Tuesday, February 5, 2013

ULIMWENGU: TUTAWACHINJA CAMEROON KESHO


Ulimwengu akiwa mazoezini Stars jana

MSHAMBULIAJI wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Thomas Ulimwengu amesema kwamba ana imani wataifunga Cameroon katika mchezo wa kesho wa kirafiki wa kimataifa, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza  baada ya mazoezi ya jana, Uwanja wa Taifa, Ulimwengu alisema kwamba kwa kuwa kikosi chao kimekamilika kambini na wachezaji wa ari kubwa, anaamini watashinda mchezo wa kesho.
Uli, anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alisema kwamba wachezaji wa Tanzania sasa wana uzoefu wa kucheza dhidi ya timu kubwa na anaamini kesho watashinda.
“Kweli Cameroon ina wachezaji wengi wanaocheza Ulaya, wazoefu na wazuri hata kiufundi kuliko sisi, lakini hata sisi kwa maana ya wachezaji wa Tanzania tunabadilika sana siku hadi siku, hivyo wapenzi watarajie burudani nzuri kesho,”alisema.
Kwa upande wake, kiungo Simon Msuva alisema kwamba anafurahi sana kuwapo katika kikosi cha timu ya taifa na kupata mechi za kumkomaza kisoka.
“Mechi hizi zinamjenga mchezaji, sana tena. Naamini nikipewa nafasi Jumatano nitafanya vizuri na mashabiki watafurahia,”alisema Msuva, anayechezea Yanga.
Amri Kiemba alisema kwamba anafurahia umoja uliopo ndani ya timu yao kwa sasa na hiyo ni chachu ya ushindi kesho.
“Wachezaji tunakaa vizuri, pamoja na tunapendana, viongozi wanatujali, kwa kweli tupo katika mazingira mazuri na hii naamini ni chachu ya ushindi kwetu,”alisema Kiemba, anayechezea Simba SC.       
Wachezaji 21 wapo kambini Stars katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ambao ni makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

No comments:

Post a Comment