Friday, September 28, 2012

BOBAN BADO HASOMEKI ZANZIBAR

Mtaalamu Boban

Na tano juma
LABDA leo, lakini jana wamemsubiri hadi boti ya mwisho hakushuka. Haruna Moshi Shaaban, mchezaji pekee ambaye hayupo kambini Simba SC, alitarajiwa kuungana na wenzake jana, visiwani Zanzibar kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Yangas SC, lakini wapi.
Sasa uongozi wa Simba utamsikilizia mchezaji huyo leo kama atatimiza wajibu wake na tofauti na hapo, watachukua.  
Boban hakucheza mechi iliyopita ya Ligi Kuu kati ya Simba na Ruvu Shooting, kwa sababu alikuwa anaumwa na hakwenda kambini wenzake, kwa kuwa alikuwa anajisikilizia afya yake, ila kuanzia jana alitarajiwa kuungana na wenzake kambini.
Kuna uwezekano mkubwa Boban akapanda boti na wenzake na baada ya mechi ya kesho, dhidi ya Prisons.
Japo Boban hayupo kambini Zanzibar, lakini Simba SC inaendelea vizuri na maandalizi yake ya pambano dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, Oktoba 3, mwaka huu, ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislam, Kwerekwe, visiwani Zanzibar na kambi yao ipo Chukwani.
Morali ya kambi ipo juu na wachezaji wote wako fiti, wakijifua kwa shauku kubwa ili kumvutia kocha Mserbia, Milovan Cirkovick awape nafasi ya kucheza Oktoba 3, kuanzia sa 1:00 usiku.
Simba itarejea Dar es Salaam kesho kucheza mechi na Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa, kisha kurejea tena visiwani humo kuendelea na maandalizi ya mchezo wa Jumamosi ijayo.
Hata hivyo, katika michezo miwili ijayo, Simba itamkosa mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi ambaye amefungiwa na Kamati ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, chini ya Mwenyekiti wake, Wallace Karia, sambamba na kumtoza faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa JKT Ruvu, Kessy Mapande.
Okwi alifanya hivyo akilipa kisasi cha kuchezewa rafu Jumatano iliyopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tayari Okwi amekosa mechi moja dhidi ya Ruvu Shooting na wakati, na sasa atakosa mechi mbili zaidi, dhidi ya Prisons na dhidi ya Yanga na baada ya hapo atakuwa huru kuendelea kumtumikia mwajiri wake.
Siyo siri, kuelekea pambano la watani wa jadi, Okwi alikuwa ni homa kwa Yanga, hasa wakikumbuka namna alivyowanyanyasa katika mechi iliyopita, akifunga mabao mawili kwenye ushindi wa 5-0 na kusababisha mawili.

KOCHA MPYA YANGA AWASILI KIMYAKIMYA

Brandts

Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA mpya wa Yanga, Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, beki wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya PSV Eindhoven ya Holanzi, atawasili wakati wowote kuanzia leo kusaini mkataba na kuanza kazi katika klabu hiyo.
Hata hivyo, Yanga imeamua kufanya siri ujio wa kocha huyo, kwa sababu haitaki mapokezi ya mbwembwe, kutokana na rekodi yake ya kutodumu na makocha.
Yanga, imetimiza malengo yake ya kuwa kocha mpya, kabla ya kucheza na wapinzani wao wa jadi, Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada ya kumfukuza Mbelgiji, Tom Saintfiet, kutokana na kufikia makubaliano na Brandts.
Mholanzi huyo aliyefukuzwa APR ya Rwanda baada ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Agosti mwaka huu amepewa ukocha wa Yanga, baada ya Mbrazil Marcio Maximo kukataa nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Mtaalamu huyo, alizaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na PSV Eindhoven, alichezea pia Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, ambako ‘riziki’ yake imeisha miezi miwili iliyopita na sasa amepata maisha mapya Yanga.
Akiwa APR, Brandts alifungwa mechi zote mbili na Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Mbelgiji Tom Saintfiet katika Kombe la Kagame, moja ya makundi 2-0 na nyingine ya Nusu Fainali 1-0. Yanga iliibuka bingwa, ikiifunga Azam FC 2-0 kwenye fainali.
Brandts atakutana na wachezaji wake wa zamani wawili Yanga, beki Mbuyu Twite anayeanza msimu wa kwanza katika klabu hiyo na kiungo Haruna Niyonzima anayeingia katika msimu wa pili, ambao alifanya nao kazi APR.

AZAM KURUDI KILELENI LIGI KUU LEO?

Azam FC

Na Prince Akbar
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, leo inaingia katika mzunguko wake wa nne kwa mechi za Super Weekend, ambazo zitaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
Mechi ya kwanza ambayo itachezwa leo itakuwa kati ya Azam FC na JKT Ruvu Stars, itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku kwa viingilio vya Sh. 3,000 mzunguko, sh. 5,000 kwa VIP C na VIP B wakati VIP A kiingilio kitakuwa sh. 10,000.
Kesho kutakuwa na mechi kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayofanyika Uwanja wa Taifa, pia mjini Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni, wakati Yanga na African Lyon zitapambana keshokutwa kwenye Uwanja huo huo kuanzia saa 11:00 jioni.
Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam wenyewe utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar itakayochezwa Oktoba 1, mwaka huu kuanza saa 10:30 jioni.
Mechi ya mwisho ya Super Weekend itachezwa Oktoba 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikwakutanisha watani wa jadi, Yanga na Simba kuanzia saa 1:00 usiku.
Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Katibu Mkuu mstaafu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Erasto Zambi kilichotokea juzi mjini Dar es Salaam kutokana na maradhi.
Zambi ambaye anatarajiwa kuzikwa Jumapili, kabla ya kuwa kiongozi TOC, kwa muda mrefu alikuwa mwalimu wa michezo katik Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo wanamichezo wengi hasa waliokuwa wanafunzi katika chuo hicho wamepita kwake.
Msiba huo ambao uko nyumbani kwake Ubungo Kibangu, Dar es Salaam ni pigo kwa familia ya Zambi, TFF na wanamichezo kwa ujumla nchini kutokana na mchango na mawazo aliyotoa kwa shirikisho wakati akiwa kiongozi wa TOC.
TFF imetoa pole kwa familia ya Zambi, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito.

MSIMAMO WA LIGI KUU BARA

                               P    W  D   L    GF       GA      GD     P
Simba SC                3    3    -     -     7          1          6       9
Azam FC                 3    2    1    -     3          1          2       7
Coastal                    3    2    1    -     5          3          2       7
JKT Oljoro               3    1    2    1    2          1          1       5
Mtibwa Sugar          3    1    1    1    3          1          2       4
Yanga SC               3    1    1    1    4          4          -        4
Toto African            3    -     3    1    3          2          1       3
Ruvu Shooting        3    1    -     2    4          5          -1     3
African Lyon            3    1    -     2    2          5          -3     3
JKT Ruvu                3    1    -     2    3          7          -4     3
Prisons                   2    -     2    -     1          1          -        2
Polisi Moro              3    -     2    1    -           1          -1     2
Kagera Sugar         3    -     1    2    2          4          -2     1
JKT Mgambo           3    -     -     3    1          3          -2     0
No comments:

No comments:

Post a Comment