Monday, December 24, 2012

MTIGINJOLA KUONGOZA KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI TFF


Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemteua Idd Mtiginjola kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF iliyoundwa kutokana na marekebisho ya Katiba yaliyofanyika hivi karibuni. Mtiginjola ambaye ni Wakili wa kujitegemea ataongoza kamati hiyo yenye wajumbe watano ambayo sasa itakuwa chombo cha mwisho kusikiliza rufani zinazotokana na uchaguzi wa TFF, na wanachama wa TFF ambao hawatakubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Kabla ya uteuzi huo, Mtiginjola alikuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana. Nafasi yake katika kamati hiyo na ile ya mjumbe mwingine Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Shabani Semlangwa aliyefariki dunia Julai mwaka huu zitajazwa hivi karibuni. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambayo vinara wake (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti) wanatakiwa kitaaluma kuwa wanasheria ni Francis Kabwe. Kabwe ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Wajumbe wengine walioteuliwa na Kamati ya Utendaji ya TFF katika kikao chake cha jana (Desemba 23 mwaka huu) ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria. Wengine ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa sasa ni Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini.

MECHI YA STARS, CHIPOLOPOLO YAINGIZA MIL 109/-
 
 Pambano la kirafiki la kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zambia (Chipolopolo) lililochezwa juzi (Desemba 22 mwaka huu) limeingiza sh. 109,197,000. Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 17,383 waliokata tiketi kushuhudia mechi kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 20,000 na sh. 30,000. Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 16,657,169.49, maandalizi ya mchezo sh. 55,339,510, tiketi sh. 5,803,900, ulinzi na usafi kwa Uwanja wa Taifa sh. 2,350,000, Wachina (technical support) sh. 2,000,000, umeme sh. 300,000 na maandalizi ya uwanja (pitch marking) sh. 400,000. Nyingine ni bonasi kwa Taifa Stars sh. 13,826,313, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 2,504,022, asilimia 10 ya uwanja sh. 1,252,011, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 626,005 na asilimia 65 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 8,138,070. Mapato ya mechi nyingine za Taifa Stars ilizocheza nyumbani mwaka huu yalikuwa Taifa Stars vs Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC (Leopards) iliyofanyika Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam sh. 32,229,000. Taifa Stars vs Msumbiji (Mambas) iliyochezwa Februari 29 mwaka huu sh. 64,714,000. Taifa Stars vs Malawi (The Flames) iliyochezwa Mei 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliingiza sh. 40,980,000. Taifa Stars vs Gambia (The Scorpions) iliyochezwa Juni 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zilipatikana sh. 124,038,000 na Taifa Stars vs Kenya (Harambee Stars) iliyofanyika Novemba 14 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza iliingiza sh. milioni 45.

CASILLAS AKATAA KUMKOSOA MOURINHO.

NAHODHA wa klabu ya Real Madrid, Iker Casillas amekataa kukosoa maamuzi ya kocha wake Jose Mourinho baada ya kumuweka benchi katika mchezo wa Jumamosi ambao walifungwa mabao 3-2 na Malaga. Uamuzi wa kumuacha Casillas ulielezewa na kocha huyo Mreno kama la kiufundi lakini ilisababisha Madrid kupoteza alama tatu muhimu katika mchezo huo wa La Liga. Akihojiwa Casillas amekiri kuwa hakuzoea hali hiyo ya kutocheza lakini siku zote kocha ndio anachagua nani acheze na asicheze hivyo akiwa kama mchezaji lazima aheshimu maamuzi yao kocha. Amesema wachezaji wenzake wote wamekuwa wakimfariji kama walivyokuwa wakimfariji Antonio Adan ambaye ni golikipa namba mbili aliyechukua namba ya Casillas katika mchezo dhidi ya Malaga. Suala la Mourinho kumuacha Casillas limechukuliwa tofauti na wadau wengi wa soka mmojawapo akiwa mkurugenzi wa zamani wa michezo wa Madrid Jorge Valdano ambaye anaamini kuwa kocha huyo alikuwa akifikisha ujumbe kwamba yeye ndiye bosi katika klabu hiyo. 

CHELSEA YAVUTA PAUNDI MILIONI 12 KWA STURRIDGE.

KLABU ya Chelsea imekubali kumuuza mshambuliaji wake Daniel Sturridge kwenda Liverpool kwa ada ya paundi milioni 12. Mshambuliaji huyo ambaye alifanyiwa vipimo vya afya Jumapili anategemewa kusaini mkataba wa miaka mitatu na nusu na Liverpool katika muda wa saa 24 zijazo. Mshambuliaji huyo ambaye alikuwa akitaka kupigania namba Chelsea mpaka mkataba wake utakapomalizika mizei 18 ijayo, atakuwa akilipwa na Liver mshahara wa paundi 60,000 kwa wiki. Chelsea itakuwa imepata faida kubwa kwa kumuuza mshambuliaji huyo ambaye walimnunua kwa ada ya paundi milioni 1.5 akitokea klabu ya Manchester City mwaka 2009.

MDOGO WAKE BALOTELLI AKAMATWA.

KAKA wa mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Italia, Mario Balotelli alikamatwa Jumapili kwa tuhuma za kujeruhi maofisa wawili wa polisi wakati wa vurugu zilizotokea mtaani. Enoch Barwuach ambaye ni mdogo wake Balotelli ambaye anacheza katika klabu ya Manchester City anakabiliwa na mashtaka ya kushambulia na kukataa kukamatwa baada ya kujihusisha na ugomvi katika klabu ya usiku Jumamosi huko Brescia, Italia. Barwuah mwenye umri wa miaka 20 ambaye amezaliwa tumbo moja na Balotelli alilala lupango kabla ya kuhamishwa ambapo anatarajiwa kupelekwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili. Mdogo wake Balotelli ameonyesha kufuata nyendo za kaka yake ambaye amekuwa akikumbwa na matukio mbalimbali ya vurugu ndani na nje ya uwanja.

HUNTERLAAR AKUBALI KUONGEZA MKATABA SCHALKE.

KLABU ya Schalke 04 ya Ujerumani imethibitisha kuwa mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Uholanzi, Klaas-Jan Hunterlaar amekubali kuongeza mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo. Hunterlaar mwenye umri wa miaka 29 amekuwa akihusishwa kuhamia katika vilabu mbalimbali vya Ulaya ikiwemo Inter Milan, Arsenal na Liverpool lakini sasa tayari amesaini mkataba mpya utakaombakisha hapo mpaka 2015. Mhsmabuliaji huyo aliwaambia wavuti wa klabu hiyo kuwa amefikiri kwa muda mrefu na makini kabla ya kuamua kusaini mkataba mpya na anajisikia furaha kuendelea kuwepo katika klabu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili mingine. Hunterlaar alijunga na Schalke akitokea AC Milan mwaka 2010 akiwa pia amepitia katika vilabu vya Real Madrid ya Hispania na Ajax Amsterdam ya nyumbani kwao.

VAN ANA BAHATI KUWA HAI - FERGUSON.

MENEJA wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson amedai kuwa beki wa Swansea City Ashley Williams angewewa kumuua Robin van Persie wakati wa mchezo baina ya timu hizo uliochezwa katika Uwanja wa Liberty jana. Beki huyo wa kimataifa wa Wales alipiga mpira uliomgonga kichwani Van Persie katika kipindi cha pili na kupelekea mshambuliaji huyo kunyanyuka kwa hasira na kumvaa Williams na wote kupelekea kupewa kadi nyekundu. Ferguson amesema kuwa tukio hilo ni bay asana kwani lingeweza kusababisha madhara makubwa kama kifo hivyo aliomba Chama cha Soka cha Uingereza-FA kuchunguza na kutoa adhabu. Williams akihojiwa mara baada ya mchezo huo alidai kuwa lilikuwa tukio la bahati mbaya hakudhamiria kumbutua na mpira kichwani Van Persie na kusababisha nyota huyo kushikwa na jazba. Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 hiyo ikiwa ni sare ya kwanza United katika michezo 21 waliyocheza ambapo bado wamebakia kileleni mwa Ligi Kuu nchini humo wakiongoza kwa alama 43.

No comments:

Post a Comment