Tuesday, January 8, 2013

MFARANSA SIMBA ATAKA DVD ZA LIBOLO NA TIMU YAKE DHIDI YA TIMU KALI MECHI KAMA MBILI AU ZAIDI

MFARANSA SIMBA ATAKA DVD ZA LIBOLO NA TIMU YAKE DHIDI YA TIMU KALI MECHI KAMA MBILI AU ZAIDI

Liewig
KOCHA Mfaransa wa Simba SC, Patrick Liewig amesema kwamba anataka DVD za mechi ngumu za timu hiyo pamoja na DVD za mechi za karibuni za wapinzani wao wa kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Recreativo de Libolo ya Angolal.
Simba SC itaanza na Recreativo de Libolo ya Angola, katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Februari 17 hadi 19 na kurudiana nayo kati ya Machi 2 na 4, mwakani.
Akizungumza  jana, Mfaransa huyo alisema kwamba anahitaji DVD hizo ili kuijua vema Simba ilikuwa inachezaji na ina wachezaji wa aina gani.
Aidha, kuhusu DVD za Recreativo de Libolo, Liewig alisema ni vema akizipata ili awajue wapinzani wake, lakini kwake muhimu zaidi ni DVD za Simba.
Akizungumzia suala hilo, Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alisema kwamba DVD za mechi za Simba tayari zipo na watampatia kocha huyo, wakati DVD za Recreativo de Libolo bado wanazitafuta.
Simba SC inatarajiwa kuondoka kesho Dar es Salaam kwenda Oman kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na Ligi Kuu pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika. 
Liewig aliyesaini mkataba wa miezi 18 wiki iliyopita kuifundisha Simba, akimpokea Mserbia Milovan Cirkovick aliyetupiwa virago baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara ni kocha wa zamani wa Akademi ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Club Africain ya Tunisia.
Babu huyo ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller.
Liewig pia amehudhuria kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.
Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990:  alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia

No comments:

Post a Comment