Saturday, October 13, 2012


SIMBA YAPUNGUZWA KASI MKWAKWANI

Kiungo wa Coastal aliyeruka juu kumdhibiti mshambuliajin wa Simba, Jerry Santo


SIMBA SC imepunguzwa kasi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni hii, baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Cosatal Union iliyomaliza pungufu ya mchezaji mmoja, baada ya mshambuliaji wake, Nsa Job Mahenya kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 65, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Pamoja na sare hiyo, Simba imeendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 17, baada ya kucheza mechi saba, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 16, baada ya kuifunga Polisi Morogoro leo 1-0 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, bao pekee la Kipre Herman Tcheche dakika ya 54, hilo likiwa bao lake la nne msimu huu. Hata hivyo, Azam iko nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya Simba.
Simba ndiyo iliyouanza mchezo huo kwa kasi na kuwakimbiza Coastal kwa takriban dakika tano mfululizo na baada ya hapo mchezo ukawa wa pande zote mbili.
Hakukuwa na shambulizi la maana ndani ya dakika ya zote 45 za kipindi cha kwanza kutokana na uimara wa safu zote mbili za ulinzi za timu hizo.
Kipindi cha pili pia timu hizo zilishambuliana kwa zamu na hata baada ya Nsa Job kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano na refa Simon Mberwa kutoka Pwani aliyekuwa akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Abdallah Uhako wote kutoka Arusha.
Kocha Mserbia Milovan Cirkovick alifanya mabadiliko kwenye kikosi cha Simba leo, akiwaanzisha beki Pachal Ocheng badala ya Juma Nyosso, kiungo Haruon Chanongo badala ya Edward Christopher na mshambuliaji Daniel Akuffo badala ya Emmanuel Okwi ambaye yupo kwao Uganda kwa majukumu ya kitaifa.
Baada ya mchezo huo, Milovan pamoja na kujutia nafasi walizopoteza alisema hakuvutiwa na uchezaji wa timu yake leo na anadhani ilichangiwa na Uwanja mbaya, lakini kwa ujumla akaponda uchezaji wa Akuffo.
“Sikuvutiwa kabisa na Akuffo,”alisema Cirkovick ambaye alipongeza uchezaji wa Ochieng leo.
Milovan pia alisikitika kuwakosa wachezaji wake watatu nyota, Mrisho Ngassa, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ ambao ni wagonjwa na Okwi, aliyekwenda kuichezea timu ya taifa ya Uganda, dhidi ya Zambia kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani.
Kocha wa Coastal, Ahmad Morocco alipongeza vijana wake kwa kufuata maelekezo yake, lakini akasikitikia nafasi walizopoteza na kadi nyekundu ya Nsa kwamba viliwanyima ushindi.             
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; Juma Kaseja, Nassor Masud ‘Chollo’, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi ‘Boban’, Felix Sunzu, Daniel Akuffo/Salim Kinje na Haroun Chanongo/Uhuru Suleiman.
Coastal; Jackson Chove, Said Swedi, Juma Jabu, Mbwana Hamisi, Jamal Machelanga/Ismail Khamis, Jerry Santo, Mohamed Athumani/Daniel Lyanga, Selemani K Selemani, Atupele Green, Nsa Job Mahenya na Razack Khalfan/Lameck Mbonde.