Wednesday, October 10, 2012

WABABE WA YANGA WAKALIWA KOONI NA JKT KAITABA

Wachezaji wa Kagera wakiwasalimia wachezaji wa JKT leo Uwanja wa Kaitaba. Picha kwa hisani ya Bukoba Sports.


WABABE wa Yanga, Kagera Sugar jioni hii wamelazimishwa sare ya bila kufungana na JKT Ruvu ya Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Sare hiyo imeisaidia JKT kupanda kwa nafasi moja kutoka ya 13 hadi ya 12, juu ya JKT Mgambo ya Tanga, wakati Kagera imelingana kila kitu sasa na Yanga, pointi na wastani wa mabao, zikiwa katika nafasi ya nne na ya tano.
 
Sare hii, maana yake Kagera imeshindwa kuendeleza wimbi la ushindi waliloanza nalo juzi, wakiifunga Yanga 1-0, kwa bao pekee la Themi Felix katika dakika ya 67 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
 
Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.
Ligi hiyo, itaendelea kesho kwa mchezo mmoja, utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza baina ya wenyeji Toto African na Yanga SC.

NGASSA, KIGGI WAENGULIWA SAFARI YA SIMBA TANGA GHAFLA

Ngassa


VIUNGO wa zamani wa Yanga, Mrisho Khalfan Ngassa na Kiggi Makassy Kiggi wameenguliwa katika kikosi cha Simba kilichoondoka leo kwenda Tanga kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
 
 
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, Ngassa ameondolewa kwa sababu bado hajapona Malaria iliyomkosesha mechi iliyopita ya ligi hiyo dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, wakati Makassy aliumia jana kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Azam FC.
 
 
Awali, Kamwaga alisema leo mchana kwamba, katika safari hiyo timu hiyo itawakosa nyota watano, Emanuel Okwi ambaye amekwenda kujiunga na timu yake ya taifa, Uganda, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ anayesumbuliwa na Malaria, Haruna Shamte, Hamadi Waziri na Komabil Keita ambao ni majeruhi.
 
 
Katika kujiandaa na mechi ya Tanga, Simba jana ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
 
 
Mabao ya Simba leo yalifungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
 
 
Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
 
 
Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.     
 
 
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.

ZEN C NA WENGINE WATANO WAWEKEWA PINGAMIZI UCHAGUZI TWFA

Zen C; Atatoka kwenye pingamizi nne?

MWANDISHI wa Habari Mwandamizi wa magazeti ya serikali, Daily News, Habari Leo na Spoti leo, Zena Chande ‘Zen C’, ni miongoni mwa wagombea sita wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Chama cha Soka kwa Wanawake Tanzania (TWFA) waliowekewa pingamizi na wadau wa mchezo huo.
 
 
 
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo amesema  ‘mida hii’ kwamba, Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Ombeni Zavala, wagombea wengine ni Joan Minja anayewania nafasi ya Mwenyekiti ambaye amewekwa pingamizi na wadau sita na Isabellah Kapera ambaye anagombea Uenyekiti amewekewa pingamizi moja.
 
Wagombea watatu wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF nao wamewekewa pingamizi akiwemo Zen C, aliyewekewa pingamizi nne, wengine ni Julliet Mndeme (pingamizi sita), na Jasmin Soud mwenye pingamizi tatu, wakati Rahim Maguza anayewania ujumbe wa Kamati ya Utendaji amewekewa pingamizi moja.
 
Wambura amesema pamoja na pingamizi hizo, wagombea wote wanatakiwa kuhudhuria usaili wakiwa na vyeti vyao halisi vya kitaaluma utakaofanyika Oktoba 12, 13 na 14 mwaka huu kwenye ofisi za TFF zilizopo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi.

MANJI AENDA MWENYEWE MWANZA KUICHEZA MECHI YA TOTO

Manji


MWENYEKITI wa Yanga, Yussuf Mehboob Manji anakwenda Mwanza kuongeza morali ya wachezaji kwa ajili ya mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kesho.
 
 
Habari kutoka ndani ya Yanga, ambazo  nimezipata  imezipata zimesema kwamba Manji ameamua kwenda mwenyewe Mwanza, kufuatia timu kupoteza mechi ya Bukoba juzi mbele ya wenyeji Kagera Sugar kwa kufungwa 1-0.
 
“Mwenyekiti anakwenda Mwanza, ili kwenda kuongeza morali ya wachezaji, timu iweze kushinda mechi ya kesho,”kimesema chanzo chetu kutoka Yanga ‘mida hii’.
 
 
Baada ya kufungwa na Kagera, Yanga wamedai wamegundua Simba SC ‘wanatia mkono’ kwenye mechi zao na ndio maana zinakuwa ngumu, ila kuanzia sasa na wao wanaanza ‘fitina’.
 
 
“Simba ilituma watu Bukoba watie mkono mechi yetu, sisi tuliwashitukia hao watu baadaye sana, lakini tunashangaa kwa nini wanafanya hivi, wakati sisi tulizungumza nao tukakubaliana haya mambo tuyaache, tucheze mpira, sasa wao wanatuzunguka wanaendeleza mchezo mchafu,”alisema kiongozi Mjumbe mmoja wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, ambaye hakutaka kutajwa jina.
 
 
Mjumbe huyo alisema kwamba wao walijua baada ya makubaliano na Simba kutofanyiana fitina, waliamini mambo hayo hayatakuwapo, lakini baada ya kugundua wenzao wamewageuka sasa na wao wanaanza ‘mchezo huo’.
 
 
“Na sisi sasa tunaanza kuzicheza mechi zao, wakumbuke tu wao ndio walichokoza nyuki, sasa subirini kuanzia mechi yao na Coastal, wakishinda wao wanaume, na pamoja na kuzicheza mechi zao, tunajizatiti katika mechi zetu. Uzuri watu wote wanaowatumia tumekwishawajua, ni wale wale waliokuja Morogoro, na wale wale waliokuja Bukoba. Tumekwishawajua,”alisema Mjumbe huyo.   
 
Bao pekee la Themi Felix katika dakika ya 67, juzi liliwapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
 
Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.
 
Hiyo inakuwa mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo Simba SC.
 
Aidha, hiyo ilikuwa ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.  
 
Kwa ujumla Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa, ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na jana imechapwa 1-0 na Kagera Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini Mwanza.
 
Katika mechi hiyo ya juzi, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete.
 
Tangu ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati ya hayo kwa penalti.  

WALIMBWENDE MISS WAMTEMBELEA LOWASSA NYUMBANI MONDULI

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa na Mkewe Mama Regina Lowassa wakiwa kenye picha ya pamoja na Warembo wanaowania Taji la Miss Tanzania 2012 pamoja na Viongozi wa Kamati ya Miss Tanzania.

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akisalimia na Msimamizi (Matron) wa warembo wa Miss Tanzania 2012, Irene Karugaba wakati warembo hao walipotembelea Nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Monduli.

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa akizungumza na Warembo wanaowania Taji la Miss Tanzania 2012 waliofika nyumbani kwake Monduli leo na kupata wasaa kwa kuzungumza nae mambo mawili matatu juu ya mafanikio ya Mashindano hayo na Maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla.

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa akizungumza na Warembo wanaowania Taji la Miss Tanzania 2012 waliofika nyumbani kwake Monduli leo na kupata wasaa kwa kuzungumza nae mambo mawili matatu juu ya mafanikio ya Mashindano hayo na Maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla.

AZIM DEWJI AMFICHUA MBAYA WA YANGA

Azim Dewji


MFANYABIASHARA maarufu nchini na mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji amesema baadhi ya wanahabari nchini wanachangia matokeo mabaya ya Yanga katika michuano ya mwaka huu ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Amesema wamekuwa wakiingiza zaidi ushabiki, badala ya kuisaidia timu hivyo kuwafanya wachezaji kulewa sifa mapema hata pasipostahili, hali inayozifanya klabu nyingine kucheza kwa kukamia kwa hofu ya kubebesha kapu la magoli.
 
Dewji aliyasema hayo jana, alipokuwa anazungumzia kupepesuka kwa Yanga, licha ya kufanya usajili tishio msimu huu.
 
Katika mechi sita za ligi msimu huu, Yanga imeshapoteza mechi mbili, imetoka sare mara mbili na kushinda mara mbili, hivyo kuifanya kufikisha pointi nane ambazo ni nusu ya pointi zilizokusanywa na watani wao Simba wanaoongoza ligi baada ya kukusanya pointi 16 kutokana na mechi sita pia.
 
Akiichambua Yanga, alisema imesajili vizuri, lakini waandishi wa habari wamechangia kuwavimbisha vichwa wachezaji kwa kuupamba mno usajili wao, ilhali ni wachezaji wa kawaida.
 
“Kama mwanamichezo, sioni tatizo kwa timu wala benchi la ufundi, nadhani waandishi wanaoishabikia Yanga wanaimaliza timu yao bila kujijua. 
 
Wanaikuza mno kuanzia kipindi cha usajili..kila anayesajiliwa anapambwa kupita maelezo.
 
“Matokeo yao wanavimba vichwa, mashabiki wanajazwa matumaini makubwa, na timu pinzani, hata kama ni ndogo zinakamia zikihofia kugeuzwa kapu la magoli na hii timu inayotajwa kuwa tishio kabisa, wakati ukweli sivyo…” anasema.
 
Aliongeza kusema: “Nashukuru Simba tulifungwa na Azam 3-1 katika Kagame. Ile ilitushitua, tukatuliza akili na ndiyo maana unaona timu imesukwa upya na iko imara. 
 
Tungetwaa ubingwa hakika Simba hii ingekuwa nyeupe, tungelewa sifa tu. Soka haiko hivyo, kwa hiyo waandishi wasiegemee ushabiki pekee, wazisaidie timu zao pia.”
 
 
Dewji alisisitiza kuwa, pamoja na nia ya kufanya biashara, vyombo vya habari vinapaswa kusimama katika ukweli, badala ya kusifia kila kinachoonekana, huku mambo yasiyofaa yakifunikwa kwa hofu ya kuwakera wahusika.
 
 
“Haya yanayotokea katika soka, hasa Simba na Yanga hayana tofauti na jinsi waandishi wanavyojaribu kukuza kila kitu cha Chadema, kiasi cha kujiona wamefika juu mno kisiasa, sikatai ni chama chenye wafuasi wengi, lakini washauriwe jinsi ya kujipanga hatua kwa hatua kuliko
kuwajaza matumaini na matokeo yake utakuta kila kinachofanyika, wanajiona wanaonewa…waandishi wawe washauri wazuri jamani,” alisema Dewji.

MIYEYUSHO MBABE WA MBWANA MATUMLA ULINGONI DESEMBA 9

Bondia Fransic Miyayusho kushoto akisaini mkataba wa kucheza na bondia Nasibu Ramadhani wa pili kulia wanaoshudia kulia ni wakili wa promota Nyasebwa Berious na Mohamed Bawazir. Mara ya mwisho Miyeyusho alipopanda ulingoni, alimpiga Mbwana Matumla na kuweka rekodi ya kuwa bondia wa kwanza kumdondosha kigogo huyo.   

Promota  wa mchezo wa masumbwi Mohamed Bawazir katikati akiwainua mikono juu bondia Fransic Miyayusho kushoto na Nassibu Ramadhani wakati wa kutambulisha mpambano wao utakaofanyika katika ukumbi wa PTA Sabasaba, Desemba 9, mwaka huu.



Mabondia Fransic Miyayusho kushoto akitunishiana misuri na Nassibu Ramadhani wakati wa kutambulisha mpambano wao wa ubingwa utakaofanyika Desemba 9, mwaka huu.

PAMBANO LA UZITO WA BANTAM (KILO 53.5)LA UBINGWA WA INTERCONTINETAL UNAOTAMBULIWA NA WORLD BOXING FORUM (WB-FORUM) NA KUSIMAMIWA NA PST CHINI YA EMMANUEL MLUNDA. 

SIMBA WAENDA TANGA MCHANA HUU BILA NYOTA WATANOI KUIVAA COASTAL UNION

Basi la Simba safari ya kwanza Tanga


SIMBA SC inaondoka kwa basi lake mchana huu kwenda Tanga, tayari kwa mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
 
 
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amewaambia Waandishi wa Habari mchana huu kwamba, katika safari hiyo timu hiyo itawakosa nyota watano, Emanuel Okwi ambaye amekwenda kujiunga na timu yake ya taifa, Uganda, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ anayesumbuliwa na Malaria, Haruna Shamte, Hamadi Waziri na Komabil Keita ambao ni majeruhi.
 
 
Kamwaga alisema kwamba Mrisho Ngassa aliyekuwa anaumwa Malaria amepona na yumo kwenye msafara wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu unaokwenda Tanga kwa basi jipya la kisasa, walilopewa na wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
 
 
Katika kujiandaa na mechi ya Tanga, Simba jana ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
 
 
Mabao ya Simba leo yalifungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
 
 
Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
 
 
Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.      
 

Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.

SIMBA SC YAITANDIKA AZAM 3-2 LEO CHAMAZI

Akuffo amefunga leo


SIMBA SC imeifunga Azam FC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika leo asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
 
Mabao ya Simba leo yamefungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
 
 
Hii inakuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
 

Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.