Sunday, January 20, 2013

AUSTRALIA OPEN: SHARAPOVA, FERRER WATINGA ROBO FAINALI.


MWANADADA nyota katika mchezo wa tenisi, Maria Sharapova amefanikiwa kutinga kirahisi hatua ya robo fainali ya michuano ya wazi ya Australia baada ya kufanikiwa kumfunga Kirsten Flipkens wa Ubelgiji kwa 6-1 6-0. Sharapova amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu katika michuano hiyo na kuweka rekodi ya kushinda michezo miwili bila kupoteza alama katika michezo miwili ya kwanza kabla ya kumuondosha bingwa mara saba wa mataji ya Grand Slam Venus Williams katika mzunguko wa tatu. Sharapova sasa atakutana na Mrusi mwenzake Ekaterina Makarova baada ya mwanadada huyo kufanikiwa kumg’oa Angelique Kerber kwa 7-5 6-4 katika mzunguko wa nne wa michuano hiyo. Kwa upande wanaume David Ferrer anayeshika namba nne katika orodha za ubora duniani alifanikiwa kutumia udhaifu wa Kei Nishikori wa Japan alieumia mguu na kufanikiwa kumsambaratisha na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. Nishikori aliingia katika mchezo huo akiwa na matatizo katika mguu wake wa kushoto na katika seti ya pili alijitonesha mguu wake huo na kumpa nafasi Ferrer kumuadhibu kwa 6-2 6-1 6-4 ambapo sasa atakutana na aidha Janko Tipsarevic wa Serbia au Mhispania mwenzake Nicolas Almagro katika robo fainali.

No comments:

Post a Comment