Saturday, February 2, 2013

SAMATTA NA ULI WAJA KESHO KUIKABILI CAMEROON JUMATANO TAIFA


Samatta na Ulimwengu kulia

WASHAMBULIAJI wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanatarajia kutua nchini kesho (Februari 3 mwaka huu) tayari kwa mechi ya Cameroon itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Samata na Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) watawasili saa 11.10 jioni kwa ndege ya PrecisionAir na kwenda moja kwa moja kambi hoteli ya Tansoma.
Wachezaji wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wanaanza kuripoti kambini leo jioni (Februari 2 mwaka huu) mara baada ya mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar.
Mechi hiyo iliyo katika Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) pia itatumika kwa ajili ya kutoa ujumbe wa vita dhidi ya Malaria viwanjani, ugonjwa unaoongoza barani Afrika kwa kusababisha vifo vya watoto na wajawazito.
TFF kama ilivyo Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na FIFA imekuwa msitari wa mbele katika kueneza kampeni ya vita dhidi ya Malaria inayoongozwa United Against Malaria (UAM). Rais wa TFF, Leodegar Tenga na nahodha wa Cameroon, Samuel Eto’o ni miongoni mwa mabalozi wa vita dhidi ya Malaria barani Afrika.
Wakati huo huo: Kundi la kwanza la Cameroon likiongozwa na kiungo wa zamani wa Toulouse ya Ufaransa ambaye sasa yuko Al Ahli ya Falme za Kiarabu (UAE), Achille Emana na Meneja wa timu hiyo Rigobert Song litatua nchini kesho (Februari 3 mwaka huu) saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM.
Wachezaji wengine katika kundi hilo ni Vincent Aboubakary anayechezea timu ya Valenciennes iliyoko Ligi Kuu ya Ufaransa, kipa Charles Itandje anayedakia timu ya POAK FC ya Ugiriki, Kocha wa viungo Sylvain Monkam.
Mshambuliaji wa Anzhi Makhachkala ya Urusi ambaye ndiye nahodha wa Cameroon, Samuel Eto’o ataongoza kundi la pili litakalowasili nchini Februari 4 mwaka huu (saa 3.45 asubuhi) kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi, Kenya.
Wengine katika ndege hiyo Herve Tchami wa Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa, mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk. Boubakary Sidik wakati Kocha wa timu hiyo Jean Paul Akono na msaidizi wake Martin Ndtoungou watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways akitokea Afrika Kusini.
Februari 4 mwaka huu kuna kundi lingine litakaloingia saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM ambalo lina beki Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga wa Malaga FC ya Hispania, beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa mkopo Granada ya Hispania na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya Ufaransa.
Wachezaji waliobaki wakiongozwa na kiungo wa Barcelona, Alexandre Song watawasili Februari 5 mwaka huu kwa muda tofauti kwa ndege za KLM na Kenya Airways.

No comments:

Post a Comment