Monday, December 24, 2012

AZAM BINGWA KOMBE LA UHAI, NI FURAHA DABO DABO CHAMAZI


TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Azam, maarufu kama Azam Academy, imehitimisha wiki ya furaha kwa klabu hiyo, baada ya kunyakua ubingwa wa Kombe la Uhai, linaloshirikisha timu za vijana za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Azam Akademy imetwaa ubingwa huo, baada ya kushinda kwa penalti 3-1, kufuatia sare ya 2-2 na Coastal Union ya Tanga ndani ya dakika 120 za pambano kali na la kusisimua.
Ushindi wa Azam Academy, unakuja siku moja tu baada ya kaka zao, Azam FC kutwaa ubingwa wa Kombe la Hisani juzi mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa kuwafunga wenyeji Dragons FC kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
Juzi Azam walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kabla ya Dragons kusawazisha dakika ya 75 na katika mikwaju ya penalti, kipa Mwadini Ally alicheza mikwaju miwili ya Dragons, wakati Gaudence Mwaikimba, Himid Mao, Joackins Atudo na Samih Hajji Nuhu walifunga penalti za Azam.
Katika mchezo wa leo, Azam ilimenyana kiume na Coastal ambayo inaonekana kuinukia vizuri katika uwekezaji kwenye soka ya vijana kabla ya bingwa kupatikana kwa mikwaju ya penalti.  
Mapema asubuhi katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, Simba waliokuwa mabingwa watetezi, waliifunga 3-0 Mtibwa Sugar na kunyakua nafasi hiyo.
Aidha, Bakari Shime wa Coastal Union ametwaa tuzo ya Kocha bora, Mansur A. Mansur wa Coastal Union kipa bora, Ramadhan wa Simba aliyefunga mabao sita, ameibuka mfungaji bora, Ruvu Shooting timu yenye Nidhamu, Joseph Kimwaga wa Azam mchezaji bora na Isiaka Mwalile refa bora.

No comments:

Post a Comment