Saturday, January 26, 2013

BAADA YA VIJANA WA SIMBA KUFUNGWA NA VIBONDE WA SOUTH JUZI LEO SIMBA YAUA KWA SUMU YA OMAN, AZAM NAYO MOTO ULE ULE KWELI LIGI MSIMU HUU NI BALAA





SIMBA SC leo imeanza vyema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa mabao 3-1 African Lyon ya Dar es Salaam katika mchezo wa ufunguzi wa duru hilo.
Ushindi huo, unaifanya  
Hadi mapumziko Simba SC walioweka kambi ya wiki mbili Oman kujiandaa na mzunguko huu, tayari walikuwa mbele kwa mabao 3-0, yaliyotiwa kimiani na Mrisho Khalfan Ngassa mawili dakika za 19 na 39 na Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’ dakika ya tatu ya mchezo huo.
Redondo aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya tatu, akiunganisha krosi nzuri ya Ngassa kutoka wingi ya kushoto na kufumua shuti akiwa katikati ya msitu wa mabeki wa Lyon.
Bao hilo liliwatia chaji Simba SC na kuanza kucheza soka maridadi zaidi, wakionana kwa pasi za mitindo yote, ndefu, fupi, za juu, chini hadi visigino na haikushangaza dakika ya 19 walipopata bao la pili.
Ilikuwa ni kazi nzuri ya Ngassa mwenyewe, ambaye baada ya kupata pasi ya Mwinyi Kazimoto Mwitula aliitoka ngome ya Lyon kabla ya kumchambnua kipa wa timu hiyo, Abdul Seif.
Baada ya kufunga bao hilo, Ngassa alikwenda moja kwa moja kwenye benchi la wachezaji wa akiba na kukumbatiana na Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ kisha kuwapa mikono wachezaji kadhaa na kurejea uwanjani.
Lyon walipoteza nafasi nzuri ya kupata bao dakika ya 31, baada ya Shamte Ally Kilalile kukosa penalti.
Refa Israel Mujuni alitoa penalti hiyo baada ya beki Paul Ngalema kumkwatua beki Fred Lewis aliyepanda kusaidia mashambulizi, hata hivyo mkwaju wa kwanza wa Shamte ulipanguliwa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja, lakini mwamuzi akaamuru irudiwe kwa madai kipa huyo alitokea kabla ya mpira kupigwa na safari hiyo mpigaji akapiga nje kabisa.
Simba iliongeza kasi ya mashambulizi ikitumia mipira ya pembeni, kulia akiteleza Chanongo na kushoto Ngassa, timu ikichezeshwa vyema na viungo watatu katikati, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Jonas Mkude. Ilikuwa burudani kwa mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi, kwa jinsi ambayo timu yao ilitawala mchezo.
Kazi nzuri ya Chanongo aliyeteleza wingi ya kulia huku akiruka madaluga ya mabeki wa Lyon, iliipatia Simba bao la tatu baada ya krosi yake nzuri kuunganishwa vyema kimiani na Ngassa.  
Baada ya kufunga, Ngassa alishangilia kwa aina yake bao hilo, kwanza akitambaa hadi langoni na kisha kujilaza kwenye nyavu kubwa kama yeye ndio mpira.
Baada ya hapo, aliinuka na moja kwa moja kwenda tena kwenye benchi la wachezaji wa akiba akianza kushangilia na Boban, baadaye wachezaji wengine na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ambaye alitumia kama sekunde 30 akizungumza naye jambo.  
Kipindi cha pili, Lyon walibadilika na kuwabana Simba SC wasiongeze mabao zaidi, huku wao wakifanikiwa kupata bao la kufutia machozi, lililofungwa na Bright Ike dakika ya 59, pasi ya Fred Lewis.
Katika mechi nyingine, Mtibwa Sugar ililala 1-0 nyumbani mbele ya Polisi Morogoro, Coastal Union iliifunga Mgambo JKT 3-1, Ruvu Shooting iliilaza 1-0 JKT Ruvu, Azam FC imeshidna 3-1 dhidi ya Kagera Sugar na JKT Oljoro imeilaza 3-1 Toto Africans.
Ligi hiyo itaendelea kesho wakati vinara, Yanga SC watakapomenyana na TZ Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Ngalema/Kiggi Makassy, Mussa Mudde/Komabil Keita, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo, Mrisho Ngassa/Abdallah Seseme, Amri Kiemba na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
African Lyon; Abdul Seif, Fred Lewis, Jacob Massawe, Mohamed Samatta, Abdulaghan Gulam/Hood Mayanja, Yussuf Mlipili, Jackson Kanywa, Aman Kyata/Yussuf Mgwao, Job Ibrahim, Shamte Ally/Bright Ike na Juma Seif ‘Kijiko’.
MSIMAMO WA LIGI KUU YA VODACOM 2012/2103:   
                                P    W  D   L    GF GA GD Pts
1    Yanga                13 9    2    2    25 10 15 29
2    Azam                 14 8    3    3    20 12 8    27
3    Simba SC           14 7    5    2    23 12 11 26
4    Mtibwa Sugar     14 6    4    4    18 13 5    22
5    Coastal Union    14 7    4    3    19 15 4    25
6    Kagera Sugar     14 5    6    3    16 13 3    21
7    Ruvu Shooting   14 7    2    5    20 17 3    23
8    Mgambo JKT      14 5    2    7    11 16 -5  17
9    JKT Ruvu            14 4    3    7    13 21 -8  15
10 JKT Oljoro           14 5    5    5    16 17 -1  17
11 TZ Prisons           13 3    5    5    8    12 -4  14
12 Toto African         14 2    6    6    11 18 -7  12
13 African Lyon         14 2    3    9    10 23 -13 9
14 Polisi Moro           14 1    4    9    5    16 -11 7
MATOKEO KAMILI MECHI ZA LEO:
Mtibwa Sugar 0-1 Polisi Morogoro
Coastal Union 3-1 Mgambo JKT
Ruvu Shooting 1-0 JKT RUVU
Azam FC 3-1 Kagera Sugar
JKT Oljoro 3-1 Toto Africans
KESHO; Januari 27, 2013
Yanga SC Vs TZ Prisons

LIVE MATCH CENTRE: SIMBA 3 - 1 AFRICA LYON,KAGERA VS AZAM



DK 90: Mpira umemalizika Simba 3-1 African Lyon

 Dk 87. Simba imefanya mabadiliko. Ametoka Ngassa ameingia Abdallah Seseme.

Dk 84. Lyon imefanya mabadiliko. Ametoka Amani Kyata ameingia Yusuf Mgwao.

Kwa dakika 10 Lyon inacheza soka safi na kuitawala kiungo.

Dk 66. Lyon imefanya mabadiliko. Ametoka Abdulghan Gulam ameingia Hood Mayanja.

DK 63: Simba wanapata penati na Mrisho Ngassa anapiga lakini anakosa akipoteza nafasi ya kupiga hat trick.

Dk 58. Gooo..,! Bright Ike anaipatia Lyon bao la kwanza akimalizia pasi ya Fred Lewis. Lyon 1-3 Simba

Dk 52. Lya imefanya mabadiliko. Ametoka Shamte Ally ameingia Bright Ike.

Dk 45. Simba imefanya mabadiliko. Wametoka Mussa Mude na Paul Ngalema wameingia Komanbil Keita na  Kigi Makassi.

Hapa uwanja wa taifa mechi inaanza kipindi kati ya Simba wanaoongoza kwa mabao matatu kwa bila
AZAM VS KAGERA: Abdi Kassim na Khamis Mcha wameifungia Azam FC magoli katika kipindi cha kwanza, pasi za Brian Umony, Azam FC 2-0 Kagera
Dk 45. HALF TIME...! Lyon 0-3 Simba

 Dk 35. Gooo..,! Ngassa anaipatia Simba bao la tatu akimalizia pasi ya Haruna Chanongo. Lyon 0-3 Simba

Dk 29: Shamte Ally anapiga penalti anakosa. Lyon wanashambulia sana.

 Dk 29: Penaltiii..! Lyon inapata penalti baada ya Fred Lewis kukwatuliwa na Paul Ngalema ndani ya eneo la hatari.

Simba inapata bao la pili dakika ya 18, mfungaji Mrisho Ngassa lakini cha ajabu amefunga na hajashangilia bao lake.

DK. 2 - Ramadhan Chombo Redondo anaipatia Simba bao la kuongoza akiunganisha pasi nzuri ya Mrisho Ngassa

DK . 14 - Simba inakosa bao la wazi baada ya Ngassa kubaki na kipa na kupiga shuti hafifu na kipa anadaka


SIMBA:
Juma Kaseja, Nassoro Masoud, Paul Ngalema, Mussa Mude, Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, Ramadhan Chombo


AFRICAN LYON: Abdul Seif, Fred Lewis, Jacob massawe, Mohamed Samatta, Abdulgham Gulam, Yusuf Mlipili, Jackson Kanywa, Amani Kyata, Ibrahim Isaac, Shamte Ally, Juma Seif

BURKINAFASO WALIVYOWATESA JANA ETHIOPIA,,,,,,HATARI SANA ALLAN TRAORE

TAIFA STARS KUKIPIGA NA CAMEROUN FEBRUARI 6, TAYARI KIKOSI CHA CAMEROUN KIPO HADHARANI


Panoramic


Goal keepers
Itandje Charles (Atromitos, Greece), Mayébi Joslain (Wrexham, Wales)
Defenders
Nyom Allan Roméo (Grenade, Spain ), Angbwa Ossoemeyang Benoît (FC Rostov, Russia), Assou Ekotto Benoît (Tottenham, Englan), Bédimo Henri (Montpellier, France), Nkoulou Ndoubena Nicolas (Marseille, France), Kana-Biyik Jean Armel (Rennes, France), Wome Nlend Pierre (Canon, Cameroon),
Midfielders
Aminou Bouba (Coton Sport, Cameroon), Matip Joël (Schalke 04, Germany), Song Alexandre (FC Barcelone, Spain), Nguémo Landry (Bordeaux, France), Tchami Hervé (Honved Fc, Hongary), Makoun Jean II (Rennes, France), Eloundou Charles (Coton Sport, Cameroon)
Attackers
Olinga Essono Fabrice (Malaga, Spain), Emana Achille (Al-Wasl, United Arab Emirates), Eto’o Fils Samuel (Anzhi Makachkala, Russia), Aboubakar Vincent (Valenciennes, France), Yontcha Jean Paul (Sc Olhanense, Portugal)

UNITED HUENDA WAKAPATA NAFUU KUFUATIA IKER CASILLAS KUPATWA NA MAJERAHA MAKUBWA YA MKONO WA KUSHOTO


Iker Casillas
Pigo: Iker Casillas akiugulia maumivu ya mkono ambayo huenda yakamuweka nje dhidi ya Manchester United mwezi ujao.
 Iker Casillas yuko katika mashaka makubwa ya kuwepo katika kikosi cha Real Madrid kitakachoshuka dimbani dhidi ya Manchester United mchezo wa ligi ya vilabu bingwa Ulaya kufuatia taarifa awali kusema kuwa mlinda mlango huyo wa kimataifa wa Hispania kuvunjika mkono.
Casillas amepatwa nadhahma hiyo katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Valencia mchezo wa kombe la mfalme 'Copa del Rey' uliopigwa jumatana ya kusukumwa na mchezaji mwenzake Alvaro Arbeloa katika harakati za kuokoa mpira katika eneo la hatari.
Madrid inatarajia kutoa maelezo ya ukubwa wa maumivu ya mlinda mlango huyo na aina ya tiba wakati ambapo Adan Garrido akiwa katika hali ya maandalizi kuziba pengo la mlinda malango huyo mzoefu namba moja wa Hispania.
Iker Casillas
Casillas pia atakosekana katika mchezo wa ligi ya La liga kesho kutwa jumapili dhidi ya Getafe na mchezo wa marudiano wa Copa Del Rey dhidi ya Valencia wiki ijayo.
Pia atakuwa katika vita ya kupigania kurejesha hali yake ya mkono katika kawaida ili kuwemo katika kikosi kitakachokuwa dimbani Februari 13 dhidi ya United katika dimba la Santiago Bernabeu.
Taarifa ya klabu yake imesema baada ya kufanyiwa uangalizi wa awali kupitia kipimo cha 'x-rays' imethibitika kuwa Iker Casillas amepata mpasuko mdogo katika mfupa unaotambuliaka kama metacarpal katika mkono wake wa kushoto.
'hiyo italazimu apate uangalizi mwingine kutoka mtaalamu zaidi leo (yaani jana jioni) na kuamua aina gani ya tiba afanyiwe'
Real Madrid's goalkeeper Iker Casillas
Real Madrid's goalkeeper Iker Casillas
Vita? Casillas na meneja wake Jose Mourinho walikuwa katika vita katika siku za hivi karibuni.
 
Hata hivyo maumivu makubwa kwa mlinda mlango huyo yanakuja katika kipindi nyeti cha kusubiri wiki mbili cha kampeni kubwa ya michuano mikubwa ya vilabu barani ulaya.
 Casillas amerejeshwa katika kikosi cha kwanza baada ya mzozo mkubwa mkubwa baina yake yeye na Mourinho ulioibuka kipindi cha majira ya baridi ambapo Mourinho aliamua kumuweka benchi bila sababu ya kueleweka.
Maamuzi ya Mourinho yaliibua hasira kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo na kutiwa utambi na vyombo vya habari.
Main man: Casillas' injury will be a blow to the Spanish champions ahead of the Champions League last 16

SERIKALI :SIMBA HAWANA ADABU BAADA YA KUCHEZESHA KIKOSI CHA SIMBA B



 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhxNhRWqQLHTYmdrWi42_YmUFoQblVMd8uzQQ0nJBLkauhmy6Mpjc7_fN8dr1FC5jxdy1973Wx3jsrO6QXyYTHR1wEc0CS5hgjiL2jyBXprHgKjrymwZUYyOuZDtBIfx50pCX0WlMo16eY/s400/moro13.jpg 

Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla amekosoa kitendo cha mabingwa wa Bara, Simba kuchezesha kikosi B katika mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya Black Leopards ya Afrika Kusini juzi kwa kuwa kitendo hicho kiliwanyima raha wapenzi wa soka.

Mechi hiyo ilimalizika kwa wageni hao waliofungwa mara mbili mfululizo na Yanga Dar es Salaam na Mwanza, kushinda 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini.


 Makalla amesema Simba haikuwatendea haki mashabiki walioingia uwanjani kushuhudia mechi hiyo kwa kuwa walitegemea kuona kikosi cha kwanza cha 'Wekundu wa Msimbazi'.


"Mechi hiyo ilitangazwa sana, nilikuwapo uwanjani , Kwa kweli sikutegemea kuona Simba wanaingiza kikosi chao cha vijana katika mechi hiyo. Mashabiki walinunua tiketi kushuhudia Simba yenyewe na siyo kikosi cha pili," alisema Makalla.


"Katika hali kama hii tunapunguza utamu wa mpira. Watu wataacha kuingia viwanjani kwa sababu ya vitu kama hivi," alisema kwa sababu "leo unawaambia kuna mechi kubwa, wanaingia uwanjani wanakutana na timu tofauti.


"Kesho hawataingia watasita kuingia uwanjani wakihofia kudanganywa."

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' amesema kuwa waliamua kuingiza kikosi B katika mechi hiyo ili kuwapa 'yosso' wao uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa.

"Watu wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wachezaji wenye umri mdogo hawapewi nafasi za kutosha katika timu zetu. Sisi tumewapa nafasi vijana wetu, kwanini tunalalamikiwa?" alihoji Kaburu akionyesha dhahiri kushindwa kuona ama kuelewa wasiwasi wa Makalla.

MABONDIA WAPIMA UZITO KWA AJILI YA MPAMBANO WA KESHO


Bondia Antony Mathias (kushoto) akitunishiana misuri na Fadhili Majia baada ya kupima uzito, Dar es salaam  kwa ajili ya mpambo wao kesho utakaofanyika katika ukumbi wa CCM Tandare.(Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com)    


Mabondia Hassan Mandulla na Jems Martin wanatarajia kupanda ulingoni  Kesho jumapili Janual 27 katika ukumbi wa wa CCM Tandare Dar es salaam akizungumza mpambano huo mwandaaji Waziri Rosta
amesema  wamepima uzito leo pamoja na kujua Afya zao mabondia wote watakaocheza kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi yakiwemo ya mabondia maarufu na chipkizi alisema mapambano ya utangulizi ni Fadhiri Majia na Anton Matiasi mpambano mwingine

Utamkutanisha Kalama Nyilawila atakaezidunda na Athumani Pendeza mpambano wa raundi nane kalama anapanda ulingoni baada ya mpambano wake wa mwisho kupondeza kwa K,O raundi ya sita na Francis Cheka

michezo mingine ni  Shabani Kilumbelumbe na Mwaite Juma na Chaeles Mashali atavaana na Adam Ngange, Julias Noro atapambana na Abdallah Luwajempambano mwingine utawakutanisha Rajabu Tumaini na Daudi Anton na Rashid Mohamed Atavaana na Eliman Richard wakati Rashid Hamisi atamvaa Omary Shabani


Super D, alisema katika mpambano huo atasambaza DVD zake mpya tofauti na kanda yake ya awali iliyokwenda kwa SUPER D BOXING COACH, DVD za sasa zimeandaliwa kisasa na zikiwa na mchanganyiko wa ‘clips’ za michezo ya nyota wa Dunia katika kuwafunza watu namna ya kupigana ngumi.Super D, alisema mbali na michezo ya nyota hao wa Dunia akiwemo Manny Pacquio,Juan Emanuel Marquez, Floyd Maywether, Roy Jones na wakali wengine DVD hizo zina.

 michezo
ya tamasha lao la ngumi wanaloendesha kwa kushirikiana na kocha mkongwe Habibi Kinyogoli.”katika muendelezo wa kuwafunza watu ngumi kwa njia rahisi, nimetoa dvd pamoja na CD nyingine tofauti zilizokusanya michezo ya mabingwa wa dunia na mafunzo ya ngumi tunayoendesha kupitia tamasha letu na Kinyogoli Foundition ” alisema.
 Super D ambae ni kocha wa timu ya ngumi ya Ashanti pamoja na timu ya mkoa wa Ilala kimichezo alisema anamini kupitia njia  hii watu wengi wenye kupenda kujifunza mchezo wa ngumi kwa kuangalia mbinu na ufundi katika mchezo huo kupitia michezo ya mabondia waliopo kwenye dvd hizo.   
Aliongeza kuwa, mbali na dvd hizo bado wanaitajika vijana wenye vipaji kujitokeza kuja kushiriki katika mazoezi ya ngumi ili wajiunge na wenzao wa
timu ya Ashanti na Amana kujifunza ‘live’ chini ya makocha Habibu Kinyogoli, Kondo Nassoro, na yeye mwenyewe Super D na wengine wanaowanoa vijana

FERGUSON AWAJIA JUU WANAOMPONDA KIPA WAKE.


MENEJA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amemkingia kifua golikia wake David de Gea baada ya nyota huyo wa kimataifa wa Hispania kulaumiwa kuruhusu bao la kusawazisha katika mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs mwishoni mwa wiki iliyopita. Wachambuzi wa soka wa luninga Alan Hansen na Gary Neville walimlaumu De Gea kwa makosa aliyofanya na kuruhusu Clint Dempsey kuisawazishia timu yake bao lakini Ferguson amesema hatilii maanani habari hizo. Ferguson amesema bado anamwamini De Gea kuwa golikipa wake namba moja na maneno ya watangazaji hao hayawezi kumbadilisha anavyofikiria. Katika mchezo huo United ambao ndio vinara wa Ligi Kuu nchini Uingereza ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Tottenham bao ambalo lilisawazishwa katika dakika za lala salama.

BEBETO KUKABIDHIWA TIMU YA VIJANA.


SHIRIKISHO la Soka nchini Brazil linajipanga kumteua mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa nchi hiyo, Bebeto kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 20 itakayoshiriki katika michuano ya Amerika Kusini. Akihojiwa kuhusu suala hilo Bebeto amesema kuwa matokeo mabovu katika siku za karibuni yamechangia mabadiliko hayo katika timu za vijana kwakuwa ndio msingi wa kupata timu nzuri ambayo itapambana kuhakikisha wanabakisha nyumbani Kombe la Dunia 2014. Shirikisho hilo limedai kuwa nyota huyo ambaye anakumbukwa kwa aina ya ushangiliaji wake akiwa kama amempakata mtoto katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1994 iliyofanyika Marekani atateuliwa rasmi kushika nafasi hiyo wiki ijayo. Hatahivyo wadau wa soka nchini humo wamedai kuwa Bebeto ana uwezo mdogo katika kufundisha akiwa amewahi kufundisha klabu moja ya Amerika iliyopo jijini Rio de Janeiro mwaka 2010.

EURO 2020 KUCHEZWA KATIKA MIJI 13 TOFAUTI.


SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA limetangaza kuwa michuano ya Ulaya 2020 itaandaliwa katika nchi 13 huku nusu fainali na fainali za michuano hiyo zitachezwa katika uwanja mmoja. Katibu Mkuu wa UEFA Gianni Infantino amesema hakuna uwanja zaidi ya mmoja utakaotumika katika nchi ambayo itapewa nafasi kuandaa mechi, katika timu 24 zinazoshiriki michuano hiyo na viwnaja hivyo vitachaguliwa Septemba mwaka 2014. UEFA walipiga kura Desemba mwaka jana kuandaa michuano hiyo katika miji tofauti kuzunguka bara hilo kuliko ilivyokuwa kawaida ambapo michuano hiyo imekuwa ikiandaliwa na nchi moja au mbili. Shirikisho limedai kuwa kufanya hivyo kutasaidia nchi ndogo ambazo hazitaweza kuzihudumia nchi 24 zinazoshiriki michuano hiyo kupata uhondo kwa kuandaa mojawapo ya mechi. Rais wa UEFA Michel Platini amesema uwanja utakaotumika kwa ajili ya mechi za nusu fainali na fainali unatakiwa kuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 70,000 na mashabiki 60,000 kwa viwanja vya robo fainali huku hatua ya makundi ambayo itakuwa na mechi 16 viwanja vyake vinatakiwa kuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 50,000.

KIPYENGA CHALIA LEO LALA SALAMA LIGI KUU BARA, NANI ANA NINI?


Simba na Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu iliyoisha kwa sare ya 1-1


MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unatarajiwa kuanza leo, nyasi za viwanja sita tofauti nchini zikiwaka moto katika mechi za ufunguzi za mzunguko huo wa lala salama.
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,Watoto wa Zamunda, African Lyon watamenyana na mabingwa watetezi, Simba SC wakati Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Polisi ya Morogoro mjini.
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Coastal Union watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT wakati Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Ruvu Shooting watawakaribisha ndugu zao, JKT Ruvu, huku Azam FC wakiwa wenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, JKT Oljoro wataikaribisha Toto Africans ya Mwanza.
Vinara wa Ligi hiyo, Yanga SC wao wataanza mbio za kurejesha taji Jangwani keshokutwa, watakapomenyana na Maafande wa jeshi la Magereza, Prisons kutoka Mbeya.
Je, timu zinaingia kwenye mzunguko wa pili zikiwa katika nafasi gani na zimejiandaaje kuelekea hatua hiyo ya lala salama? Endelea.
Yanga SC
YANGA SC:
Walimaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni mwa Ligi Kuu, wakiwa na pionti zao 26, baada ya kucheza mechi 13, kufungwa mbili dhidi ya Mtibwa Sugar 3-0 na Kagera Sugar 1-0, zote ugenini, kutoa sare mbili 1-1 dhidi ya Simba SC na 0-0 dhidi ya Prisons.
Yanga ambayo msimu uliopita ilishika nafasi ya tatu Ligi Kuu, ilipanda kileleni Novemba 4, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 na kuwashusha mabingwa watetezi, walioongoza ligi hiyo tangu mwanzoni.
Katika ya mzunguko wa kwanza, Yanga ilifikia kuzidiwa pointi saba na Simba lakini Oktoba 31, ikafanikiwa kuwafikia Wekundu hao wa Msimbazi, siku hiyo wao wakiifunga Mgambo JKT 3-0 Dar es Salaam na wapinzani wao0 wakilazimishwa sare ya bila kufungana na Polisi Morogoro.
Baada ya mapumziko mafupi, Yanga walianza kujifua Dar es Salaam, kabla ya kwenda kwenye ziara ya mafunzi Uturuki kwa wiki mbili ambako pamoja na mazoezi walipata mechi tatu za kujipima nguvu na waliporudi, pia wamecheza mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya Black Leopard ya Afrika Kusini, ambazo wameshinda zote. Katika dirisha dogo, Yanga imeongeza mchezaji mmoja tu, Kabange Twite kutoka APR ya Rwanda. 
                                   P    W  D   L    GF GA GD Pts
1    Yanga                   13 9    2    2    25 10 15 29
KOCHA; Ernie Brandts (Uholanzi)
Azam FC
AZAM FC:
Ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya pili, kwa pointi zake 24, ikiwazidi pointi moja tu mabingwa watetezi, Simba SC. Azam walikuwa na mwelekeo wa kumaliza katika nafasi nzuri zaidi kama si kufungwa mechi mbili mfululizo za mzunguko wa kwanza, dhidi ya Yanga 2-0 na Mgambo JKT 2-1.
Azam ilianza vema tu ligi hiyo, ikiwa nyuma ya Simba tangu mwanzo hadi Oktoba 31, ilipoenguliwa na Yanga katika nafasi ya pili. Ikielekea kwenye mechi yake ya mwisho dhidi ya Mgambo, Azam ilifukuza wachezaji wake wanne, Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris kwa madai walipokea hongo waifungishe timu hiyo dhidi ya Simba na wanadai wana ushahidi hadi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Dhahiri kuondolewa kwa wachezaji hao tegemeo kikosini kulichangia matokeo ya kufungwa na Mgambo katika mechi ya mwisho.
Baada ya mapumziko mafupi, Azam ilianza kujifua tena na ikaenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kucheza Kombe la Hisani, walilofanikiwa kutwaa. Waliporudi wakaenda kwenye Kombe la Mapinduzi, ambako pia walitwaa taji hilo. Baada ya hapo, wakafanya ziara ya wiki moja Kenya, ambako walicheza mechi tatu za kujipima nguvu, wakishinda mbili na kufungwa moja.
Katika dirisha dogo, Azam imesajili wachezaji saba, ambao ni Humphrey Mieno kutoka Kenya, Brian Umony (Uganda), Jockins Atudo (Kenya), David Mwantika (Prisons), Abdallah Seif (Ruvu Shooting), Malika Ndeule (Mtibwa Sugar) na Uhuru Selemani kwa mkopo kutoka Simba SC.
                                  P    W  D   L    GF GA GD Pts
2    Azam                    13 7    3    3    17 11 6    24
KOCHA: Stewart Hall (Uingereza)
Simba SC
SIMBA SC:
Mabingwa hao watetezi, waliianza Ligi Kuu vema wakionyesha dalili zote za kutetea ubingwa wao kwa kufanikiwa kuwa kileleni hadi mwishoni mwa mzunguko huo, kabla ya mambo kugeuka ghafla.
Zilianza sare kwanza, 1-1 na Yanga, 0-0 na Coastal Union, 2-2 na Kagera Sugar na baadaye 0-0 na Mgambo, 0-0 na Polisi Morogoro kabla ya kufungwa mechi ya kwanza msimu huu, mbele ya Mtibwa Sugar na kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kipigo cha 1-0 kutoka kwa Toto Africans.
Matokeo haya kwa kiasi kikubwa yameivuruga Simba SC na inasemekana Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ anafikiria kujiuzulu na baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar, hakujihusisha na chochote juu ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Toto, wakati huo Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage yuko bize na shughuli za kisiasa Dodoma.
Baada ya mapumziko mafupi, Simba walirudi mazoezini na Desemba wakaenda Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi, ambako walitolewa Nusu Fainali na baada ya hapo, wakaenda Oman, kwenye kambi ya wiki mbili ya mafunzo. Waliporejea, juzi walicheza mchezo wa kujipima nguvu na Black Leopard ya Afrika Kusini.
Habari mbaya, au njema kwa wapenzi wa Simba ni kumpoteza mshambuliaji wake hatari, Emmanuel Okwi aliyeuzwa dola za Kimarekani 300,000 katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia. Simba imeingiza fedha nyingi, ambazo ni rekodi katika historia yao ya kuuza wachezaji, ila wamepoteza kifaa cha maana sana.
Katika dirisha dogo, Simba imesajili wachezaji wawili tu kutoka Uganda, kipa Abbel Dhaira na kiungo anayeweza kucheza kama beki pia, Mussa Mudde. Aidha, Simba SC imebadilisha benchi lake Ufundi, imemuondoa Mserbia, Milovan Cirkovick na kuleta Mfaransa, Patrick Liewig ambaye atakuwa anasaidiwa na Mganda, Moses Basena na Mzalendo Jamhiri Kihwelo ‘Julio’.
                                   P    W  D   L    GF GA GD Pts
3    Simba SC             13 6    5    2    20 11 9    23
KOCHA: Patrick Liewig (Ufaransa)
Mtibwa Sugar
MTIBWA SUGAR:
Ilianza vizuri, katikati ikavurunda na mwishoni mwa mzunguko wa kwanza ikazinduka tena hatimaye imemaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Inaonekana Mtibwa Sugar inaanza kurejesha makali yake iliyoingia nayo katika soka ya Tanzania miaka ya 1990 hadi wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo mara mbili mfululizo 1999 na 2000, wakiweka rekodi ya kuwa timu pekee nje ya Simba na Yanga kutetea taji hilo.
Hiyo si kwa sababu tu ipo nyuma ya Yanga, Azam na Simba, bali katika mzunguko wa kwanza msimu huu imefanikiwa kuvifunga vigogo vyote vya soka nchini, Simba na Yanga.  Baada ya mapumziko mafupi, Mtibwa walianza mazoezi Desemba na mapema mwezi huu walikwenda kucheza Kombe la Mapinduzi, ambako hata hivyo hawakufanya vizuri. Waliporejea Morogoro, waliendelea na mazoezi na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu. Katika dirisha dogo, Mtibwa Sugar imesajili wachezaji wane tu, wote huru Rajab Mohamed, Zakayo Joseph, Baraka Anthony na Mussa Chambo.
                               P    W  D   L    GF GA GD Pts
4    Mtibwa Sugar    13 6    4    3    18 12 6    22
KOCHA: Mecky Mexime (Mzalendo)
Coastal Union
COASTAL UNION:
Wana Mangushi wamerudi tena kwenye makali yao yaliyowafanya wakawa mabingwa wa ligi hiyo mwaka 1988, kwani hadi sasa wameonyesha upinzani wa kutosha kwenye Ligi Kuu. Wagosi hao wa Kaya wamemaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zao 22 sawa na Mtibwa walio nafasi ya nne, lakini wanazidiwa wastani tu wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hata hivyo, Coastal walianza Ligi Kuu kwa kusuasua kiasi cha kufikia kuwafukuza makocha wake wa awali waliosajili na kuandaa timu kwa ajili ya ligi hiyo, Juma Mgunda na Habib Kondo ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hemed Morcco na Alloy Kiddy.
Baada ya mapumziko mafupi, Coastal walianza kujifua Desemba na mapema mwezi huu walikwenda Zanzibar kucheza Kombe la Mapinduzi, ambako hata hivyo hawakufanhya vizuri. Waliporejea waliweka kambi Tanga wakiendelea kujifua na kucheza mechi kadhaa za majaribio.
Katika dirisha dogo, Coastal wamewasajili Shabani Kado kutoka Yanga, aliyekuwa anacheza kwa mkopo Mtibwa Sugar, Rashid Simba, Zuberi Hamisi, Shaongwe Ramadhan, Castory Mumbara na Tinashe Machemedze, wote huru.
                                P    W  D   L    GF GA GD Pts
5    Coastal Union    13 6    4    3    16 14 2    22
KOCHA: Hemed Morocco (Zanzibar)
Kagera Sugar
KAGERA SUGAR:
Kagera Sugar wamemaliza katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 21 na wangeweza kumaliza juu ya hapo, kama wangeutumia vizuri mchezo wao wa mwisho kwenye Uwanja wa nyumbani dhidi ya vibonde Polisi Morogoro.
Wakipewa nafasi kubwa ya kushinda, katika mastaajabu ya wengi, Kagera wakalazimishwa sare ya bila kufungana na Maafande hao wa Morogoro kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, hivyo kuwapa nafasi Coastal na Mtibwa kuendelea kuwa juu yao.
Kagera inajivunia kutofungwa na vigogo wa soka nchini, kwani waliifunga Yanga 1-0 na wakatoa sare ya 2-2 na Simba na Dar es Salaam.   Baada ya mapumziko mafupi, Kagera walianza kujifua Desemba na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu.
Katika dirisha dogo, Kagera Sugar wamesajili wachezaji wawili tu na wote huru; Edmund Kashamila na Julius Mrope.
                                  P    W  D   L    GF GA GD Pts
6    Kagera Sugar      13 5    6    2    15 10 5    21
KOCHA: Abdallah Athumani Seif ‘Kibadeni’ (Mzalendo)
Ruvu Shooting
RUVU SHOOTING:
Katika timu zote za majeshi kwenye ligi hiyo, Ruvu Shooting ndio inaonekana kuwa imara zaidi na ndiyo maana ilimaliza katika nafasi nzuri zaidi, ya saba. Ruvu ipo katikati ya msimamo wa ligi, nafasi ya saba kwa pointi zake 20.
Timu hii inayotumia Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani ni moja kati ya timu zilizoonyesha kandanda safi ya kuvutia, tena ikiundwa na wachezaji wengi chipukizi, kama Seif Abdallah anayegombea kiatu cha dhahabu.  
Baada ya mapumziko mafupi, Ruvu Shooting walianza kujifua na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu na katika dirisha dogo, Ruvu Shooting wamesajili wachezaji watatu tu na wote huru; Juma Mdindi, Njaidi Mohamed na Mahmoud Mbulu. Habari mbaya kwa wapenzi wa timu hiyo, ni kumpoteza kinara wake wa mabao katika mzunguko wa kwanza, Seif Abdallah aliyesajiliwa Azam FC.
                                P    W  D   L    GF GA GD Pts
7    Ruvu Shooting   13 6    2    5    19 17 2    20
KOCHA: Charles Boniface Mkwasa (Mzalendo)
Mgambo JKT
MGAMBO JKT:
Ligi Kuu ya Bara imepokea timu mpya tushio ambayo imeongeza ladha katika ligi hiyo. Hiyo si nyingine zaidi ya JKT Mgambo ua Handeni, Tanga inayotumia Uwanja wa Mkwakwani, Tanga pamoja na Coastal Union. Mgambo ilimaliza katika nafasi ya nane, kwa pointi zake 17. Mgambo walianza kwa kusuasua na watu wakaitabiria itashuka daraja, ila ilipokuja kuzinduka mwishoni mwa msimu, watu wamebadilisha kauli zao. 
Baada ya mapumziko mafupi, Mgambo JKT walianza kujifua na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu, wakati katika dirisha dogo Mgambo JKT wamesajili wachezaji watatu, ambao ni Moaka Shabani, Ismail Mkaima na Damas Milanzi.
                                P    W  D   L    GF GA GD Pts
8    Mgambo JKT      13 5    2    6    10 13 -3  17
KOCHA: Mohamed Kampira (Mzalendo)
JKT Ruvu
JKT RUVU:
Imeshuhudiwa katika msimu mwingine, timu hii inazidi kupoteza makali yake, baada ya kumaliza katika nafasi ya tisa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
Siyo JKT ile ambayo ilikuwa tishio kwa vigogo, Simba na Yanga bali hii ya sasa ni ‘urojo’ na hali hii inatokea huku ikiwa inaundwa karibu na asilimia kubwa ya wachezaji wake wale wale, walioifanya iwe tishio misimu michache iliyopita, tena wakiwa chini ya kocha yule yule, kiungo wa zamani wa Yanga, Charles Killinda.
Baada ya mapumziko mafupi, Ruvu JKT walirudi mazoezini na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu na katika dirisha dogo, JKT Ruvu imesajili wachezaji wanne, Zahoro Pazi kwa mkopo kutoka Azam, ambaye hata hivyo amekwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa Afrika Kusini, Emmanuel Linjechele, Kisimba Luambano na Nashon Naftali.
                                   P    W  D   L    GF GA GD Pts
9    JKT Ruvu              13 4    3    6    13 20 -7  15
KOCHA: Charles Kilinda (Mzalendo)
JKT Oljoro
JKT OLJORO:
Haina makali yake iliyoingia nayo kwenye Ligi Kuu msimu uliopita yaliyowafanya wamalize mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni. Msimu huu JKT Oljoro imemaliza katika nafasi ya 10 kwa pointi zake 14 na huwezi kusita kusema ipo kwenye hatari ya kushuka daraja hadi sasa.
Ina pointi 14, sawa na Toto Africans iliyo nafasi ya 11 na inabebwa juu kwa wastani wa bao moja tu katika mabao ya kufunga na kufungwa, huku ikiwa inaizidi kwa pointi mbili tu Africans Lyon iliyo nafasi ya 12- JKT Oljoro hakika imemaliza mzunguko wa kwanza katika eneo baya.  Baada ya mapumziko mafupi, Oljoro ilianza kujifua Desemba mwaka jana na katika kujisuka upya, ilimfukuza kocha wake Mbwana Makatta, na hadi sasa haijamtaja kocha wake mpya.
Katika dirisha dogo, Oljoro imesajili wachezaji wapya wanane, ambao ni Nurdin Selemani, Shaibu Nayopa, Hamidu Hassan, Paul Malipesa, Josephat Moses, Muharami Mnyangamala, Majaliwa Mbaga na Alphonce Peter.
                                 P    W  D   L    GF GA GD Pts
10 JKT Oljoro           13 3    5    5    13 16 -3  14
KOCHA: Hajatajwa baada ya Makatta kufukuzwa
TZ Prisons
TZ PRISONS:
Imerejea Ligi Kuu msimu huu na hadi sasa unaweza kusema inapambana kuhakikisha inabaki kwenye ligi hiyo msimu ujao. Prisons ilimaliza katika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 14.
Ipo katika hali mbaya na inakabiliwa na vita ngumu ya kupigana kuhakikisha inabaki Ligi Kuu. Mbaya zaidi katika dirisha dogo, limpoteza beki wake kisiki, David Mwantika aliyesajiliwa Azam FC.
Hata hivyo, nayo imejiimarisha katika usajili wa dirisha dogo, baada ya kusajili wapya wawili, akiwemo mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Emmanuel Gabriel na Mohamed Kayi, ambao wote ni huru.
Prisons ilianza kujifua kwa ajili ya mzunguko wa pili tangu Desemba mwaka jana na imepata mechi kadhaa za kujipima nguvu, hadi za ugenini ikiwemo ya wiki hii dhidi ya Mtibwa Sugar huko Morogoro, ambako walifungwa 1-0 Manungu.
                                 P    W  D   L    GF GA GD Pts
11 TZ Prisons           13 3    5    5    8    12 -4  14
KOCHA: Jumanne Charles (Mzalendo)
Toto Africans
TOTO AFRICANS:
Wana Kishamapanda bado wapo katika wakati mgumu, kwani walimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu wakiwa katika nafasi ya 12, ambayo ni ndani ya nafasi tatu za kushuka Daraja.
Washukuru sana ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza, kwani umewainua kidogo, vinginevyo wangemaliza ligi hiyo vibaya zaidi.
Lakini hii ni timu ambayo inacheza kwa ushindani zaidi inapokutana na timu tishio, ila kwa timu ambao zinaonekana si tishio, Toto hufanya vibaya. Bila shaka kuna kudharau mechi, ambako ndiko kunawaponza na kama watabadilika mzunguko wa pili, wanaweza kufanya vizuri na kubaki Ligi Kuu.  Baada ya mapumziko mafupi, Toto walianza kujifua na kupata mechi kadhaa za kujipima nguvu na katika dirisha dogo, waliimarisha kikosi chao kwa kusajili wachezaji wapya wanne, ambao ni Donald Obimma, Exavery Muhollery, Mohamed Hussein na Ulugbe Odia.
                               P    W  D   L    GF GA GD Pts
12 Toto African       13 2    6    5    10 15 -5  12
KOCHA: John Tegete (Mzalendo)
African Lyon
AFRICAN LYON:
African Lyon, ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya 13 kwa pointi zalke tisa. Licha ya kunolewa na kocha Muargentina, Pablo Ignacio Velez, lakini Lyon walikuwa vibonde tu mzunguko wa kwanza.
Mmiliki wa timu hiyo, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ amejitahidi kuboresha kikosi kwa kusajili wachezaji wapya wa kuongeza nguvu, ingawa si wale alioahidi Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa wa Simba na Mbuyu Twite wa Yanga.
Katika dirisha dogo, Zamunda amemudu kuwasajili Obadi Mungusa, Juma Seif, Yusuf Mgwao wote huru, Ibrahim Job na Shamte Ally wote kwa mkopo kutoka Yanga SC, Buya Jamwaka, Takang Valentine, Nurdin Mussa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na Jarufu Kizombi huru pia.
Aidha, Mmarekani huyo mwenye asili ya Tanzania, pia amemtupia virago kocha kocha Pablo Ignacio Velez na kwa sasa timu itakuwa chini ya Mkurugenzi wa Ufundi, Mkenya Charles Otieno. Lyon imekuwa ikijifua kwenye Uwanja wa TCC, Chang’ombe tangu Desemba mwaka jana, baada ya mapumziko mafupi.
                               P    W  D   L    GF GA GD Pts
13 African Lyon       13 2    3    8    9    20 -11 9
KOCHA: Pablo Ignacio Velez (Argentina)
Polisi Morogoro
POLISI MOROGORO:
Imerejea Ligi Kuu msimu huu, lakini haitakuwa ajabu mwishoni mwa msimu ikarudi tena kucheza Ligi Daraja la kwanza. Timu ya Morogoro, ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inashika mkia. Polisi haijashinda mechi hata moja zaidi ya kutoa sare nne na kufungwa mechi nyingine tisa.
Sijui maajabu gani yatokee, msimu ujao tuendelee kuwa na timu ya Morogoro, kwani kulingana na ushindani wa Ligi Kuu msimu huu, hakuna dalili za Polisi kupona. Lakini hakuna linaloshindikana, timu hiyo inaonekana kufanyia kazi suala hilo na imeboresha kikosi kwa kusajili wachezaji kadhaa wenye uzoefu wa Ligi Kuu wainusuru timu, ingawa bahati mbaya kwao, wamepoteza kocha wao John Simkoko.
Katika dirisha dogo, Polisi Moro imewasajili Shukuru Kassim, Chacha Marwa, Salum Machaku, Mzamiru Said, Victor Bundala, Delta Thomas, Edward Mzeru na Tizzo Chomba.
                               P    W  D   L    GF GA GD Pts
14 Polisi Moro         13 0    4    9    4    16 -12 4
KOCHA: adolph rishard  (Mzalendo)
Brian Omony aliyetua Azam kutoka Uganda 
WALIOINGIA DIRISHA DOGO LIGI KUU BARA:
Yanga SC; Kabange Twite (APR, Rwanda/FC Lupopo DRC)
Coastal FC; Shabani Kado (Kutoka Mtibwa Sugar/Yanga SC) Rashid Simba, Zuberi Hamisi, Shaongwe Ramadhan, Castory Mumbara, Tinashe Machemedze (Huru).
Azam FC; Humphrey Mieno (Kenya), Brian Umony (Uganda), Jockins Atudo(Kenya), David Mwantika(Prisons), Abdallah Seif (Ruvu Shooting), Malika Ndeule (Mtibwa Sugar) na Uhuru Selemani (mkopo, Simba SC).
Ruvu Shooting; Juma Mdindi, Njaidi Mohamed na Mahmoud Mbulu (Huru),
Prisons; Mohamed Kayi na Emmanuel Gabriel (Huru).
JKT Oljoro; Nurdin Selemani, Shaibu Nayopa, Hamidu Hassan, Paul Malipesa, Josephat Moses, Muharami Mnyangamala, Majaliwa Mbaga na Alphonce Peter (Huru)
Polisi Moro; Shukuru Kassim, Chacha Marwa, Salum Machaku, Mzamiru Said, Victor Bundala, Delta Thomas, Edward Mzeru na Tizzo Chomba (Huru)
Kagera Sugar; Edmund Kashamila na Julius Mrope (Huru).
Mtibwa Sugar; Rajab Mohamed, Zakayo Joseph, Baraka Anthony na Mussa Chambo (Huru)
JKT Ruvu; Zahoro Pazi (mkopo, Azam), Emmanuel Linjechele, Kisimba Luambano na Nashon Naftali (Huru)
Mgambo JKT; Moaka Shabani, Ismail Mkaima na Damas Milanzi (Huru)
Toto Africans; Donald Obimma, Exavery Muhollery, Mohamed Hussein na Ulugbe Odia (Huru).
African Lyon; Obadi Mungusa, Juma Seif, Yusuf Mgwao (Huru), Ibrahim Job (mkopo, Yanga SC) Shamte Ally(mkopo, Yanga SC), Buya Jamwaka, Takang Valentine, Nurdin Mussa, Salvatory Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na Jarufu Kizombi (Huru)
Simba SC; Mussa Mudde (Uganda) na Abel Dhaila (Uganda).
Kipa Abbel Dhaira kulia akibadilishana mikataba na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe kushoto