MABAO YA DROGBA YALIVYOCHAFUA AMANI SENEGAL, DAKAR YANUKA MOSHI
MIAKA 13 TANGU KIFO CHA MWALIMU NYERERE MWENYE KADI NAMBA MOJA YANGA, WATANZANIA TUTAMKUMBUKA SANA
KADI namba moja ya uanachama wa klabu ya Yanga SC ya Dar es
Salaam, inadaiwa alipewa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye leo
anatimiza miaka 13 tangu kifo chake, Oktoba 14, mwaka 1999.
Wakati Mwalimu Nyerere anafariki dunia, mimi nilikuwa mwandishi
mchanga sana- wakati huo nipo kampuni ya Habari Corporation Limited, chini ya
wamiliki wake wa awali akina Jenerali Ulimwengu.
Aliyekuwa bosi wangu wakati huo, Kenny Manara, aliyekuwa Mhariri
wa gazeti DIMBA alinipa kazi ya kwenda Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru ulipowekwa
mwili wa marehemu kwa ajili ya kuagwa ili kuandika habari juu ya wanamichezo
waliojitokeza kuuaga mwili wa marehemu na kuchukua maoni yao.
Hakika nilijifunza mengi sana kupitia msiba huo kwa kusikia,
kuambiwa na kujionea. Miongoni mwa niliyoambiwa ni kwamba, Mwalimu Nyerere
ndiye alikuwa ana kadi namba moja ya Yanga SC na kadi namba mbili, alikuwa nayo
hayati Abeid Amaan Karume, rais wa zamani wa Zanzibar.
Sijabahatika kuiona ‘leja’ ya Yanga hadi leo tangu nisikie
habari hizo, kwa hivyo siwezi kusadiki, lakini kulingana na historia ya klabu
ya Yanga katika harakati za ukombozi wa taifa letu, siwezi kupinga hilo.
Nashukuru Mungu nikiwa Mwandishi wa Habari, nimewahi kufanya
kazi za kuandika habari katika tukio ambalo Mwalimu Nyerere alikuwepo.
Ilikuwa ni Aprili mwaka 1998 katika mechi ya mpira wa kikapu,
iliyoandaliwa maalum kusherehekea kuzaliwa kwake, Mwalimu Nyerere Uwanja wa Ndani
wa Taifa, kati ya Pazi na Don Bosco.
Nakumbuka siku hiyo, mtangazaji wa East Africa TV, Patrick Nyembele
alikuwa bado anacheza mpira wa kikapu na ndiye alikuwa Nahodha wa Pazi ambayo ilishinda
na kukabidhiwa na Kombe.
Mechi hiyo iliandaliwa na Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es
Salaam (DABA), likiwa wazo la aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa DABA, Fakhrudin Amijee.
Vyama vyote vya michezo vilialikwa kushiriki sherehe hiyo na
vilitoa zawadi mbalimbali kwa Mwalimu.
Bendi ya Varda Arts ilikuwepo kutumbuiza na ilimpigia wimbo
mzuri Mwalimu wa Happy Birth Day. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa Waziri wa Mambo
ya Ndani na Ushirikiano wa Kimataifa wakati huo, alikuwepo na ndiye aliyekuwa
amekaa meza kuu pamoja na Nyerere.
Nilifarijika sana siku hiyo kufanya kazi mbele ya baba wa
taifa na kwa kuwa pia nimefanya kazi mara kibao mbele ya marais waliomfuatia,
Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete, najivunia
sana hayo.
Nilimpenda Mwalimu Nyerere tangu nasoma shule ya msingi pale Mgulani,
Dar es Salaam na ninavutiwa sana na sera na misimamo yake enzi za uhai wake.
Sijui, nasema sijui kama bila ya Nyerere Tanzania ingekuwepo
na hata hiyo Tanganyika ingekuwaje. Sijui! Leo tunaishuhudia Tanzania ambayo
mambo mengi yaliyoonekana ya ajabu wakati wa Nyerere yamekuwa ya kawaida.
Rushwa, ukatili, unafiki, ulafi wa madaraka, ubifansi,
ukabila, udini, ufisadi na uzandiki haya si ya ajabu tena katika Tanzania ya
leo. Tena watu hawana aibu wala woga, wamekuwa jasiri wa uovu na hawamuogopi
hata Mungu.
Tuna kila sababu ya kumlilia Mwalimue Nyerere na kumkumbuka
sana leo akitimiza miaka 13, tangu kifo chake.
HUYU NDIYE NYERERE
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa rais wa kwanza wa
Tanzania. Alizaliwa Butiama, mkoani Mara pembezoni mwa Ziwa Nyanza Aprili, 13,
mwaka 1922. Alifariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999. Aliiongoza Tanzania tangu
mwaka 1961 hadi mwaka 1985.
Yeye ni mwasisi wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea. Kabla ya
kuingia kwenye siasa alikuwa ni mwalimu. Kazi hii ndiyo ilimpatia jina ambalo
lilimkaa maisha yake yote la ‘Mwalimu’.
Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao
wameacha madaraka kwa hiyari baada ya kutawala kwa muda mrefu.
Alipostaafu urais mwaka 1985 alirudi kijijini kwake Butiama
ambako aliendesha shughuli za kilimo. Aliendelea kuwa na athari kubwa katika
siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika kijiji
cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara, Tanzania (wakati ule: Tanganyika).
Alikuwa miongoni mwa watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa
kabila la Wazanaki. Alipokuwa mtoto Nyerere alichunga mifugo ya baba yake na
alipofikisha umri wa miaka 12 aliingia shule akitembea kilomita 30 hadi Musoma.
Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusoma shule ya Wamisionari
Wakatoliki huko Tabora. Katika umri wa miaka 20 alibatizwa akawa mkristo
Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.
Mapadri wakaona akili yake wakamsaidia kusomea Ualimu katika
Chuo Kikuu cha Uganda, Makerere kilichopo Kampala, kuanzia mwaka 1943 hadi
1945.
Akiwa Makerere, Mwalimu akaanzisha tawi la Umoja wa Wanafunzi
Watanganyika pia amejihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA).
Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akifundisha shule ya
St.Mary´s. Mwaka 1949 alipata skolashipu ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha
Edinburgh huko, Scotland ambako alisoma M.A. ya historia na uchumi, akiweka rekodi
ya kuwa Mtanzania wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na Mtanzania
wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanzania.
Aliporejea Tanganyika kutoka masomoni, Nyerere alifundisha
Historia, Kingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis iliyo karibu na
Dar es Salaam.
Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Tanganyika
African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa
mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere.
Mwaka 1954 alikibadilisha chama cha TAA kwenda katika chama
cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi
kuliko TAA.
Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kilikuwa tayari chama cha
siasa kinachoongoza Tanganyika.
Uwezo wa Mwalimu Nyerere uliwashitua viongozi wa kikoloni na
kumlazimisha Nyerere kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Nyerere
alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati
mbaya.
Alijiuzuru ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza
na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika mapigano ya uhuru.
Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship council
na Fourth committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York. Uwezo wake wa
kimaongezi na kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru
bila umwagaji wa damu. Ushirikiano mzuri aliouonyesha aliyekuwa gavana wa
wakati huo bwana Richard Turnbull ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa
uhuru.
Nyerere aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na
kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1960. Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru
wake na Desemba 9, 1961 na Nyerere alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika
huru na mwaka mmoja baadae Nyerere alikuwa raisi wa kwanza wa Jamhuri ya
Tanganyika.
Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika
na Zanzibar kutengeneza Tanzania baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964
yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah.
Februari 5, mwaka 1977 aliongoza chama cha TANU katika tendo
la kuungana na chama tawala cha Zanzibar ASP na kuanzisha chama kipya cha CCM
(Chama cha Mapinduzi) akiwa Mwenyekiti wake.
Nyerere aliendelea kuongoza Taifa hadi 1985 alipomwachia
nafasi rais wa pili Ali Hassan Mwinyi. Aliendelea kuongoza Chama cha CCM hadi
1990 na kuwa na hadhi kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
Inasadikika kuwa Nyerere alishawishi uteuzi wa Benjamini
W.Mkapa kama mgombea wa rais wa mwaka 1995 na ambaye aliteuliwa kuwa rais
kwenye uchaguzi wa mwaka 1995.
Nyerere alikaa muda mwingi kwake Butiama akilima shamba lake.
Pamoja na haya alianzisha taasisi yenye jina lake; mwaka 1996 alionekana akiwa mpatanishi
wa pande mbalimbali wa vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi.
SIASA ZA UJAMAA NA KUJITEMEA…
Baada ya kuona kuwa uchumi wa Tanzania hautaweza kusimama kwa
siasa za kijamaa na kutoweza kuvumilia kuendesha nchi kwa siasa ambazo yeye
hakuwa muumini, Nyerere kwa maamuzi yake mwenyewe aliamua kustaafu nafasi ya urais
baada ya uchaguzi wa mwaka 1985 na kumwachia usukani Ali Hassan Mwinyi
aliyetawala kwa siasa za uchumi wa soko huria.
Katika hali ya kukubali ukweli, Nyerere alitamka katika
tafrija ya kumuaga juu ya siasa yake kiuchumi “Nimefeli. Tukubali hivyo.”
Wapo ambao wanamlaumu Mwalimu Nyerere kwa siasa zake za ujamaa
kwa madai zilichelewesha maendeleo ya kiuchumi wa Tanzania.
Mwalimu bado anakumbukwa na Watanzania hasa wa hali ya chini
kutokana na sera zake za kujali utu na ubinadamu na pia ataendelea kukumbukwa
na Waafrika kote barani hasa kwa mchango wake mkubwa wakati wa harakati za
kupigania uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika.
Ni mmoja wa viongozi wachache wanaokumbukwa kwa
kutojilimbikizia mali pamoja na kutawala kwa miaka zaidi ya 24.
Mwishoni mwa maisha yake Nyerere aliishi kama mkulima wa
kawaida kijijini kwake Butiama, ingawa wakati mwingine alikuwa akija kwenye
nyumba yake ya Msasani, Dar es Salaam.
Alipatwa na kansa ya damu (leukemia) na kufariki dunia nchini
Uingereza wakati wa kutibiwa katika mji wa London Oktoba 14, 1999. Alizikwa
mahali pale alipozaliwa, kijiji cha Butiama.
Ni miaka 13 leo tangu, mwenye kadi namba moja ya Yanga afariki
dunia, Watanzania bado tunamkumbuka na kumlilia.
MASHALI ULINGONI NA MGANDA LEO MANZESE
Kushoto ni Thomas Mashali wa Tanzamia na kulia ni Sebyala Med wa Uganda wakiwa na rais wa ECAPBA Onesmo Ngowi wakati wa kupima uzito jana |
MAGDALENA NDIYE TOP MODEL MISS TANZANIA 2012
Top 5 |
Mshindi wa Top Model Miss Tanzania 2012,Magdalena Roy |
MISS Dar City Center ambaye pia alishika nafasi ya pili
katika shindano la Miss ilala, Magdalena Roy amefanikiwa kuingia 15 Bora ya Miss
Tanzania baada ya juzi usiku kufanikiwa kutwaa taji la Top Model.
Magdalena anakuwa mshindi wa pili kuingia katika hatua hiyo,
akiungana na Miss Mbulu, Lucye Stephano ambaye wiki iliyopita alitwaa taji la
Miss Photogenic.
Katika shindano la Top Model lililofanyika kwenye hoteli ya
Naura Spring, mjini hapa lilikuwa na upinzani mkali kutoka kwa washiriki wote
wa Miss Tanzania.
Mbali na Magdalena warembo wengine waliofanikiwa kuingia
katika tano bora walikuwa ni Mary Chizi (Ilala), Irene Veda (Lindi), Belinda
Mbogo (Dodoma) na Sina Revocatus (Elimu ya Juu).
Warembo hao jana waliondoka kuelekea Tanga kwa ajili ya
kutembelea mapango ya Amboni, kabla ya kurejea Dar es Salaam.
Warembo wapatao 30 wanawania taji la Miss Tanzania, ambalo
kwa sasa linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake
cha Redd’s Original.
MILOVAN AKIKASIRIKA HASIKILIZI LA MTU, MTAZAME HANS POPPE SASA...
Vigogo wa SimbaSC
|
|
Mwenyekiti wa Friends Of Simba, Zacharia Hans Poppe kulia akijadiliana na wenzake wakati wa mchezo wa jana wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. timu hizo zilitoka 0-0. |
KOMBE la DUNIA: Higuain hatihati kucheza na Chile
>>ARGENTINA kileleni huko Marekani ya Kusini!!
Straika
wa Real Madrid Gonzalo Higuain ameumia mguu na yupo kwenye hatihati
kama atachea Mechi ya Mchujo Kanda ya Marekani ya kuwania kucheza
Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014 huko Brazil hapo Jumatano dhidi
ya Chile baada ya kupata majeruhi hayo kwenye Mechi ya Ijumaa ambayo
Nchi yake Argentina iliifunga Uruguay bao 3-0.
Katika Mechi hiyo bao za Argentina zilifungwa na Lionel Messi, bao mbili, na Sergio Aguero.
Hadi sasa Argentina ndio wapo kileleni
mwa Kundi hilo wakiwa na Pointi 17 kwa Mechi 8 na wapinzani wao wa
Jumatano, Chile, wapo nafasi ya 5 wakiwa Pointi 5 nyuma yao.
========================
MATOKEO:
Jumamosi Oktoba 13
Ecuador 3 Chile 1
Argentina 3 Uruguay 0
Ijumaa Oktoba 12
Bolivia 1 Peru 1
Colombia 2 Paraguay 0
RATIBA:
Jumatano Oktoba 17
Bolivia v Uruguay
Venezuela v Ecuador
Paraguay v Peru
Chile v Argentina
MSIMAMO KANDA ya NCHI za MAREKANI ya KUSINI:
Timu zote zimecheza Mechi 8
1 Argentina Pointi 17
2 Colombia 16
3 Ecuador 16
4 Uruguay 12
5 Chile 12
6 Venezuela 11
7 Peru 8
8 Bolivia 5
9 Paraguay 4
No comments:
Post a Comment