KLABU ZASUBIRI FEDHA ZAO TRA ZICHEZE LIGI KUU
Klabu 14 ambazo timu zao zinashiriki
Ligi Kuu ya Vodacom zimesema hazitacheza hatua ya pili ya Ligi hiyo
inayotarajiwa kuanza Januari 26 mwakani hadi zitakaporejeshewa fedha zao
zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka kwenye moja
ya akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Novemba 23 mwaka huu, TRA kwa uwezo
ilionao kisheria iliielekeza benki ya NMB kuilipa fedha hizo (sh.
157,407,968) kutoka kwenye moja ya akaunti za TFF ikiwa ni Kodi ya Lipa
Kama Unavyopata (PAYE) kutoka kwenye mishahara ya waliokuwa makocha wa
timu za Taifa.
Serikali ndiyo inayolipa mishahara ya
makocha hao moja kwa moja kwenye akaunti zao, lakini ilikuwa haikati
PAYE kutoka kwenye mishahara hiyo, hivyo malimbikizo kufikia sh.
157,407,968.
TFF bado inaendelea na mazungumzo na
pande husika (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa upande
mmoja na TRA kwa upande mwingine) ili fedha hizo zirejeshwe kwani
zilitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu (kampuni ya Vodacom) kwa ajili ya
maandalizi ya timu hizo tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.
OFISA WA CAF KUTUA MWAKANI KUKAGUA VIWANJA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) litamtuma nchini ofisa wake Abbas Sendyowa kukagua viwanja na
hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa klabu kupata
leseni zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na Shirikisho
hilo.
Ofisa huyo kutoka Uganda atawasili
nchini Januari 7 mwakani ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo
Januari 14 mwakani na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.
Utekelezaji wa kazi yake nchini
utahusisha mwakilishi kutoka TFF, mwakilishi kutoka Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, mameneja wa viwanja husika na Ofisa
Usalama wa TFF.
NAZARIUS KILUNGEJA AONDOLEWA UCHAGUZI RUREFA
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) kumuondoa
Nazarius Kilungeja kugombea uenyekiti katika uchaguzi wa chama hicho.
Kutokana na uamuzi huo, Kamati ya
Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA kuendelea na
mchakato wa uchaguzi huo kama ilivyopangwa awali.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment