Tanzania
(Taifa Stars) imepoteza mchezo wa kirafiki dhidi ya Ethiopia uliochezwa
leo (Ijumaa Januari 11, 2013) kwenye Uwanja wa Addis Ababa hapa jijini
Addis Ababa, Ethiopia.
Mechi hiyo iliyochezeshwa na Bamlak
Tesema wa Ethiopia ilikuwa ya kusisimua, hasa kutokana na timu zote
kucheza kwa kasi kwa muda wote. Wenyeji Ethiopia ndiyo walioanza kupata
bao dakika ya 13 lililofungwa na Fuad Ibrahim akiwa wastani wa hatua
sita kutoka kwa mlinda mlango Juma Kaseja wa Taifa Stars.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi
kama kilivyokuwa cha kwanza, huku Ethiopia wakiwa wamefanya mabadiliko
kwa wachezaji watano. Tanzania ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika
ya 50 likifungwa na Mbwana Samata baada ya kumzidi maarifa beki mmoja wa
Ethiopia.
Bao la ushindi kwa Ethiopia lilifungwa
kwa kichwa dakika ya 69 na mshambuliaji Shemelis Bekele aliyeingia
kipindi cha pili akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na winga Yossuf
Sallah kutoka upande wa kushoto.
Taifa Stars inarejea nyumbani kesho
(Jumamosi, Januari 12 mwaka huu) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7 kamili mchana kwa ndege ya
Ethiopian Airlines.
Taifa Stars: Juma
Kaseja, Erasto Nyoni, Issa Rashid, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Amri
Kiemba, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu/Khamis Mcha,
mwinyi Kazimoto na Mbwana Samata.
Boniface Wambura
No comments:
Post a Comment