Tuesday, February 5, 2013

POULSEN: NATAKA MECHI NGUMU ZAIDI KUJENGA STARS IMARA YA KUFUZU KOMBE LA DUNIA 2014


Kim katikati akizungumza na Waandishi mchana wa leo, kulia Nahodha Juma Kaseja na kushoto, Katibu wa TFF, Angetile Osiah


KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Poulsen amesema kwamba anataka mechi ngumu zaidi ili kujenga timu imara ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari mchana huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Pouslen alisema kwamba yuko tayari kwa mchezo wowote dhidi ya timu ngumu kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake.
Kaseja akizungumza na Waandishi leo TFF
Poulsen alisema kwamba ameiandaa vyema timu yake kwa ajili ya mchezo wa kesho na vijana wake wameonyesha kabisa wako tayari kwa mechi hiyo, inayotarajiwa kuwa kali na ya kusisimua.
“Tulikuwa tuna mazoezi mazuri jana, wachezaji wote wameripoti na wako vizuri, wanafahamiana na wamecheza baina yao, Mtibwa Sugar, Yanga na Azam, wanapeana changamoto. Wanapendana. Napenda sana kaulimbiu ya Umoja ni nguvu, wachezaji ni wamoja, sisi wote ni wamoja”alisema.
Poulsen alisema kwamba wachezaji wake wanajua wanatakiwa kucheza vizuri kesho, ili kuwapa changamoto Cameroon katika mchezo huo, ambao mashabiki wanausubiri kwa hamu.
Kim alisema wananawaheshimu Cameroon ni timu nzuri na kubwa, yenye wachezaji wazuri, lakini hilo haliwazuii kusema watashinda mechi ya kesho.
“Tunaamini staili yetu ya uchezaji itatupeleka katika zama nyingine. Mtindo wetu ni kupiga pasi kwa wingi na kutengeneza nafasi na kufunga, tukicheza kwa haraka. Na hata tukipoteza mpira, tunajituma wote kuutafuta. Nina uhakika wachezaji wako tayari kwa mechi,”alisema.
Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo Juma Kaseja amesema kwamba wako tayari kwa mchezo huo na wanaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani kesho kuiunga mkono timu yao.
“Sisi wote ni Watanzania, na wote tunahitaji furaha, wenyewe watakuwa 11 na sisi tutakuiwa 11 na tunatarajia utakuwa mchezo mzuri, mgumu na tutaonyesha kile tulichokionyesha kwenye mchezo uliopita na Zambia,”alisema Kaseja.
Wachezaji 21 wapo kambini Stars katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ambao ni makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Cameroon ilianza kutua jana kwa mafungu, kundi la kwanza lenye watu 13 likiingia nchini saa 4.40 usiku, kundi la pili linaloongozwa na Nahodha, Eto’o linatarajiwa kutua leo saa 3.45 asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Eto’o anayechezea timu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi atatua kwa ndege ya Kenya Airways akiwa na Herve Tchami wa Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa, mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk. Boubakary Sidik.
Saa moja baadaye baada ya Eto’o kutua na wenzake, Kocha wa timu hiyo Jean Paul Akono na msaidizi wake Martin Ndtoungou watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Afrika Kusini.
Leo pia kuna kundi lingine litakaloingia saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM ambalo lina beki Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga wa Malaga FC ya Hispania, beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa mkopo Granada ya Hispania na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya Ufaransa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa inashika nafasi ya pili katika kundi lake kuwania tiketi ya Brazil mwakani, nyuma ya Ivory Coast inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo ni Gambia.

No comments:

Post a Comment