Saturday, October 6, 2012

AZAM YAIPUMULIA SIMBA NG'ADO KWA NG'ADO



Shujaa wa Azam leo; John Bocco
AZAM FC imeisogelea zaidi Simba kileleni mwa Ligi Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuifunga African Lyon bao 1-0 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
 
 
Azam ambayo ilimaliza mechi hiyo ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja, baada ya beki wake Samir hajji Nuhu kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 83 kwa kuonyeshwa kadi ya pili ya njano, imefikisha pointi 13 sawa mabingwa watetezi Simba, ambao wapo kileleni sasa kwa wastani wa mabao tu.
 
 
Hadi mapumziko, Azam walikuwa tayari mbele kwa bao hilo, lililotiwa kimiani na mfungaji bora wa Ligi Kuu, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ katika dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Hilo linakuwa bao lake la pili Adebayor msimu huu ndani ya mechi tano za Ligi Kuu, hali ambayo inaashiria kasi yake yake si ya kuridhisha msimu huu.
 
 
Kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Samir Hajji Nuhu, Aggrey Morris, Said Mourad, Ibrahim Mwaipopo/Salum Abubakar dk57, Jabir Aziz, Himid Mao/Abdulhalim Humud dk60, John Bocco ‘Adebayor’m, Kipre Tcheche na Abdi Kassim ‘Babbi’.  
 
 
Katika mchezo mwingine, wa leo wenyeji Ruvu Shooting wameifunga Coastal Union ya Tanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani, mabao yaliyotiwa kimiani na Hussein Sued dakika ya sita na Hassan Dilunga dakika ya 12.
 
 
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mabingwa watetezi na vinara wa ligi hiyo, Simba kuumana na Oljoro JKT kwenye  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati vibonde wa ligi hiyo, Mgambo Shooting watakuwa wenyeji wa vibonde wengine wa ligi hiyo, Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, wakati Toto Africans wataikaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Kirumba mjini Mwanza na Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
 
 
Kagera Sugar wataikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Jumatatu. Hadi sasa, mwenendo wa ligi unaonyesha ushindani ni kati ya mabingwa watetezi, Simba SC na washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam FC ambazo zinakabana kileleni.
 
 
Hali bado si nzuri kwa mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, Yanga SC ambayo inazidiwa pointi tano na mabingwa watetezi, Simba SC ambao pia ni wapinzani wao wa jadi.
 
 
Timu mbili kati ya tatu zilizopanda Ligi Kuu msimu huu JKT Mgambo na Polisi Morogoro ndizo zipo mkiani, wakati Prisons ndio inaonekana kuwa imara zaidi, kwani ipo nafasi ya tano katika msimamo huo.

P       W       D       L        GF     GA     GD     Pts
Simba SC             5          4          1          0          10       3          7          13
Azam FC             5          4          1          0          7          1          6          13
Yanga SC           5          2          2          1          8          6          2          8
Coastal             6          2          2          1          7          7          0          8
Mtibwa Sugar 4          2          1          1          6          3          3          7
Prisons              4          1          2          1          4          4          0          5
JKT Oljoro        4          1          3          1          4          3          1          6
Ruvu Shooting 6          2          0          4          8          10       -2        6
African Lyon   6          2          0          4          5          10       -5        6
Kagera Sugar4         1          1          2          4          4          0          4
Toto African   4          0          3          1          4          4          0          3
JKT Ruvu            4          1          0          3          3          10       -7        3
Polisi Moro       3          0          2          1          0          1          -1        2
JKT Mgambo     3          0          0          3          1          3          -2        0

No comments:

Post a Comment