Wednesday, January 2, 2013

UMONY AWASILI DAR, AENDA NA AZAM ZANZIBAR LEO


Umony
MCHEZAJI bora wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Kagame, Brian Umony amewasili jana kujiunga na timu yake mpya, Azam FC na leo mchana atakuwamo kwenye msafara unaokwenda Zanzibar kutetea Kombe la Mapinduzi.
Brian alirejea nyumbani Uganda mwaka jana na kujiunga na KCC baada ya kumaliza mkataba wake katika klabu ya Becamex Binh Duong F.C. ya Vietnam.
Mwaka 2009, ilikuwa aje kuichezea Simba SC ya Dar es Salaam, lakini Wekundu hao wa Msimbazi wakazidiwa kete na SuperSport United ya Afrika Kusini.
Umony aliichezea Supersport United hadi 2010 alipohamia University of Pretoria ya Afrika Kusini pia hadi mwaka 2011 alipohamia Portland Timbers ya Marekani kwa mkopo na mwaka huu akatua Becamex Binh Duong F.C. kabla ya kurejea Uganda na sasa anakuja kuanza maisha mapya Azam FC 2013.
Azam wamepangwa Kundi B, katika Kombe la Mapinduzi pamoja na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union  ya Tanga na Miembeni ya Unguja, wakati Kundi A lina timu za Simba SC, Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo hadi kilele cha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka ndani na nje ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment