Wednesday, January 23, 2013

BIN KLEB AIGAWA TUZO YAKE KWA WAPIGANAJI WENZAKE YANGA


Bin Kleb

MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kwamba tuzo aliyopewa kwenye Mkutano wa Jumapili ni kwa ajili ya watu wote ambao amekuwa akifanya nao kazi bega kwa bega katika kuijenga klabu hiyo.
Bin Kleb alipewa tuzo ya kiongozi mwenye mchango mkubwa ndani ya Yanga katika mkutano wa Jumapili, Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam kutokana na mchango wake wenye kuonekana katika klabu hiyo.
Hata hivyo, Mtanzania huyo mwenye asili ya Kiarabu alisema kwamba ingawa yeye anaonekana anafanya kazi kubwa Yanga, lakini wapo watu ambao amekuwa akishirikiana nao na pengine wakifanya makubwa zaidi kuliko yeye, lakini ama hawaonekani au hawapendi kuonekana.
Bin Kleb alisema kwamba hadi kufikia hapa Yanga imerejesha heshma yake kuna watu ambao wamefanya kazi kubwa pamoja na Kamati ya Utendaji kwa ujumla, Baraza la Wadhamini na Kamati zote zilizoundwa.
“Kwenye Kamati yangu pekee kuna watu kama Beda Tindwa, Isaac Chanji, Mussa Katabaro na wengineo, lakini kuna watu ambao pia wamefanya kazi kubwa sana, tena sana pengine kuliko hata mimi, watu kama Seif Ahmad, Davis Mosha na wengineo ambao hawapendi kutajwa, hakika wana mchango mkubwa sana Yanga,”alisema Bin Kleb.
Aidha, Bin Kleb ameomba ushirikiano kwa wana Yanga ili kuhakikisha timu inaendelea kufanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unaoanza Jumamosi.
“Kuongoza Ligi si maana yake tumechukua ubingwa, tunatakiwa kuendeleza mshikamano ambao ulileta mafanikiko haya, ili tufanikishe azma ya kutwaa ubingwa na pia kulipa kisasi cha 6-0 kwa watani wetu, Simba SC,”alisema Kleb.
Yanga ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 29, baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na Azam iliyomaliza na pointi zake 24 na mabingwa watetezi, Simba SC waliomaliza na pointi 23. 

No comments:

Post a Comment