Thursday, January 31, 2013

KATIKA UKURASA WA HABARI ZA KIMATAIFA>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>


KLABU ya Queens Park Rangers inakaribia kukamilisha uhamisho wa beki Christopher Samba kutoka klabu ya Anzhi Makhachkala baada ya kufikia makubaliano na mchezaji huyo kufaulu vipimo. Beki huyo wa zamani wa Blackburn mwenye umri wa miaka 28 amesajili kwa ada ya paundi milioni 12.5 ambapo atakuwa akipokea kitita cha paundi 100,000 kwa wiki ikiwemo posho na mambo mengine. Nyota huyo alithibitisha kufanyiwa vipimo vya afya jijini London katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter jana. Mbali na Samba lakini pia meneja wa QPR Harry Redknapp yuko mbioni kumfukuzia mshambuliaji wa klabu ya Stoke City Peter Crouch.
KAGAWA AITWA TENA JAPAN.
KIUNGO nyota wa klabu ya Manchester United, Shinji Kagawa ameitwa tena katika kikosi cha timu ya taifa ya Japan kitakachocheza mchezo wa kirafiki na Latvia Jumatano ijayo baada ya kupona na kurejea katika kiwango. Kagawa alikosa baadhi ya michezo ya nchi yake ukiwemo mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia ambao walipata ushindi mwembamba wa mabao 2-1 dhidi ya Oman Novemba mwaka jana kwasababu majeraha ya mguu aliyopata wakati anaichezea United. Kagawa alirejea katika kikosi cha United Desemba baada ya kupona na ameonyesha kurejea katika kiwango chake wakati timu yake hiyo ikiongoza Ligi Kuu nchini Uingereza kwa alama saba zaidi ya mahasimu wao Manchester City wanaoshika nafasi ya pili. Kocha wa Japan Alberto Zaccheroni amesema amekuwa akimfuatilia nyota huyo katika mechi alizocheza karibuni na ameshawishika kumuita tena kuimarisha kikosi chake baada ya kurejea katika kiwango chake.

ADEBAYOR AIPONDA CAF KUHUSU UWANJA WA MBOMBELA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Togo, Emmanuel Adebayor amewabwatukia Shirikisho la Soka la Barani Afrika na Kamati ya Maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon kwa hali mbaya ya Uwanja wa Mbombela uliopo jijini Nelspruit. Adebayor ambaye anacheza katika klabu ya Tottenham Hotspurs ya Uingereza aliulalamikia uwanja huo kuwa na mchanga na mabonde baada ya Togo kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambapo watacheza na Burkina Faso Jumapili. Mbali na Adebayor, nahodha wa timu ya taifa ya Zambia Christopher Katongo naye alilalakia uwanja huo mapema wiki hii akidai kuwa inafanya timu yake ishinde kucheza mchezo wake wa kupasiana kama walivyozoea. Adebayor alidai michuano ya Afcon ni mikubwa barani Afrika na dunia nzima wanaangalia hivyo kuwa na viwanja vya aina hiyo ni jambo la kusikitisha. Nyota huyo amesema CAF lazima litafutie ufumbuzi suala hilo haraka ili wasiitie doa michuano hiyo ambayo mpaka sasa inaendelea vyema.

NFF YAWAJAZA MAPESA WACHEZAJI SUPER EAGLES.

WACHEZAJI wa timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles wamepokea posho ya dola 30,000 kila mmoja kutoka kwa Shirikisho la Soka nchini humo-NFF baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon. Nigeria iliigaragaza Ethiopia kwa mabao 2-0 na kufanikiwa kusonga mbele pamoja na Burkina Faso katika Kundi na kuziacha Ethiopia pamoja na mabingwa watetezi wa michuano hiyo kuyaaga mashindano hayo. Nigeria imeshiriki Afcon mara 17 na kufanikiwa kuvuka hatua ya makundi mara 15 na sasa nchi hiyo itakwaana na Ivory Coast timu ambayo inapewa nafasi kubwa ya kunyakuwa taji la michuano hiyo. Pamoja na Ivory Coast kupewa nafasi kubwa lakini kocha Nigeria Steven Keshi amesema ameandaa mbinu madhubuti ya kupambana na wapinzani wao ili kuhakikisha wanasonga mbele kwenye michuano hiyo.

BWALYA ASIKITISHWA NA KUTOLEWA KWA ZAMBIA.

RAIS wa Shirikisho la Soka la Zambia, Kalusha Bwalya amesema amesikitishwa na matokeo ya timu ya taifa ya nchi hiyo yaliyopelekea kuvuliwa ubingwa wao katika hatua ya makundi ya michuano ya Mataifa ya Afrika inayoendelea. Zambia walilazimishwa sare ya bila ya kufungana na Burkina Faso katika mchezo wao wa mwisho wa kundi C uliochezwa katika Uwanja wa Mbombela na matokeo hayo yalishindwa kuwavusha kwenda robo fainali baada ya Nigeria kuifunga Ethiopia kwa mabao 2-0 kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo uliochezwa katika Uwanja wa Royal Bafokeng, Rustenburg. Kalusha aliuambia mtandao wa shirikisho hilo kuwa wachezaji wa timu hiyo inabidi wajilaumu wenyewe kwa kutolewa mapema kwasababu hakuna timu yoyote kwenye mashindano hayo iliyopata maandalizi mazuri kama wao. Kalusha ambaye aliwahi kuwa mchezaji nyota wan chi hiyo amesema waliiandaa timu kwa muda wa kutosha na mategemeo yao ilikuwa ni kufika mbali zaidi ikiwezekana kutetea taji hilo lakini imeshindikana. Kwasasa Kalusha amesema inabidi wasahau michuano hiyo na kuhakikisha wanajiandaa vyema zaidi ili waweze kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Brazil 2014.

No comments:

Post a Comment