Wednesday, October 3, 2012

YULE REFA WA MEI 6 ALIKUWA KIBOKO, MAREFA WETU NA MECHI

 


 tano juma

JIONI ya leo kuanzia saa 11:00, nyasi za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitawaka moto kwa mpambano mkali wa watani wa jadi, Simba na Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo itarushwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini.
Nakumbuka, wachambuzi na watangazaji wa SuperSport waliwahi kuiingiza mechi ya Simba na Yanga katika orodha ya mechi tatu kali za wapinzani wa jadi Afrika - nyingine zikiwa ni kati ya Orlando Pirates na Kaizer Chiefs za Afrika Kusini na Al Ahly dhidi ya Zamalek za Misri.
Lakini mimi naongeza mechi ya wapinzani wa Ghana, Hearts Of Oak na Asante Kotoko, ingawa Kenya nako upinzani wa Gor Mahia na AFC Leopard umeanza kuja juu tena, baada ya kuporomoka miaka ya karibuni, kutokana na kuyumba kwa timu zenyewe.
Hakuna ubishi upinzani wa Ahly na Zamalek huo ni dunia nzima - ni zaidi ya upinzani, lakini kwa Afrika fuatilia ligi nyingi, utagundua Simba na Yanga ni mechi yenye mvuto wa kipekee na ndiyo maana hivi sasa SuperSport wamekuwa wakionyesha mfululizo mechi za watani hao, ingawa hawana mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wa kuonyesha mechi za Ligi Kuu.
Unaweza kutilia shaka kiwango cha soka cha timu hizo, lakini si upinzani wao kwa maana ya upinzani. Upinzani wao ni sehemu ya burudani na kama iko siku zitakuwa imara na kucheza soka ya kuvutia, basi burudani itakuwa mara mbili.
Hata hivyo kuna mambo mawili au matatu ambayo kwa kiasi fulani yamekuwa yakipunguza ladha ya mechi za watani hao wa jadi.
Awali tatizo kubwa lilikuwa Uwanja mdogo wa Uhuru, lakini tangu kukamilika kwa Uwanja wa Taifa ambao tumeshuhudia mechi zote zilizochezwa hapo, haijatokea mechi hata moja mashabiki wakajaza viti, mambo yamekuwa mazuri.
Matatizo mawili yaliyobakia ni viwango vya timu kuboreshwa, ili ifike wakati pamoja na upinzani, kukamiana lakini watazamaji washuhudie soka safi.
Tatizo la pili ni marefa, kweli ilipofikia na kama kweli lengo ni kuiongezea msisimko zaidi mechi ya watani, waamuzi wa Tanzania wawekwe kando na watumike waamuzi kutoka nje ya nchi, tena ikibidi nje kabisa ya nchi tatu za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.
Rejea mchezo uliopita wa Mei 6, 2012, refa alitoa penalti tatu na kadi moja nyekundu kwa Yanga, ikichapwa 5-0 na Simba.
Hii si sahihi katika mechi za wapinzani wa jadi, dhahiri refa huyu alishindwa kuumudu mchezo wa watani hata kama alifuata sheria 17. Katika mechi ya wapinzani wa jadi, ukishatoa kadi moja nyekundu kwa timu moja, unajifikiria sana kurudia kutoa kadi ya pili kwa timu hiyo hiyo.
Katika mechi za wapinzani wa jadi, ukishatoa penalti moja kwa timu moja, unajifikiria sana kutoa penalti ya pili kwa timu hiyo hiyo. Unafikiria mengi. Tena mengi sana.
Jana Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga alizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu refa Mathew Akrama atakayechezesha pambano la leo watani wa jadi kesho, akishangaa kwamba anapewaje mechi mbili mfululizo za Yanga, wakati ndiye aliyechezesha mechi iliyopita ya Yanga na African Lyon.
“Tunajua sekretarieti ya TFF ndiyo huwa inahusika kupanga marefa, na ndiyo hii hii ambayo tunailalamikia haitutendei haki, sasa sisi tunamuomba mambo mawili makubwa Akrama, kwenye mechi ya Simba na Yanga; kuna watu huwa wanapoteza maisha wakifungwa. Kuna watu huwa wanapoteza fahamu, wanaweka rehani nyumba zao, mali zao kucheza kamari, na wanaliwa.kuna viongozi wengine wamewahi kutimuliwa madarakani kwa sababu ya kufungwa na Simba na Yanga.
Kwa hiyo, hii mechi ina mambo mengi sana, sasa sisi tunamuomba Akrama asiue watu, asifanye watu wakaliwa, asifanye watu wakapata mateso yasiyo na sababu,”alisema.
Labda Kamwaga alikuwa akizungumza kama propaganda tu siasa za soka ya nchi hii, lakini aliongea mambo mazito na yenye mantiki. Kweli Simba na Yanga zimekwishaua watu.
Lakini sitaki kuegemea upande wa Kamwaga, kuua watu kwa maumivu ya kufungwa- hapana, zinapoibuka hisia za timu fulani kuumizwa na refa, mfano ule wa kutoa penalti tatu na kadi nyekundu juu, kuna hatari ya vurugu zaidi na mauaji kutokea.
Haya ni mambo ambayo umefika wakati sasa, TFF wanapoingia kwenye mechi ya watani, wanatakiwa kuyafikiria.
Rejea mechi ya Machi 5, mwaka 2011 Uwanja wa Taifa, refa Orden Mbaga aliivuruga mno mechi hiyo, kutokana tu na pengine mchecheto ama kutaka kufanya kile ambacho kinaitwa ‘kubalansi’ mchezo au kukwepa lawama, matokeo yake anafanya madudu.
Dakika ya 58 Juma Said Nyosso alimkwatua Davies Robby Mwape kwenye eneo la hatari akawapa penalti Yanga na kilichofuatia wengi walijua beki huyo wa Simba atatolewa nje kwa kadi nyekundu, badala yake akampa kadi ya njano.
Ngumu kuamini Mbaga, refa mwenye beji ya Shrikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hajui alipaswa kufanya nini kwa Nyosso, lakini kwa sababu ni refa wa nyumbani na aliongoza wapinzani wa jadi katika mechi ya nyumbani, alihofia kumtoa mchezaji kwa kadi nyekundu angeshushiwa lawama nzito. Marefa hufanyiwa fujo na kupigwa na mashabiki, labda alihofia hali hiyo pia.
Dakika ya 73 Simba walipata bao safi la kusawazisha lililofungwa kwa kichwa na Mussa Hassan Mgosi, aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Yaw Berko  kufuatia shuti la mpira wa adhabu, lililogonga mwamba wa juu na kudondokea nyavuni kabla ya kuokolewa na mabeki wa Yanga.
Halikuwa bao lenye shaka yoyote, hakukuwa na kuotea wala dosari yoyote, lakini haieleweki kwa nini Mbaga alilikataa bao hilo awali.
Ilikuwa offside au mpira haukutinga nyavuni hadi akalikataa kwanza? Haijulikani, lakini alilikubali baada ya wachezaji wa Simba kumuambia aangalie kwenye TV iliyokuwapo uwanjani marudio ya tukio lile na baada ya hapo akaenda kujadiliana na msaidizi wake, ndipo akalikubali.
Mbaga alichemsha- lakini si Mbaga tu, marefa wengi wa Tanzania waliwahi kutokota kabla yake na nitakumbushia baadhi ya mechi.  
Machi 31, mwaka 2002 katika fainali ya Kombe la Tusker, Simba ikishinda 4-1, refa Abdulkadir Omar ‘Msomali’ aliivuruga mechi na kuvuruga amani uwanjani pia kwa madudu yake.
Kwa nini? Katika mechi hiyo ya fainali iliyohudhuriwa na rais mstaafu wa awamu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka Suleiman kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa.
Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, (FAT), sasa TFF kabla ya kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo baadaye.
Agosti 18, mwaka 2002 Simba na Yanga zikitoka sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu, refa Victor Mwandike aliwaacha mashabiki wa Simba midomo wazi kwa kuwapa Yanga penalti dakika ya 89 na ushehe, ambayo Sekilojo Chambua aliitumia vema kuisawazishia bao timu yake, baada ya Simba kutangulia kufunga kupitia kwa Madaraka Suleiman dakika ya 65.
Oktoba 24, mwaka 2007, refa Osman Kazi alikataa mabao matatu yaliyofungwa na Yanga, yote akidai kipa Juma Kaseja alisukumwa na wachezaji wa Yanga, lakini kwa yeyote atakayerudia kuangalia DVD ya mchezo ule, hawezi kuona ukweli wa madai ya Kazi.
Awali ya hapo, Kazi aliwahi kupuliza filimbi ya kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la Tusker mwaka 2005 mjini Mwanza, wakati mchezaji wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ amekwishawatoka mabeki wa Simba na anakwenda na mpira mbele yake amebaki Juma Kaseja tu.
Refa ni mwamuzi wa mwisho- lakini kwa wana Yanga walijutia mno tukio lile kwenye mchezo ambao mwishowe walifungwa 2-0, kwa mabao ya kipindi cha pili ya Emmanuel Gabriel na Mussa Mgosi.
Aprili  19, mwaka 2009, Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la kusawazisha kwa mkono na kutengeneza sare ya 2-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Refa makini asingeweza kukubali bao lile, hivyo kwa haya yote lazima tukubali marefa wa Tanzania hawawezi tena kuchezesha mechi za watani wa jadi.
Sababu nyingine za marefa wetu kuzishindwa mechi hizo ni mapenzi yao kwa moja ya timu hizo, kitu ambacho Misri wamekiepuka na mechi ya Zamalek na Ahly inachezeshwa na marefa kutoka nje ya nchi yao.
Nakumbuka refa kutoka Uganda, Dennis Bate aliyechezesha Nusu Fainali ya Kombe la Tusker mwaka 2009 kati ya Simba na Yanga, aliiongoza vizuri mechi hiyo na akadhibiti ujanja wote wa wachezaji kutaka kumdanganya na hatimaye aboronge.
Kuna wachezaji wanaitwa wazoefu wa mechi za Simba na Yanga na hawa wamekuwa wakiwapoteza sana marefa kwa uzoefu wa kucheza mechi hizo, lakini kama marefa watatoka nje ya Tanzania, tena wa kiwango cha beji za FIFA, uhondo wa mechi za watani utaongezeka maradufu.
Zaidi ya mara mbili sasa naandika juu ya mechi za watani wa jadi kubadilishiwa marefa, lakini wakubwa wameendelea kukaa kimya- labda wanajua wanachokifanya, ila ukweli ulivyo
kwa sasa, marefa wetu hawaziwezi tena mechi hizi.

No comments:

Post a Comment