Saturday, October 20, 2012

Kiongozi FIFA ataka ‘Wabaguzi’ Serbia wafungiwe, Terry bado Kepteni Chelsea, Shabiki amtwanga Kipa Uwanjani!


FREDINAND-TERRY_MKNO_HAMNAKufuatia vitendo vya Mashabiki wa Serbia vilivyokithiri vya Ubaguzi, Kiongozi wa juu wa FIFA ameitaka Nchi hiyo ifungiwe na huko Stamford Bridge, Chelsea imetamka John Terry atabaki kuwa Kepteni licha ya kusulubiwa kwa Ubaguzi wakati huko Uwanja wa Hillsborough Shabiki mmoja alivamia Uwanjani na kumpiga Kipa hadi akamwangusha chini.


UBAGUZI Serbia v England:  Makamu Rais FIFA, Jim Boyce, aitaka Serbia ifungiwe!
Makamu wa Rais wa FIFA, Jim Boyce, ameitaka UEFA ifikirie kuifungia Serbia katika Mashindano yajayo kufuatia tuhuma za Ubaguzi wa Washabiki wao zilizotokea kwenye Mechi ya kuwania kuingia Fainali za EURO 2013 kwa Vijana wa Chini ya Miaka 21 iliyochezwa huko Nchini Serbia Jumanne iliyopita na England kufuzu kwenda Fainali baada ya kushinda Mechi zote mbili kwa bao 1-0 kila moja.
Tayari UEFA imeshaifungulia Serbia Mashitaka ya Ubaguzi na pia kushindwa kudhibiti Wachezaji wake kosa ambalo pia FA ya England imeshitakiwa.
Kuhusu shutuma za Ubaguzi, Jim Boyce, ametamka: “Lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya FA ya Serbia! Wafungiwe Viwanja vyao na pia uangaliwe uwezekano wa kutowashirikisha Mashindano yajayo.”
Boyce pia alidai vitendo vya Ubaguzi vya Serbia si mara ya kwanza na inabidi hatua kali zichukuliwe kuvikomesha.


Terry abakishwa Kepteni Chelsea
Licha ya kusulubiwa kwa Ubaguzi na FA pamoja na Klabu yake mwenyewe, Nahodha wa Chelsea, John Terry, ataendelea kubaki kama Kepteni wa Timu hiyo kufuatia uamuzi huo kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Bruce Buck.
Terry amefungiwa na FA Mechi 4 na pia kupigwa Faini Pauni 220,000 na pia Chelsea imethibitisha kumpiga ‘Faini kubwa.’ kwa kosa la kumkashifu Kibaguzi Beki wa QPR Anton Ferdinand kwenye Mechi iliyochezwa Loftus Road hapo Oktoba 23, 2011.


Kipa Chris Kirkland apigwa Uwanjani na Shabiki wa Leeds!
Kipa wa Sheffield Wednesday Chris Kirkland hapo jana alivamiwa Uwanjani wakati wa Mechi ya Timu yake na Leeds United na kushambuliwa na Shabiki wa Leeds kwa nguvu kubwa na kumfanya aanguke chini na kuhitaji matibabu.
Hata hivyo, Kipa huyo wa zamani wa Liverpool mwenye Miaka 31, na ambae pia aliwahi kuichezea England Mechi moja, aliweza kuendelea na kumaliza Mechi hiyo iliyokwisha matokeo yakiwa 1-1.
Akiongelea tukio hilo, Meneja wa Sheffield Wednesday, Dave Jones, alisema: “Hawa ni kama Wanyama. Wapigwe marufuku kwenye Viwanja vyote vya ugenini ikiwa tabia yao ni hii!”
Kwenye Mechi hiyo waliyocheza ugenini, Leeds ilikuwa na Mashabiki 5,300 kati 28,582 waliokuwepo Uwanjani.
Mara baada ya Mechi hiyo Klabu ya Leeds iliomba radhi kwa tukio hilo na kusema itashirikiana na Polisi ili kumtambua Shabiki huyo.

No comments:

Post a Comment