Thursday, October 4, 2012

MWINYI KAZIMOTO YUKO FITI 100%, ILIKUWA MISULI TU, SIMBA HAINA MAJERUHI, YACHEZA MECHI KINESI LEO

Mwinyi Kazimoto


KIUNGO Mwinyi Kazimoto Mwitula yupo fiti kabisa kuendelea kuitumikia Simba SC katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, licha ya jana kuumia katika mchezo dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga.
 
 
Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga amesema  mida hii kwamba wachezaji wote wa Simba wapo fiti, bali kuna wachache wanaokabiliwa na uchovu wa kawaida wa mechi.
 
 
“Kazimoto ni misuli tu ilimshika jana, yuko fiti kabisa, hana maumivu, kwa kifupi sina majeruhi,”alisema Kapinga.
 
 
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba wachezaji ambao hawakucheza mechi ya jana, leo watacheza mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Kinesi jioni.
 
 
“Kuna utaratibu ambao tunao ili kutunza viwango vya wachezaji wetu, siku moja baada ya mechi ya Ligi, wachezaji wote ambao hawakucheza, wanacheza mechi ya kirafiki, sasa leo pia kuna mechi hiyo jioni Uwanja wa Kinesi,”alisema Kamwaga.  
 
 
Simba jana ilishindwa kuendeleza ubabe wake kwa Yanga, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao hao wa jadi, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02 usiku.
 
 
Yanga ambao walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso, ndio waliohaha kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la kiungo Amri Kiemba.  
 
 
Hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba dakika ya pili.
 
 
Simba walicheza vizuri kipindi chote cha kwanza wakigongeana pasi za uhakika na kuwazidi kasi uwanjani wapinzani wao, wakati Yanga pamoja na kuzinduka baada ya kufungwa bao, lakini makosa yalikuwa mengi.
 
 
Pasi zao zilikuwa nyingi hazifiki, walikuwa wanapokonyeka mipira kirahisi, wanazidiwa nguvu na wapinzani wao katika kugombea mipira na hata mashambulizi yao hayakuwa ya mpangilio, zaidi ya kuonekana kubahatisha zaidi.
 
 
Katika kubahatisha huko, Mbuyu Twite alifumua shuti zuri dakika ya 38 kutoka wingi ya kulia, ambalo lilitoka nje sentimita chache.    
 
 
Kabla hata ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika, kocha Mholanzi Ernie Brandts alimtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Frank Domayo ili kuimarisha safu ya kiungo, ambayo ilionekana kuzidiwa na Simba inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick.
 
 
Kipindi cha pili, Yanga walianza na mabadiliko, kocha Ernie Brandts akimtoa kiungo Nizar Khalfan na kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu, ambaye alikwenda kuongeza nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
 
 
Angalau, kipindi cha pili Yanga walionekana kucheza vizuri na kupeleka mashambulizi yenye uhai langoni mwa Simba, ingawa safu imara ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi ilikuwa kikwazo.
 
 
Katika dakika ya 63, beki Paul Ngalema aliunawa mpira katika harakati za kuokoa na refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani kiufundi na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
 
 
Katika dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso, aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’. 
 
 
Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari refa alikwishapuliza filimbi na kumpa kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na hasira za kitoto.
 
 
Pamoja na Yanga kubaki pungufu, waliendelea kucheza vema na mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili. Refa Akrama alishindwa kuumudu mchezo na maamuzi yake mengi yalikuwa chungu kwa Yanga, mfano Haruna Moshi ‘Boban’ alipomchezea rafu mbaya beki Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake ikachukuliwa na Juma Abdul alimpoza kwa kadi ya njano.
 
 
Hakumchukulia hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana kupoteza muda tangu mwanzo, na alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.
 
 
Alipingia Abdul alikwenda kucheza beki ya kulia na Mbuyu Twite akahamia katikati kucheza na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
 
 
Baada ya mchezo huo, kocha wa Simba, Milovan alisema kwamba ulikuwa mchezo mzuri na Yanga walicheza vizuri, lakini timu yake ilicheza vizuri na anajivunia. Alisema Yanga imeimarika tofauti na ilivyokuwa awali na kwamba hizo ni dalili Ligi Kuu msimu huu itakuwa ngumu.
 
 
Kwa upande wake, kocha wa Yanga, mwanzoni hawakucheza vizuri, lakini baadaye walitulia na kucheza vizuri. “Hii ni mechi ya kweli ya upinzani, unaweza kuona rafu na kadi nyingi,”alisema Brandts.
 
 
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 13, ndani ya mechi tano na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, wakati Yanga imefikisha pointi nane na kubaki nafasi ya tano, kwani Coastal Union imetoa sare ya 2-2 na JKT Oljoro mjini Arusha na kufikisha pointi tisa.   
 
 
 
SIMBA: Juma Kaseja, Nassor Chollo, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Shomary Kapombe, Jonas Mkude/Haruna Moshi, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Edward Christopher/Daniel Akuffo na Mrisho Ngassa.
 
 
YANGA: Yaw Berko, Mbuyu Twite, Stefano Mwasyika, Nadir Cannavaro, Kevin Yondan/Juma Abdul, Athumani Iddi, Simon  Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza/Frank Domayo na Nizar Khalfan/Didier Kavumbangu.

MATUKIO MBALIMBALI SIMBA NA YANGA JANA TAIFA NDANI NA NJE YA UWANJA

Ally Mustafa 'Barthez' akisalimiana na Amri Kiemba baada ya mechi

Barthez na Chollo

Waghana; Yaw Berko na Daniel Akuffo wa Simba

Barthez na Kaseja

Kocha wa Yanga, Ernie Brandts


Simba wanapsaha


Yanga wanapasha


Msafiri Mgoyi kazini


Mashabiki wa Simba


Kiemba akipongezwa kwa bao la kuongoza


Simba wakishangilia bao la kutangulia


Bahanuzi anaweka mpira gambani mbele ya Kapombe, Paul Ngalema akiwa tayari kusaidia


Hapa Bahanuzi alimuumiza Kapombe, anatibiwa huku wachezaji wa Simba wakimlalamikia refa Akrama 


Hesabu za Kapombe kwenye mpira...kubali, kataa, dogo bonge la beki


Kapombe anamdhibiti Bahanuzi


Haruna anatafuta maarifa ya kumtoka Jonas Mkude


Cannavaro chupuchupu afunge kwa kichwa hapa


Paul Ngalema akimdhibiti Kiiza Diego


Niyonzima akimsema ovyo Nyosso baada ya kufanyiwa 'undavaku'


Nizar Khalfan kulia na Mrisho Ngassa kushoto


Mrisho anamkaba Mwasyika


Mashabiki wa Simba


Chollo anamdhibiti Bahanuzi


Kavumbangu anawashughulisha mabeki wa Simba..ameenda hewani kutoa pasi ya kichwa kwa Bahanuzi
Iddi Moshi akiingia na mwanawe Amran

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga katikati

Kocha Mkuu wa taifa Stars, Kim Poulsen kulia, katikati kocha wa timu za vijana, Jacob Michelsen na mpenzi wake kushoto 

Makamu Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Isaac Shekiondo

Wadau

Alex Mgongolwa kushoto akiwa na Mohamed Bhinda
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange 'Kaburu' kulia akiwa na beki na kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo
Alikuwa anaangalia mpira nyuma ya lango la Simba
Simba wanaingia

Friends Of Simba 'wanakaba'

Friends Of Simba 
Yanga wanapasha
Vigogo wa Simba

No comments:

Post a Comment