Saturday, October 6, 2012

BAHANUZI AMTEGUA BEGA KAPOMBE, KUWAKOSA OLJORO KESHO, NGASSA MALARIA IMEPANDA

Bahanuzi nyuma ya Kapombe


MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC kesho katika mchezo wao dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha watawakosa wachezaji wao wanne, wakiwemo beki Shomary Kapombe aliyeumizwa na mshambuliaji Said Bahanuzi wa Yanga Jumatano na Mrisho Ngassa, ambaye ana Malaria.   
 
 
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi kwamba, mbali na nyota hao wawili, wengine watakaokosekana kwenye mechi ya kesho ni mabeki Amir Maftahi anayetumikia adhabu ya kadi na Haruna Shamte, ambaye pia ni majeruhi.
 
 
Kamwaga alisema kwamba Kapombe aliumizwa na mshambuliaji wa Yanga, Said Bahanuzi Jumatano katika mechi baina ya watani hao wa jadi wa soka ya Tanzania, iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya 1-1.
 
 
Kuhusu Ngassa, Kamwaga alisema kwamba baada ya mechi hiyo ya Jumatano, naye amepata Malaria, ambayo itamuweka nje ya Uwanja kesho, wakati Haruna aliumia mazoezini, timu hiyo ilipokuwa kambini Zanzibar ikijiandaa na mechi ya Yanga.
 
 
Lakini Kamwaga alisema pamoja na kuwakosa nyota hao, anaamini wachezaji wengine watakaochukua nafasi zao watafanya vizuri. Kumbuka Emmanuel Okwi amemaliza adhabu na kesho anaweza kuiongoza Simba kwenye mechi hiyo.  

RICK ROSS AAHIDI BONGE LA SHOW SERENGETI FIESTA LEO

Rick Ross tayari yupo Dar
MKALI wa muziki wa Hip hop kutoka Marekani, William Leonard Roberts II anayetambulika kama Rick Ross au The Boss, ameahidi kukonga nyoyo za mashabiki watakaohudhuria tamasha la Serengeti Fiesta 2012 jioni ya leo kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam.
 
 
Rapa huyo, aliyefikia katika hoteli ya Hyatt, zamani Kilimanjaro Kempensky, Dar es Salaam, ambaye alizaliwa JanuarI 28, mwaka 1976 huko Carol City, Florida, Marekani alisema hayo baada ya kutua Dar es Salaam usiku wa jana.
 
 
“Rick Ross ametua na ameahidi kufanya shoo kali sana,”alisema Allan Chonjo, Meneja wa Bia ya Serengeti, wadhamini wakuu wa Fiesta.
 
 
Rapa huyo mwenye miraba minne, ambaye ana bifu kali na Curtis Jackson ’50 Cent’ aliyewahi kuzuru Tanzania pia, aliwasili Dar es Salaam usiku wa jana na anatarajiwa kuwapagawisha wapenzi wa Serengeti Fiesta kwa nyimbo kali kutoka kwenye albamu zake za Port of Miami aliyoitoa mwaka 2006, Trilla ya 2008, Deeper Than Rap ya 2009, Teflon Don ya 2010 na God Forgives, I Don't ya mwaka huu.
 
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, wadhamini wakuu wa Serengeti Fiesta 2012, Ephraim Mafuru Balozi alisema kwamba wanajisikia fahari kubwa kwa bia ya Serengeti kuwa mdhamini mkuu wa tamasha hilo kwa muda wa miaka minne sasa.
 
 
 
“Bia ya Serengeti inafahamika kwa umahiri wake katika ubora na ladha yake. Imejinyakulia medali za dhahabu kutoka katika mashirika ya ushindanishaji bia duniani DLG na Monde na pia ni fahari kwa kuwa bia ya kwanza Tanzania kuwa na kimea cha asilimia 100. Bia hii imejiwekea historia ya kuwa bia inayokua kwa haraka katika ujazo na thamani yake,”alisema Mafuru.
 
 
Mkurugenzi huyo aliwaomba wakazi wa Dar es Salaam kujitokeze kwa wingi jioni ya leo katika viwanja vya Leaders Club wakaburudike na muziki wa vijana wa Tanzania na pia kumshuhudia mwanamuziki Rick Ross kutoka Marekani. “Pia tunawahakikishia kwamba watapata bia ya Serengeti yenye muonekano mpya, na ladha yake ni ile ile yenye ubora thabiti. Kwa hiyo watapata bia yenye muonekano tofauti, burudani ile ile,”alisema. Mafuru aliongeza; “Tunazo Bia za aina  nyingi kutoka Kampuni ya Bia ya Serengeti pia zitakuwepo kama vile; Tusker Lager, Pilsner Lager, Tusker Malt Lager, Uhuru Peak Lager, Smirnoff Ice Black na Red, na kwa wanaopendelea vinywaji vikali watapata Johnnie Walker Whisky, Smirnoff Vodka, VAT 69, Captain Morgan, Baileys na Gilbeys Gin.  Pia kutakuwa na vinywaji visivyo na kilevi cha Malta Guinness na Alvaro.  Tumejiandaa vya kutosha kuwapatia vinywaji hivyo kwa bei ya shilingi 1,800 tu,”alisema.

MECHI YA YANGA NA KAGERA YASOGEZWA MBELE WAGENI WAKIWA WAMEKWISHAFIKA BUKOBA

Yanga SC


KAMATI ya Ligi imesogeza mbele kwa siku moja mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Kagera Sugar na Yanga iliyokuwa ichezwe kesho mjini Bukoba kutokana na Uwanja wa Kaitaba kuwa na shughuli nyingine za kijamii.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo amesema kwamba sasa mechi hiyo itachezwa Jumatatu kwenye Uwanja huo huo.
 
 
Wambura alisema kwamba mabadiliko hayo pia yameathiri mechi kati ya Toto Africans na Yanga iliyokuwa ichezwe Oktoba 10 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na sasa itachezwa Oktoba 11 mwaka huu. Yanga tayari wapo Bukoba tangu asubuhi, baada ya kuondoka Dar es Salaam kwa ndege.
 
 
Katika hatua nyingine, Wambura amesema kwa vile msimu huu mdhamini mwenyewe ndiye anayegawa vifaa kwa timu, Kamati ya Ligi imeagiza Vodacom iandikiwe barua na nakala kwa klabu zote ili kujua timu ambazo tayari zimekabidhiwa vifaa hivyo zikiwemo logo na siku ambapo timu husika zilipokea.
 
 
Baada ya majibu ya Vodacom ndipo Kanuni za Ligi Kuu zitakapotumika kutoka adhabu kwa timu ambazo zitabainika kuwa zilipokea vifaa lakini hazikuvitumia. Hatua hiyo inafuatia timu za Yanga na African Lyon kutovaa jezi za wadhamini wa ligi hiyo hadi sasa, kwa sababu mbalimbali.
 
 
Wakati Yanga wanakataa nembo nyekundu kwenye jezi za wadhamini, Lyon wao wana mkataba wa kampuni nyingine ya simu, Zantel.
Wakati huo huo: Wambura amesema kwamba, Kamati ya Ligi ya TFF iliyokutana jana imepanga Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ianze kutimua vumbi Oktoba 20 mwaka huu.
 
 
Alisema timu zimepangwa katika makundi matatu ya timu nane nane ambapo zitacheza ligi hiyo kwa mtindo wa nyumbani na ugenini. Mshindi wa kila kundi ndiye atakayepata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao wakati timu ya mwisho kila kundi itashuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa.
 
 
Kundi A lina timu za Burkina Moro ya Morogoro, Kurugenzi Mufindi ya Iringa, Majimaji ya Songea, Mbeya City ya Mbeya, Mlale JKT ya Ruvuma, Mkamba Rangers ya Morogoro, Polisi Iringa na Small Kids ya Rukwa.
 
 
Ndanda FC ya Mtwara, Ashanti United, Green Warriors, Moro United, Polisi, Tessema, Transit Camp na Villa Squad zote za Dar es Salaam ndizo zinazounda kundi B wakati kundi C ni Kanembwa JKT ya Kigoma, Morani ya Manyara, Mwadui ya Shinyanga, Pamba ya Mwanza Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora na Rhino Rangers ya Tabora.
 
 
Ada ya ushiriki wa ligi ni sh. 200,000 zinazotakiwa kulipwa kabla ya Oktoba 13 mwaka huu. Pia Oktoba 13 mwaka huu kutakuwa na kikao kati ya wenyeviti wa klabu zote zinazoshiriki ligi hiyo na Kamati ya Ligi ambapo pia itafanyika draw (ratiba).

REFA ADUI WA YANGA, SWAHIBA WA SIMBA AENDA NA MAJI LIGI KUU

Mathew Akrama


KAMA ilivyotarajiwa na wengi, refa Mathew Akrama wa Mwanza aliyechezesha ovyo mechi ya watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga, Jumatano wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ‘amekwenda na maji’.  
 
 
Taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura imesema kwamba, Kamati ya Ligi imewaondoa marefa watatu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na kuvurunda.
 
 
Mbali na Akrama ambaye ‘Yanga hawana hamu naye’ tangu siku hiyo, wengine ni Paul Soleji wa Mwanza aliyechezesha mechi kati ya Simba na Tanzania Prisons, na mwamuzi msaidizi namba mbili kwenye mechi hiyo Mwarabu Mumbi wa Morogoro, wakati mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi ya Yanga na Simba, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam amepewa onyo.
 
 
Kamishna wa mechi namba 28 kati ya Yanga na African Lyon, Pius Mashera ameondolewa kwenye orodha ya makamishna wa ligi hiyo kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (Pre match meeting) na uwanjani.
 
 
Vilevile Mashera kwenye ripoti yake aliwasilisha malalamiko dhidi ya msimamizi wa kituo cha Dar es Salaam, na kwa vile suala hilo ni la kinidhamu ametakiwa alipeleke kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
 
 
Nayo Simba imepigwa faini ya jumla ya sh. 600,000 kwa kuchelewa kufika kwenye pre match meeting ya mchezo wao dhidi Tanzania Prisons (sh. 100,000) na kwa washabiki wake kuwatupia chupa za maji waamuzi wa mechi hiyo (500,000).
 

Pia Kamati ya Ligi imeagiza kuwa kwa vile suala la kipa Shaabani Kado wa Mtibwa Sugar kudaiwa kumpiga kiongozi mmoja wa Ruvu Shooting mara baada ya mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex ni la kinidhamu lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.

No comments:

Post a Comment