Tuesday, February 5, 2013

MAMIA SIMBA KUMPOKEA TAJIRI WAO, MALKIA WA NYUKI


Mama Rahma akiwa na Simba Oman

WANACHAMA wa klabu ya Simba SC, wametakiwa kufika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Februari 10, mwaka huu kumpokea mfadhili wao wa ziara ya Oman, Mama Rahma Al Kharoos, Malkia wa Nyuki, anayetarajiwa kutua nchini siku hiyo.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, wanachama na wapenzi wa klabu hiyo wanatakiwa kufika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam siku hiyo kumpokea mfadhili huyo.
“Mama huyu ametusaidia sana kwa kweli, katika kambi yetu ya Oman alitumia zaidi ya Sh. Milioni 80 ambazo ziliisaidia sana timu kwa maandalizi, kwa hiyo tunaomba twende tukampokee, ili kulipa fadhila kwake,”alisema Kamwaga.
Kamwaga alisema kwamba Mama Rahma atakuwa Mkuu wa Msafara wa Simba itakapokwenda nchini Angola kucheza na Libolo ya huko katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu wiki iliyopita, Simba iliweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na hatua hiyo kwa ufadhili kamili wa Malkia wa Nyuki. Hayo yalikuwa majibu kwa wapinzani wao wa jadi, Yanga SC walioweka kambi ya wiki mbili pia nchini Uturuki.
Matunda ya ziara ya Oman ni Simba kuanza Ligi Kuu ya kishindo ikiitandika 3-1 African Lyon na keshokutwa itaingia kwenye mchezo wa pili kusaka pointi dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani.

No comments:

Post a Comment