Tuesday, February 5, 2013

BIN KLEB: YANGA TUNAWAHOFIA AZAM KULIKO SIMBA SC MBIO ZA UBINGWA



Bin Kleb
MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga SC, Abdallah Ahmad Bin Kleb amesema kwamba wanaihofia sana Azam FC kuliko Simba SC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza  jana, Kleb alisema kwamba hadi sasa safari bado ni ndefu kuelekea kwenye kilele cha ubingwa na timu zote tatu, Yanga, Azam na Simba SC zina nafasi ya kutwaa taji hilo.
“Lakini kwa mwenendo wa ligi jinsi ulivyo, kuna kila sababu ya kuihofia Azam kuliko Simba ambao ni mabingwa watetezi. Kwanza hawa ndio wapo nyuma yetu tukiwa tunawazidi pointi tatu tu. Pili, ni timu nzuri na ina nyenzo za kutosha za kupambana,”alisema Bin Kleb.
Mwenyekiti huyo alisema anafurahia ushindani uliopo katika Ligi Kuu, kwani ni kipimo kizuri kwa timu na ndiyo maana wao wameamua kujipanga upya kwa ajili ya mechi zijazo.
“Tumetoa sare ambayo kwa kweli haikutarajiwa (dhidi ya Mtibwa), tumepunguza idadi ya pointi ambazo tulikuwa tunawazidi Azam kutoka tano hadi tatu, sasa hii maana yake tukiteleza tena, watatukamata, hatuko tayari kwa hilo, tunajipanga upya kuelekea mechi zijazo,”alisema Bin Kleb.
Bin Kleb alisema kwamba wana imani na timu yao na maandalizi waliyofanya kabla ya kuanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, hivyo ndoto za ubingwa zipo pale pale. “Matumaini ya ubingwa yapo sana tu, nachozungumzia hapa ni changamoto ambazo tutakabiliana nazo, ndiyo kama hivyo Azam ni timu ambayo tunaihofia zaidi kuliko Simba,”alisema.
Yanga ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 33, ikifuatiwa na Azam yenye 30, wakati SImba ina pointi 27, timu zote zikiwa zimecheza mechi 15 kila moja.

No comments:

Post a Comment