Monday, January 7, 2013

MAPAMBANO BADO HAYAJAISHA - VILANOVA

.

MENEJA wa klabu ya Barcelona, Tito Vilanova amekiri kuwa mapambano yake dhidi ya ugonjwa wa kansa unaomsumbua bado hayajaisha na kwamba anaweza kupumzika tena kuinoa timu hiyo kwa ajili ya matibabu. Vilanova mwenye umri wa miaka 44 alifanyiwa upasuaji kwa mara ya pili kuondoa uvimbe wa kansa katika koo lake Desemba 20 mwaka jana. Kocha huyo alikosa mchezo wa ugenini dhidi ya Valladolid lakini alirejea jana wakati Barcelona ilipopata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Espanyol ambao umeifanya kung’ang’ania kileleni kwa tofauti ya alama 11 dhidi ya Atletico Madrid ambao wanashika nafasi ya pili. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Vilanova amesema vita anavyopambana na ugonjwa huo bado kwani kuna siku ambazo hataweza kuhudhuria mazoezini na shughuli nyingine lakini aliwaomba watu wa habari kujua kwamba ugonjwa huo ni wake na jambo binafsi hata kama yeye ni maarufu. Kocha huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wote ambao wameonyesha kuwa pamoja naye katika kipindi chote toka alipogundulika kuwa na ugonjwa huo wakiwemo wachezaji, viongozi na mashabiki wa klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment