Tuesday, November 13, 2012

mtangazaji wa clauds fm mbwiga mbwiguke msikilize alichokisema.

LEO NAKULETEA Vimbwanga na rekodi za Kombe la Dunia toka mwaka 1962

BAO la mapema zaidi kufungwa katika fainali za Kombe la Dunia ni lile la Vaclav Masek wa Czechoslovakia, ambalo alilifunga sekunde la 16 wakati timu hiyo ilipomenyana na Mexico mwaka 1962.
Pia bao la Asamoah Gyan wa Ghana katika fainali za mwaka 2006 nchini Ujerumani dhidi ya Czech la sekunde 68 ndilo linalofuatia.

Bao lililochukua dakika nyingi ni lile lililofungwa na David Pllatt wa England. Alifunga bao hilo dakika ya 119 wakati timu hiyo ilipomenyana na Ubelgiji katika fainali za mwaka 1990.

Mabao mengi yaliyofungwa haraka na kwa muda mfupi ni yale ya mwaka 1982. Mabao hayo yalifungwa na Laszlo Kiss wa Hungary. Alifunga mabao hayo dakika ya 70, 74 na 77.

Mchezaji mwenye umri mkubwa kufunga bao katika fainali za michuano hiyo ni Roger Milla wa Cameroon. Alifunga bao hilo katika fainali za mwaka 1994 dhidi ya Russia akiwa na umri wa miaka 42 na siku 39.

Mchezaji pekee aliyefunga bao na kujifunga katika mechi moja ni Ernie Brandts wa Uholanzi. Alijifunga na baadaye kufunga bao wakati Uholanzi ilipomenyana na Italia mwaka 1978. Katika mechi hiyo, Uholanzi iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Goli la kwanza la kujifunga lilikuwa la Ramon Gonzalez wa Paraguay katika fainali za mwaka 1930. Alijifunga bao hilo wakati Paraguay ilipochapwa mabao 3-0 na Marekani.

Mchezaji aliyezifungia mabao nchi mbili tofauti katika fainali za kombe hilo ni Robert Prosineck. Aliichezea Yugoslavia mwaka 1990 na kuipachikia bao dhidi ya Falme za Kiarabu. Pia aliichezea Croatia katika fainali za mwaka 1998 na kuifungia bao dhidi ya Jamaica.

Wachezaji waliofunga mabao katika fainali mbili tofauti za kombe hilo ni Vava wa Brazil (1958 na 1962), Pele wa Brazil (1958 na 1970) na Paul Breitner wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi (1974-1982).

Mchezaji mwenye umri mdogo kufunga bao katika fainali hizo alikuwa Pele wa Brazil. Alifunga bao hilo katika fainali za mwaka 1958 timu hiyo ilipomenyana na Wales, akiwa na umri wa miaka 17.

Mchezaji aliyefunga bao katika kila mechi alizocheza katika fainali hizo ni Jairzinho wa Brazil mwaka 1970 na Alcide Ghiggia wa Uruguay mwaka 1950.

Mchezaji mdogo kuonyeshwa kadi nyekundu ni Rigobert Song, aliyepewa kwenye fainali za 1994 nchini Marekani akiwa na miaka 17 na siku 358.

Je Wajua?

Miji 23 imewahi kutumika mara mbili kwa fainali za Kombe la Dunia. Miji hiyo ni Berlin, Dortmund, Frankfurt, Gelsenkirchen, Hamburg, Hanover, Munich, Stuttgart na miji mingine minane katika nchi za Mexico na Ufaransa na miji saba ya Italia.

Miji saba iliyoandaa fainali za mwaka 1974 pia ilitumika tena katika fainali za mwaka 2006 zilizofanyika Ujerumani. Mji pekee ulioachwa ni Dusseldorf. Miji mipya ilikuwa Cologne, Kaiserslautern, Leipzig na Nuremberg.

Kombe la mwanzo la dunia lililoitwa Jules Rimet, lilizawadiwa moja kwa moja kwa Brazil mwaka 1970 baada ya kushinda fainali hizo mara tatu. Kombe hilo lililotengenezwa kwa madini ya dhahabu, liliibwa nchini humo na kuyeyushwa.

Kombe la pili liliibwa mwaka 1966 nchini England, lakini liligunduliwa baadaye likiwa limefukiwa ardhini chini ya mti. Aliyeligundua alikuwa mbwa mdogo aliyejulikana kwa jina la Pickles.

Licha ya kuwa majirani, vyama vya soka vya Argentina na Uruguay vilikuwa vikitumia mipira tofauti na kusababisha ubishani mkali katika mechi ya fainali kati ya timu hizo mwaka 1930 kuhusu mpira upi utumike. Mwamuzi Jean Langenus kutoka Ubelgiji aliamua mpira mwepesi wa Argentina utumike kipindi cha kwanza na mpira mzito wa Uruguay utumike kipindi cha pili.

Nchi zilizofuzu kucheza mara nyingi mechi ya fainali ya Kombe la Dunia ni Brazil, Ujerumani, Italia na Argentina. Brazil imemcheza fainali mara saba na kushinda mara tano. Ujerumani imecheza fainali mara saba na kushinda mara tatu. Italia imecheza fainali mara tano na kushinda mara nne. Argentina imecheza fainali mara tatu na kushinda mara mbili.

Brazil ndiyo nchi pekee iliyofuzu kucheza fainali zote 19 za kombe la dunia, ikifuatiwa na Italia na Ujerumani, zilizofuzu kucheza fainali 17 na Argentina iliyofuzu kucheza fainali 15.

Haijawahi kutokea kwa bingwa mtetezi kufanya vibaya katika fainali za kombe la dunia kama ilivyokuwa kwa Ufaransa mwaka 2002 na Italia fainali za mwaka huu zilizofanyika nchini Afrika Kusini. Si tu kwamba ilishindwa kuvuka raundi ya kwanza, bali pia hazikushinda hata mechi moja.

Wachezaji waliocheza mechi nyingi za fainali za Kombe la Dunia ni kipa Antonio carbajal wa Mexico (1950-66) na Lothar Matthaus wa Ujerumani (1982-98). Wachezaji hao walicheza fainali tano za kombe la dunia kila mmoja.

Norman Whiteside wa Ireland Kaskazini alikuwa mchezaji wa kwanza mwenye umri mdogo kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 1982. Alicheza fainali hizo akiwa na umri wa miaka 17 na siku 41 wakati timu hiyo ilipomenyana na Yugoslavia.

Wanasoka wawili waliweka rekodi ya kutwaa Kombe la Dunia wakiwa wachezaji na makocha. Mario Zagallo wa Brazil alitwaa kombe la dunia akiwa mchezaji mwaka 1958 na 1962 na pia akiwa kocha 1970. Franz Beckenbauer wa Ujerumani alitwaa kombe hilo akiwa mchezaji mwaka 1974 na akiwa kocha 1990.

Oliver Kahn wa Ujerumani alikuwa kipa wa kwanza kupewa tuzo ya ya mpira wa dhahabu akiwa mchezaji katika fainali za mwaka 2002 zilizofanyika Japan na Korea Kusini.

Pele wa Brazil ni mchezaji pekee aliyecheza fainali tatu za kombe hilo na nchi hiyo kutwaa ubingwa. Alicheza fainali za mwaka 1958, 1962 na 1970. Hakucheza fainali za mwaka 1966 kutokana na kuwa majeruhi. Cafu wa Brazil pia alicheza fainali tatu mfululizo za mwaka 1994, 1998 na 2002.

Wachezaji wanne tu ndio waliocheza fainali nne tofauti za Kombe la Dunia nao ni Diego Maradona, Rigobert Song, Cafu na Paolo Maldini.

Bora Milutinovic wa Serbia ndiye kocha pekee aliyeziongoza nchi tano katika fainali tano tofauti za kombe la dunia kati ya mwaka 1986 hadi 2002. Alizifundisha nchi za Mexico, Costa Rica, Marekani, Nigeria na China.

Carlos Alberto Parreira wa Brazil ameziongoza nchi tanoe katika fainali tano tofauti za kombe hilo. Nchi hizo ni Brazil, Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu, Kuwait na Afrika Kusini.

Makocha watano waliziwezesha nchi zao kucheza fainali za kombe hilo mara mbili. Makocha hao ni Pozzo wa Italia (1934 na 1938), Schon wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi (1966-1970), Zagallo wa Brazil (1970-1998), Beckenabauer wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi (1986-1990) na Bilardo wa Argentina (1986-1990).

Mechi 16 ziliamuliwa kwa penalti kuanzia mwaka 1982 wakati Ujerumani ilipoishinda Ufaransa katika mechi ya nusu fainali. Mechi maarufu ilikuwa ya fainali ya mwaka 1994wakati Brazil ilipoichapa Italia kwa penalti 3-2 baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa suluhu. Italia pia ilifungwa mara mbili kwa njia ya penalti na Argentina na Ufaransa katika fainali za 1990 na 1998.

Wajua kuwa Uholanzi ndio tiumu pekee kali duniani ambayo haijawahi kutwaa taji la Kombe la Dunia, licha ya kuingia fainali mara mbili mwaka 1974 na 1978 na jana ilifuzu kwa mara ya tatu na tunasubiri kuona itafanya nini tena siku ya Jumapili huko Afrika Kusini.

BALOZI WA HENNESSY AFUNGUKA DAR

Balozi wa kampuni ya Hennessy, Cyrile Auriol akizungumza na Waandishi wa Habari asubuhi ya leo katika ukumbi wa Kivukoni, ndani ya hoteli ya Serena, Dar es Salaam. Balozi Auriol alitua Dar es Salaam jana akitokea Paris, Ufaransa na atakuwa nchini kwa ziara ya siku tatu kabla ya kuelekea Nairobi kwa muendelezo wa ziara yake nchi za Afrika Mashariki. Akiwa Dar es Salaam Balozi Auriol atahudhuria matukio mbalimbali, maalum ya chakula cha jioni na uonjaji wa kinywaji hicho ambazo, zimeandaliwa ili kuwazawadia watumiaji wa kinywaji hicho nchini ambao sasa wanafurahia kampeni ya kinywaji hicho iitwayo ‘ Flaunt Your Taste’.

Balozi akizungumza

Meneja Masoko wa Hennessy, Omar Salisburry

Balozi wa Hennessy akiwa maofisa wenzake

BAHANUZI, CANNAVARO 'WATEREMSHWA' KWENYE NDEGE WAKIMFUATA DROGBA CHINA

Bahanuzi

WACHEZAJI wawili wa Yanga, beki Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ na mshambuliaji Said Rashid Bahanuzi waliotarajiwa kuondoka leo saa 10:00 jioni kwa ndege ya Qatar Airways kwenda China, kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa, wamezuiwa na klabua yao hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb  amesema  mida hii kwamba, sababu za kuzuiwa kwa wachezaji hao ni kutokana na klabu inayowataka kutofuata taratibu.
“Hawajatuma barua, hawa wanataka kwenda kienyeji tu, na sisi si kama tumewazuia, tumeitaka kwanza hiyo klabu ifuate taratibu kwa kutuma barua huku na kujitambulisha, ili hata hao wachezaji wakipata matatizo tujue tunaanzia wapi,”alisema Bin aKleb.
Mapema leo, Cannavaro, Nahodha Msaidizi wa Yanga alisema  kwamba wanakwenda China kwa wiki mbili na baada ya majaribio kama wakifuzu, klabu inayowataka itafanya mazungumzo na klabu yao.
“Sisi wote tuna mikataba na klabu, hivyo tukifuzu jamaa itabidi watuhamishe Yanga,”alisema  beki huyo kati aliyezaliwa Februari 10, mwaka 1982.
Cannavaro yupo Yanga tangu mwaka 2006, aliposajiliwa kutoka Malindi ya Zanzibar wakati Bahanuzi amesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Mwaka 2009, Cannavaro alichukuliwa kwa mkopo na klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada na baada ya miezi sita alirejeshwa Yanga alikoendelea kucheza hadi leo anakwenda kujaribu bahati yake China.
Bahanuzi ameingia na zali la aina yake Yanga SC, kwani katika mashindano ya kwanza kuichezea klabu hiyo alifanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame.
Hadi sasa, Said Bahanuzi   maarufu kama Spider Man, ameifungia Yanga mabao 12 katika mechi 14, yakiwemo matatau ya penalti tangu ajiunge na timu hiyo Julai mwaka huu.
Kwa sasa China ni nchi ambayo mastaa wengi waliokuwa Ulaya wanakwenda kumalizia soka yao, mfano washambuliaji wawili wa zamani wa Cheslea, Didier Drogba na Nicolas Anelka waliopo Shenghua Shanghai. Anelka ni kocha mchezaji.

STARS YAPANGWA NA KAVUMBANGU CHELLENGE

Stars
MICHUANO ya mwaka huu ya CECAFA Tusker Senior Challenge itafanyika nchini Uganda kuanzia Novemba 24 hadi Desemba 8 na Tanzania Bara imepangwa kundi moja, B na timu ya mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbangu, Burundi.
KUNDI A: Uganda, Kenya, Ethiopia and South Sudan
KUNDI B: Tanzania, Sudan, Burundi and Somalia
KUNDI C: Malawi, Eritrea, Rwanda and Zanzibar
ZINGATIA: Timu mbili za juu kutoka kila kundi zitafuzu Robo fainali kwa pamoja na washindi watatu bora wawili kutoka makundi yote.
KUNDI A RATIBA:
24 Novemba: Ethiopia v Sudan (Saa 9:00); Uganda v Kenya (Saa 12:00)
27 Novemba: Sudan Kusini v Kenya (Saa 9:00); Uganda v Ethiopia (Saa 12:00)
30 Novemba: Kenya v Ethiopia (Saa 9:00); Sudan Kusini v Uganda (Saa 12:00)
KUNDI B RATIBA:
25 Novemba: Burundi v Somalia (Saa 9:00); Tanzania v Sudan (Saa 12:00)
28 Novemba: Somalia v Sudan (Saa 9:00); Tanzania v Burundi (Saa 12:00)
1 Desemba: Sudan v Burundi (Saa 9:00); Somalia v Tanzania (Saa 12:00)
KUNDI C RATIBA:
26 Novemba: Zanzibar v Eritrea (Saa 9:00); Rwanda v Malawi (Saa 12:00)
29 Novemba: Malawi v Eritrea (Saa 9:00); Rwanda v Zanzibar (Saa 12:00)
1 Desemba: Malawi v Zanzibar (Saa 9:00); Eritrea v Rwanda (Saa 12:00)
ROBO FAINALI:
3 Desemba (Saa 10:00): Mshindi Kundi C vs Mshindi wa pili kundi B
3 Desemba (Saa 1:00): Mshindi Kundi A vs Mshindi wa tatu Bora wa pili
4 Desemba (Saa 10:00): Mshindi Kundi B vs Mshindi wa tatu bora wa kwanza
4 Desemba (Saa 1:00): Mshindi wa pili Kundi A vs Mshindi wa pili Kundi C
NUSU FAINALI
Desemba 6
Saa 10:00 (Nusu Fainali ya kwanza
Saa 1:00 (Nusu Fainali ya pili)
KUTAFUTA MSHINDI WA TATU:
Desemba 8 (Saa 10:00)
FAINALI: Desemba 8 (Saa 1:00)

BAHANUZI, CANNAVARO WAMFUATA DROGBA CHINA

Cannavaro

WACHEZAJI wawili wa Yanga, beki Nadir Haroub  Ally ‘Cannavaro’ na mshambuliaji Said Rashid Bahanuzi wanaondoka leo saa 10:00 jioni kwa ndege ya Qatar Airways kwenda China, kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa.
Cannavaro, Nahodha Msaidizi wa Yanga amesema  kwamba watakuwa huko kwa wiki mbili na baada ya majaribio kama wakifuzu, klabu inayowataka itafanya mazungumzo na klabu yao.
“Sisi wote tuna mikataba na klabu, hivyo tukifuzu jamaa itabidi watuhamishe Yanga,”alisema  beki huyo kati aliyezaliwa Februari 10, mwaka 1982.
Cannavaro yupo Yanga tangu mwaka 2006, aliposajiliwa kutoka Malindi ya Zanzibar wakati Bahanuzi amesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Mwaka 2009, Cannavaro alichukuliwa kwa mkopo na klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada na baada ya miezi sita alirejeshwa Yanga alikoendelea kucheza hadi leo anakwenda kujaribu bahati yake China.
Bahanuzi ameingia na zali la aina yake Yanga SC, kwani katika mashindano ya kwanza kuichezea klabu hiyo alifanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame.
Hadi sasa, Said Bahanuzi   maarufu kama Spider Man, ameifungia Yanga mabao 12 katika mechi 14, yakiwemo matatau ya penalti tangu ajiunge na timu hiyo Julai mwaka huu.
Kwa sasa China ni nchi ambayo mastaa wengi waliokuwa Ulaya wanakwenda kumalizia soka yao, mfano washambuliaji wawili wa zamani wa Cheslea, Didier Drogba na Nicolas Anelka waliopo Shenghua Shanghai. Anelka ni kocha mchezaji.
Said Bahanuzi
   

MWIMBAJI MELODY AFARIKI DUNIA

MWIMBAJI nyota wa miondoko ya Taarab, Mariam Khamis “Paka Mapepe” amefariki alfajiri ya leo katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili.
Mariam Khamis ambaye hadi anafariki alikuwa ni mwajiriwa wa TOT Taarab alipelekwa Muhimbili kwa ajili ya uzazi na inasemekana mtoto ametoka salama lakini yeye Mungu amempenda zaidii.
Mtu wa karibu sana na mwimbaji huyo, Thabit Abdul ameithibitishiawww.saluti5.com kuwa ni kweli Mariam Khamis amefariki dunia.
Aidha mwimbaji Isha Ramadhan “Mashauzi” naye akiongea na saluti5 kutoka Muhimbili nae alithibitisha kutokea kwa kifo hicho “Ni kweli Mariam amefariki na hivi tunavyoongea tayari tupo hapa Muhimbili” Alisema Isha.
Mariam Khamis alitamba sana na wimbo wa Mapaka Mapepe alouimba akiwa na Melody, kabla ya kujiunga na Zanzibar Stars, Five Stars na hatimae TOT.
Wimbo wake wa kwanza kurekodi na TOT ni Sidhuriki na lawama ambao unatamba sana hadi leo hii

WAGENI LIGI KUU, NANI WA UKWELI NANI FEKI?

Didier Kavumbangu wa Yanga aliyeruka kama mkizi kushoto, mchezaji wa kigeni aliyeoongoza kwa mabao Ligi Kuu Bara baada ya mzunguko wa kwanza


KAMA ilivyo nchi nyingi duniani, Tanzania pia katika Ligi Kuu yake kuna wachezaji wa kigeni na haijaanza leo, bali tangu miaka ya 1970, ingawa katika siku za karibuni, idadi ya wageni imekuwa ikiongezeka katika ligi hiyo. Awali, mgeni alipatikana katika klabu mbili kongwe pekee, Simba na Yanga lakini sasa hata klabu nyingine za mikoani pia nazo zina wachezaji wa kigeni. Lakini vipi kuhusu michango yao katika klabu zao na mustakabali wao mzima baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo? TANOJUMA IN SPORTS  inakupa jibu. Endelea.
Yaw Berko
YAW BERKO (Yanga SC, Ghana):
Kuna dalili za kutosha huu ukawa msimu wake wa mwisho Yanga, kutokana na uhusuiano wake na viongozi wa klabu hiyo kuzidi kuharibika. Yaw Berko pamoja na umahiri wake langoni, kipa huyu kutoka Ghana anadaiwa anaringa na pia anatuhumiwa wakati mwingine eti anahujumu timu. Msimu uliopita aliletewa Shaaban Kado lakini akashindwa kumuondoa langoni, ila msimu huu Ally Mustafa ‘Barthez’ anaonekana kufanya vizuri, hivyo kumtengenezea Berko mazingira ya kupewa mkono wa kwaheri Yanga. Amecheza mechi kadhaa za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwemo dhidi ya watani wa jadi, Simba, lakini Barthez amecheza zaidi.
Felix Sunzu
FELIX SUNZU (Simba SC, Zambia):
Ameendelea kuwa mshambuliaji tegemeo katika klabu ya Simba, licha ya kusajiliwa kwa washambuliaji wapya akina Daniel Akuffo kutoka Ghana na Abdallah Juma. Mchezaji huyu mrefu kutoka Zambia ambaye ndiye analipwa mshahara mkubwa zaidi Tanzania, Sh. Milioni 5, amekuwa akiisaidia mno timu yake kutokana na kucheza kwa kujituma hata kwenye mechi ngumu. Kwa kiwango chake katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Sunzu bado anastahili kuendelea kupiga kazi Simba na hata mshahara wake anaolipwa anautumikia vizuri.
Kipre Balou
KIPRE BALOU (Azam FC, Ivory Coast):
Msimu huu anafanya kazi, tofauti sana na msimu uliopita ambao ulikuwa wa kwanza kwake nchini. Hadi mzunguko wa kwanza unamalizika, Kipre Michael Balou amekuwa ana wastani mzuri wa kucheza kuanzia chini ya kocha Mserbia, Boris Bunjak na hata kwa Muingereza, Stewart Hall. Baada ya Azam kuwasimamisha wachezaji wake wanne wa safu ya ulinzi, kipa Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris, katika mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza, Balou alicheza beki ya kulia na akafanya kazi yake vizuri tu pamoja na kufungwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mbuyu Twite
MBUYU TWITE (Yanga SC, Rwanda):
Yanga imelamba dume hapa, hakuna shaka kabisa kusema hivyo. Beki huyo wa kimataifa wa Rwanda, aliyesajiliwa kutoka APR ya Rwanda, amecheza vema mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kiasi cha kujikusanyia mashabiki wengi. Amekuwa akitumika kama beki wa pembeni, lakini alionyesha ubora wake zaidi, wakati ambao Kevin Yondan alikuwa anaumwa naye akaanza kutumika kama beki wa kati. Na katika mechi hizo, ambazo Yanga ilicheza bila Yondan, Twite akicheza katikati na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, uimara wa ukuta wa timu hiyo ulioneikana kuongezeka. Twite mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni kifaa na si katika ulinzi tu, bali ameweza pia kufunga mabao matatu hadi mwisho wa mzunguko wa kwanza.










EMANUEL OKWI (Simba SC, Uganda):
Emanuel Okwi
Hii mashine, acha masikhara. Mganda huyu ambaye amemaliza mkataba na Simba SC na hivi sasa yupo katika majadiliano ya kuongeza mkataba, ameendelea kufanya kazi yake vizuri. Akitumiwa kama mshambuliaji wa pembeni, Okwi ameendelea kutengeneza nafasi na kufunga yeye mwenyewe pia. Amefunga mabao ya kusisimua katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, mfano lile lililokuwa la tatu katika mechi dhidi ya Azam. Ni mchezaji ambaye Simba ikishindwa kumshawishi kuongeza mkataba na akaenda kwa hasimu yeyote, Simba watakuwa wamefanya kosa kama ambalo Arsene Wenger alifanya Arsenal, kwa kumruhusu Robin Van Persie aende Manchester United. Watajilaumu.
Joseph Owino
JOSEPH OWINO (Azam FC, Uganda):
Mustakabali wake sasa haujulikani katika klabu ya Azam, baada ya kujikuta anaendelea kukaa benchi kwa makocha wote waliofundisha timu hiyo hadi mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu. Hakuwa mwenye umuhimu mbele ya Boris Bunjak na watu wakadhani Msrebia huyo alikuwa anakosea, lakini mbele ya Muingereza, Stewart Hall mambo ndiyo yamezidi kuwa magumu kwa beki huyu wa zamani wa Simba SC. Fikiria, baada ya Azam kuwasimamisha wachezaji wake wanne wa safu ya ulinzi, kipa Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris, katika mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza, mshambuliaji Kipre Balou alichezeshwa beki ya kulia wakati Owino yupo na angeweza kucheza katikati, Samir Hajji  Nuhu akacheza pembeni. Nini kinafuata kwa Owino Azam?



HARUNA NIYONZIMA (Yanga SC, Rwanda):
Haruna Niyonzima
Mwanasoka bora zamani Afrika, Abedi Ayew Pele kutoka Ghana amemvulia kofia kiungo huyu wa Rwanda na kushangaa anafanya nini Afrika. Pele alimuona Haruna katika dakika 90 tu za mechi moja dhidi ya Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Nomvemba 4, mwaka huu Yanga ikishinda 2-0.  Hicho ni kielelezo tosha kwamba Haruna ni mchezaji bora na Yanga ina kila sababu ya kujivunia kikungo huyu, ambaye anaingia msimu wa pili katika klabu hiyo tangu asajiliwe kutoka APR ya Rwanda. Yanga wana bahati sana kuwa na mchezaji huyu, ambaye amewahi kufanya majaribio na kufuzu Ujerumani, lakini mizengwe ya klabu yake ya zamani, APR ikamkwamisha kucheza huko.
Paschal Ochieng
PASCHAL OCHIENG (Simba SC, Kenya):
Beki huyu wa zamani wa Yanga, hadi sasa mambo hayamuendei vizuri Simba SC na lolote linaweza kutokea juu yake kuelekea mzunguko wa pili. Anaweza akarudi, au asirudi. Aseme na Mungu wake, maana kwa hali iliyopo Simba, hawana muda wa kumvumilia mchezaji na hilo ndilo linalomnyima usingizi beki huyu Mkenya kwa sasa. Amekuja Simba wakati mbaya, unaweza kusema hivyo, lakini Ochieng si beki mbaya akama angeikuta timu hiyo imetulia. Ushahidi wa hilo, Juma Said Nyosso naye msimu huu ameonekana anafaa kuchezea Simba B, sasa utasemaje kwa Ochieng?

























Kipre Tcheche
KIPRE TCHECHE (Azam FC, Ivory Coast):
Kijana safari hii ameonyesha yeye ni nani, hadi mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu unafikia tamati yeye ndiye mfungaji bora wa mabao wa Azam, akipokea nafasi ya John Bocco ‘Adebayor’, ambaye maumivu yamempunguza kasi msimu huu. Kama kuna kitu Kipre Herman Tcheche alikuwa anajifunza msimu uliopita, basi ameweza na msimu huu anatenda inavyotakiwa. Kama Azam walikuwa wana wasiwasi na uwezo wake, bila shaka mechi 13 za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu zimewapa jibu, kwamba hawakukosea kumsajili mchezaji huyu kutoka Ivory Coast. 



Hamisi Kiiza
HAMISI KIIZA (Yanga SC, Uganda):
Aliuanza vibaya msimu huu na hiyo ilitokana na ubinafsi uliotaka kuanza kuitafuna Yanga, kabla ya viongozi kuushitukia na kupambana nao. Kiiza alikuwa kama anatengwa na wenzake, hapewi pasi hata akiwa anatazama na nyavu. Uongozi ukaligundua hilo na ukawakaripia wachezaji mno, hatimaye baada ya hapo, ufedhuli huo ukatoweka na Yanga ikawa kitu kimoja, dhamira moja na hapo ndipo Hamisi Kiiza alipowaonyesha wana Yanga ni kwa sababu gani Uganda walimuita Diego Milito. Alifunga mabao katika mechi mbili muhimu za ukingoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, dhidi ya Azam na dhidi ya Coastal na baada ya hapo amerejesha heshima.   
Komabil Keita
KOMANBIL KEITA (Simba SC, Mali):
Amecheza mechi moja tu ya mwisho, dhidi ya Toto African katika Ligi Kuu tangu alipocheza siku Simba ikitandikwa 3-0 na Sofapaka ya Kenya katika mchezo wa kirafiki. Ukitazama uchezaji wake katika mechi hiyo, akicheza pamoja na Shomari Kapombe haukuwa mbaya, ila tu wachezaji wa uwezo kama wa kwake ni wengi tu hapa nchini. Obadia Mungusa anaweza kuwa bora kuliko Keita. Huwezi kuiona tofauti ya Victor Costa na Keita. Kwa kweli mustabali wa mchezaji huyu kutoka Mali ndani ya Simba  ni mgumu, ana asilimia kubwa ya kutorudi mzunguko wa pili. 
Ibrahim Shikanda
IBRAHIM SHIKANDA (Azam FC, Kenya):
Ameendelea kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Azam mbele ya makocha wote, Boris Bunjak aliyeondolewa na hata Muingereza Stewart Hall aliyerejeshwa kurithi mikoba ya Mserbia huyo. Ingawa Tanzania hivi sasa hatuna tatizo sana na mabeki wa pembeni, lakini kwa sababu Mkenya huyu amekuwa mchezaji wa Azam kwa takriban misimu mitatu sasa, si vibaya akiendelea na maisha katika klabu hiyo. Ni mzuri, lakini wapo wazalendo wazuri kama au kuliko yeye, na hata Azam wakiamua kuachana naye iwapo watapata mbadala wake wa uhakika, haitashangaza.
Didier Kavumbangu
DIDIER KAVUMBANGU (Yanga SC, Burundi):
Yanga msimu huu wanastahili pongezi katika uundaji wa timu yao kwa ujumla, nadhani wamejifunza kutokana na madudu ambayo wamekuwa wakiyafanya miaka ya karibuni. Hapana shaka huyu ni mchezaji mwingine wa maana sana ndani ya kikosi cha Yanga katika wachezaji wa kigeni, baada ya Kiiza, Niyonzima na Mbuyu Twite. Jamaa ameonyesha uwezo mkubwa mno katika kuwapa ‘karaha’ mabeki na makipa. Ni mpambanaji. Shujaa. Jasiri. Ana uwezo wa kumiliki mpira, kuuficha, kasi na kwa ujumla unaweza kusema Kavu anajua. Amemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, akiwa anaongoza kwa mabao na wengi wamemkubali.  
DANIEL AKUFFO (Simba SC, Ghana):
Ana asilimia chache mno za kurejea kwenye kikosi cha Simba Januari, kwani mtu wa kwanza ambaye hamkubali kabisa mshambuliaji huyo kutoka Ghana ni kocha, Profesa Milovan Cirkovick kutoka Serbia. Cirkovick amesema amekwishampa nafasi ya Dani, lakini ameshindwa kudhihirisha uwezo wake na sasa hamtaki tena kwenye kikosi chake. Lakini ingekuwa vema kama Simba wangempa nafasi zaidi mshambuliaji huyo kwa kumrudisha Januari ili acheze kwa miezi mingine mitano ili kuona zaidi juu yake. Labda amechelewa kuendana na mazingira na soka ya Tanzania kwa ujumla. Labda. Labda kweli uwezo wake mdogo, labda!
Suleiman Jingo
MOHAMED SULEIMAN JINGO (Toto Africans, Uganda):
Kwa sababu wengi macho yetu yapo Simba, Yanga na Azam tunashindwa kujua kwamba kuna klabu nyingine zina wachezaji wazuri tu wa kigeni zimesajili, mojawapo ni Toto Africans ya Mwanza, ambayo ina winga mmoja matata kutoka Uganda, anaitwa Mohamed Suleiman Jingo. Jamaa mmoja mfupi, ambaye amesajiliwa kutoka Express ‘Red Eagles’ ya Uganda msimu huu. Kwa Toto, wakiendelea kuishi vizuri na mchezaji huyo, kuna uwezekano mkubwa baadaye wakamuuza Azam, Simba au Yanga kwa bei nzuri tu.
WILLFRED OJODALE AMMEH (Kagera Sugar, Nigeria):
Jina lake kamili ni Wilfred Ojodale Ammeh, mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Abuja Stars ya Nigeria katika klabu ya Kagera Sugar ya Bukoba mkoani Kagera. Mara nyingi huwa anacheza kama mshambuliaji wa pembeni kushoto na amekuwa mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Kagera. Miongoni mwa makocha ambao wana uwezo wa kuwajua wachezaji wazuri nchini, ni Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ wa Kagera, hivyo kitendo cha kumpa namba ya kudumu kwenye kikosi chake Mnigeria huyu, maana yake kweli anajua.
Benjamin Effe
BENJAMIN EFFE OFUYAH (Kagera Sugar, Nigeria):
Bonge la beki, akili, maarifa, mbinu, ufundi, nguvu na kujituma unavipata kwake. Kama Simba wangemuona Effe kabla ya kuwasajili Keita na Ochieng, bila shaka wangepambana na Kagera Sugar kugombea saini ya mchezaji huyu. Lakini bahati mbaya hawakumuona. Wachezaji wa Yanga walimsifia sana beki huyu baada ya mechi yao na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba na baadaye mashabiki wa Dar es Salaam wakajionea uwezo wake, siku timu hiyo ilipomenyana na Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Jamaa alicheza soka nzuri sana na alivutia. Haikushangaza baada ya mechi hiyo, ikaibuka minongo’no kwamba Simba, Yanga na Azam zote zimevutiwa na kijana huyo.








Hannington Kalyesebula
HANNINGTON KALYSEBULA BOSA (Kagera Sugar, Uganda):
Amekuwa kipa wa kwanza wa Kagera Sugar hadi msimu uliopita, lakini mambo yamembadilikia msimu huu amejikuta akisubiri mbele ya Andrew Ntala. Kipa huyu kutoka Uganda, ni mzuri na hata msimu uliopita alipambana na upinzani wa Amani Simba, ingawa baadaye akaushinda, sasa haijulikani kama safari hii Ntala amekuja kumuondoa moja kwa moja, au naye atachemsha kama Amani. Ana nafasi ya kurejea kwenye kikosi cha Kagera Sugar Januari mwakani na hapo ndipo atakapopata fursa ya kujinusuru kutupiwa virago kwa Wakata Miwa hao wa Misenyi.
ENYINNA DARLINGTON ARIWODO (Kagera Sugar, Nigeria):
Ni mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Kagera Sugar ambaye anafunga na kutengeneza nafasi za wenzake kufunga. Mnigeria huyu aliyesajiliwa kutoka Toto Africans msimu huu, ni mzuri na kwa timu anayochezea si vibaya akaendelea kuwapa changamoto wachezaji wazalendo. Ila tu, Obinna anahitaji kuongeza juhudi na si kubweteka, kwani akiwa mchezaji ambaye anaiingiza gharama za ziada kwa klabu, kwamba mbali na mshahara analipiwa kibali cha kufanya kazi pia, anatakiwa afanye kazi kweli.
Da Silva na mkewe na mwanawe
DEANGELIS GABRIEL DA SILVA (Coastal Union, Brazil):
Coastal Union walimsajili kiungo huyu kutoka Nepal, nchi ambayo Mtanzania Castory Mumbara amewahi kucheza. Mchezaji huyo aliomba nafasi ya kusajiliwa Coastal kupitia ukurasa wa Facebook wa timu hiyo. Alituma DVD zake ambazo viongozi walipoziona wakaridhika naye na kumsajili. Hata hivyo alichelewa kuja na alipotua kocha Hemed Morocco akagundua kiungo huyo Mbrazil anahitaji muda zaidi wa mazoezi kabla ya kuanza kucheza, hivyo akampa programu ya kufanya mazoezi na kikosi cha pili cha Wana Mangushi. Tusubiri mzunguko wa pili itakuwaje juu yake.  
Philip Kaira
PHILIP METUSELA MUGENZI (Coastal Union, Uganda):
Amewahi kucheza URA ya Uganda pamoja na Joseph Owino, ni beki mzuri tu na wakati fulani hata Simba na Yanga walimtaka. Lakini ameshindwa kumshawishi kocha hata mmoja wa Coastal Union kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Wagosi wa Kaya. Juma Mgunda akiwa anasaidiwa na Habib Kondo, walikuwa wanampiga mkeka beki huyo Mganda na hata sasa Hemed Morocco akiwa anasaidiwa na Ally Kiddy wanamuweka benchi mchezaji huyo. Nini mustakbali wake ikiwa makocha wote wanaoletwa katika timu hiyo wanamchunia? Tutajua Januari.
OBINNA ONYIEKECHI SALAMASUSA (African Lyon, Nigeria):
Mmiliki wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ anasema Mnigeria huyu ni mchezaji mzuri, lakini hajitambui hivyo anaweza kuachana naye mzunguko wa pili. Inawezakana, kwa sababu kulingana na mikakati mipya ya Lyon, wanataka kufanya usajili wa kufa mtu, ikiwemo wa wachezaji wa kigeni. Katika orodha ya wachezaji wanaowataka, wapo Mbuyu Twite wa Yanga, Emmnauel Okwi na Mrisho Ngassa wa Simba, ambao Zamunda amesema usajili wao kwa pamoja watatu hao wote utagharimu dola 200,000 za Kimarekani. Kwa hivyo unaweza kusema Obinna anachungulia mlango wa kutokea Lon.
HOOD ABDUL SEEWA MAYANJA  

Hood Mayanja
(African Lyon, Uganda):
Huyu jamaa anatekeleza wajibu wake vizuri African Lyon na mabao yake kwa sasa ndiyo ambayo yanaibeba timu hiyo. Kwa kukumbushia tu, mchezaji huyu kutoka Uganda amewahi kufanya majaribio Yanga, chini ya kocha Mserbia, Kostadin Papic, lakini pamoja na kuvutia, idadi ndogo ya kikanuni ya wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ikamsukumia  nje ya kikosi cha Wana Jangwani. Akaenda Mtibwa Sugar ya Morogoro na tangu msimu uliopita yupo African Lyon ambako anaendelea vizuri.

 

 

 

 

 

ASHANTI HAIKAMATIKI LIGI DARAJA LA KWANZA, YAIGARAGAZA VILLA SQUAD KARUME

Mchezaji wa Ashanti akijaribu kumtoka beki wa Villa wakati wa mchezo uliochezwa leo uwanja wa Karume
Wachezaji wa Ashanti wakishangilia bao la pili
Mnanda na mdundiko uliamua kuingia uwanjani baadaa ya mchezo kumalizika, huku golikipa wa Ashanti akishindwa kujizuia akaanza kuyarudi
Mashabiki wakambeba kutokana na kazi yake kubwa aliyoifanya ya kupangua mashuti makali
TIMU ya Ashanti aka watoto wa mjini leo wameichapa bila huruma Villa Squad mabao 2-0 kwenye mchezo wa ligi daraja la kwanza uliochezwa uwanja wa Karume, jijini Dar es salaam.

Ashanti walijipatia bao la kwanza dakika ya nne kupitia kwa Jerome Lembeli bao lililodumu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana lakini Villa watajutia nafasi za wazi tatu ambazo mashuti yalitoka nje kutokana na washambuliaji kutokuwa makini.

Dakika ya 88 Jerome Lembeli tena aliahamsha ramsharamsha za kidedea na mnanda uliokuwa unapigwa nje ya uzio wa uwanja wa Karume baada ya kufunga bao la pili lililozima matumaini ya kusawazisha.

Dakika ya 59 Villa Squad walipata pigo baada ya mchezaji

Raymond Zablon kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea kwa makusudi tena mchezo ukiwa haupo mchezoni mhezaji wa Ashanti United.

Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani Wanajeshi wa JW Green Warriors waliwachezesha kwata wenzao Transit Camp kwa kuifunga bao 1-0.
 Bao pekee hilo lilitiwa kimiani na  Zamkufo Elius  dakika ya 40

Kwa matokeo haya Ashanti inaendelea kuongoza kundi B baada ya kucheza michezo mitano na kufikisha pointi 15

Kundi A, Mjini Iringa Polisi Iringa wameifunga Burkina Fasso ya Morogoro mabao 2-0.
Mabao yamefungwa na Dimosi Malisa dakika ya 53 na Japhet Mamboleo dakika ya 57.

MASHINDANO YA MBIO ZA BOTI UKEREWE, YALIYODHAMINIWA NA BALIMI KATIKA PICHA

Katibu Tawala wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Mariam Kaondo Mseleute (kushoto) akimkabidhi kitita cha shilingi laki saba nahodha wa timu ya Sala wanawake, Malgareth Selemani, kutoka eneo la Muruseni wilayani Ukerewe, baada ya kuibuka mabingwa kwenye mashindano ya Mitumbwi  ngazi ya mkoa baada ya wilaya hiyo kupewa hadhi ya Mkoa kwa mashindano hayo ambapo washiriki walishindana kuendesha mitumbwi kwa makasia

Nahodha wa timu ya wanawake ya Sala kutoka eneo la Muruseni Ukerewe Malgareth Selemani akionyesha laki saba za ubingwa


 Nahodha wa timu iliyoshika nafasi ya kwanza wanaume Bandiho Ignas akionyesha laki tisa.

washindi wa pili wanaume timu ya Yatakamoyo kutoka ngoma wakifurahi baada ya kuwasili.


MANATSA NDIE BINGWA WA MICHUANI YA JOHNNIE WALKER WAITARA 2012

Mshindi wa jumla wa mashindano ya kombe la Johnnie Walker Waitara 2012 Sudson Manatsa akinyanyua juu vikombe vyake viwili alivyoshinda wakati wa Mashindano hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Gofu Lugalo jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yalidhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti kupitia kinywaji chake kikali cha Johnnie Walker

Mgeni rasmi wa Mashindano ya Johnnie Walker Waitara Trophy,  Mlezi wa Gofu nchini Kenya na Mkurugenzi wa ICEA LION, Dunkan Nderitu Ndengwa kutoka nchini Kenya  akimkabidhi zawadi Mshindi wa jumla wa mashindano ya  kombe la Johnnie Walker Waitara 2012 Sudson Manatsa. Kampuni ya Bia ya Serengeti ilidhamini mashindano hayo kupitia kinywaji chake cha Johnnie Walker.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Stephen Gannon  akimkabidhi zawadi Mshindi wa pili wa  daraja A, Aidan Nziku  kikombe na zawadi nyingine baada ya kuibuka mshindi wa kundi hilo katika mashindano ya kuwania kombe la Johnnie Walker Waitara 2012. Kampuni ya Bia ya Serengeti ilidhamini mashindano hayo kupitia kinywaji chake cha Johnnie Walker.

MAANDALIZI YA AFCON 2013.

IVORY Coast ni mojawapo ya nchi 14 zilizofuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2013 ambazo zitaanza maandalizi yake kwa kucheza michezo ya kimataifa ya kirafiki sehemu mbalimbali duniani wiki hii. 

 Ghana na Cape Verde zenyewe zitapimana nguvu jijini Lisbon, Ureno ikifuatiwa na Nigeria ambao watapimana nguvu na Venezuela jijini Miami, Marekani huku wenyeji Afrika Kusini watawakaribisha mabingwa wa Afrika Zambia jijini Johanneburg.

 Ivory Coast, Ghana, Cape Verde, Afrika Kusini, Angola, Morocco, Niger, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Nigeria, Burkina Faso, Algeria, Tunisia na Togo ni timu zilizofuzu ambazo zote zitakuwa katika viwanja tofauti kucheza michezo ya kirafiki.

 Timu za Mali na Ethiopia ndio timu pekee kati ya 16 zitazoshiriki michuano ya ya Mataifa ya Afrika ambayo itaanza kutimua vumbi Januari 19 mpaka Februari 10 mwakani nchini Afrika Kusini ambazo hazitacheza michezo ya kirafiki.

ZAHA KUZIBA PENGO LA ROONEY ENGLAND



WINGA wa Crystal Palace mwenye thamani ya pauni milioni 20, Wilfried Zaha (20) amejumuishwa kwenye kikosi cha England, kitakacho cheza pambano la kirafiki dhidi ya Sweden, Jumatano hii.
Wayne Rooney, Theo Walcott, Jonjo Shelvey, Kyle Walker, Aaron Lennon, Jermain Defoe na Alex Oxlade-Chamberlain watakosa mechi hiyo itakayochezwa Stockholm, Sweden kutokana na majeruhi.


Kutokana na kukosekana kwa wachezaji hao, Roy Hodgson ameamua kumuita kinda huyo mzaliwa wa Ivory Coast kuziba baadhi ya nafasi zilizoachwa na mastaa hao.
Zaha amekuwa akitajwa kama mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa sana anayeibukia kwenye soka la England na amekuwa akihusishwa kujiunga na klabu kadhaa kubwa za ligi kuu huku Arsenal wakionekana kuongoza mbio za kumsajili.

DROGBA AKIRI KUSUMBULIWA NA MOURIHNO USINGIZI




MSHAMBULIAJI wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba amekiri kwamba amekuwa akitumia meseji usiku wa manane kutoka kwa kocha wake wa zamani Jose Mourinho.
 Drogba, ambaye kwa sasa anacheza soka nchini China, kwenye klabu ya Shanghai Shenua, alisema kwamba ataendelea kuwa karibu na Mourinho na Roman Abramovich, milele na ndio maana wameendela kuwasiliana.
“Lakini tatizo la Jose (Mourinho), bado hajajua kama kuna tofauti ya muda kati ya China na Hispania na amekuwa akinitumia meseji usiku wa manane nikiwa nimelala.” Alisema Drogba.

AVB AJITWISHA ZIGO LA LAWAMA



ANDRE Villas-Boas, amesema yeye ndiyo anastahili lawama baada ya timu yake ya Tottenham Hotspurs, kupoteza nafasi ya kuwafunga mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Manchester City, na kujikuta wakilala kwa mabao 2-1.
Tottenham walionekana kuwa na nafasi ya kushinda pambano hilo baada ya kuanza kufunga kupitia kwa Steven Caulker katika dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza.
Lakini AVB amekiri kwamba kocha wa Man City, Roberto Mancini alifanya mabadiliko sahihi katika kipindi cha pili cha mchezo huo na kuamua kutumia mabeki watatu.
AVB alishindwa kujibu mapigo na kujikuta akilala kwenye pambano hilo baada ya Sergio Aguero kuirudisha Man City mchezoni na supa sub Edin Dzeko akafunga bao la ushindi.
Kocha huyo alisema kwamba wakati matokeo yakiwa 1-1 aliamua kupaki basi ilikupata sare lakini kitendo hicho kiliwapa nafasi Man City kuwashambulia sana kitu kilichoamsha mashabiki, na kufanya mechi kuwa ngumu kwao kutokana na mashambulizi mfululizo ya Man City mpaka pale Dzeko alipofunga bao la ushindi

GYAN AMUENZI MAMA YAKE KWA KUFUATA USHAURI WAKE

MSHAMBULIAJI wa Ghana, Asamoah Gyan amesema kuwa hatapiga penati tena kwa ajili ya timu ya taifa ya nchi hiyo kwa heshima ya ushauri wa mama yake ambaye alifariki dunia Jumanne iliyopita. Mshamuliaji huyo anayecheza katika klabu ya Al Ain ya Falme za Kiarabu amekuwa akiandamwa nchini kwao kwa kukosa penati mbili muhimu katika michuano ya Kombe la Dunia 2010 na Mataifa ya Afrika mwaka 2012. Gyan mwenye umri wa miaka 26 aliinyima nafasi Ghana ya kufuzu nusu fainali ya kihistoria katika michuano ya Kombe la Dunia iliyopita baada ya kukosa penati dhidi ya Uruguay dakika chache kabla ya muda wa nyongeza kumalizika na kuishia timu hiyo kutolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-2. Katika michuano ya Mataifa ya Afrika 2012, Gyan alikosa penati katika dakika ya nane ya mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo dhidi Zambia ambapo mwishoni Ghana ilitolewa kwa kufungwa baoa 1-0. Akihojiwa kuhusiana na sula hilo Gyan amesema kuwa mama yake alimshauri kutopiga penati tena hivyo kwa heshima yake kwakuwa ameshafariki sitafanya hivyo tena katika timu ya Ghana. Ghana maarufu kama Black Stars wamepangwa katika kundi B na timu za mali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Niger katika michuano ya Mataifa ya Afrika 2013 nchini Afrika Kusini.

 

No comments:

Post a Comment