Saturday, January 5, 2013

JAMBO MOJA TU LAMKERA MFARANSA SIMBA SC, KUTAKA MABAO RAHISI


Liewig akiwa na wasaidizi wake katika mchezo wa jana wakijadiliana kabla ya mechi
KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig amekubali yote kutokana na mechi ya timu yake jana dhidi ya Tusker ya Kenya, lakini amekerwa na jambo moja tu, timu yake kutaka kufunga mabao mepesi.
Akizungumza  baada ya mechi ya jana, Liewig alisema timu inabadilika taratibu na anaamini watafanikiwa kuwa na timu bora, lakini jambo moja tu amesema wachezaji wake lazima wabadilike haraka wanapofika kwenye eneo la hatari la wapinzani kwa kuonyesha uchu.
“Wanapofika kwenye eneo la hatari la wapinzani, wanakuwa wanataka kufunga bao la rahisi sana, hapana, wakati mwingine lazima ujifunze kufunga bao katika mazingira magumu. Hili lazima tulifanyie kazi haraka na wachezaji wabadilike,”alisema Liewig.
Simba SC jana ilitoka sare ya kufunga bao 1-1  na Tusker ya Kenya katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Kwa matokeo hayo, Tusker inaendelea kuongoza Kundi A, kwa piointi zake tatu sawa na Simba, lakini mabingwa hao wa Kenya wana wastani mzuri zaidi wa mabao.
Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Simba wakitangulia kupata bao dakika ya 18 mfungaji Haruna Moshi Shaaban, maarufu kama Boban au Balotelli wa Bongo kabla ya Tusker kusawazisha dakika ya 39, mfungaji Khalid Aucho.
Boban alifunga bao tamu sana kwa ufundi wa hali juu akiwa amedhibitiwa na beki ngongoti wa Tusker, Joseph Shikokoti na kuirukia pasi ya Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kuitumbukiza nyavuni.
Baada ya kufunga bao hilo, Boban aliangukia mkono na kuumia, hivyo hakushangilia bao lake na moja kwa moja alianza kutibiwa na Daktari Cossmas Kapinga wa Simba.
Baada ya bao hilo, Simba iliongeza mashambulizi langoni mwa Tusker na Boban alikaribia kufunga tena dakika ya 30 kama si shuti lake kutoka nje sentimita chache.
Aucho alifunga bao lake akiunganisha krosi ya Jeremiah Bright kutoka upande wa kushoto wa Uwanja.
Baada ya hapo, timu zilianza kushambuliana kwa zamu hadi refa Ramadhani Kibo alipopuliza kipyenga cha kuhitimisha ngwe ya kwanza.
Kipindi cha pili timu zote zilirudi vizuri na kucheza kwa umakini wa hali ya juu, jambo ambalo lilisababisha dakika 90 zimalizike zikiwa zimefungana 1-1.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Shomary Kapombe, Komabil Keita, Jonas Mkude, Haroun Athumani/MKussa Mudde75, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Ramadhan Chombo ‘Redondo’/Edward Christopher dk 52.
Tusker FC; Samuel Odhiambo, Luke Ochieng, Jeremiah Bright/Humphrey Okoth, Mark Odhiambo, Joseph Shikokoti, Khalid Aucho, Edwin Manono/Benson Amanda, Justin Monda, Ismail Dunga/Michael Olunga, Jesse Were na Robert Omonuk.
Katika mchezo uliotangulia, Jamhuri ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Bandari kwenye Uwanja wa Mao Dze Tung. Mabao ya Jamhuri yalifungwa na Fahad Abdallah Athumani dakika ya 25 na Ally Bilal dakika ya 67, wakati la Bandari lilifungwa na Faudhi Ally dakika ya tano.

No comments:

Post a Comment