Friday, October 19, 2012

USAILI WA MAJINA MKOANI TABORA WAMALIZIKA NA BAADHI YA WAGOMBEA WAENGULIWA KUTOKANA NA KUTOKIDHI VIGEZO VYA TAREFA

Na tano juma

Kamati ya utendaji ya uchaguzi wa mkoa wa tabora TAREFA ambayo ilikutana jana na kupitia majina ya wagombea uongozi wa mkoa wa tabora  ambao wanachuana katika nyasifa mbalimbali ilikamilika na baadhi ya wagombea kuenguliwa kutokana na kutokidhi vigezo vya kugombea uongozi wa chama cha mpira wa miguu mkoa wa tabora TAREFA.

Wagombea ambao wamepitishwa  katika nafasi ya MWENYEKITI  ni paul raulent werema,,yusuph khamis kitumbo pamoja na musa Ntimizi na katika nafasi ya KATIBU waliopitishwa ni Fatty remtula pamoja na albert sitta ambaye amemaliza muda wake na ameamua tena kurejea kutetea nafasi yake hiyo.

Mtunza fedha amepitishwa katika usaili huo ni musa mrisho msananga na wale wagombea wa nafasi ya wajumbe wa mkutano mkuu TFF mkoa wa tabora ambao wamepitishwa katika usaili huo ni Ramadhani khamisi,Abdul amani seif,MIrambo kamili,pamoja na Dick mlimka ndio hawa wanachuana katika ujumbe na nafasi ya mwakilishi wa vilabu tff ni acheri amosi manjoli amepitishwa.

Na mwakilishi  wa vilabu TFF kwa upande wa wanawake amepitishwa dada loisa nicholaus kangabo na uchaguzi rasmi unatarajia kufanyika november 4 mwaka huu katika mkoa huu wa municipal ya tabora

              NA mwenyekiti wa kamati ya utendaji TFF  mkama bwire ambaye amezungumzia kuhusu na mchakato huu wa uchaguzi pale alipokuwa anazungumza na jamaa tano juma 



YUVU SHOOTING NA YANGA KUCHEZA TAIFA KESHO, MECHI ZOTE ZA AZAM NA SIMBA NA YANGA KUCHEZWA TAIFA PIA

Ruvu Shooting; Wenyeji mechi ya kesho

MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Yanga na Ruvu Shooting uliopangwa kuchezwa kesho Uwanja wa Chamazi, sasa umehamishiwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.
 
 
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema leo kwamba, mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na maombi ya timu hizo mbili kutaka mechi ichezwe Uwanja wa Taifa kutokana na sababu mbalimbali ambazo zimeridhiwa na Kamati ya Ligi ya TFF, ikiwemo siku hiyo uwanja huo kutokuwa na mechi.
 
 
Wambura amesema katika mechi hiyo, itakayochezeshwa na refa Amon Paul kutoka Mara ni viingilio vitakuwa Sh. 5,000 viti vya kijani na bluu, Sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, Sh. 15,000 VIP B na C na sh. 20,000 kwa VIP A.
 
 
Amesema pia, Kamati ya Ligi imekataa ombi la timu ya Azam kutaka mechi zake za nyumbani za ligi hiyo zichezwe dhidi ya Simba na Yanga zichezwe Uwanja wa Chamazi kutokana na sababu za kiusalama.
 
Mechi nyingine za kesho, Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ambayo itachezeshwa na refa Israel Nkongo atakayesaidiwa na Hamis Chang’walu na Omari Kambangwa, wote kutoka Dar es Salaam.
 
Ligi hiyo itaendelea tena Jumapili kwa mechi tatu, JKT Ruvu itaonyeshana kazi na Azam FC kwenye Uwanja wa Chamazi, Mgambo Shooting itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Tanzania Prisons na Toto Africans zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

MCHAKATO WA UCHAGUZI TWFA WAZIDI KUNOGA


KAMATI ya Uchaguzi ya Chama cha Soka kwa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya Mwenyekiti wake, Ombeni Zavala imewataka wanachama wa TWFA ambao ni mikoa ya Tanzania Bara kuwasilisha orodha ya wajumbe wao wa mkutano wa uchaguzi.
 
 
Wajumbe wenye sifa ya kuhudhuria Mkutano wa TWFA ni kutoka vyama vya mikoa ambavyo tayari vimefanya uchaguzi. Wajumbe hao ni Mwenyekiti, Katibu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TWFA.
 
 
Mikoa ambayo imeshafanya uchaguzi mpaka sasa ni Iringa, Kigoma, Mwanza, Pwani na Tanga. Mikoa ambayo bado inahimizwa kufanya uchaguzi, na mwisho wa kutuma majina ya wajumbe kwa Mwenyekiti Zavala ni Oktoba 25 mwaka huu.
 
 
Mkoa ambao utakuwa haujafanya uchaguzi utakuwa umenyimwa haki ya kushiriki uchaguzi wa TWFA utakaofanyika Novemba 4 mwaka huu.
 
 
Wakatin huo huo: Wambura amesema Chama cha Madaktari wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) leo kimetangaza kuanza mchakato wa uchaguzi wa chama hicho uliopangwa kufanyika Novemba 28 mwaka huu.
 
 
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dk. Francis Mchomvu, fomu kwa wanamichezo wanaotaka kugombea uongozi wa chama hicho zitaanza kutolewa Oktoba 21 mwaka huu.
 
 
Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu hizo zinazopatikana ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni saa 10.00 alasiri ya Oktoba 26 mwaka huu. 
 
Ada ya fomu kwa nafasi nne za juu ni sh. 200,000 wakati kwa nafasi nyingine zilizobaki ni sh. 100,000. Kati ya Oktoba 27-31 mwaka huu Kamati ya Uchaguzi ya TASMA itapitia fomu na kutangaza majina ya waliojitokeza kuomba uongozi.
 
 
Nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mhazini, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji.
 
 
Kipindi cha pingamizi kwa waombaji ni kuanzia Novemba 1-6 mwaka huu, na pingamizi zinatakiwa kuwasilishwa kwa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 6 mwaka huu. Hakuna ada kwenye pingamizi.
 
 
Pingamizi zitajadiliwa na kufanyiwa uamuzi kati ya Novemba 7-9 mwaka huu. Usaili utafanyika kati ya Novemba 10-11 mwaka huu ambapo matokeo ya usaili huo vilevile yatatangazwa ili kutoa fursa kwa rufani ambazo zinatakiwa kukatwa kati ya Novemba 11-13 mwaka huu.
 
 
Rufaa ambazo zinaambatana na ada y ash. 500,000 zinatakiwa kufikishwa kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 13 mwaka huu.

MTANZANIA KUKIPIGA MAREKANI


MTANZANIA Millan Mbise ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), itakayomwezesha kucheza mpira wa miguu nchini Marekani.
 
Boniface Wambura, Ofisa Habari wa TFF, amesema Shirikisho la Soka Marekani (USSF) limemuombea hati hiyo Mbise kama mchezaji wa ridhaa ili ajiunge na timu ya Virginia Youth Soccer.
 
 
Wambura amesema klabu ya zamani ya Mbise aliyezaliwa Agosti 18, 1994 imetajwa kuwa Super Sport FC, na mechi ya mwisho kwenye timu hiyo alicheza Novemba 15 mwaka juzi.
 
 
Amesema TFF inafanya mawasiliano na pande husika kabla ya kutoa hati hiyo kwa mchezaji huyo kama ilivyoombwa na shirikisho hilo la Marekani.

ETI HAWA WANAANGALIA MPIRA, JAMANI!

Tazama picha hii, wadau mbalimbali wa soka wakiwa Uwanja wa Taifa juzi wakati wa mchezo kati ya Simba na Kagera Sugar. Lakini ukiwatazama kwa makini mtu ambaye anaonekana kufuatilia mchezo ni mmoja tu, Crescentius Magori wa kwanza kushoto. Wengine wote kila mtu ana shughuli zake. Ndiyo mambo ya mpira hayo, wengine wanakwenda uwanjani kama fasheni tu, kupiga stori na nini, lakini si kuangalia mpira. Ila inasikitisha baadaye, wanapokuwa wazungumziaji wazuri wa mchezo, ambao hawakuufuatilia.

"KASEJA, KULIKONI KUKAA BENCHI NA KIBADENI HUKU, SI BORA NIJE NIKAE NA MILOVAN HUKO, NIFANYIE MPANGO BASI KAKA

Kipa wa akiba wa Kagera Sugar, Mganda Hannington Kalyesebula, akisalimiana na kipa namba moja wa Simba SC na Nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja, baada ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baina ya timu hizo juzi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka 2-2.

BEKI LA KAGERA LAZIMWAGA MATE SIMBA NA YANGA

Benjamin Effe akumdhibiti Mrisho Ngassa

BEKI Mnigeria wa Kagera Sugar, Benjamin Effe Ofuyah ameanza kuvitoa udenda vigogo vya soka Tanzania, Simba na Yanga kutokana na soka yake maridadi anayoonyesha katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
 
 
Beki huyo wa kati aliwavutia Yanga walipokwenda Bukoba kucheza na Kagera Sugar Oktoba 8, katika mechi ambayo wenyeji walishinda 1-0, bao pekee la mkongwe Themi Felix kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Effe aliwavutia pia Simba katika mchezo wa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Kagera ikilazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji wao.
 
 
Effe ambaye anacheza kama sentahafu, akiwa pacha wa Amandus Nesta katika mechi na Simba alionyesha uwezo mkubwa wa kulinda na kusaidia mashambulizi.
 
Ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kasi kuruka hewani kuicheza mipira kwa kichwa- nguvu za kupambana na washambuliaji na zaidi ni mtulivu, asiye na papara, mwenye maamuzi ya haraka.
 
Mara kadhaa alishinda mipira dhidi ya washambuliaji hatari wa Simba, akina Mzambia Felix Mumba Sunzu Jr., Mganda Emmanuel Arnold Okwi na mzalendo Mrisho Khalfan Ngassa.
 
 
Beki huyo amesajiliwa na Kagera Sugar kwa pamoja na mwenzake, mshambuliaji Wilfred Emmeh kutoka klabu ya Abuja FC ya kwao Nigeria. Kwa ujumla, katika kikosi cha Kagera kuna Wanigeria watatu, mwingine ni Enyinna Darlington ambaye amesajiliwa kutoka Toto African ya Mwanza, ambayo nayo ilimtoa Abuja FC ya Nigeria.  
 
 
Kagera Sugar ni moja yenye timu zenye kusifika kwa kuvumbua vipaji, ambavyo baadaye vinanunuliwa kwa bei chafu na vigogo wa soka nchini, Simba, Yanga na hata Azam FC.
 
 
Mrisho Ngassa, Amri Kiemba wa Simba, Said Mourad wa Azam FC, Godfrey Taita na David Luhende wa Yanga, wote hawa wametokea Kagera Sugar.
 
 
Aidha, Kagera pia imekuwa ikiwarudisha wachezaji ambao wameonekana hawafai timu nyingine na kuwa na thamani tena, mfano Gaudence Exavery Mwaikimba aliyetupiwa virago Yanga akaenda kufufua makali yake huko, hatimaye kusajiliwa na Azam FC msimu uliopita.
 
 
Salum Kanoni Kupela aliyetupiwa virago Simba SC hivi sasa anang’ara Kagera Sugar na ndiye aliyeifungia timu hiyo bao la kusawazisha kwa penalti katika mechi dhidi ya Wekundu wa Msimbazi, siku ambayo alionekana kumdhibiti vizuri Okwi.

YANGA WAKIGARAGAZA TENA KIDOA CHEKUNDU CHA VODA, WAPEWA VIDOA VIPYA VITATU WACHAGUE




WADHAMINI wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kampuni ya Vodacom Tanzania, wameikubalia klabu ya Yanga kutotumia jezi zenye nembo nyekundu na kuipa nembo tatu ichague mojawapo, ambazo hazina rangi nyekundu.
 
 
Nembo hizo ni njano na nyeusi, kijani na nyeusi na nyeupe na nyeusi, ambazo Yanga itatakiwa kuchagua mojawapo kutumia katika Ligi Kuu.
 
Yanga walikuwa wana mgomo wa kutumia nyembo nyekundu, ambayo ndio nembo kuu ya kampuni hiyo kwa sasa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga akasema wanawaachia Vodacom watumie busara kumalizana na klabu ya Yanga, juu ya mgogoro wao kuhusu nembo ya ligi hiyo.
 
 
Tenga alisema kwamba kwa kuwa msimu uliopita Vodacom walimalizana na Yanga bila kulishirikisha shirikisho lake, na mwaka huu wanawaachia pia.
 
 
“Kitendo kilichofanywa na Vodacom mwaka jana, kumalizana na Yanga bila kutushirikisha kuhusu utata wa nembo, sisi tulijua kitaleta matatizo baadaye, na kweli sasa yametokea, na ndiyo maana unaweza kuona, sekretarieti yetu inalipeleka taratibu hili suala,”alisema Tenga.
 
 
Tenga alisema Vodacom ingewaacha TFF msimu uliopita wakaihukumu Yanga kwa mujibu wa kanuni, hata msimu huu ingekuwa rahisi kwao kuingilia, lakini kwa kuwa msimu uliopita waliingilia na wakaibadilishia klabu hiyo nembo, basi na msimu huu pia wanawaachia wamalizane wenyewe.
 
 
Hatua hiyo ya Vodacom kuibadilishia Yanga nembo ya jezi, inakuja siku mbili baada ya Wazee wa klabu hiyo, kutoa tamko la kusema wapo tayari klabu hiyo ishushwe daraja kwa mujibu wa kanuni, lakini si kuvaa nembo nyekundu.

NGASSA AAHIDI MAMBO YA HATARI SIMBA SC

Mrisho Ngassa; Nipeni muda muone mambo ya hatari

KIUNGO Mrisho Khalfan Ngassa, amesema kwamba bado anaizoea taratibu staili ya uchezaji ya timu yake mpya, Simba SC na nafasi mpya anayopangwa kwa sasa na anaamini hadi Januari mwakani atakuwa ameizoea na kufanya ‘mambo ya hatari’.
Akizungumza  jana, Ngassa alisema kwamba Simba wanacheza mfumo tofauti na ambao ulikuwa unatumiwa na timu yake ya zamani, Azam FC hivyo anaendelea kujifunza na kuizoea.
“Mchezaji unapoingia timu mpya, kawaida unakutana na mambo mengi mapya, inabidi sana ujifunze na kuzoea.  Unacheza na watu wapya, ambao inabidi ujifunze namna ya kucheza nao na kuzoeana nao,”alisema Ngassa.
Ngassa alisema angalau anekutana na wachezaji ambao anacheza nao timu ya taifa, lakini safu ya ushambuliaji ya Simba inaundwa na wachezaji wengi wa kigeni kama Emmanuel Okwi, Daniel Akuffo na Felix Sunzu.
“Inabidi sana nijifunze taratibu, hata hivyo najisifu kwamba naendelea vizuri na hadi kufika Januari hivi, nitakuwa nimekwishazoea na kufanya mambo ya hatari,”alisema Ngassa na kusistiza hajashuka kiwango, ni mazingira mapya tu.    
Ngassa juzi alifunga bao lake la tatu tangu ajiunge na Simba Agosti mwaka huu, akitokea Azam FC wakati Simba ikilazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Kagera kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hiyo ikiwa sare ya pili mfululizo kwa Wekundu hao wa Msimbazi, baada ya Jumamosi pia kulazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union mjini Tanga.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 18 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, kutokana na Azam FC kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. dakika ya nane, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’ kutoka wingi ya kulia.
Kwa ujumla kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu, ingawa ni Simba walioonekana kufanya mashambulizi ‘yenye akili’ zaidi.
Kipindi cha pili Simba ilirudi na moto tena na katika dakika ya 51, Mrisho Khalfan Ngassa aliifungia timu hiyo bao la pili kwa shuti kali lililowababatiza mabeki wa timu hiyo na kutinga nyavuni.
Baada ya hapo, Kagera walizinduka na kuanza kulishambulia lango la Simba kupitia pembeni na katika dakika ya 64 Themi Felix aliunganisha kwa kichwa krosi ya George Kavilla na kuifungia Kagera bao la kwanza.
Bao liliwazindua Kagera, ambao waliongeza kasi ya kulishambulia lango la Simba na katika dakika ya 66, Juma Nyosso alimkwatua kwenye eneo la hatari Paul Ngwai na Salum Kanoni akaenda kumtungua Juma Kaseja, akiisawazishia Kagera.
Baada ya hapo timu zilianza kushambuliana kwa zamu na mpira ulinoga zaidi kutokana na mashambulizi ya pande zote mbili.

AZAM WAPO CHAMAZI TANGU JANA USIKU TAYARI KWA KIPUTE NA JKT RUVU JUMAPILI

Kikosi cha Azam


AZAM FC imerejea Dar es Salaam jana majira ya saa 1:00 ikitokea Mbeya, ambako juzi ililazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
 
 
Azam sasa wanaingia kambini kujiandaa na mchezo wao ujao, Jumapili dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, Dar es Salaam. 
 
 
Pamoja na sare hiyo, Azam wamelalamikia uchezeshaji mbaya wa marefa wa mechi hiyo, kwamba uliwapokonya ushindi.
 
Azam FC wanadai refa alikataa mabao yao mawili yaliyofungwa na Abdi Kassim ‘Babbi’ na penalti ya wazi, baada ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’ kuangushwa kwenye eneo la hatari
Wanadai bao la kwanza, refa alilolikataa ulikuwa ni mkwaju wa mbali wa Abdi Kassim ambao ulitinga nyavuni, kabla ya kurudi uwanjani na refa licha ya kuona kuwa lilikuwa ni bao halali, bado akaamua kukataa
Wanadai baadaye, Sure Boy alifanyiwa madhambi kwenye eneo la hatari na kwa mshangao wa wengi, wakiwemo viongozi na wachezaji wa Prisons ambao walishashika vichwa, refa akapeta na mpira kuendelea
 
 
Zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya mpira kumalizika, Azam FC wanadai walipata adhabu ndogo na Abdi Kassim aliupiga mpira ule na kutinga nyavuni, lakini kwa mara nyingine tena refa akakataa bao kwa madai kuwa kabla ya kufunga, Babbi alikuwa ameotea.
Baada ya ‘kufanyiwa dhuluma’ hiyo, Azam wanaendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakiwa wana pointi 17, baada ya kucheza mechi sana, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wapo kileleni kwa pointi zao 18 na wamecheza mechi nane.  

BAHANUZI, YONDAN HAWAPO KESHO YANGA NA RUVU

Bahanuzi

BEKI Kevin Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi wataendelea kuwa nje ya Uwanja mwishoni mwa wiki, wakati timu yao, Yanga SC itakapokuwa ikiwania pointi tatu katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na hali zao kutoimarika.
Wawili hao ambao ni majeruhi, wapo kwenye programu ya mazoezi mepesi na hadi jana hakuna mmoja kati yao aliyekuwa tayari kuanza programu kamili ya mazoezi ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts.
Maana yake, Mbuyu Twite ataendelea kucheza pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika beki ya kati, wakati Jerry Tegete ataendelea kucheza na Didier Kavumbangu katika safu ya ushambuliaji.
‘Dogo’ Simon Msuva amemaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa Oktoba 3, mwaka huu katika mechi dhidi ya Simba na Hamisi Kiiza amerejea kutoka Uganda, alipokwenda kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes katika mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini.
Uganda ilitolewa na Zambia kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda nyumbani 1-0 na Uganda wakashinda kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
Yanga imeweka kambi katika hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam huku ikiendelea kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Beki Kevin Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu, wakati Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Oktoba 8, mwaka huu.
Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba iliyocheza mechi nane, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 18, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 17, iliyocheza mechi saba.