PREVIEW SIMBA NA YANGA LEO, KAZI IPO TAIFA
Mechi iliyopita...5-0 |
VIKOSI VYA LEO:
SIMBA: Juma Kaseja, Nassor Chollo, Paul Ngalema, Juma Nyosso,
Shomary Kapombe, Amri Kiemba, Edward Christopher, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu,
Haruna Moshi na Mrisho Ngassa.
BENCHI: Wilbert Mweta, Komabil Keta, Paschal Ochieng, Kiggi
Makassy, Salum Kinje, Daniel Akuffo, Abdallah Juma na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
KOCHA; Milovan Cirkovick (Serbia)
![]() |
Yanga SC |
YANGA: Yaw Berko, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Cannavaro,
Kevin Yondan, Athumani Iddi, Simon Msuva,
Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza.
BENCHI: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Godfrey Taita,
Stafano Mwasyika, Job Ibrahim, Frank Domayo, Nizar Khalfan, Shamte Ally, Idrisa
Rajab na Jerry Tegete.
KOCHA; Freddy Minziro
![]() |
Simba SC |
WATANI wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga
wanashuka dimbani leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambao utarushwa moja kwa moja na
Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini, kuanzia saa 11:00 jioni.
Simba, ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, wanaingia
kwenye mchezo wa leo, wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 5-0 katika
mchezo uliopita Mei 6, mwaka huu dhidi ya wapinzani hao wa jadi.
Aidha, Simba inaingia kwenye mchezo wa leo, ikiwa inaongoza
Ligi, baada ya kushinda mechi zake zote nne na kuvuna pointi 12, wakati Yanga inashika nafasi ya
tano kwa pointi zake saba, zilizotokana na sare moja, kufungwa mechi moja na
kushinda mbili katika mechi nne ilizocheza.
Simba inatokea Zanzibar ilipoweka kambi kwa zaidi ya wiki
moja kujiandaa na mchezo huo, wakati Yanga wanatokea hapa hapa Dar es Salaam,
Double Tree By Hilton, walipoingia Jumapili usiku wakitokea Uplands,
Changanyikeni walipoanzia kuweka kambi yao.
Simba leo itawakosa beki wake Amir Maftah na mshambuliaji
wake Emmanuel Okwi, ambao wanatumikia adhabu za kadi nyekundu, wakati Yanga ina
majeruhi mmoja tu na wa muda mrefu, Salum Telela.
Hapana shaka, Mserbia Milovan Cirkovick ataendelea kuwapanga
pamoja Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ na Felix Sunzu katikati na Mrisho Ngassa na
Edward Christopher watashambulia kutokea pembeni.
Yanga kadhalika- kuna uwezekano Freddy Felix Minziro akawatumia
Didier Kavumbangu na Said Bahanuzi katikati na Hamisi Kiiza na Simon Msuva
watashambulia kutokea pembeni.
Haruna Niyonzima katika kiungo cha Yanga na Mwinyi Kazimoto
katika kiungo cha Simba ni burudani nzuri inayotarajiwa Taifa leo.
Amri Kiemba atacheza kama kiungo wa ulinzi upande wa Simba, wakati
kwa Yanga bila shaka atakuwa Athumani Iddi ‘Chuji’.
Beki wa kulia wa Yanga atakuwa Juma Abdul au Mbuyu Twite, wakati
kushoto atakuwapo Oscar Joshua au Mbuyu hata Stefano Mwasyika.
Beki wa kulia wa Simba bila shaka atakuwa Nassor Masoud
‘Chollo’ na kushoto atakuwa Paul Ngalema, au Kiggi Makassy.
Katikati Yanga, Minziro anaweza kuamua kumpanga Nadir Haroub
‘Cannavaro’ na Kevin Yondan na haitakuwa ajabu pia Twite akimuweka benchi
mmojawao.
Simba hapana shaka Milovan ataendelea kuwachezesha pamoja
katikati Shomary Kapombe na Juma Nyosso. Langoni Simba piga, ua atasimama
Kaseja tu labda awe mgonjwa wa kushindwa kucheza hata kwa sindano ya ganzi.
Yanga bila shaka atadaka Mghana Yawe Berko.
JE WAJUA?
1.Mara ya
mwisho Simba na Yanga kukutana ilikuwa ni Mei 6, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam na Wekundu wa Msimbazi walishinda 5-0, mabao ya yakifungwa na Emmanuel
Okwi (dk 2 na 62), Felix Sunzu (penalti 56), Juma Kaseja (penalti dk 67) na
Patrick Mafisango (penalti dk 72).
2.Pambano la
kwanza la Ligi Kuu, wakati huo klabu ya bingwa ya taifa baina ya watani wa jadi
lilifanyika Juni 7, mwaka 1965 Uwanja wa Ilala (sasa Karume), wakati huo Simba
bado inaitwa Sunderland na Yanga ndio walioshinda mechi hiyo, bao pekee la Mawazo
Shomvi dakika ya 15.
3.Ushindi
mkubwa zaidi kwa Yanga dhidi ya watani wao wa jadi, Simba ni wa mabao 5-0 Juni
1, 1968, siku hiyo Maulid Dilunga ‘Mexico’ akifunga mabao mawili katika dakika
ya 18 kwa penalti na na 43, wakati mengine yalifungwa na Salehe Zimbwe dakika
ya 54 na 89 na Kitwana Manara dakika ya 86.
4.Ushindi mkubwa
kwa Simba dhidi ya Yanga ulikuja Julai 19, mwaka 1977, mabao 6-0 Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam- siku hiyo Abdallah ‘King’ Kibadeni akifunga mabao matatu
peke yake katika dakika za 10, 42 na 89 wakati mengine yalifungwa na Jumanne
Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73 na beki wa Yanga, Suleiman Sanga
akajifunga dakika ya 20.
5.Sare ya
mabao 4-4 Novemba 9, mwaka 1996 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha,
inabakia kuwa sare ya kihistoria katika mapambano ya watani wa jadi kufungana
mabao mengi. Mabao ya Yanga yalifungwa na Edibilly Lunyamila kwa penalti dakika
ya 28, Mustafa Hozza alijifunga dakika ya 64, Said Mwamba 'Kizota' dakika ya 70
na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ dakika ya 75. Simba mabao yao yalifungwa na Thomas
Kipese dakika ya saba, Ahmed Mwinyimkuu dakika ya 43 na Dua Saidi dakika ya 60
na 90.
6.Leo Yanga
inatarajiwa kuongozwa na kocha mzalendo, beki wake wa zamani Freddy Felix
Minziro wakati Simba ina Mserbia, Milovan Cirkovic- hii ni mara ya pili
mfululizo benchi la Yanga kuwa na kocha mzawa katika mechi dhidi ya watani,
kwani hata Mei 6, timu hiyo ikilala 5-0, kocha alikuwa huyo huyo. Kabla ya
hapo, kocha mzalendo wa mwisho Yanga kuiongoza timu hiyo dhidi ya Simba alikuwa
Kenny Mwaisabula mwaka 2004.
7.Hadi sasa, Juma
Kaseja ndiye mchezaji wa Simba aliyecheza mara nyingi zaidi dhidi ya Yanga,
mara 23, akifuatiwa na Malota Soma mara 21. Kaseja akipangwa leo, atafikisha
mechi 25 za kucheza kwenye mapambano ya watani wa jadi, tangu mwaka 2003
ikiwemo na ile ya Aprili 19, 2009 aliyoidakia Yanga dhidi ya Simba SC, mechi
yake ya kwanza ikiwa ni ya Aprili 20, mwaka 2003 akikaribishwa na kipigo cha
mabao 3-0, yaliyotupiwa nyavuni na Kudra Omary dakika ya 30, Heri Morris dakika
ya 32 na Salum Athumani dakika ya 47.
8.Kenneth Pius
Mkapa anabakiwa kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi za Simba na Yanga, 33
akifuatiwa na Edibily Lunyamila pia wa Yanga aliyecheza mechi 26, Kaseja 24, Malota
Soma 21.
9.Hili
linakuwa pambano la 12, kwa watani wa jadi kukutana Uwanja mpya wa Taifa tangu
ufunguliwe, awali katika mapambano 11 yaliyopita, Yanga ilishinda mechi tano,
Oktoba 26, 2008 (1-0), Oktoba 29, 2011 (1-0), Julai 10, 2011 (1-0), Desemba 25,
2009 (2-1) na Agosti 18, 2010, iliposhinda kwa penalti 3-1 baadaya ya sare 0-0,
wakati Simba imeshinda mechi nne, Oktoba 31, 2009 (1-0), Aprili 18, 2010 (4-3),
Agosti 17, 2011 (2-0) na Mei 6, 2012 (5-0), wakati timu hizo zimetoka sare mara
mbili Uwanja huo, Aprili 19, 2009 (2-2) na Machi 5, 2011 (1-1).
No comments:
Post a Comment