Monday, January 7, 2013

STARS KAMBINI BILA WAKALI WA YANGA


Kim Poulsen
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars itakayocheza mechi ya kujipima nguvu na Ethiopia Januari 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Addis Ababa, Ethiopia inatarajiwa kuingia kambini leo mjini Dar es Salaam kujiandaa na mechi hiyo.
Stars chini ya Kocha Mkuu Mdenmark, Kim Poulsen, itakuwa na timu ya mwisho kucheza na Ethiopia kabla ya Wahabeshi hao kwenda Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Januari 19 mwaka huu.
Ethiopia iko kundi C pamoja na mabingwa watetezi Zambia, Nigeria na Burkina Faso. Ethiopia itacheza mechi yake ya kwanza Januari 21 mwaka huu dhidi ya Zambia.
Katika mechi yake ya mwisho, Taifa Stars iliifunga Zambia bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Desemba 22 mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ya kirafiki dhidi ya Ethiopia ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo dhidi ya Morocco kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014. Mechi hiyo itachezwa Machi mwaka huu.
Wachezaji wanaotakiwa kambini ni Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ally wote kutoka Azam. Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Wakati benchi la Ufundi lina Kim, Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Hata hivyo, kocha Poulsen atawakosa wachezaji wa Yanga, Kevin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athuman Idd ‘Chuji’, Frank Domayo na Simon Msuva ambao wapo na timu yao Uturuki.

No comments:

Post a Comment