HAKUNA UFISADI KATIKA USAJILI SIMBA, HANS POPPE AKANUSHA MADAI YA MRWANDA
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe kushoto akimkabidhi jezi ya Simba Daniel Akuffo baada ya kusajiliwa. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu' |
SIMBA SC imesema kwamba hakuna ‘ufisadi’ wa aina yoyote
katika zoezi la usajili katika klabu hiyo kutokana na utaratibu mzuri uliowekwa
na mshambuliaji Danny Mrwanda aliachwa kwa sababu ya dau kubwa alilotaka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe
amekanusha kwa nguvu zote madai kwamba wachezaji huombwa ‘twenty percent’ ili
kusajiliwa na kusistiza kwamba Mrwanda alishindana na klabu hiyo ndiyo maana
akaachwa.
“Alitaka dau kubwa, baadaye akakubali dau tulilotaka kumpa,
baadaye tena ajaka anatutajia timu nyingine inamtaka, sisi tukamuambia basi
nenda kwenye hiyo timu nyingine, ndivyo tulivyoachana naye huyo bwana,”alisema Hans
Poppe.
Mrwanda alijiunga tena na Simba na Juni mwaka huu, akitokea
Vietnam alipokuwa anacheza soka ya kulipwa, lakini baada ya michuano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu akatemwa.
Baada ya kutemwa Mrwanda, akasajiliwa mshambuliaji Daniel
Akuffo kutoka Ghana ambaye hata hivyo, kocha Mserbia Milovan Cirkovick haridhishwi
na uwezo wake.
Mrwanda aliwahi kumzungumzia Akuffo na kusema tatizo ni
twenty percent, jambo ambalo sasa Hans Poppe anakanusha. LIGI DARAJA LA KWANZA YAANZA OKTOBA 24, MAJIMAJI, ASHANTI ZARUDI KIVINGINE
LIGI Daraja la Kwanza Tanzania Bara inatarajiwa kuanza rasmi
Oktoba 24, mwaka huu kwa timu 18 kati ya 24 kujitupa kwenye viwanja tisa
tofauti katika ligi hiyo inayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface
Wambura amesema leo kwamba Mechi za raundi ya kwanza za kundi A
zitakazochezwa Oktoba 24 mwaka huu ni Burkina Faso dhidi ya Mbeya City
(Jamhuri, Morogoro), Mlale JKT na Small Kids (Majimaji, Songea) na Kurugenzi
Mufindi dhidi ya Majimaji (Uwanja wa Wambi, Mufindi mkoani Iringa).
Amesema Mkamba Rangers na Polisi Iringa zitakamilisha raundi
ya kwanza kwa kundi hilo Oktoba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro, wakati mechi za raundi ya pili kwa kundi hilo zitachezwa Oktoba 27
mwaka huu kwa Polisi Iringa vs Mbeya City (Samora, Iringa), Majimaji vs Small
Kids (Majimaji, Songea), Burkina Faso vs Mkamba Rangers (Jamhuri, Morogoro) na
Kurugenzi Mufindi vs Mlale JKT (Wambi, Mufindi).
Amesema raundi ya tatu ni Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati
ya Mbeya City vs Mlale JKT (Sokoine, Mbeya), Small Kids vs Mkamba Rangers
(Nelson Mandela, Sumbawanga), Majimaji vs Burkina Faso (Majimaji, Songea) na
Polisi Iringa vs Kurugenzi Mufindi (Samora, Iringa).
Amezitaja timu za Kundi B ambazo zitamenyana Oktoba 24, mwaka
huu ni Ndanda vs Transit Camp (Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara), Villa
Squad vs Moro United (Mabatini, Pwani) wakati Oktoba 25 mwaka huu ni Green
Warriors vs Tessema (Mabatini, Pwani) na Polisi Dar es Salaam vs Ashanti United
(Chamazi, Dar es Salaam).
Amesema raundi ya pili kwa kundi hilo ni Oktoba 27, mwaka huu
Ndanda vs Green Warriors (Nangwanda Sijaona, Mtwara), Villa Squad vs Tessema
(Mabatini, Pwani) wakati Oktoba 28 mwaka huu ni Ashanti United vs Transit Camp
(Mabatini, Pwani) na Oktoba 29 mwaka huu ni Moro United vs Polisi Dar es Salaam
(Chamazi, Dar es Salaam).
Amesema Novemba 1, mwaka huu Green Warriors itamenyana na
Ashanti United (Mabatini, Pwani), Novemba 2 mwaka huu ni Polisi Dar es Salaam
vs Villa Squad (Chamazi, Dar es Salaam), Novemba 4 mwaka huu ni Tessema vs
Ndanda (Chamazi, Dar es Salaam) na Transit Camp vs Moro United (Mabatini,
Pwani).
Amesema Kundi C nalo ambalo mechi zake zitachezwa Oktoba 24,
mwaka huu ni kati ya Kanembwa FC vs Polisi Dodoma (Lake Tanganyika, Kigoma),
Mwadui vs Morani (Kambarage, Shinyanga), Pamba vs Polisi Mara (Kirumba, Mwanza)
na Rhino Rangers vs Polisi Tabora (Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Amesema Raundi ya pili ni Oktoba 27 mwaka huu; Polisi Tabora
vs Polisi Dodoma (Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mwadui vs Polisi Mara (Kambarage,
Shinyanga), Kanembwa FC vs Morani (Lake Tanganyika, Kigoma) na Pamba vs Rhino
Rangers (Kirumba, Mwanza), wakati Oktoba 31 mwaka huu ni raundi ya tatu; Polisi
Mara vs Rhino Rangers (Karume, Musoma), Morani vs Polisi Tabora (Kiteto,
Manyara), Polisi Dodoma vs Pamba (Jamhuri, Dodoma) na Kanembwa FC vs Mwadui
(Lake Tanganyika, Kigoma).
MBAGA AZICHEZESHA KENYA, BAFANA BAFANA
Oden Mbaga kulia akimuonya Haruna Moshi 'Boban' wakati wa mechi kati ya Taifa Stars na Malawi, Mei 26, mwaka huu. Kulia ni kiungo wa The Flames, James Sangala aliyechezewa rafu na Haruna. |
REFA Oden Mbaga wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Soka
la Kimataifa (FIFA) ndiye anayechezesha mechi ya kirafiki kati ya Kenya
(Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana Bafana).
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface
Wambura amesema leo kwamba mechi hiyo inachezwa leo Uwanja wa
Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Nairobi na Mbaga atasaidiwa na marefa
wasaidizi wa FIFA, John Kanyenye kutoka Mbeya na Erasmo Jesse wa Morogoro.
Amesema TFF imeteua marefa hao baada ya kupata maombi kutoka
kwa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) ambao ndiyo waandaaji wa mechi hiyo ambayo
ni moja ya vipimo kwa kocha mpya wa Harambee Stars, Henry Michel kutoka
Ufaransa.
Wakati huo huo: Wambura Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha
Makocha wa Soka Tanzania (TAFCA) imeongeza muda kwa wagombea kuchukua fomu kwa
ajili ya uchaguzi wa chama hicho ambao sasa utafanyika Novemba 25 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA,
Ramadhan Mambosasa, jana ndiyo ilikuwa mwisho wa kuchukua fomu lakini mwitikio
wa wagombea bado umekuwa mdogo ambapo ni watano tu waliojitokeza.
Hivyo, amesema wameongeza muda wa kuchukua na kurudisha fomu
ambapo mwisho itakuwa ni Oktoba 19 mwaka huu saa 10 kamili alasiri. Fomu
zinapatikana ofisi za TAFCA ambazo ziko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam.
Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu
Mkuu, Katibu Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Mhazini na wajumbe watatu
wa Kamati ya Utendaji.
NGASSA AANZA KUJIFUA NA SIMBA, LAKINI ASEMA HALI YAKE BADO TETE
Ngassa |
MRISHO
Khalfan Ngassa ameanza mazoeizi jana timu yake Simba SC kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam, lakini amesema bado
hayuko sawa sawa, maana yake uwezekano wa kucheza mechi ya kesho dhidi ya timu
yake ya zamani, Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni mdogo.
Akizungumzajana, Ngassa ambaye aliugua Malaria baada ya mechi dhidi ya
Yanga, Oktoba 3, mwaka huu alisema kwamba bado anahisi hana nguvu.
“Nimeanza
mazoezi na timu, lakini hata hivyo bado hali yangu haiko sawa sawa kwa kweli,
najisikia mwili hauna nguvu, hii Malaria ilinipelekesha sana, ila najikongoza
hivyo hivyo,”alisema Ngassa.
Kiungo
mwingine wa Simba SC aliyekuwa anaumwa Malaria, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ naye
ameanza mazoezi na timu na anaweza kucheza kesho.
Mbali na
Redondo, katika mchezo huo, Simba inatarajiwa kuwapokea wachezaji wake wengine watatu
iliyowakosa kwenye mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union Jumamosi Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana, Emmanuel Okwi
aliyekuwa kwao Uganda kuichezea timu yake ya taifa, Komabil Keita, Haruna
Shamte na Kiggi Makasy waliokuwa majeruhi.
Mechi
nyingine za kesho zitakuwa kati ya Prisons na Azam FC kwenye Uwanja wa Sokoine,
Mbeya, Polisi Morogoro na JKT Ruvu Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Mgambo JKT na
Toto Africans Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na JKT Oljoro dhidi ya African Lyon
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Simba bado
ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 17, baada ya kucheza mechi saba,
ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, ambayo hata hivyo imecheza mechi sita,
wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza mechi
saba pia.
YANGA SC SASA KUINGIA KAMBINI LEO BAADA YA KUKWAMA JANA
Wachezaji wa Yanga wakipasha |
KIKOSI cha Yanga
kinatarajiwa kuingia kambini leo katika hoteli ya Uppland, Changanyikeni, Dar
es Salaam kujiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga
ilikwama kuingia kambini jana ilivyopanga na badala yake sasa wataingia leo
Changanyikeni, ili kuziweka fikra za wachezaji pamoja kuelekea mechi hiyo ya
Jumamosi.
Habari njema ni kwamba, beki Kevin Yondan jana alianza
mazoezi mepesi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam, ikiwa ni
mara ya kwanza tangu agongwe na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika
mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu.
Pamoja na Yondan, mshambuliaji Said Bahanuzi aliyekuwa
anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja naye alianza pia mazoezi mepesi jana kwenye
Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam.
Bahanuzi
‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba
Jumatatu wiki iliyopita.
Bahanuzi aliumia
dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na
kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika
mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi
ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo
akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo
ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka.
Yanga kwa
sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11,
baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba
iliyocheza mechi saba pia, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 17, ikifuatiwa
na Azam FC yenye pointi 16, iliyocheza mechi sita.
AZAM FC KUIONJA SOKOINE LEO
Azam FC |
AZAM FC leo jioni
watafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, ili kuuzoea kabla ya
mechi ya kesho dhidi ya wenyeji, Prisons katika mfululizo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara.
Mabingwa hao
wa Kombe la Mapinduzi na washindi wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame wapo mjini Mbeya tangu juzi saa 1:00 usiku na jana
walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Iyunga mjini humo.
Kikosi kizima
cha Azam kipo vizuri kuelekea mchezo unaitarajiwa kuwa mgumu kwao na wachezaji
wa morali ya ushindi, ili kuweka vizuri mazingira ya kutwaa taji la kwanza la
ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara.
Azam
waliondoka Morogoro juzi asubuhi baada ya mechi yao na Polisi kwenye Uwanja, Jamhuri
Jumamosi ambayo walishinda 1-0, bao pekee la mshambuliaji kutoka Ivory Coast,
Kipre Herman Tchetche.
Mbeya ni
kati ya vituo ambavyo vinawaogopesha vigogo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, Azam, Simba na Yanga kutokana na imani kwamba Prisons haifungiki kwenye
Uwanja wake.
Sababu kubwa
ni ubovu wa Uwanja wa Sokoine, ambao wenyewe Prisons wameuzoea na wanaujulia,
wakati timu nyingine hupata tabu mno.
Kati ya
vigogo hao watatu, ambao wanafukuzana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu, Azam inakuwa
timu ya pili kwenda Mbeya, baada ya Yanga iliyolazimishwa sare ya bila
kufungana na Wajelajela hao kwenye mechi yao ya kwanza ya ligi hiyo.
Simba
imeanzia Dar es Salaam kucheza na Prisons, Septemba 29, mwaka huu katika mechi
ambayo walishinda kwa taabu mabao 2-1 na sasa watarudiana na Wajelajela hao
mjini Mbeya katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo.
Mikoa
mingine tishio ni Kanda ya Ziwa, ambako Azam tayari imekwishamaliza na
kukusanya pointi nne baa ya kuifunga 1-0 Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba kabla
ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Yanga pia
imemaliza deni la Kanda ya Ziwa, ikiambulia pointi tatu, baada ya kufungwa 1-0
na Kagera na kushinda 3-1 dhidi ya Toto. KATIBU MKUU Osiah atoa Taarifa kuhusu Chaguzi za Wanachama wa TFF
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana Oktoba 11, 2012 kujadili
michakato ya chaguzi mbalimbali za wanachama wa Shirikisho. Katika kikao
chake, Kamati ilijadili michakato ya chaguzi za viongozi wa Chama cha
Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Chama cha Waamuzi wa Mpira wa
Miguu (FRAT), Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA)
na Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Dar es salaam (DRFA),.
Pia Kamati ilijadili mchakato wa chaguzi
za Chama cha Madaktari wa Michezo (TASMA) na kupokea mchakato wa Chama
cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Mbeya (MRFA).
Baada ya kujadili chaguzi hizo kwa kina, Kamati ilifikia uamuzi ufuatao:
1. FRAT
Uchaguzi
wa FRAT haukufanyika baada ya wajumbe kugoma wakipinga kuondolewa kwa
baadhi ya wagombea. Kamati ilikubaliana kuiagiza Kamati ya Uchaguzi ya
FRAT kuhakikisha uchaguzi unafanyika Novemba 17, 2012 na kufanya
maandalizi yote muhimu ikiwa ni pamoja na sehemu ambako uchaguzi huo
utafanyika. Mkutano utatakiwa kuwapigia kura wajumbe waliopitishwa
kugombea uongozi tu.
2. RUREFA
Baada ya
kufuta uchaguzi wa viongozi wa RUREFA na kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya
RUREFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitaka Kamati ya Utendaji ya RUREFA
kuteua kamati mpya ya uchaguzi ya chama hicho kabla ya Oktoba 20, 2012
na kuiagiza kamati mpya kuwa imeshatangaza mchakato wa uchaguzi ifikapo
Oktoba 24, 2012.
3. SHIREFA
Kamati ilipokea pingamizi dhidi ya
baadhi ya wagombea uongozi wa SHIREFA na hivyo kuagiza walioweka
pingamizi na waliowekewa pingamizi pamoja na mwakilishi wa Kamati ya
Uchaguzi ya SHIREFA kuhudhuria kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF
kitakachofanyika Alhamisi ya Oktoba 18, 2012 kwa ajili ya maamuzi ya
mwisho.
4. MRFA
Kamati ilipokea rufaa na pingamizi
kutoka kwa baadhi ya wagombea walioenguliwa kuwania uongozi wa chama
hicho na hivyo imewataka walioweka pingamizi na waliokata rufaa
kuhudhuria kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Oktoba
18, 2012 jijini Dar es salaam.
5. TASMA
Kamati iliona mapungufu katika mchakato
wa uchaguzi wa viongozi wa TASMA na kuamua chama hicho kifanye uchaguzi
ifikapo Desemba mosi badala ya uchaguzi kufanyika Oktoba 27, 2012 kama
ilivyokuwa imepangwa awali. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaiagiza Kamati
ya Uchaguzi ya TASMA kuhakikisha kasoro zilizojitokeza zinarekebishwa
ili uchaguzi ufanyike kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na Kanuni za
Uchaguzi.
6. DRFA
Awali, Kamati ya Uchaguzi ya TFF
ilitangaza kuwa hatma ya uchaguzi wa DRFA itajulikana baada ya kikao cha
leo, lakini kutokana na wajumbe kutoweza kuhudhuria kwa sababu tofauti,
mustakabali wa suala hilo sasa utajulikana baada ya kikao cha Oktoba
18, 2012.
Wagombea na wadau wanaotakiwa kuhudhuria
kikao cha Oktoba 18, 2012 wanataarifiwa kuwa kikao hicho kitafanyika
kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za TFF kuanzia saa 08:2012.
Kamati inawaomba wajumbe wote kuhudhuria bila ya kukosa.
Angetile Osiah
Katibu Mkuu TFF
TAFCA YAONGEZA MUDA WA KUCHUKUA FOMU
Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha
wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) imeongeza muda kwa wagombea kuchukua
fomu kwa ajili ya uchaguzi wa chama hicho ambao sasa utafanyika Novemba
25 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, jana ndiyo ilikuwa mwisho wa
kuchukua fomu lakini mwitikio wa wagombea bado umekuwa mdogo ambapo ni
watano tu waliojitokeza.
Hivyo, amesema wameongeza muda wa
kuchukua na kurudisha fomu ambapo mwisho itakuwa ni Oktoba 19 mwaka huu
saa 10 kamili alasiri. Fomu zinapatikana ofisi za TAFCA ambazo ziko
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti,
Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu
wa TFF, Mhazini na wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji.
CAF yaitimua Senegal AFCON 2013!
>>IVORY COAST yathibitishwa Mshindi!!
LEO
Shirikisho la Soka Afrika, CAF, limetoa tamko rasmi la kuitoa nje ya
Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2013, Senegal kufuatia
vurugu zilizotokea kwenye Mechi ya majuzi Jumamosi ya marudiano ya
Raundi ya Mwisho ya Mtoano kuwania kuingia Fainali zitakazochezwa Afrika
Kusini Januari Mwakani na kusababisha Mechi kati yao na Ivory Coast
kuvunjika katika Dakika ya 72.
Hiyo Jumamosi, Ivory Coast walikuwa
wakiongoza kwa bao 2-0 katika Mechi iliyochezwa Stade Leopold Senghor na
kuwafanya waongoze kwa jumla ya bao 6-2 katika Mechi mbili lakini Mechi
hiyo ilivunjwa baada ya Mashabiki wa Senegal waliochukizwa kuwasha moto
Majukwaani na kurusha vitu Uwanjani.
CAF imethibitisha kuwa matokeo ya Mechi
hiyo yatabaki kama yalivyo, ikimaanisha Ivory Coast ndio watatinga
zitakazoanza Januari 19 Mwakani huko Afrika Kusini na Senegal kutupwa
nje.
Katika Taarifa yake, CAF imetamka: “CAF
imeamua kuthibitisha rasmi matokeo ya bao 2-0 kwa Ivory Coast…na
kuichukulia Senegal kuwa wameshindwa na kutolewa nje ya Mashindano na
hili halihusishwi na adhabu yeyote ambayo itatolewa na Bodi ya Nidhamu
ya CAF.”
Sheria za CAF ziko wazi kuwa: “Ikiwa
Refa atalazimika kuvunja pambano kabla ya muda wake kumalizika kwa
sababu ya uvamizi wa Uwanja au fujo dhidi ya Timu ngeni, Timu mwenyeji
ndio itahesabiwa imeshindwa na kutolewa nje ya Mashindano na hili
halihusiana na adhabu zinazostahili Kisheria.”
Tayari CAF imeshapanga mgawanyiko wa
Timu katika Vyungu vinne ambavyo vitatumika hapo Oktoba 24 kwenye Droo
ya kupanga Makundi manne ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika
zitakazochezwa huko Afrika Kusini kuanzia Tarehe 19 Januari 2013 hadi 10
Februari 2013.
++++++++++++++++++++++++++++++++
VYUNGU:
CHUNGU 1: South Africa, Zambia, Ghana, Ivory Coast
CHUNGU 2: Mali, Tunisia, Angola, Nigeria
CHUNGU 3: Algeria, Burkina Faso, Morocco, Niger
CHUNGU 4: Togo, Cape Verde, Congo DR, Ethiopia
FAHAMU: Kila Chungu kitatoa Timu moja ili kupata Makundi manne ya Timu 4 kila moja.
++++++++++++++++++++++++++++++++
Mgawanyo huu wa Vyungu umechukuliwa kwa
kutathmini matokeo ya kila Nchi katika Mashindano matatu yaliyopita ya
Kombe la Mataifa ya Afrika na si Ubora kwa mujibu wa Listi ya Ubora
Duniani ya FIFA.
MWESINGWA AOMBA RADHI KUFUATIA KUTOLEWA KWA CRANES.
The Cranes walifanikiwa kuwafunga Zambia maarufu kama Chipolopolo bao 1-0 katika muda wa kawaida mwishoni mwa wiki iliyopita lakini waliotolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penati 8-9 baada ya kumaliza kwa sare.
Mwesigwa alikosa mojawapo ya penati mbili za Uganda huku Patrick Ochan naye akishuhudia penati yake ikizuiwa na kipa wa Chipolopolo Kennedy Mweene na kuwafanya mabingwa hao wa Afrika kukata tiketi ya kwenda kutetea kombe lao katika michuano hiyo.
Mwesingwa amesema katika suala la upigaji penati hakuna mchezaji ambaye anaweza kutamba kwamba yeye ni mjuzi zaidi haswa mchezo kama ule hivyo kukosa kwake kuchukuliwe kama ni bahati mbaya na kuomba mashabiki kuendelea kuwaunga mkono kwa ajili ya ajili ya mashindano mengine yaliyopo mbele yao.
FSF YAMLAUMU DIOUF VURUGU ZA SENEGAL.
Senghor amesema kuwa mtu binafsi alinunua tiketi na kusisambaza kwa mashabiki wakorofi kwa madhumuni ya kuvuruga mchezo kati ya Senegal na Ivory Coast ambao ulikuwa ni mchezo wa pili wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kitendo ambacho kilifanikiwa kwani mchezohuo uliisha katika dakika ya 76 baada ya vurugu kuzuka.
Rais huyo aliendelea kusema kuwa wanaamini kuwa tukio hilo ni la hujuma na lilifanywa na mtu au kikundi cha watu ili kufuruga soka nchini humo. Kauli hiyo ya Senghor inakuwa kama inamlenga mshambuliaji nyota wa klabu ya Leeds United, El Hadji Diouf ambaye mapema Jumatatu alikiri kuwa FSF ilizuia tiketi zake 1,000 alizoagiza kwa ajili ya kusambaza kwa mashabiki wake kwa kuogopa nyota huyo anataka kuwapatia tiketi hizo wahuni ili wavuruge mchezo huo.
Kwa mujibu wa chanzo kilichikaribu na FSF, Diouf ndiye pekee aliyelipia tiketi nyingi zaidi katika mchezo huo ingawa mwenyewe amekunusha kuhusika katika kuchochea vurugu hizo
KIRAFIKi: Brazil yaibonda Japan 4-0!
>>NEYMAR apiga 2, Kaka 1, Paulinho 1
Brazil wamemaliza Ziara yao ya Ulaya kwa
kupiga jumla ya Bao 10-0 katika Mechi mbili baada ya leo kuibonda Japan
4-0 huko Stadion Miejski, Mjini Poznan, Poland kipigo ambacho kimekuja
baada ya Ijumaa kuifumua Iraq 6-0 huko Malmo, Sweden.
Kikosi cha Brazil, chini ya Kocha Mano
Mezes, hakikuwapa nafasi hata chembe Japan waliocheza mfumo usiokuwa na
Straika maalum na walimudu kuwapiga bao la kwanza katika Dakika ya 12
mfungaji akiwa Paulinho.
Neymar alipiga bao la pili katika Dakika
ya 25 kwa Penati na Kipindi cha Pili Neymar akapiga Bao la 3 na Mkongwe
Kaka akafunga Bao la 4.
Brazil wangeweza kupata Mabao zaidi baada ya Mashuti ya Kaka na Hulk kugonga mwamba.
Vikosi vilivyoanza:
Brazil (Mfumo 4-4-2): Diego Alves; Adriano, Silva, Luiz, Castan; Paulinho, Ramires, Kaka, Oscar; Neymar, Hulk.
Japan (Mfumo 4-3-3): Kawashima; Sakai, Konno, Yoshida, Nagatomo; Endo, Hasebe, Nakamura; Kiyotake, Kagawa, Honda
LEO Poland v England: Kocha Poland aionya England
>>HODGSON akiri LEWANDOWSKI ndie tishio kwao!!
>>POLAND wamwogopa ROONEY!!
Kocha wa Poland Waldemar Fornalik
ameionya England wasiidharau Poland licha ya rekodi na historia
kuwahukumu kwa kuifunga England mara moja tu-Mwaka 1974-kutoka sare mara
6 katika Mechi 17 zilizopita na leo Usiku Nchi hizo zinategemewa
kukutana Uwanja wa Kazimierz Gorski kwenye Mechi ya Kundi H la Barani
Ulaya kuwania kucheza huko Brazil Mwaka 2014 katika Fainali za Kombe la
Dunia.
+++++++++++++++++++++++
MSIMAMO:
KUNDI H
1 England Mechi 3 Pointi 7
2 Montenegro Mechi 2 Pointi 4
3 Poland Mechi 2 Pointi 4
4 Ukraine Mechi 2 Pointi 2
5 Moldova Mechi 3 Pointi 1
6 San Marino Mechi 2 Pointi 0
+++++++++++++++++++++++
Wakati Fornalik akitoa onyo hilo, Kocha wa England Roy Hodgson ametoboa kuwa kwa upande wao tishio kubwa litatoka kwa Straika hatari wa Mabingwa wa Germany, Borussia Dortmund, Robert Lewandoeski.
Akizungumzia mtanange huo, Fornalim
alisema: “Poland na England ni Mechi muhimu. Tunajua uwezo wao ni
kiwango cha juu lakini hata sie tuna thamani yetu.”
Katika Kundi H, Poland wamecheza Mechi 2 na kutoka 2-2 na Montenegro na kuifunga Moldova 2-0.
Leo Poland wataingia kwenye Mechi hii
bila Nahodha wao Kuba Blaszczykowski, ambae ni Kiungo wa Borussia
Dortmund, kwa kuwa ameumia enka na utepe wa Ukepteni umekwenda kwa Beki
wa Klabu ya Anderlecht, Marcin Wasilewski, Miaka 32, mwenye miguvu.
Akizungumzia Mechi hii, Marcin
Wasilewski amesema: “Siku zote Poland tunahusudu Soka la England.
Napenda kuitazama Ligi Kuu England na ilikuwa ndoto yangu kucheza huko.
Hatari kwetu toka kwao ni Wayne Rooney!”
VIKOSI VINATARAIWA:
Poland: Kuszczak; Perquis, Wasilewski, Wojtkowiak, Wawrzyniak; Borysiuk, Mierzejewski, Krychowiak, Wszolek; Lewandowski, Piech
England: Hart; Johnson, Cahill, Jagielka, Cole; Milner, Carrick, Gerrard, Oxlade-Chamberlain; Defoe, Rooney
RATIBA:
Jumanne Oktoba 16
[SAA za BONGO]
2145 Albania v Slovenia
2000 Andorra v Estonia
1900 Belarus v Georgia
2145 Belgium v Scotland
2100 Bosnia-Hercegovina v Lithuania
2100 Czech Republic v Bulgaria
2130 Hungary v Turkey
2130 Iceland v Switzerland
1900 Israel v Luxembourg
2000 Latvia v Liechtenstein
2130 Macedonia v Serbia
2245 Portugal v Northern Ireland
2100 Romania v Netherlands
1800 Russia v Azerbaijan
2130 San Marino v Moldova
2130 Slovakia v Greece
2200 Spain v France
2100 Ukraine v Montenegro
2100 Cyprus v Norway
2100 Faroe Islands v Rep of Ireland
2130 Austria v Kazakhstan
2100 Croatia v Wales
2145 Germany v Sweden
2145 Italy v Denmark
2200 Poland v England
FAHAMU:
-ULAYA yapo Makundi 9
-Washindi 9 wa kila Kundi
wataingia Fainali moja kwa moja na Washindi wa Pili 8 bora wenye rekodi
nzuri dhidi ya Timu zilizomaliza nafasi za Kwanza, Tatu, Nne na Tano
kwenye Kundi lao watapelekwa kwenye Droo kupanga Mechi 4 za Mchujo,
zitakazochezwa nyumbani na ugenini, ili kupata Timu nne zitakazoingia
Fainali.
BIN HAMMAM AIKATIA RUFANI FIFA, CAS.
Bin Hammam ambaye alichuana na Sepp Blatter katika kinyang’anyiro cha urais wa FIFA mwaka jana amefungiwa na shirikisho hilo Julai 26 mwaka huu ikiwa ni wiki moja baada ya CAS kutengua adhabu yake ya kufungiwa maisha kujishughulisha na masuala ya michezo.
Wakili wa Bin Hammam, Eugene Gulland katika taarifa yake alithibitisha kuwa mteja wake ambaye pia amewahi kuwa rais wa Shrikisho la Soka barani Asia-AFC ameamua kukata rufani kupinga adhabu hiyo aliyopewa na FIFA. Katika taarifa yake ya kutengua kifungo cha aisha cha Bin Hammam, CAS katika taarifa imesema kuwa FIFA walishindwa kuwasilisha ushahidi uliokamilika juu ya tuhuma kwamba aliwanunua maofisa wa soka wan chi za Carribean katika uchaguzi mwaka uliopita ingawa walimalizia kuwa uamuzi huo haumaanishi kwamba hakutenda kitendo hicho.
Bin Hammam alikuwa natuhumiwa kujaribu kuwanunua maofisa wa soka wa nchi za Caribbean ili waweze kumpigia kura kwa kuwapa bahasha zilizokuwa na kiasi cha dola 40,000 kila mmoja katika mkutano na viongozi hao uliofanyika nchini Hispania mwezi mmoja kabla ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment