Saturday, January 5, 2013

AZAM NA MIEMBENI ILIYOIPIGA MTIBWA NNE MAPINDUZI LEO, COASTAL NA WAKATA MIWA WA MANUNGU LEO


Kikosi cha Azam
MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi inatarajiwa kuendelea leo visiwani hapa kwa mechi mbili za Kundi B kupigwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Mtibwa Sugar kutoka Morogoro wataanza kushuka dimbani kumenyana na Coastal Union ya Tanga saa 10:30 jioni kwenye Uwanja huo, kabla ya mabingwa watetezi, Azam kumenyana na Miembeni SC saa 2:30 usiku.
Mechi zote zinatarajiwa kuwa kali na za kusisimua, kutokana na matokeo ya awali ya timu zote.
Mtibwa walifungwa 4-1 na Miembeni katika mchezo wa kwanza na ili kufufua matumaini ya kubaki katika michuano hii watatakiwa kushinda leo. Coastal walilazimishwa sare ya bila kufungana na Azam FC katika mchezo wa kwanza, hivyo nao watahitaji ushindi kuweka hai matumaini ya kuendelea na Kombe la Mapinduzi.
Azam na Miembeni, hiyo ni mechi inayotarajiwa kuteka hisia za wengi zaidi leo visiwani hapa, kwani timu zote ziko madhubuti.
Miembeni imeimarishwa upya kwa usajili kamambe chini ya kocha Salim Bausi, aliyeiwezesha Zanzibar kushika nafasi ya tatu kwenye Kombe la Challenge mjini Kampala, Uganda mwezi uliopita wakati Azam pamoja na kuwa mabingwa watetezi wa Kombe hilo, ndiyo yenye kuvutia hisia za wengi Bara baada ya Simba na Yanga.
Kikosi cha Coastal

No comments:

Post a Comment