Saturday, January 5, 2013

MONJA 'ANELKA' AMALIZIA SOKA YAKE KISIWANI


Monja 'Anelka'
MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Monja Privas Liseki amejiunga na Miembeni ya Daraja la Kwanza Zanzibar kwa mkataba wa miaka miwili.
Monja yupo kwenye kikosi cha Miembeni FC kinachoshiriki Kombe la Mapinduzi visiwani hapa, ambayo leo usiku itamenyana na Azam FC, ikitoka kuifunga 4-1 Mtibwa Sugar katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi B.
“Nipo hapa Miembeni, nadhani nitastaafu nikiwa na timu hii. Huku nimekuja kumalizia soka yangu nafikiri,”alisema Monja leo .
Monja alizaliwa Agosti 8, mwaka 1975, Kinondoni Muslim mjini Dar es Salaam na alipata elimu yake pekee, ya Msingi katika shule ya Muhimbili, Upanga mjini Dar es Salaam. “Mimi nilikuwa napenda sana soka, nilipomaliza shule ya Msingi tu, nikaachana na shule kabisa nikaanza mitikasi ya soka hadi nikasajiliwa Sigara mwaka 1991 nikiwa bado mdogo sana nina miaka 16 tu,”alisema Monja.
Alicheza Sigara hadi mwaka 1996 iliposhushwa daraja, akahamia Simba SC ambako alidumu hadi mwaka 1998 alipotolewa kwa mkopo Yanga ili aichezee kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, Monja anasema baada ya kwisha kwa Ligi ya Mabingwa, Yanga walitaka kumsajili moja kwa moja, ila yeye akakataa na kwenda kujiunga na Mtibwa Sugar ambayo aliichezea hadi mwaka jana alipotua Miembeni.
“Nikiwa Mtibwa nilikuwa nikitoka mara moja moja kwenda kubadilisha upepo kwa kucheza Uarabuni na kurudi Mtibwa, kwa mfano mwaka juzi nilitolewa kwa mkopo niende kuisaidia Ocean View ya Zanzibar, niliichezea hadi ikachukua ubingwa wa Zanzibar,”alisema.  
Mbali na kujivunia kuwa mchezaji mkongwe zaidi katika soka ya Tanzania, lakini pia Monja anajivunia kucheza timu ya taifa, kucheza klabu kubwa Simba na Yanga na pia kucheza soka ya kulipwa Uarabuni.
Katika hayo amecheza michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Washindi, Kombe la CAF, Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia katika hatua za awali za kuwania tiketi ya kushiriki fainali za michuano hiyo.
“Mimi ndiye mchezaji wa kwanza wa Tanzania kufunga bao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kama utakumbuka Yanga ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza michuano hii. Sasa mimi nikiwa na Yanga mwaka 1998, wakati huo naitwa Andy Cole kwa jina la utani, niliifungia Yanga bao katika mechi na Manning Rangers ya Afriika Kusini huu Uwanja ambao siku hizi mnauita Uhuru, wakati huo unaitwa Taifa. Hiyo mechi tulitoka 1-1. Nikarudia kufunga tena kwenye mechi na hao jamaa jamaa kwao, siku wakitufunga 4-1,”alisema.
Monja alisema kwa sasa anataka aitwe Nicolas Anelka wa Tanzania kwa sababu huyo ndiye mchezaji mkongwe ambaye anaendelea kucheza soka ya ushindani.
WASIFU WAKE:
JINA: Monja Privas Liseki
KUZALIWA: Agosti 8, 1975
ALIKOZALIWA: Kinondoni
KLABU YA SASA: Miembeni FC
KUJIUNGA: 2012
KLABU ZA AWALI:
Mwaka          Klabu
1991- 1995   Sigara FC
1996- 1998   Simba SC
1998- 1999   Yanga SC
1999-2012    Mtibwa Sugar

No comments:

Post a Comment