Saturday, January 5, 2013

YANGA KUCHEZA MECHI YA KWANZA ULAYA LEO


Yanga wakiwa Antalya
KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam, leo inashuka dimbani kucheza mchezo wa kirafiki na Arminia Bielefeld ya Ujerumani, mchezo utakaofanyika katika mji wa Antalya, Uturuki.
Yanga ambayo imeweka kambi ya mafunzo mjini Antalya, itatumia mchezo huo kama fursa pekee ya kuweza kujipima uwezo dhidi ya timu hiyo ya Ujerumani ambayo pia imekuja kuweka kambi ya mafunzo kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Pili Ujerumani.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi Ernest Brandts amesema kwao ni furaha kwa kupata nafasi ya kucheza na timu kubwa kama ya Armini Bielefeld ambayo ina wachezaji wa kiwango cha kimataifa, hivyo anaamini utakua ni mchezo safi na kuwavutia.
“Unajua tuna siku sita tangu tufike hapa (Antalya Uturuki) na tumeshafanya mazoezi kwa siku nne, hivyo fursa ya kupata mchezo wa kirafiki ni nzuri sana kwetu kwani itanipa nafasi ya kuona wachezaji wangu wameshayashika kwa kiasi gani mafunzo yangu,” alisema Brandts.
Arminia Bielefeld  imeshawasili mjini Antalya kwa ajili ya kambi yake ya mafunzo na hivyo kwao pia ni fursa nzuri ya kuweza kujipima uwezo na timu ya Yanga ambao ni mabingwa mara 23 Tanzania Bara.
Yanga imeendelea na mazoezi katika viwanja wa Fame Residecne tayari kabisa kujiandaa na mchezo huo.
Kikosi cha wachezaji 27 waliopo mjini Antalya wote wako katika hali nzuri na hakuna majeruhi hata mmoja hali itakayompa kocha Brandts kuamua kumtumia mchezaji yoyote katika mchezo huo.

No comments:

Post a Comment