Saturday, February 2, 2013

KIIZA AINUSURU YANGA KUZAMA KWA MTIBWA


Kiiza akitoka eneo la lango la Mtibwa baada ya kufunga bao la kusawazisha, kulia Tegete akimpongeza


YANGA SC leo imepunguzwa kasi, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
Hadi mapumziko, Mtibwa walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na kiungo wa zamani wa Simba SC, Shaaban Kisiga ‘Malone’ dakika ya 44.
Kisiga aliyewika pia SC Villa ya Uganda na Azam FC ya Dar es Salaam alifunga bao hilo akiunganisha kwa kichwa kona maridadi ya beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.
Pamoja na kufungwa, Yanga ndio waliotawala zaidi kipindi cha kwanza na walikosa mabao matatu ya wazi, mawili kupitia kwa Didier Kavumbangu na moja Jerry Tegete.
Kwa ujumla umaliziaji mbovu ndio uliowagharimu Yanga kutoka uwanjani baada ya dakika 45 za kwanza wakiwa hawajapata bao.
Kipindi cha pili, Yanga walipigana haswa kusaka mabao, lakini Mtibwa walikuwa imara hiio leo.
Kipa Hussein Sharrif ‘Cassillas’ alizuia michomo mingi ya washambuliaji wa Yanga ambao hakika siku ya leo bahati haikuwa yao.
Alikuwa ni mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Didier Kabumbangu aliyeinusuru Yanga kuzama katika mchezo wa leo baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika ya 86, akiunganisha pasi nzuri ya Said Bahanuzi aliyetokea benchi pia kuchukua nafasi ya Frank Domayo.
Baada ya bao hilo, Yanga waliongeza kasi kusaka bao la ushindi, hata hivyo Jerry Tegete alipoteza nafasi nzuri ya mwisho baada ya kupewa pasi nzuri na Simon Msuva, lakini akashindwa kuumiliki vyema mpira.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga itimize pointi 33 baada ya kucheza mechi 14 na inaendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 32, zote zimecheza mechi 14.      
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’/Nurdin Bakari, Simon Msuva, Frank Domayo/Said Bahanuzi, Didier Kavumbangu/Hamisi Kiiza, Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
Mtibwa Sugar; Hussein Sharrif ‘Casillas’, Said Mkopi, Issa Rashid, Rajab Mohamed, Salum Swedi, Shaaban Nditi, Vincent Barnabas, Rashid Gumbo, Hussein Javu, Shaaban Kisiga ‘Malone’ na Ally Mohamed ‘Gaucho’.

No comments:

Post a Comment