Tuesday, October 23, 2012

UKUTA WA AZAM WATIA FORA LIGI KUU, BORA 'DIFENSI' YA MGAMBO KULIKO SIMBA NA YANGA

Azam FC; Wenye ukuta tishio zaidi Ligi Kuu


WAKATI Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ipo katika mzunguko wake wa tisa, hadi sasa Azam FC ndio imeonyesha kuwa timu yenye ukuta mgumu zaidi na ikiwa kesho inamenyana na Ruvu Shooting katika mfululizo wa ligi hiyo, imefungwa mabao mawili tu katika mechi saba.
Azam ilifungwa mabao hayo katika mechi yake ya pili, dhidi ya wenyeji Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na tangu hapo imecheza dakika 450 bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa na katika mechi zote hizo alidaka Mwadini Ally.
Kwa kawaida safu ya ulinzi ya Azam huwa haibadiliki sana na katika mechi zote hizo ambazo hawajafungwa, Mwadini amekuwa akilindwa na Ibrahim Shikanda kulia, kushoto Erasto Nyoni na katikati Aggrey Morris na Said Mourad, juu yao kiungo mkabaji Ibrahim Mwaipopo.
Unasemaje kuhusu ukuta huu, upo ukuta unaostahili kuitwa jina gumu katika Ligi Kuu hadi sasa zaidi ya huu? Hakuna hakika.
Kasi ya ufungaji wa mabao ya Azam hadi sasa ni ya wastani wa kati, katika mechi saba walizocheza wamefunga mabao manane, bado ni wastani wa bao moja katika kila mechi na hii ni kwa sababu mfungaji bora wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’ bado hajafunguka.
Kwa wenye kufuatilia rekodi ya Bocco katika Ligi Kuu, amekuwa tishio zaidi katika mzunguko wa pili, hivyo bado hatuwezi kusema chochote juu yake hadi sasa hadi wakati utakapofika.
Timu inayoifuatia Azam kwa kuwa na ukuta mgumu ni JKT Mgambo Shooting, ambao wamepanda Ligi Kuu msimu huu. Timu hiyo ya Muheza, katika mechi zake nane ilizocheza hadi sasa, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne tu, ingawa na yenyewe pia haina makali sana ya kufunga, kwani imefunga mabao sita tu.
Ingawa haijafunga hata bao moja katika Ligi Kuu msimu huu, Polisi ya Morogoro iliyopanda pia Ligi Kuu msimu huu, ni timu ya tatu kwa ubora wa beki yake hadi ligi ilipofikia, hadi sasa katika mechi zake sita wamefungwa mabao matano tu. Hii ni timu ambayo inashika mkia katika Ligi Kuu na kesho inamenyana na Yanga.
Prisons ya Mbeya ambayo nayo imepanda Ligi Kuu msimu huu, pia ina ukuta mgumu, kwani katika mechi zake nane ilizocheza hadi sasa, imefungwa mabao matano tu, ingawa nayo pia haina safu tishio sana ya ufungaji, kwani imefunga mabao matano pia.
Tazama utaona timu zote zilizopanda Ligi Kuu msimu huu zimewekeza vizuri katika safu zake za ulinzi- Mgambo, Prisons na Moro, zote zimefungwa mabao machache kuliko hata vigogo Simba na Yanga waliotumia mamilioni mengi kusajili hadi mabeki wa kigeni.
Mabingwa watetezi Simba SC, wakiwa wanaongoza kwa safu kali zaidi ya ushambuliaji, iliyovuna mabao 16 katika mechi tisa, ndiyo wanaofuatia kwa kuwa na ukuta mgumu, wakiwa wamefungwa mabao sita tu katika mechi hizo.
Kagera Sugar ya Bukoba ndiyo inayofuatia kuwa na ukuta mgumu, ikiwa imefungwa mabao sita pia katika mechi zake saba na yenyewe imefunga mabao saba.
Coastal Union ya Tanga katika mechi zake nane, pia imefungwa mabao manane, wakati yenyewe imefunga mabao 10, sawa na JKT Oljoro ambayo katika mechi nane pia, imefunga mabao nane, ingawa yenyewe imefunga mabao saba wakati Mtibwa Sugar katika mechi saba imefunga mabao manane na imefungwa manane pia.
Yanga ndiyo wanafuatia sasa kwa ‘ukuta bora’, wakiwa wamefungwa mabao 10 katika mechi nane, ingawa hawa sasa wanaonekana pia kuwa na safu kali ya ushambuliaji, ambayo hadi sasa imefunga mabao 14.
Hiyo ni safu ya ushambuliaji ya pili kwa ukali wa mabao, baada ya safu ya mabingwa watetezi Simba SC, iliyofunga mabao 16 hadi sasa katika mechi tisa.
African Lyon inafuatia kuwa na safu kali ya ulinzi, katika mechi nane ikiwa imefungwa mabao 11 na hatari zaidi ni kwamba hata safu yake ya ushambuliaji haitishi sana, kwani imefunga mabao matano tu.
Toto African ambayo ndio pekee inajua utamu wa nyavu za Azam hadi sasa, nayo imefungwa mabao 11 katika mechi nane, ikiwa nayo imefunga mabao matano tu.
Timu mbili za mkoa mmoja, Pwani, Ruvu Shooting na JKT Ruvu ndizo ambazo zinaongoza kuwa na kuta zenye nyufa nyingi, kwani hadi sasa zimeruhusu mabao 13 kila timu.
Ruvu Shooting pamoja na kufungwa mabao 13, angalau nayo imeonyesha uhai katika safu yake ya ushambuliaji kwa kufunga mabao 11, lakini JKT iliyofungwa ‘dazeni’ ya mabao na nyongeza ya bao moja, yenyewe imefunga mabao saba tu.
Katika msimamo wa Ligi Kuu, mbio za ubingwa hadi sasa bado ni za farasi watatu tu, Simba, Yanga na Azam zinazofukuzana kileleni, wakati kule kwenye mlango wa kutokea, Mtibwa Sugar, JKT Ruvu, African Lyon, Toto African na Polisi Moro zimebanana kisawasawa. Yote tisa, ukuta wa Azam umetia fora hadi sasa katika Ligi Kuu na safu ya ushambuliaji ya Simba ndiyo inayotisha zaidi.
MSIMAMO WA LIGI KUU BARA
                              P    W  D   L    GF GA GD Pts
Simba SC               9    5    4    0    16 6    10 19
Azam FC                7    5    2    0    8    2    7    17
Yanga SC               8    4    2    2    14 10 4    14
Coastal                   8    3    3    2    10 8    2    13
JKT Oljoro              8    2    5    2    7    8    -1  11
JKT Mgambo          8    3    2    3    6    4    2    10
Prisons                   8    2    4    2    5    5    0    10
Kagera Sugar         7    2    3    2    7    6    1    9
Ruvu Shooting        8    3    0    5    11 13 -2  9
Mtibwa Sugar          7    2    2    3    8    8    0    8
JKT Ruvu                8    2    2    4    7    13 -6  8
African Lyon            8    2    1    5    5    11 -6  7
Toto African             8    1    3    4    7    11 -4  6
Polisi Moro               6    0    2    4    0    5    -5  2
(P idadi ya mechi ambazo timu imecheza, W mechi ambazo imeshinda, D sare, L kufungwa, GF mabao iliyofunga, GA mabao iliyofungwa, GD mabao iliyonayo ukitoa mabao iliyofungwa, -maana yake imefungwa zaidi ya ilivyofunga na Pts ni idadi ya pointi)

 

 

KIBOSILE TFF AULA CAF

Boniface Wambura


OFISA Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura ameteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwa mmoja wa maofisa watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili ya kufanikisha uendeshaji wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizopangwa kuanza Oktoba 28, 2012 na kumalizika Novemba 11, 2012.
Wambura atakuwa mmoja wa maofisa watatu watakaoshughulikia habari kwenye fainali hizo. Wengine ni ofisa kutoka makao makuu ya CAF, Mahmoud Garga na Arlindo Macedo kutoka Angola.
Wambura atakuwa ni Mtanzania pekee kwenye Kamati ya Maandalizi ya fainali hizo, kitu ambacho TFF inajivunia kutoa mwakilishi kwenye moja ya mashindanoi makubwa ya mpira wa miguu Tanzania.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameelezea uteuzi  huyo kuwa ni matokeo ya kazi nzuri ambayo Wambura amekuwa akiifanya tangu ajiunge na Shirikisho Januari mwaka 2011.
“Taarifa zake mbalimbali zimeifanya Tanzania iwe inang’ara CAF na hata FIFA kwa kuwa kwa sasa wanajua kila kinachoendelea kwenye soka la Tanzania,” alisema Rais Tenga na kumtakia Wambura kila la kheri kwenye kazi hiyo atakayoifanya kwa takriban siku 14.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, akizungumza kwa niaba ya Sekretarieti, amemtakia Wambura kazi njema na kwamba awe kioo cha mabadiliko makubwa yanayoendelea kwenye soka la Tanzania.
Wambura alijiunga na TFF Januari, 2011 akiwa mmoja wa waajiriwa watatu wapya kwenye Shirikisho baada ya wsatendajiu wengine wawili kumaliza muda wao wa mikataba.
Wambura ni mwandishi wa habari mwandamizi ambaye ameshafanya kazi kwenye vyombo mbalimbali kuanzia kazi ya uandishi hadi Mhariri Mtendaji wa gazeti la Jambo Leo ambalo alikuwa akifanya kazi kabla ya kujiunga na TFF.

 

MISS TANZANIA 2012 KUZAWADIWA GARI NA MILIONI 8 JUU

Lundenga kulia, akizungumza na Waandishi wa Habari. Kushoto ni mmoja wa wadhamini wa shindano hilo

 
MSHINDI wa shindano Tanzania 2012, litakalofanyika Novemba 3, mwaka huu kwenye ukumbi wa Blue Pearl Hotel, uliopo ndani ya jengo la Ubungo Plaza, ataondoka za fedha taslimu Sh. Milioni 8 na gari ambalo aina yake na thamani yake vitajulikana baadaye.
Mkurugenzi wa Lino International Agency, waandaaji wa Miss Tanzania Waandishi wa Habari asubuhi hii katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) kwamba mshindi wa pili atapewa Sh. Milioni 6.2, wa tatu Milioni 4, wa nne Milioni 3, wa tano Milioni 2.4 na wa sita hadi 15 kila mmoja atapata Milioni 1.2, wakati washiriki wengine kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh. 700,000.
Lundenga amesema washiriki watatu wamepata tiketi ya kuingia 15 bora moja kwa moja kutokana na kushinda mataji madogo ya shindano hilo, ambao ni Lucy Stefano (Miss Photogenic), Magdalena Roy (Top Model) na Mary Chizi ambaye ni Top Sports Woman.
Alisema mashindano mengine madogo, Miss Talent litafanyika Ijumaa wiki hii na Jumapili Miss Personalty ambayo, washindi wake wote wataingia moja kwa moja 15 Bora ya  Miss Tanzania 2012.
Mapema mwaka huu, Kamati hiyo iliendesha shindano dogo na kumpata Lissa Jensen ambaye aliwakilisha nchi katika fainali za Dunia kutokana na mabadiliko ya kalenda yaliyofanywa na Kamati ya Miss World na mrembo atakayetwaa taji hilo katika fainali hizo zitakazofanyika hivi karibuni atapata muda mrefu wa kufanya maandalizi.
Shindano la Miss Tanzania lilianza rasmi mwaka 1994 na Aina Maeda alikuwa mshindi wa kwanza, akifuatiwa na Shose Senare 1995, Emily Adolf 1996, Saida Kessy 1997, Basila Mwanukuzi 1998, Hoyce Temu 1999, Jacqueline Ntuyabaliwe 2000, Happiness Magese 2001, Angela Damas 2002, Sylvia Bahame 2003, Faraja Kotta 2004, Nancy Sumary 2005, Wema Sepetu 2006, Richa Adhia 2007, Nasreem Kareem 2008, Miriam Gerald 2009, Geneveive Mpangala 2010 na Salha Israel 2011.
Awali ya hapo, mwaka 1967 lilifanyika shindano la kwanza kabisa la Miss Tanzania na Theresa Shayo akashinda katika shindano lililofanyika kwenye bwawa la kuogelea la hoteli ya Kilimanjaro, lakini serikali ya Tanzania wakati huo, chini ya rais wa kwanza, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikapiga marufuku mashindano kwa sababu hayaendani na mila na desturi za Mtanzania.
Lakini Lino International Agency, ikajenga hoja ambazo ziliishawishi serikali ya Tanzania, chini ya rais wake wa pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi kuruhusu mashindano hayo yafanyike tena, ingawa mwaka 2001 yaliponea chupuchupu kufutwa tena, enzi za rais wa awamu wa tatu, Benjamin William Mkapa.
Ilitokana na vazi la kuogelea ‘kichupi’, ambalo lilipingwa kwa sababu linamdhalilisha mwanamke wa Tanzania, lakini Lino ikaboresha kipengele cha vazi hilo, kutoka la kuogelea hadi la ufukweni, ambalo kidogo linamsitiri binti na serikali ikaruhusu mashindano yaendelee.
Hata hivyo, mabinti wanapokwenda kwenye shindano la dunia, wanavaa vazi la kuogelea kupanda jukwaani, katika shindano ambalo linaonyeshwa moja kwa moja nchi zaidi ya 100 duniani na picha zao kuchapishwa kwenye majarida, magazeti na mitandao mbalimbali duniani.  

Warembo

Warembo

Irene Karugaba, mwalimu wa warembo 

Warembo

Mkuu wa Itifaki wa Kamati ya Miss Tanzania, Makoye akiwa mbele ya baadhi ya warembo

SIMBA WAENDA ZANZIBAR KUIANDALIA KIPIGO AZAM

Wachezaji wa Simba


SIMBA SC imefanya mazoezi kwenye ufukwe wa Coco leo asubuhi na wachezaji wote wameruhusiwa kurudi manyumbani kwao, kujiandaa kwa safari ya Zanzibar jioni kwenda kuweka kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya Azam FC Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa kawaida Simba SC huenda Zanzibar katikati ya Ligi Kuu kuweka kambi linapokaribia pambano dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC lakini kwa kitendo cha kwenda kujichimbia huko kwa ajili ya Azam, maana yake wanaipa uzito huo mechi hiyo.
Kikosi cha Simba kilirejea Dar es Salaam jana mchana kutoka Tanga ambako kilitoka sare ya bila kufungana na wenyeji Mgambo JKT Jumapili katika mfululizo wa ligi hiyo.
Matokeo hayo, yanaifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ingawa wameuweka rehani usukani wa ligi hiyo kwa Azam ambayo kesho inacheza na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
Azam yenye pointi 17, ikishinda itafikisha pointi 20 na kupanda kileleni, tena ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja, kwani hadi sasa imecheza mechi saba. Yanga iliyocheza mechi nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu nayo itacheza na Polisi Morogoro keshokutwa.
Baada ya sare ya Jumapili, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amewataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kuwa watulivu na wasikatishwe na tamaa na sare tatu mfululizo za timu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani safari bado ni ndefu.
Rage amesema kwamba, hadi sasa timu yao haijafungwa katika Ligi Kuu kuashiria kwamba bado ni timu bora na matokeo ya sare hizo tatu mfululizo pia ni kutokana na uimara wa timu yao.
Rage ameonya wanachama wenye desturi ya kutoa maneno ya uchochezi timu inapoyumba kidogo, waache kufanya hivyo kwa sababu wanaweza kuvuruga amani iliyopo sasa klabuni.

SIMBA SC SASA WAIGEUZIA KIBAO TFF, YANGA SAKATA LA MBUYU TWITE

Hans Poppe


SIMBA SC wamesema kwamba sasa inatosha kufanywa wajinga, wanataka kuwapa somo na Yanga ili wajue kwamba wao siyo klabu ya kuchezewa.
Kufanya wajinga kivipi na wanataka kutoa somo gani?
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba wanakusanya vielelezo vya vyombo vya Habari juu ya mwenendo mzima wa sakata la beki Mbuyu Twite na kuvipeleka Mahakama ya Usuluhishi (CAS) ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Kisa nini? Hans Poppe amesema ni ukimya wa TFF kutowapa rasmi taarifa ya hukumu ya pingamizi lao la Twite katika klabu ya Yanga na pia kushindwa hata kusimamia hukumu waliyotoa.
Lengo nini? Hans Poppe amesema wanaamini kesi hiyo ikifika CAS, Twite atafungiwa kucheza soka na hata Yanga wataadhibiwa pia kwa kufanya kitendo kisicho cha kiungwana, kumsajili mchezaji ambaye tayari alikwishaini mkataba na klabu nyingine.
“Sisi kama Simba hadi leo hatuna taarifa rasmi kutoka TFF juu ya hukumu waliyotoa katika kikao chao cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji. Tumekuwa tukisikia tu kupitia vyombo vya habari, wakati sisi tuliwasilisha pingamizi letu kwa maandishi, naamini huu si utendaji sahihi,”alisema Hans Poppe.
Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo ambaye ni Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba TFF pia iliamuru Yanga wawe wamekwishalipa fedha ambazo Twite alichukua Simba hadi kufika Oktoba 3, mwaka huu, lakini sasa mwezi huo unaelekea ukingoni na klabu yao haijalipwa.
“Tunashindwa kuelewa hii ina maana gani, kwa sababu hukumu wametoa wao, na wao ndio wenye wajibu wa kusimamia utekelezaji wake, lakini hadi leo Yanga hawajalipa na TFF pamoja na Kamati ya Sheria na Maadili wamekaa kimya, sasa sisi tunachukua hatua ambayo baadaye tusije kulaumiana,”alisema Hans Poppe.
Alisema anashangaa TFF wamekuwa wepesi katika kusimamia na kutekeleza adhabu za Simba, kwa mfano barua barua ya hukumu ya mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi kufungiwa mechi tatu waliipata mapema tu baada ya kikao cha Kamati cha Ligi kupitia ripoti ya mechi ambayo Mganda huyo aliadhibiwa.
“Tumekwishawaandikia barua ya kuwaomba hati ya hukumu siku nyingi, lakini bado hadi leo hawajatupa, sasa tunashindwa kuelewa nini lengo lao, tunafikiria wanajua tukikata rufaa CAS tutashinda, sasa wamejawa hofu na wanaogopa kutoa hukumu kwa maandishi,” alisema Hans Poppe.
Septemba 10, mwaka huu Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa ilitoa maamuzi ambayo hayakuwaridhisha walalamikaji, Simba SC juu ya Twite na Yondan na sasa wanataka kulipeleka suala hilo CAS.
Kamati hiyo, iliitaka Simba kuthibitisha madai yake ya kuingia mkataba na Yondan na kuwasilisha upya malalamiko yake kwenye kamati hiyo.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake halali.
Kwa vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika,”alisema Mgongolwa.
Kuhusu suala la Mbuyu Twite, Mgongolwa alisema kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake halali.
Hata hivyo, alisema kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Wajumbe sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.
Siku 21 walizopewa Yanga kurudisha fedha za Twite alizochukua Simba, zilimalizika Oktoba 3, siku ambayo watani hao wa jadi katika soka ya Tanzania, walimenyana katika mchezo wa Ligi Kuu, mzunguko wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kutoka sare ya 1-1.
Simba walitarajia TFF ingeikata Yanga fedha hizo katika mapato yake ya mechi hiyo, lakini hawakufanya hivyo na hadi leo pia bado hawajalipwa na ndiyo maana wanaamua kupeleka vielelezo hivyo CAS.
Mgongolwa aliwahi kuiambia BIN ZUBEIRY kwamba, kutokana na Yanga kushindwa kutekeleza agizo, hilo amemuagiza Katibu wa TFF aitishe kikao kingine cha Kamati hiyo ili kujadili hatua ya kuichukuliwa klabu hiyo kuwa kukaidi agizo hilo.
Hata hivyo, yapata wiki mbili sasa tangu Mgongolwa amesema hivyo na hakuna dalili za Kamati yake kukutana kumaliza mgogoro huo.   

YONDAN, BAHANUZI HAWAPO NA KESHO YANGA NA POLISI TAIFA

Yondan


BEKI Kevin Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi wataendelea kuwa nje ya Uwanja kesho, wakati timu yao, Yanga SC itakapokuwa ikiwania pointi tatu katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na hali zao kutoimarika na habari mbaya zaidi ni kwamba, beki Job Ibrahim naye hatashiriki mechi ya kesho.
Job, ambaye amekuwa beki wa akiba tangu mwanzoni mwa msimu, aliumia kifundo cha mguu mazoezini juzi na jana hakufanya mazoezi kabisa, wakati Yondan na Bahanuzi wanaendelea na programu ya mazoezi mepesi na hadi jana hakuna mmoja kati yao aliyekuwa tayari kuanza programu kamili ya mazoezi ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts.
Maana yake, Mbuyu Twite ataendelea kucheza pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika beki ya kati, wakati Jerry Tegete ataendelea kucheza na Didier Kavumbangu katika safu ya ushambuliaji.
‘Dogo’ Simon Msuva amemaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa Oktoba 3, mwaka huu katika mechi dhidi ya Simba na ilikuwa aanze kucheza tangu Jumamosi, ila kutokana na kiwango duni cha Hamisi Kiiza alichoonyesha kwenye mechi na Ruvu Shooting Jumamosi, kesho kinda huyo anaweza kurudishwa uwanjani.
Kiiza aliichezea Yanga kwa mara ya kwanza siku hiyo akitokea benchi kipindi cha pili, tangu atolewe kipindi cha kwanza katika mechi dhidi ya Simba, Oktoba 3, mwaka huu.
Kiiza alikuwa kwao, Uganda, alipokwenda kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes katika mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini.
Uganda ilitolewa na Zambia kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda nyumbani 1-0 na Uganda wakashinda kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
Yanga imeweka kambi katika hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam huku ikiendelea kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu, wakati Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Oktoba 8, mwaka huu.
Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 14, baada ya kucheza nane, kushinda nne, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba iliyocheza mechi tisa, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 19, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 17, iliyocheza mechi saba.

RAGE AOMBA UTULIVU SIMBA

Rage


MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amewataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kuwa watulivu na wasikatishwe na tamaa na sare tatu mfululizo za timu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani safari bado ni ndefu.
Rage amesema kwamba, hadi sasa timu yao haijafungwa katika Ligi Kuu kuashiria kwamba bado ni timu bora na matokeo ya sare hizo tatu mfululizo pia ni kutokana na uimara wa timu yao.
Rage ameonya wanachama wenye desturi ya kutoa maneno ya uchochezi timu inapoyumba kidogo, waache kufanya hivyo kwa sababu wanaweza kuvuruga amani iliyopo sasa klabuni.
Kikosi cha Simba kilirejea Dar es Salaam jana mchana kutoka Tanga na kuingia kambini moja kwa moja kuanza maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Azam FC, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba SC itakuwa na wiki nzima ya kujiandaa na mechi hiyo, ikitoka kulazimishwa sare ya tatu mfululizo jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, baada ya kutoka 0-0 na wenyeji Mgambo Shooting katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Matokeo hayo, yanaifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ingawa wameuweka rehani usukani wa ligi hiyo kwa Azam ambayo kesho inacheza na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
Azam yenye pointi 17, ikishinda itafikisha pointi 20 na kupanda kileleni, tena ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja, kwani hadi sasa imecheza mechi saba. Yanga iliyocheza mechi nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu nayo itacheza na Polisi Morogoro keshokutwa. 


RAMIRES ni 100 kwa Chelsea, THEO WALCOTT mambo bado Arsenal


Ramires 300x225
Wakati Mbrazil Ramires akisheherekea kutimiza Mechi 100 kwa Klabu yake Chelsea, hatima ya Theo Walcott Klabuni Arsenal bado haijulikani baada ya Meneja wa Klabu hiyo Arsene Wenger kukiri kuwa hamna makubaliano yaliyofikiwa kuhusu kuongeza Mkataba wake wa sasa unaomalizika mwishoni mwa Msimu.
Ramires
Kiungo wa Chelsea, Ramires, mwenye Miaka 25 na anaetoka Brazil, amesema anasikia fahari kufikisha rekodi ya kuichezea Klabu hiyo Mechi 100 hasa kwa vile kumekuwa na dhana kuwa Wachezaji wa Brazil hawawezi kuhimili mikikimikiki ya Soka la England.
Ramires, ambae alihamia Chelsea Mwaka 2010 akitokea Benfica ya Portugal, amesema: “Nina furaha kubwa kucheza Mechi 100 na Chelsea. Nimepata wakati mzuri hapa na hasa kutwaa Ubingwa wa Ulaya na lile Goli langu nilipoifunga Barcelona katika Nusu Fainali.”


Theo Walcott

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema bado hakujapatikana ufumbuzi wa sakata la Theo Walcott kukubali kusaini Mkataba mpya huku Winga hayo akiwa bado hajakubali kusaini Mkataba mpya wakati ule wa sasa unazidi kuyoyoma na utamalizika mwishoni mwa Msimu huu ambapo anaweza kuondoka kama Mchezaji huru na Arsenal kukosa senti hata moja.
Wenger amesema: “Mazungumzo yanaendelea lakini hamna jipya. Matakwa yangu ni kumuongezea Mkataba mwingine mbali ya kuwepo Klabu zinazomtaka.”
Kwa sasa Walcott yupo nje ya Uwanja baada ya kuumia kifuani alipogongana na Kipa wa San Marino alipokuwa akiichezea England kwenye Mechi ya Makundi ya kuwania kwenda Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014 huko Brazil Wiki iliyopita.


GERRARD ampa 5 RAHEEM STERLING!


 Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard amemsifia na kufurahia kuibuka kwa Kipaji Raheem Sterling, mwenye Miaka 17, ambae Jumamosi iliyopita alifunga bao pekee na kuipa ushindi Liverpool wa bao 1-0 ilipocheza na Reading Uwanjani Anfield na kumfanya aingie kwenye rekodi ya kuwa Mchezaji mwenye umri mdogo, akimfutia Michael Owen, kuifungia Liverpool.
Yeye mwenyewe Gerrard vile vile alianza kuichezea Liverpool akiwa na umri mdogo, Miaka 18 Mwaka 1998, lakini amevua kofia kwa Rahim Sterling na kutamka: “Nadhani amemshangaza kila mtu si kwamba anafanya vizuri bali kufuikia hapa akiwa na umri mdogo.”
Sterling alijiunga na Liverpool akiwa na Miaka 15 akitokea QPR na bado Liverpool haijamruhusu kuongea moja kwa moja na Wanahabari hadi atimize Miaka 18 Mwezi Desemba.


Alhamisi, Raheem Sterling ana nafasi nyingine ya kuonyesha cheche zake pale Liverpool itakapocheza Mechi ya Kundi lake la EUROPA LIGI na FC Anzhi Makhachkala Uwanjani Anfield lakini kazi kubwa ipo Jumapili Oktoba 28 huko Goodison Park watakapocheza na Mahasimu wao Everton katika Dabi ya Liverpool ambayo ni Mechi ya Lig Kuu England.
RATIBA MECHI ZIJAZO:
Jumamosi, Oktoba 27, 2012
[SAA 8 Dak 45 Mchana]
Aston Villa v Norwich City
[SAA 11 Jioni]
Arsenal v Queens Park Rangers
Reading v Fulham
Stoke City v Sunderland
Wigan Athletic v West Ham United
[SAA 12 na Nusu Jioni]
Manchester City v Swansea City
Jumapili, Oktoba 28, 2012
[SAA 10 na Nusu Jioni]
Everton v Liverpool
[SAA 12 Jioni]
Newcastle United v West Bromwich Albion
Southampton v Tottenham Hotspur
[SAA 1 Usiku]
Chelsea v Manchester United
 

‘MBAGUZI’ Terry kuvaa Utepe kupinga Ubaguzi Mechi UEFA!



FREDINAND-TERRY_MKNO_HAMNAHuku Wiki ya kuhamasisha kupinga Ubaguzi kwenye Soka Barani Ulaya ikishamiri kupitia Bodi yake, Football Against Racism in Europe, FARE, UEFA itamtaka Nahodha wa Chelsea, John Terry, kuvaa utepe unaotangaza kupinga Ubaguzi kwenye Mechi ya UEFA CHAMPIONZ LIGI huko Donetsk kati ya Shakhtar Donetsk na Chelsea itakayochezwa Jumanne.FARE
UEFA imetangaza kuwa Makepteni wa Timu zitakazocheza Mechi za UEFA CHAMPIONZ LIGI na EUROPA LIGI wataombwa kuvaa Utepe huo ili kutangaza Kampeni ya kupinga Ubaguzi katika Soka Barani Ulaya. 
Hivi juzi, John Terry alikubali adhabu aliyopewa na FA, Chama cha Soka England, baada ya kupatikana na hatia ya kumkashifu Kibaguzi Beki wa QPR Anton Ferdinand ambae ni mdogo wake Beki wa Manchester United Rio Ferdinand.
Mbali ya kukubali adhabu hiyo, John Terry pia aliomba radhi na pia kuadhibiwa na Klabu yake Chelsea kwa kupigwa Faini ambayo haikutangazwa kiwango chake.
Huko England, Kampeni nyingine ya kupinga Ubaguzi iliyoendeshwa na KICK IT OUT ilikumbwa na mgomo wa zaidi ya Wachezaji 30 wa Klabu 8 za Ligi Kuu England waliogoma kuvaa Tisheti zenye maandishi ya Kampeni hiyo kabla ya Mechi ikiwa ni kuonyesha kukerwa kwao na msisitizo hafifu wa kupinga Ubaguzi, hasa adhabu ndogo kwa Terry, na kati yao ni Anton Ferdinand, Rio Ferdinand na Jason Roberts.

UEFA CHAMPIONZ LIGI: 7 zawania kuendelea Ushindi wao wa Asilimia 100!!


>>MAN UNITED kutimiza Mechi 150 OLD TRAFFORD=Ushindi 104, Sare 35, kufungwa 10 tu!!
Click to zoom

Jumanne na Jumatano, UEFA CHAMPIONZ LIGI inaiingia kwenye Mechi Dei 3 ikiwa ni Raundi ya 3 ya Mechi za Makundi na zipo Timu 7, ambazo ni FC Porto, Arsenal, Real Madrid, Barcelona, Manchester United, Malaga na BATE Borisov, ambazo zimeshinda Mechi zao zote mbili za kwanza na zitataka kudumisha rekodi hiyo.
Kwenye Raundi hii ya Mechi Dei 3, Timu zitacheza na mpinzani mmoja, nje na ndani, yaani kucheza nyumbani na kisha kurudiana na mpinzani huyo huyo ugenini.
+++++++++++++++++++++++++++++++
RATIBA MECHI ZIJAZO:
[MECHI ZOTE Saa 3 Dakika 45 Usiku isipokuwa inapotajwa]
Jumanne Oktoba 23
FC Nordsjælland v Juventus
FC Shakhtar Donetsk v Chelsea FC
FC BATE Borisov v Valencia CF
LOSC Lille v FC Bayern München
FC Spartak Moskva v SL Benfica [SAA 1 USIKU]
FC Barcelona v Celtic FC
Galatasaray A.S. v CFR 1907 Cluj
Manchester United FC v SC Braga
+++++++++++++++++++++++++++++++

IFUATAYO NI TATHMINI YA KILA MECHI ZA Jumanne:
KUNDI E
Nordsjaelland v Juventus
Shakhtar Donetsk v Chelsea
MSIMAMO:
[Kila Timu imecheza Mechi 2]
KUNDI E
Chelsea Pointi 4
Shakhtar Donetsk 4
Juventus 2
Nordsjaelland 0

TATHMINI:
Meneja wa Chelsea Roberto di Matteo, tangu ashike wadhifa hapo, hajafungwa katika Mechi 8 za UEFA CHAMPIONZ LIGI na ameshinda Mechi 5 na sare 3 lakini Mechi hii itakayochezwa huko Donetsk ni ngumu.
Shakhtar Donetsk wapo Pointi sawa na Chelsea kwenye Kundi hili na katika Mechi yao ya mwisho ya Kundi hili walicheza vyema walipotoka sare ya 1-1 na Juventus huko Turin.
Shakhtar hawajafungwa na Timu ya England wakiwa kwao baada ya kushinda Mechi 3 na sare moja.
Juventus, ingawa wako kileleni huko kwao kwenye Serie A, hawajashinda katika Mechi 8 za Ulaya na zote wametoka sare lakini mechi hii na Nordsjaelland, ambao ni Timu mpya kwenye Mashindano haya, inawapa fursa njema ya ushindi.
+++++++++++++++++++++++++++++++
KUNDI F
BATE Borisov v Valencia
Lille v Bayern Munich
MSIMAMO:
[Kila Timu imecheza Mechi 2]
KUNDI F
BATE Borisov Pointi 6
Valencia 3
Bayern Munich 3
Lille 0
TATHMINI:
BATE Borisov wameanza kwa kishindo kwenye Kundi hili kwa kushinda Mechi zao zote mbili ikiwemo kipigo cha Bao 3-1 walichowashushia Wakongwe Bayern Munich. Chini ya Kocha Viktor Goncharenko na Mastraika wawili hatari Renan Bressan na Vitali Rodionov, BATE Borisov wameshapiga bao 6.
Wapinzani wa BATE Borisov, Valencia, walijikongoja hivi juzi kwenye Ligi yao huko Spain, La Liga, kwa kuifunga Athletic Bilbao bao 3-2.
Baada ya kuteleza na kuchapwa 3-1 na BATE Borisov, Bayern Munich watataka kurekebisha mambo kwa kuitwanga Lille ambayo haina hata Pointi kwenye Kundi hili.
+++++++++++++++++++++++++++++++
KUNDI G
Spartak Moscow v Benfica
Barcelona v Celtic
MSIMAMO:
[Kila Timu imecheza Mechi 2]
KUNDI G
Barcelona Pointi 6
Celtic 4
Benfica 1
Spartak Moscow 0
TATHMINI:
Wakikabiliwa na uhaba wa Mabeki ambapo Mabeki wao wanne wa Timu ya kwanza ni majeruhi, katika Siku za hivi karibuni Barcelona wamekuwa wakivujisha magoli kibao lakini Washambuliaji wao, na hasa Supastaa wao Lionel Messi, amekuwa akihakikisha wanafunga bao moja zaidi na kuwapa ushindi na hili limedhihirika hivi juzi walipoifunga Deportivo La Coruna bao 5-4 huku Messi akipiga hetitriki.
Barca itabidi wagangamale watakapocheza na Celtic ya Scotland wanaosifika kwa kupigana kiume.
Mechi nyingine ya Kundi hili ni ile kati ya Spartak Moscow na  Benfica ambapo kwa kila mmoja ushindi ni muhimu hasa baada ya kutofanya vyema katika Mechi zao za kwanza.
+++++++++++++++++++++++++++++++
Group H
Galatasaray v Cluj
Manchester United v Sporting Braga
MSIMAMO:
[Kila Timu imecheza Mechi 2]
KUNDI H
Manchester United Pointi 6
CFR Cluj 3
Braga 3
Galatasaray 0
TATHMINI:
Wako Pointi 3 juu kwenye Kundi hili, Manchester watataka kusherehekea Mechi yao ya 150 ya nyumbani Old Trafford kwa ushindi ili kuidumisha rekodi yao ya Mechi za Klabu Ulaya ya kushinda Mechi 104, sare 35 na kufungwa Mechi 10 tu na hilo linaonekana lina uwezekano baada ya Nyota wao Wayne Rooney na Robin van Persie kuonyesha ushirikiano ambao ni hatari kwa wapinzani.
Huko Instanbul, Uturuki, Galatasaray hawana budi ila kusaka ushindi kwa udi na uvumba baada ya kutwangwa Mechi mbili mfululizo.
RATIBA MECHI ZIJAZO:
[MECHI ZOTE Saa 3 Dakika 45 Usiku isipokuwa inapotajwa]
Jumatano Oktoba 24
FC Porto v FC Dynamo Kyiv
GNK Dinamo v Paris SaintvGermain FC
Arsenal FC v FC Schalke 04
Montpellier Hérault SC v Olympiacos FC
FC Zenit St. Petersburg v RSC Anderlecht [SAA 1 USIKU]
Málaga CF v AC Milan
AFC Ajax v Manchester City FC
Borussia Dortmund v Real Madrid CF
++++++++++++++++++++++++++

BAADA YA KUVULIWA UBINGWA SASA ARMSTRONG ADAIWA FEDHA ALIZOSHINDA.

NYOTA wa zamani wa mbio baiskeli, Lance Armstrong atalazimika kulipa fedha alizopata kama mshindi wa michuano ya Tour de France baada ya kunyang’anywa mataji yote saba aliyoshinda baada ya kukutwa na hatia ya kutumia madawa ambayo yamekatazwa michezoni. 
 
Muungano wa Kimataifa wa Waendesha Baiskeli-UCI ulimvua ubingwa wote aliopata Armstrong kuanzia Agosti mosi mwaka 1998 Jana. Mkurugenzi wa michuano ya Tour de France Christian Prudhomme alikubaliana na uamuzi wa UCI na kuongeza kuwa sheria za muungano huo ziko wazi kwamba mtu yoyote atakayevuliwa ubingwa atalazimika kulipa fedha alizopewa kama mshindi.
 
 Inakadiriwa kuwa Armstrong amepata kiasi cha paundi milioni 2.4 kwa kushinda michuano ya Tour de France katika kipindi cha miaka saba mfululizo kuanzia mwaka 1999 mpaka mwaka 2005.

GYAN NAHODHA MPYA BLACK STARS.

Asamoah Gyan
KOCHA wa timu ya taifa ya Ghana, Kwesi Appiah ametangaza kuwa Asamoah Gyan ameteuliwa kuwa nahodha mpya wa kikosi hicho maarufu kama Black Stars. Uteuzi huo mpya unafuatia uamuzi wa kumuengua John Mensah katika nafasi hiyo ambayo amekuwa akishikilia kwa kipindi kirefu. Akihojiwa kuhusu uteuzi wake huo Appiah amesema kuwa Mensah ataendelea kuwa mjumbe muhimu katika kikosi chake lakini kwasasa ameamua kufanya mabadiliko kwa ajili ya faida ya nchi hiyo. Appiah aliwaomba wachezaji na wadau wa soka nchini humo kumpa ushirikiano Gyan ili aweze kuingoza Ghana kupata mafanikio katika changamoto zilizoko mbele yao.

CHIPOLOPOLO KUKWAANA NA BAFANA BAFANA SOCCER CITY.

RAIS wa Chama cha Soka nchini Zambia-FAZ, Kalusha Bwalya amethibitisha kuwa mabingwa wa Afrika watachuana katika mchezo dhidi ya Bafana Bafana katika Uwanja wa Soccer City jijini Johannesburg Novemba 14 mwaka huu. Mchezo baina ya timu hizo umekuwa ukijulikana muda mrefu lakini uwanja ambao ungetumika kwa ajili ya mchezo ndio ulikuwa haujajulikana mpaka Bwalya alipothibisha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter. Itakuwa ni mara ya tatu kwa Bafana Bafana kuutumia uwanja huo ambao ulijengwa upya kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 ambapo mara ya kwanza kuutumia uwanja huo waliifunga Colombia mabao 2-1 katika mchezo wa kujipiama nguvu na baadae kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mexico katika mchezo wa ufunguzi. Afrika Kusini imecheza na Zambia mara nyingi zaidi toka nchi hiyo iliporuhusiwa kucheza michezo ya kimataifa mwaka 1992 ambapo wamekutana mara 14 huku kila nchi ikishinda michezo minne na kutoa sare michezo sita.

PIQUE KUIKOSA CELTIC.

MENEJA wa klabu ya Barcelona, Tito Vilanova amesema kuwa beki wake wa kati Gerard Pique atakosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Celtic leo usiku baada ya kushindwa kupona mguu. Majeruhi katika kikosi cha Vilanova limekuwa tatizo sugu hususani mabeki wake tegemeo kama Eric Abidal, Carles Puyol na Dani Alves kupata majeruhi ya mara kwa mara kitu ambacho kimekuwa kikiwapa wakati mgumu msimu huu. Mwishoni mwa wiki Barcelona ilipata ushindi wa tabu wa mabao 5-4 dhidi ya Deportivo Coruna huku ikishuhudia beki wake wa kati aliyebakia Sergio Busquets naye akipewa kadi nyekundu katika mchezo huo. Lakini Vilanova amesema kuwa kuwakosa nyota wake hao haiwezi kuwa sababu ya wao kushindwa kufanya vyema katika mchezo wa leo. Barcelona ndio wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga wakifuatiwa na Atletico Madrid ambao wamepisha kwa tofauti ya mabao lakini wakiwa wameruhusu wavu wao kutikiswa mara 11 sawa na Osasuna ambao wanashika mkia katika ligi hiyo.

FEDERER AANZA VYEMA MICHUANO YA SWISS INDOORS.

MCHEZAJI nyota wa tenisi namba moja katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanaume, Roger Federer ameanza vyema kampeni yake ya kutafuta taji la sita la michuano ya ndani ya Switzerland baada ya kumfunga Benjamin Becker kwa 7-5 6-3 na kutinga hatua ya pili ya michuano hiyo. Becker raia wa Ujerumani ambaye anashika nafasi ya 83 katika orodha hizo aliingia katika michuano hyo kuchukua nafasi ya Jeremy Chardy kutoka Ufaransa ambaye aliumia. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Federer amesema kuwa alijiandaa vyema kukabiliana na Becker ambaye mara ya mwisho kucheza naye ilikuwa mwaka 2010 baada ya Chardy kuumia hivyo anashukuru kumfunga mjerumani huyo na kusonga mbele. Federer ameshinda mataji matano kati ya sita ya michuano hiyo ambayo inachezwa katika viwanja vya St Jacobshalle ambako ndiko nyota huyo alipoanzia kucheza tenisi akiwa kama muokota mipira miongo miwili iliyopita.

No comments:

Post a Comment