Wednesday, January 16, 2013

DAKAR RALLY: TERRANOVA ASHINDA HATUA YA KUMI.


DEREVA Orlando Terranova amewapagawisha mashabiki wa Argentina kwa kuwa dereva wa kwanza wa nchi hiyo kuibuka kidedea katika hatua ya 10 ya mashindano ya Dakar Rally yanayofanyika huko Amerika Kusini. Dereva huyo anayeendesha gari aina ya BMW mwenye umri wa miaka 33 ambaye anashindana katika mbio hizo kwa mara ya saba alishika nafasi ya kwanza katika hatua hiyo akiwa mbele ya Nani Roma kwa dakika mbili na sekunde saba na kufuatiwa na bingwa mtetezi Stephane Peterhansel wa Ufaransa aliyeshika nafasi ya tatu. Akihojiwa mara baada ya ushindi huo Terranova amesema ilikuwa ni rahisi kushinda hatua hiyo kwasababu hawakufanya makosa mara kwa mara na gari lao halikuwaletea matatizo. Bingwa mtetezi Peterhansel mwenye umri wa miaka 47 raia wa Ufaransa anatafuta taji la 11 la mashindano hayo huku nafasi ya yeye kushinda ikiongezeka baada ya aliyekuwa mpinzani wake wa karibu Nasser al-Attiyah kutoka Qatar kujitoa Jumatatu baada ya kuharibikiwa na gari lake.

No comments:

Post a Comment