Wednesday, January 2, 2013

DHAIRA ATUA LEO SIMBA SC, KASEJA AJIENGUA KOMBE LA MAPINDUZI


Abbel Dhaira
KIPA namba moja wa Uganda, Abbel Dhaira anatarajiwa kuwasili leo saa 8:00 mchana kujiunga na klabu yake mpya, Simba SC ya Dar es Salaam, akitokea kwao Uganda.
Dhaira aliyesaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya dola za Kimarekani 40,000, na mshahara wa Sh. Mlioni 2 kwa mwezi, baada ya kutua Dar es Salaam atakwenda moja kwa moja Zanzibar, ambako Simba itashiriki Kombe la Mapinduzi.
Kikosi kizima cha Simba, kasoro Nahodha Juma Kaseja, Emmanuel Okwi, Amir Maftah na Amri Kiemba kitaondoka leo mchana kwenda Zanzibar, tayari kwa michuano ya Mapinduzi.
Dhaira aliyeibukia Express ya Uganda mwaka 2006, mwaka 2008 alihamia U.R.A. pia ya Uganda, ambayo aliichezea hadi mwaka 2010 alipohamia Ulaya.
Kwa kumpata Dhaira, Simba SC imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza, Juma Kaseja ambaye amekuwa akisoteshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha uwezo wa kumsaidia Kaseja.
Katika mechi za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
Kwa sababu hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema hataki tena kuchezea Simba.
Lakini pamoja na matatizo hayo, Kaseja ameendelea kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli. 

No comments:

Post a Comment