Friday, January 4, 2013

KIGGI ACHAFUA HALI YA HEWA KAMBINI SIMBA SC


Chanongo akimshukuru Kiggi kwa kona ya bao
KIUNGO wa Simba, Kiggi Makassy jana alimpamia kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo katika mazoezi kwenye Uwanja wa Fuoni, visiwani hapa wakati anawahi mpira akapige kona na hilo limehusishwa na kutolewa kwake dakika ya 27 katika mechi ya juzi, lakini uongozi wa klabu hiyo umesema hakuna kitu kama hicho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba SC, Daniel Manembe amesema hakuna ugomvi kati ya Kiggi na Julio, bali kama ilivyo kawaida ya wanadamu, baada ya tukio hilo la jana maneno yameanza kuwa mengi.
“Ilikuwa bahati mbaya, yule anawahi mpira akapige kona, akampamia Julio kwa bahati mbaya, naomba tafadhali msilitafsiri vibaya tukio hilo, hakuna tofauti yoyote kati ya Julio na Kiggi,”alisema Manembe.  
  asubuhi ya leo imeripoti kuwa Makassy hafurahii maisha Simba SC na lolote linaweza kutokea juu yake wakati wowote.
Kiungo huyo aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu kutoka mahasimu Yanga, amekutana na kile amabcho alikimbia timu yake ya zamani, benchi mfululizo.
Katika mchezo wa juzi wa Kombe la Mapinduzi visiwani hapa, Kiggi alionyesha dhahiri kuchukizwa na kitendo cha kutolewa dakika ya 27 nafasi yake ikichukuliwa na Edward Christopher.
Akitoka kupiga maridadi iliyounganishwa nyavuni na Haruna Chanongo, Kiggi aliitwa benchi kumpisha Edward na alionekana kutoka kwa huzuni na alipofika benchi alikataa hata kupokea chupa ya maji aliyopewa.
Habari zaidi zinasema, tayari Kiggi amekwishaanza mishemishe za kusaka timu nyingine ya kwenda kuchezea baada ya kuona yupo katika wakati mgumu Simba SC.   
Simba SC leo inashuka tena dimbani kumenyana Tusker ya Kenya katika mchezo wa pili wa Kundi A, baada ya kushinda 4-2 dhidi ya Jamhuri ya Pemba juzi. Je, Kiggi atapangwa? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.

No comments:

Post a Comment