiah
Katibu Mkuu TFF


TAFCA YAONGEZA MUDA WA KUCHUKUA FOMU
Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) imeongeza muda kwa wagombea kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa chama hicho ambao sasa utafanyika Novemba 25 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, jana ndiyo ilikuwa mwisho wa kuchukua fomu lakini mwitikio wa wagombea bado umekuwa mdogo ambapo ni watano tu waliojitokeza.
Hivyo, amesema wameongeza muda wa kuchukua na kurudisha fomu ambapo mwisho itakuwa ni Oktoba 19 mwaka huu saa 10 kamili alasiri. Fomu zinapatikana ofisi za TAFCA ambazo ziko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Mhazini na wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji.


CAF yaitimua Senegal AFCON 2013!


>>IVORY COAST yathibitishwa Mshindi!!
SENEGAL_v_IVORY_COAST_FUJOLEO Shirikisho la Soka Afrika, CAF, limetoa tamko rasmi la kuitoa nje ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2013, Senegal kufuatia vurugu zilizotokea kwenye Mechi ya majuzi Jumamosi ya marudiano ya Raundi ya Mwisho ya Mtoano kuwania kuingia Fainali zitakazochezwa Afrika Kusini Januari Mwakani na kusababisha Mechi kati yao na Ivory Coast kuvunjika katika Dakika ya 72.
Hiyo Jumamosi, Ivory Coast walikuwa wakiongoza kwa bao 2-0 katika Mechi iliyochezwa Stade Leopold Senghor na kuwafanya waongoze kwa jumla ya bao 6-2 katika Mechi mbili lakini Mechi hiyo ilivunjwa baada ya Mashabiki wa Senegal waliochukizwa kuwasha moto Majukwaani na kurusha vitu Uwanjani.
CAF imethibitisha kuwa matokeo ya Mechi hiyo yatabaki kama yalivyo, ikimaanisha Ivory Coast ndio watatinga zitakazoanza Januari 19 Mwakani huko Afrika Kusini na Senegal kutupwa nje.
Katika Taarifa yake, CAF imetamka: “CAF imeamua kuthibitisha  rasmi matokeo ya bao 2-0 kwa Ivory Coast…na kuichukulia Senegal kuwa wameshindwa na kutolewa nje ya Mashindano na hili halihusishwi na adhabu yeyote ambayo itatolewa na Bodi ya Nidhamu ya CAF.”
Sheria za CAF ziko wazi kuwa: “Ikiwa Refa atalazimika kuvunja pambano kabla ya muda wake kumalizika kwa sababu ya uvamizi wa Uwanja au fujo dhidi ya Timu ngeni, Timu mwenyeji ndio itahesabiwa imeshindwa na kutolewa nje ya Mashindano na hili halihusiana na adhabu zinazostahili Kisheria.”
Tayari CAF imeshapanga mgawanyiko wa Timu katika Vyungu vinne ambavyo vitatumika hapo Oktoba 24 kwenye Droo ya kupanga Makundi manne ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazochezwa huko Afrika Kusini kuanzia Tarehe 19 Januari 2013 hadi 10 Februari 2013.
++++++++++++++++++++++++++++++++


VYUNGU: 
CHUNGU 1: South Africa, Zambia, Ghana, Ivory Coast
CHUNGU 2: Mali, Tunisia, Angola, Nigeria
CHUNGU 3: Algeria, Burkina Faso, Morocco, Niger
CHUNGU 4: Togo, Cape Verde, Congo DR, Ethiopia
FAHAMU: Kila Chungu kitatoa Timu moja ili kupata Makundi manne ya Timu 4 kila moja.
++++++++++++++++++++++++++++++++
Mgawanyo huu wa Vyungu umechukuliwa kwa kutathmini matokeo ya kila Nchi katika Mashindano matatu yaliyopita ya Kombe la Mataifa ya Afrika na si Ubora kwa mujibu wa Listi ya Ubora Duniani ya FIFA.

MWESINGWA AOMBA RADHI KUFUATIA KUTOLEWA KWA CRANES.

NAHODHA wa timu ya taifa ya Uganda Cranes, Andy Mwesingwa ameomba radhi kwa taifa na mashabiki wa soka nchini humo kwa kushindwa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika ambayo itafanyika nchini Afrika Kusini 2013.

 The Cranes walifanikiwa kuwafunga Zambia maarufu kama Chipolopolo bao 1-0 katika muda wa kawaida mwishoni mwa wiki iliyopita lakini waliotolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penati 8-9 baada ya kumaliza kwa sare. 

Mwesigwa alikosa mojawapo ya penati mbili za Uganda huku Patrick Ochan naye akishuhudia penati yake ikizuiwa na kipa wa Chipolopolo Kennedy Mweene na kuwafanya mabingwa hao wa Afrika kukata tiketi ya kwenda kutetea kombe lao katika michuano hiyo. 
Mwesingwa amesema katika suala la upigaji penati hakuna mchezaji ambaye anaweza kutamba kwamba yeye ni mjuzi zaidi haswa mchezo kama ule hivyo kukosa kwake kuchukuliwe kama ni bahati mbaya na kuomba mashabiki kuendelea kuwaunga mkono kwa ajili ya ajili ya mashindano mengine yaliyopo mbele yao.


FSF YAMLAUMU DIOUF VURUGU ZA SENEGAL.

RAIS wa Shirikisho la Soka nchini Senegal-FSF, Augustin Senghor amesema kuwa tukio lilitokea katika mchezo Jumamosi iliyopita lilikuwa ni hujuma za makusudi zilizopangwa na watu ambao wanataka kusambaratisha soka la nchini humo na kulitia doa shirikisho hilo.

  Senghor amesema kuwa mtu binafsi alinunua tiketi na kusisambaza kwa mashabiki wakorofi kwa madhumuni ya kuvuruga mchezo kati ya Senegal na Ivory Coast ambao ulikuwa ni mchezo wa pili wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kitendo ambacho kilifanikiwa kwani mchezohuo uliisha katika dakika ya 76 baada ya vurugu kuzuka.

 Rais huyo aliendelea kusema kuwa wanaamini kuwa tukio hilo ni la hujuma na lilifanywa na mtu au kikundi cha watu ili kufuruga soka nchini humo. Kauli hiyo ya Senghor inakuwa kama inamlenga mshambuliaji nyota wa klabu ya Leeds United, El Hadji Diouf ambaye mapema Jumatatu alikiri kuwa FSF ilizuia tiketi zake 1,000 alizoagiza kwa ajili ya kusambaza kwa mashabiki wake kwa kuogopa nyota huyo anataka kuwapatia tiketi hizo wahuni ili wavuruge mchezo huo.

 Kwa mujibu wa chanzo kilichikaribu na FSF, Diouf ndiye pekee aliyelipia tiketi nyingi zaidi katika mchezo huo ingawa mwenyewe amekunusha kuhusika katika kuchochea vurugu hizo

KIRAFIKi: Brazil yaibonda Japan 4-0!


NEYMAR_v_MESSI>>NEYMAR apiga 2, Kaka 1, Paulinho 1
Brazil wamemaliza Ziara yao ya Ulaya kwa kupiga jumla ya Bao 10-0 katika Mechi mbili baada ya leo kuibonda Japan 4-0 huko Stadion Miejski, Mjini Poznan, Poland kipigo ambacho kimekuja baada ya Ijumaa kuifumua Iraq 6-0 huko Malmo, Sweden.

Kikosi cha Brazil, chini ya Kocha Mano Mezes, hakikuwapa nafasi hata chembe Japan waliocheza mfumo usiokuwa na Straika maalum na walimudu kuwapiga bao la kwanza katika Dakika ya 12 mfungaji akiwa Paulinho.
Neymar alipiga bao la pili katika Dakika ya 25 kwa Penati na Kipindi cha Pili Neymar akapiga Bao la 3 na Mkongwe Kaka akafunga Bao la 4.
Brazil wangeweza kupata Mabao zaidi baada ya Mashuti ya Kaka na Hulk kugonga mwamba.

Vikosi vilivyoanza:
Brazil (Mfumo 4-4-2): Diego Alves; Adriano, Silva, Luiz, Castan; Paulinho, Ramires, Kaka, Oscar; Neymar, Hulk.
Japan (Mfumo 4-3-3): Kawashima; Sakai, Konno, Yoshida, Nagatomo; Endo, Hasebe, Nakamura; Kiyotake, Kagawa, Honda

 

LEO Poland v England: Kocha Poland aionya England


>>HODGSON akiri LEWANDOWSKI ndie tishio kwao!!
>>POLAND wamwogopa ROONEY!!
Kocha wa Poland Waldemar Fornalik ameionya England wasiidharau Poland licha ya rekodi na historia kuwahukumu kwa kuifunga England mara moja tu-Mwaka 1974-kutoka sare mara 6 katika Mechi 17 zilizopita na leo Usiku Nchi hizo zinategemewa kukutana Uwanja wa Kazimierz Gorski kwenye Mechi ya Kundi H la Barani Ulaya kuwania kucheza huko Brazil Mwaka 2014 katika Fainali za Kombe la Dunia.
+++++++++++++++++++++++
MSIMAMO:
KUNDI H
1 England Mechi 3 Pointi 7
2 Montenegro Mechi 2 Pointi 4
3 Poland Mechi 2 Pointi 4
4 Ukraine Mechi 2 Pointi 2
5 Moldova Mechi 3 Pointi 1
6 San Marino Mechi 2 Pointi 0
+++++++++++++++++++++++
LEWANDOSKI_IN_POLANDWakati Fornalik akitoa onyo hilo, Kocha wa England Roy Hodgson ametoboa kuwa kwa upande wao tishio kubwa litatoka kwa Straika hatari wa Mabingwa wa Germany, Borussia Dortmund, Robert Lewandoeski.

Akizungumzia mtanange huo, Fornalim alisema: “Poland na England ni Mechi muhimu. Tunajua uwezo wao ni kiwango cha juu lakini hata sie tuna thamani yetu.”
Katika Kundi H, Poland wamecheza Mechi 2 na kutoka 2-2 na Montenegro na kuifunga Moldova 2-0.

Leo Poland wataingia kwenye Mechi hii bila Nahodha wao Kuba Blaszczykowski, ambae ni Kiungo wa Borussia Dortmund, kwa kuwa ameumia enka na utepe wa Ukepteni umekwenda kwa Beki wa Klabu ya Anderlecht, Marcin Wasilewski, Miaka 32, mwenye miguvu.
Akizungumzia Mechi hii, Marcin Wasilewski amesema: “Siku zote Poland tunahusudu Soka la England. Napenda kuitazama Ligi Kuu England na ilikuwa ndoto yangu kucheza huko. Hatari kwetu toka kwao ni Wayne Rooney!”

VIKOSI VINATARAIWA:
Poland: Kuszczak; Perquis, Wasilewski, Wojtkowiak, Wawrzyniak; Borysiuk, Mierzejewski, Krychowiak, Wszolek; Lewandowski, Piech
England: Hart; Johnson, Cahill, Jagielka, Cole; Milner, Carrick, Gerrard, Oxlade-Chamberlain; Defoe, Rooney

RATIBA:
Jumanne Oktoba 16
[SAA za BONGO]
2145 Albania v Slovenia
2000 Andorra v Estonia
1900 Belarus v Georgia
2145 Belgium v Scotland
2100 Bosnia-Hercegovina v Lithuania
2100 Czech Republic v Bulgaria
2130 Hungary v Turkey
2130 Iceland v Switzerland
1900 Israel v Luxembourg
2000 Latvia v Liechtenstein
2130 Macedonia v Serbia
2245 Portugal v Northern Ireland
2100 Romania v Netherlands
1800 Russia v Azerbaijan
2130 San Marino v Moldova
2130 Slovakia v Greece
2200 Spain v France
2100 Ukraine v Montenegro
2100 Cyprus v Norway
2100 Faroe Islands v Rep of Ireland
2130 Austria v Kazakhstan
2100 Croatia v Wales
2145 Germany v Sweden
2145 Italy v Denmark
2200 Poland v England
FAHAMU:
-ULAYA yapo Makundi 9
-Washindi 9 wa kila Kundi wataingia Fainali moja kwa moja na Washindi wa Pili 8 bora wenye rekodi nzuri dhidi ya Timu zilizomaliza nafasi za Kwanza, Tatu, Nne na Tano kwenye Kundi lao watapelekwa kwenye Droo kupanga Mechi 4 za Mchujo, zitakazochezwa nyumbani na ugenini, ili kupata Timu nne zitakazoingia Fainali.


BIN HAMMAM AIKATIA RUFANI FIFA, CAS.

ALIYEWAHI kuwa mgombea wa zamani wa urais na mjumbe wa kamati kuu ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Mohamed Bin Hammam amekata rufani katika Mahakama ya Michezo ya Usuluhishi-CAS juu ya kjufungiwa tena na shirikisho hilo ili kupisha uchunguzi mpya. 

  Bin Hammam ambaye alichuana na Sepp Blatter katika kinyang’anyiro cha urais wa FIFA mwaka jana amefungiwa na shirikisho hilo Julai 26 mwaka huu ikiwa ni wiki moja baada ya CAS kutengua adhabu yake ya kufungiwa maisha kujishughulisha na masuala ya michezo.

 Wakili wa Bin Hammam, Eugene Gulland katika taarifa yake alithibitisha kuwa mteja wake ambaye pia amewahi kuwa rais wa Shrikisho la Soka barani Asia-AFC ameamua kukata rufani kupinga adhabu hiyo aliyopewa na FIFA. Katika taarifa yake ya kutengua kifungo cha aisha cha Bin Hammam, CAS katika taarifa imesema kuwa FIFA walishindwa kuwasilisha ushahidi uliokamilika juu ya tuhuma kwamba aliwanunua maofisa wa soka wan chi za Carribean katika uchaguzi mwaka uliopita ingawa walimalizia kuwa uamuzi huo haumaanishi kwamba hakutenda kitendo hicho.

 Bin Hammam alikuwa natuhumiwa kujaribu kuwanunua maofisa wa soka wa nchi za Caribbean ili waweze kumpigia kura kwa kuwapa bahasha zilizokuwa na kiasi cha dola 40,000 kila mmoja katika mkutano na viongozi hao uliofanyika nchini Hispania mwezi mmoja kabla ya uchaguzi.