Wednesday, January 23, 2013

SIMBA WANATARAJIA KUREJEA LEO DSM WAKITOKEA UGHAIBUNI WALIKOKUWA WAMEFUATA SUMU ZA LIGI KUU JUMAMOSI


Wachezaji wa Simba SC
MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba SC wanatarajiwa kurejea leo Dar es Salaam, baada ya ziara ya wiki mbili nchini Oman ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Baada ya kuwasili mchana wa leo, Simba wataingia moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Black Leopard ya Afrika Kusini, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Katika ziara yake ya Oman, Simba ilipata mechi tatu za kujipima nguvu na kushinda moja na kufungwa mbili.
Katika mchezo wake wa mwisho Jumamosi, Simba SC ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Ahly Sidab kwenye Uwanja wa Sidab mjini Muscat.
Katika mchezo huo, shujaa wa Simba, alikuwa ni kiungo aliyerudi juu kisoka hivi sasa, Amri Ramadhan Kiemba aliyeifungia timu hiyo bao la ushindi.
Katika mechi hiyo nzuri na ya kusisimua, wenyeji ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kipindi cha kwanza, lililofungwa na kiungo Mbrazil, aitwaye Lopez, kabla ya kiungo wa Simba, Kiggi Makassy kusawazisha kipindi hicho hicho cha kwanza.
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1 na leo Simba walicheza soka nzuri mno, huku wachezaji vijana, Miraj Adam, Abdallah Seseme, Haroun Chanongo na Shomari Kapombe waking’ara zaidi. 
Kipindi cha pili, kocha Mfaransa, Patrick Liewig alifanya mabadiliko, akiwaingiza Rashid Ismail, Marcel Kaheza wote waliopandishwa kutoka timu B na Kiemba ambao waliongeza makali ya Mnyama na hatimaye kupata ushindi huo.
Alikuwa ni kiungo wa zamani wa Kagera Sugar, Yanga SC, Miembeni na Moro United aliyeipatia Simba ushindi wa kwanza katika ziara yake ya Oman kwa kufunga bao safi la ushindi dakika za mwishoni.
Katika mechi nyingine, Simba ilifungwa 1-0 na U23 ya Oman na 3-1 na timu ya Jeshi la nchi hiyo, Qaboos, bao la Wekundu hao wa Msimbazi, likifungwa na Haruna Moshi ‘Boban’.  

No comments:

Post a Comment