Friday, January 4, 2013

NI SIMBA SC NA TUSKER PATASHIKA KATIKA KOMBE LA MAPINDUZI USIKU LEO AMAAN


Simba SC
SIMBA SC inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa kuanzia saa 2:00 usiku wa leo, kumenyana na Tusker ya Kenya katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mapinduzi.
Mchezo huo, utatanguliwa na mchezo mwingine wa kundi hilo, kati ya Jamhuri na Bandari kwenye Uwanja wa Mao Dze Tung kuanzia saa 10:30.
Kocha Msaidizi wa Simba SC, Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’ amesema kwamba mabingwa hao wa Kenya watarajie shughuli tofauti kutoka kwa mabingwa wa Bara leo, tofauti na ilivyokuwa timu hizo zilipokutana wiki iliyopita Dar es Salaam na Tusker wakashinda 3-0.
“Tusker wajue Dar es Salaam hawakuifunga Simba, walikafunga ka Simba, sasa ndio wanacheza na Simba na watake wasitake wataumia,”alisema Julio.
Kocha mpya wa Simba SC ya Dar es Salaam, Mfaransa Patrick Liewig aliyerufahishiwa na uwezo wa wachezaji wa timu hiyo baada ya kuwashuhudia juzi wakiwachapa mabingwa wa Zanzibar, Jamhuri ya Pemba mabao 4-2 kwenye Uwanja huo huo wa Amaan mjini hapa, jana alianza kazi rasmi.
Mfaransa huyo aliyetua Dar es Salaam Jumatatu kabla ya Jumanne kusaini mkataba wa miezi 18 wa kuifundisha timu hiyo na kuja Zanzibar juzi kuungana na timu, leo anaweza kukaa kwenye benchi pamoja na wasaidizi wake, Julio na Mganda, Moses Basena.
Liewig ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia, ambaye ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller, anatarajiwa kwenda Zanzibar kesho.
Liewig pia amehudhuria kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:  alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia

WAFUNGAJI WA MABAO:
Haruna Chanongo        Simba SC    2
Jesse Were                  Tusker FC    2
Adeyum Saleh              Miembeni     2
Mfanyeje Mussa            Jamhuri       2
Ismail Dunga                 Tusker FC   1
Michael Olunga             Tusker FC   1
Andrew Tolowa              Tusker FC   1
Amour Janja                  Bandari       1
Mohamed Hamdani       Miembeni     1
Rashid Roshwa             Miembeni     1
Juma Mpakala               Mtibwa        1
Felix Sunzu                   Simba SC   1
Shomary Kapombe        Simba SC   1

No comments:

Post a Comment