Thursday, December 20, 2012

SALUM KINJE WA SIMBA MGONJWA, ASHINDWA KUFANYA MAZOEZI


KIUNGO wa Simba Salim Kinje leo alishindwa kufanya mazoezi ya asubuhi na wenzake kutokana na kuugua malaria

Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu wanafanya mazoezi ya ufukweni  Coco Beach jijini Dar es Salaam wakijiandaa na mzunguko wa pili.

Akizungumza nleo jijini wakati wenzake wakiwa mazoezini Kinje alisema kuwa ugonjwa huo ulimuanza tangu juzi na kwamba anaendelea kutumia dawa.

"Sijajumuika na wenzangu kwani naumwa na malaria ambayo yalinianza jana(juzi) lakini hata hivyo naendelea vizuri kwani dawa ninazotumia zinanisaidia," alisema.

Wakati huo huo wachezaji wa kikosi hicho wamefurahishwa kumuona kiungo mchezeshaji Haruna Moshi 'Boban' akijumuika nao katika mazoezi hayo.

Mbiyavanga, Salum Kinje wawa kivutio mazoezini Simba

Ramadhani Chombo 'Redondo' alisema kuwa Haruna Moshi ni mchezaji muhimu sana na kwamba kikosi chao kitazidi kuimarika.

"Sisi hatuna kubwa la kuongea zaidi ya kufurahi kumuona akijumuika nasi katika mazoezi,hii inaashiria kuwa timu inazidi kuimarika," alisema.

Mara baada ya mazoezi hayo kumalizika majira ya saa 2:56 asubuhi Boban alipanda gari yake aina ya Toyota Corola yenye namba za usajili T4920 CAT na kuondoka.

Boban alisimamishwa na uongozi wa timu hiyo baada ya kudanganya kuwa ni mgonjwa na kuachwa katika safari ya kwenda Tanga kupambana na Mgambo Shooting.

Hata hivyo kesho yake wakati Simba ikikwaana na Mgambo katika uwanja wa Mkwakwani Boban alionekana jijini Dar es Salaam akicheza mpira wa mchangani maarufu kama 'Ndondo'.

 

AZAM KUTINGA FAINALI LEO DRC?

Mwaikimba ataendelea kucheka na nyavu leo?
AZAM FC inashuka dimbani leo kumenyana na Shark FC katika Nusu Fainali ya Kombe la Hisani mjini hapa, kwenye Uwanja wa Martyrs.
Awali, Shirikisho la Soka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC), liliitaka Azam FC kucheza mechi moja zaidi, baada ya kufuzu Nusu Fainali, lakini baada ya majadiliano, mpango huo umefutwa na leo Wana Lamba Lamba wanacheza Nusu Fainali moja kwa moja.
Azam iliingia Nusu Fainali juzi baada ya kuilaza Real de Kinshasa kwenye Uwanja huo huo wa Martyrs, shukrani kwao, washambuliaji Gaudence Mwaikimba na Seif Abdallah waliofunga mabao hayo, moja kila kipindi.
Ikiongezewa nguvu na nyota wake watatu, Kipre Tchetche, Kipre Balou raia wa Ivory Coast na Mkenya, Joackins Atudo waliochelewa mechi mbili za awali, Azam juzi ilitawala mchezo na kama si rafu za wapinzani wao, ingevuna ushindi mtamu.
Hadi mapumziko, tayari Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na Mwaikimba dakika ya 21, ambaye aliunganisha pasi nzuri ya Kipre kutoka wingi ya kushoto.
Hilo lilikuwa bao la pili kwa Mwaikimba, mshambuliaji wa zamani wa Kahama United, Ashanti United, Yanga, Prisons na Kagera Sugar katika mechi tatu za mashindano haya alizocheza, awali alifunga katika sare ya 1-1 na Dragons.
Kipre Tchetche alilazimika kutoka nje ya Uwanja dakika ya 43 kutokana na rafu za wachezaji wa Real, nafasi yake ikichukuliwa na Samih Hajji Nuhu.
Real walikuwa wakipiga kiatu haswa na kiungo Waziri Salum aliungana na Kipre Tchetche kuuacha Uwanja kabla ya filimbi ya kuugawa mchezo, ingawa nafasi yake ilichukuliwa na Uhuru Suleiman dakika ya kwanza ya kipindi cha pili.
Awali ya hapo, refa Madila Achille alimtoa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 43 beki Muipalayi Igongo kwa kumchezea rafu mbaya Gaudence Mwaikimba, ambayo chupuchupu naye imtoe nje, kiasi cha kulazimika kumalizia mechi akichechemea.
Kipindi cha pili, Azam waliendelea kuwafundisha soka Real na katika dakika ya 73, kazi nzuri ya Mwaikimba ilisaidia kupatikana bao la pili. Mpira mrefu uliopigwa na kipa Mwadini Ally, Mwaikimba aliumiliki vema, akatoa pasi pembeni kushoto kwa Hajji Nuhu ambaye aliingia ndani kidogo na kukata krosi maridadi iliyounganishwa kimiani na Seif.
Humphrey Mieno alikuwa mwathirika mwingine wa rafu za Real, baada ya kulazimika kutoka nje dakika ya 77, akimpisha Abdi Kassim ‘Babbi’.
Azam walionekana kuridhika baada ya kuwa wanaongoza mabao 2-0 na wakafanya uzembe uliowapa bao la kufutia machozi Real, lililofungwa na Bisole Panzu dakika ya 78.
Katika mechi zake mbili za awali za Kundi B, Azam ilitoka 1-1 na Dragons na ikafungwa 2-0 na Shark FC.
Nusu Fainali nyingine itachezwa kesho wakati Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili na Azam itaondoka hapa Jumatatu kurejea nyumbani.

KIIZA AWASILI YANGA

Kiiza

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ amewasili jana Dar es Salaam jana kujiunga na timu yake, Yanga SC baada ya mapumziko kufuatia mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge.
Kiiza aliyeiongoza Uganda kutwaa ubingwa mjini Kampala, Uganda aliomba mapumziko baada ya Kombe la Challenge na jana amerejea rasmi kazini.
Yanga inatarajiwa kwenda kuweka kambi Uturuki, Desemba 28, mwaka huu kujiandaa na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame pamoja na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kikosi kizima cha Yanga kipo kambini Dar es Salaam, kikijifua vikali chini ya kocha wake Mkuu, Mholanzi Ernie Brandts.
Yanga imepania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kutetea Kombe la Kagame, michuano ambayo itafanyika Januari mwakani mjini Kigali, Rwanda.       

UMONY AOMBA UDHURU AZAM

Umony

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Brian Umony atajiunga na klabu yake mpya, Azam FC baada ya sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya, imeelezwa.
Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa alisema jana  kwamba, Umony ameomba aje kuanza kazi baada ya sikukuu na uongozi umemkubalia.
Azam inatarajiwa kuondoka hapa mapema Jumatatu kurejea Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mashindano ya Kombe la Hisani mjini hapa Jumapili.
Nassor amesema timu ikirejea Dar es Salaam wachezaji watapewa mapumziko ya siku mbili kwa ajili ya sikukuu na baada ya hapo, watarudi kambini tayari kwa safari ya Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi.
A
zam ambao ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi, leo watacheza mechi ya Nusu Fainali na Shark FC Uwanja wa Martyrs na Jumapili watacheza mechi ya mwisho, iwe ya kusaka mshindi wa tatu au ubingwa, itategemea na matokeo ya leo.

KIUNGO AZAM NJE WIKI MBILI

Waziri akisaidiwa na makipa wa timu yake kutoka uwanjani
KIUNGO Waziri Salum wa Azam FC, atakuwa nje ya Uwanja kwa wiki mbili kufuatia kuumia katika mchezo wa juzi dhidi ya Real de Kinshasa kwenye Uwanja wa Martyrs mjini hapa.
Daktari wa Azam FC, Mjerumani Paulo Gomez alisema jana toka  mjini kishansa kwamba Waziri ameumia mfupa wa pembeni wa paja la kushoto na kwa sababu hiyo atakuwa nje kwa muda wiki mbili akipata matibabu.
Kocha Muingereza Stewart Hall amepokea kwa masikitiko taarifa hizo, akisema Waziri ni mchezaji ambaye anainukia vizuri Azam na kumkosa katika mashindano haya litakuwa pigo kwake.
Hata hivyo, Stewart alisema atatumia wachezaji wengine wakati akimsubiri kiungo huyo Mzanzibari apate ahueni.
Waziri amecheza mechi zote tatu za Azam katika mashindano haya hadi juzi alipoumia dakika ya 43 na kutoka nje.
Kiungo huyo amekuwa akionyesha soka maridadi katika mashindano haya na kuashiria kwamba ataibeba Azam katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho mwakani.
Wachezaji wengine majeruhi Azam ni kiungo Mzanzibari pia, Abdulhalim Humud anayesumbuliwa na maumivu ya nyama za paja na mshambuliaji John Bocco, ambao wamebaki Dar es Salaam. 


YAYA TOURE NI BORA AFRIKA 2012

>>WACHEZAJI wa NDANI AFRIKA: MSHINDI ABOUTRIKA!!
>>TIMU BORA: ZAMBIA, KOCHA BORA wa ZAMBIA: HERVE RENARD!!
>>TUZO ya NGULI: KOCHA EL-GOHARY, MCHEZAJI RIGOBERT SONG!
>>GABON YAFUTIWA USHINDI KOMBE LA DUNIA 2014!!
YAYA_TOURE-BORA_CAFKIUNGO WA MANCHESTER CITY, na Mchezaji wa Ivory Coast, Yaya Toure, ameshinda Tuzo ya CAF ya Mchezaji Bora Afrika kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuwabwaga Didier Drogba, alietwaa nafasi ya pili, na Alex Song kukamata nafasi ya tatu.
++++++++++++++++
WACHEZAJI BORA AFRIKA MIAKA ya KARIBUNI:
-2006 Didier Drogba
-2007 Frederic Kanoute
-2008 Emmanuel Adebayor
-2009 Didier Drogba
-2010 Samuel Eto'o
-2011 Yaya Toure
-2012 Yaya Toure
++++++++++++++++
Yaya Toure alishinda kufuatia Kura zilizopigwa na Makocha Wakuu au Wakurugenzi wa Ufundi wa Vyama Wanachama wa CAF.
Hadi sasa Mchezaji anaeongoza kwa kutwaa Tuzo nyingi za Mchezaji Bora Afrika ni Samuel Eto’o wa Cameroun.
Pamoja na Toure, Zambia ilichaguliwa kuwa ndio Timu Bora ya Mwaka na Kocha wao Herve Renard kutwaa Tuzo ya Kocha Bora kwa Mwaka 2012.
Tuzo ya Klabu Bora Afrika ilikwenda kwa Al Ahly ya Misri baada ya kutwaa CAF CHAMPION LIGI Mwaka huu likiwa ni Taji lao la 7.
Kwa upande wa Wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika, Tuzo ya Mchezaji Bora ilichukuliwa na Gwiji wa Al Ahly Mohamed Aboutrika.
Kwa upande wa Vijana wanaochipukia, Mchezaji wa Egypt, Mohamed Salah, Miaka 23, alitunukiwa Tuzo ya Kipaji kinachoinukia kwa kuifungia Egypt katika Mechi 3 kati ya 4 walizocheza huko London Mwaka huu kwenye Michezo ya Olimpiki.
Watu waliotunukiwa Tuzo za kuwa Manguli, Utumishi uliotukuka, ni Kocha veterani wa Egypt, Mahmoud El-Gohary, Miaka 74, kwa kuzipa ushindi Barani Afrika Klabu na Nchi yake katika utumishi wake.
Nae Veterani wa Cameroun, Rigobert Song, alitawazwa kuwa Nguli wa Afrika.
Kwa upande wa Kinamama, Timu Bora imetajwa kuwa ni Equatorial Guinea baada ya kutwaa Ubingwa wa Afrika kwa Kinamama walipoitoa Banyana Banyana ya Afrika Kusini.
Mchezaji Bora kwa Kinamama ni Genoveva Anonman wa Equatorial Guinea ambae alipachika Bao 6 kwenye Fainali za Wanawake na ambae anang’ara huko kwenye Ligi ya German Bundesliga kwa Kinamama.


 GABON YANYANG'ANYWA USHINDI KWA KUMCHEZESHA MCHEZAJI ASIYESTAHILI YAPEWA  NIGER
WAKATI HUO HUO, FIFA imeipa ushindi Niger wa Bao 3-0 katika Mechi ya Mchujo ya Bara la 
img Afrika kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia huko Brazil Mwaka 2014 baada ya Gabon kumchezesha Mchezaji asiestahili.
FIFA imeamua kuwa Charly Moussono hakustahili kuichezea Gabon kwa vile aliiwakilisha Cameroun kwenye Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2006 za Soka la Bichi.
Kufuatia uamuzi huo, FIFA imeyafuta matokeo ya 0-0 kati ya Niger na Gabon kwenye Mechi iliyochezwa huko Niamey, Niger Mwezi Juni.
FIFA imethibitisha kuwa uamuzi huu utabaki kama ulivyo kwa vile Gabon ilishindwa kukata Rufaa katika muda uliostahili.
Kufuatia uamuzi huu Msimamo wa KUNDI E ambalo lina Timu za Congo, Burkina Faso, Niger na Gabon ni kama ifuatavywo baada ya Mechi mbili:
1 Congo Pointi 4
2 Gabon 3
3 Niger 3
4 Burkina Faso 1

HII NI MARA YA PILI kwa FIFA kuzipora Pointi Timu za Afrika ya kwanza ikiwa ni Sudan. SOMA RIPOTI ya awali:
FIFA imeinyang’anya Sudan ushindi wake wa Bao 2-0 walioifunga Zambia kwenye Mechi ya Kundi D ya Mechi za Mchujo kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014 huko Brazil baada ya kumchezesha Mchezaji mmoja ambae hakustahili kucheza Mechi hiyo.
Kamati ya Nidhamu ya FIFA imeamua kuwa Mchezaji Saif Ali hakutakiwa kucheza Mechi hiyo waliyoshinda Sudan Mjini Khartoum hapo Juni 2 Mwaka huu baada ya kuwa na Kadi za Njano alizopata katika Mechi za nyuma ikiwemo ile ambayo Zambia waliichapa Sudan kwenye Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2012, iliyochezwa huko Gabon na Equatorial Guinea.
FIFA imeamua sasa kuipa Pointi 3 Zambia na goli 3-0 na pia kukitwanga Faini ya Dola 6,340 Chama cha Soka cha Sudan.
Uamuzi huu wa FIFA unaifanya Zambia sasa iongoze Kundi D ikiwa na Pointi 6 kwa Mechi mbili ikifuatiwa na Ghana wenye Pointi 3, Sudan nafasi ya 3 wakiwa na Pointi 1 na Lesotho wako mkiani wakiwa na Pointi 1.
MSIMAMO KUNDI D:
1 Zambia Mechi 2 Pointi 6
2 Ghana Mechi 2 Pointi 3
3 Sudan Mechi 2 Pointi 1
4 Lesotho Mechi 2 Pointi 1

MECHI DHIDI ya UMASIKINI: RONALDO XI yaichapa ZIDANE XI

>>ILIPIGWA Grêmio Arena, Porto Alegre, Brazil, MASHABIKI: 50,000!!
MATCH_AGAINST_POVERTYMbele ya Mashabiki zaidi ya 50,000 waliofurika ndani ya Grêmio Arena huko Mjini Porto Alegre, Brazil Kikosi cha Ronaldo kilikifunga Kikosi cha Zinédine Zidane Bao 3-2 katika Mechi ya Kampeni ya Kupiga Vita Umaskini Duniani, rasmi kama MATCH AGAINST POVERTY.MATCH_AGAINST_POVERTY-PICTURE
Wakiwa Mabalozi wa Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNDP, Ronaldo wa Brazil na Zinedine Zidane wa France waliongoza Kombaini zao wakiwa Manahodha katika Mechi ya kila Mwaka, hii ikiwa mara ya 10 kuchezwa, kuhamasisha Ulimwengu katika Vita dhidi ya Umasikini.
Bao la ushindi kwa RONALDO XI lilifungwa na Leandro Damiao katika Dakika za mwisho huku Mabao yao mengine yakifungwa na Cacá Ferrari na Bebeto.
Bao za ZIDANE XI zilifungwa na Zidane na Falcao.
Mechi hii ilichezeshwa na Refa ambae anasifika kuwa ndie alikuwa Bora kupita wote, Pierluigi Collina wa Italy.
Akiongea baada ya Mechi Zidane alisema: “Kucheza Brazil, kwenye Moyo wa Soka, kwa mara ya kwanza na kukutana tena na Rafiki yangu Ronaldo ni kitu cha furaha kubwa! Lakini tukumbuke lengo letu ni kuhamasisha Vita dhidi ya Umasikini!”
Mapato ya Mechi hiyo, kupitia Tiketi, Udhamini na Matangazo ya TV na Radio, yatagawanywa kwenye Programu mbili za kusaidia Vijana Nchini Brazil na Cape Verde, Afrika.
Mechi nyngine zilizopita, chini ya usimamizi wa UNDP na udhamini wa UEFA, zilichezwa katika Miji ya Basle, Madrid, Dusseldorf, Marseille, Malaga, Fez, Lisbon, Athens na Hamburg, na mapato yake kwenye Miradi ya kupiga Vita Umasikini sehemu mbalimbali Duniani.
VIKOSI:
RONALDO XI:
Danrlei, Dida, Cafú, Serginho, Réver, Junior Baiano, Roque Junior, Roberto Carlos, William, Lucas, Juninho Paulista, Zinho, Djalminha, Roger, Zico, Denilson, Ronaldo, Neymar, Leandro Damião, Bebeto, Cacá Ferrari, Edmundo, Paulinho.
KOCHA: Carlos Alberto Parreira

ZIDANE XI:
Vítor Baía, Juliano Belletti, Diego Cavalieri, Emerson, Fernando Hierro, Míchel Salgado, Fernando Couto, Juan Pablo Sorín, Paolo Montero, Carlos Gamarra, Hidetoshi Nakata, Zinédine Zidane, Deco, Santiago Solari, Fredrik Ljungberg, Juan Román Riquelme, Christian Karembeu, Alex de Souza, Pedro Pauleta, Sebastián Abreu, Falcão, Mário Jardel.
KOCHA: Luiz Felipe Scolari

No comments:

Post a Comment