Monday, January 14, 2013

SHARAPOVA, VENUS, LI NA WASONGA MBELE AUSTRALIA OPEN.


WACHEZAJI nyota wa mchezo wa tenisi Victoria Azarenka, Maria Sharapova, Venus Williams na Li Na wamefanikiwa kutinga mzunguko wa pili wa michuano ya wazi ya Australia baada ya kushinda michezo yao ya kwanza. Azarenka anayeshika nafasi ya kwanza katika chati za ubora duniani kwa upande wa wanawake na Serena Williams anayeshika nafasi ya tatu wote kwa pamoja watajitupa uwanjani kesho kuanza kampeni yao ya kufukuzia taji hilo kwa mara ya sita. Bingwa wa michuano ya French Open Sharapova ambaye alifungwa na Azarenka katika fainali ya michuano hiyo mwaka jana alianza vyema michuano hiyo baada ya kumsambaratisha bila huruma Olga Puchkova wa Urusi kwa 6-0 6-0. Mwanadada Li Na kutoka China alimfunga Sesil Karatantcheva wa Kazakstan kwa 6-1 6-3 wakati bingwa mara saba wa mataji ya Grand Slam Venus Williams huku akiangaliwa na dada yake Serena alimfunga kirahisi Galina Voskoboeva kwa 6-1 6-0. Kwa upande wa wanaume Novak Djokovic anayeshika namba moja katika orodha za ubora alianza vyema kutetea ubingwa wake katika michuano hiyo baada ya kumfunga Paul-Henry Mathieu wa Ufaransa kwa 6-2 6-4 7-5 na kutinga mzunguko wa pili. Djokovic mwenye umri wa miaka 25 raia wa Serbia anafukuzia taji la tatu la mfululizo katika michuano hiyo kitu ambacho hakuna amchezaji yoyote wa mchezo huo aliyewahi kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment