Monday, January 7, 2013

SAFARI YA SIMBA SC OMAN BADO SI UHAKIKA


Simba SC ya Mapinduzi Cup
JAPOKUWA imepanga kuondoka Jumatano kwenda Oman kwa ziara ya wiki mbili, lakini hadi unaposoma habari hii, Simba SC haijapokea tiketi za safari hiyo kutoka kwa wenyeji wao, klabu ya Fanja ya huko.
Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema mchana huu kwamba, wanasubiri kutumiwa tiketi na wenyeji wao hao ndipo watangaze rasmi ziara hiyo ya Oman.
Kikosi cha Simba kwa sasa kipo visiwani hapa kikishiriki Kombe la Mapinduzi na tayari kimefuzu hatua ya Nusu Fainali.
Mapema leo, BIN ZUBEIRY ilimnukuu Kocha Mkuu wa Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig akisema anataka kwenda Oman na kikosi kamili ili aweze kuwajua wachezaji wote na kuweza kuipanga vyema timu yake.
Kuhusu wachezaji wa timu ya taifa, ambayo Januari 11 itacheza mchezo wa kirafiki na Ethiopia, Liewig alisema suala hilo linashughulikiwa na viongozi wa klabu hiyo. “Najua viongozi walikuwa wana kikao na viongozi wa shirikisho (TFF).
Sijui wamekubaliana vipi, lakini naweza kuwavumilia wachezaji hao wajiunge na timu Oman baada ya mechi na Ethiopia,”alisema.
Simba jana ilifuzu Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kutoka sare ya 1-1 na Bandari ya hapa katika mchezo wa mwisho wa Kundi A, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Bandari wakitangulia kupata bao kwa penalti, mfungaji Haitham Juma dakika ya sita kabla ya Kiggi Makassy kuisawazishia Simba SC dakika ya 16.
Refa aliwapa penalti Bandari baada ya Haruna Shamte kumchezea rafu Fauzi Ally katika eneo la hatari na Haitham akaenda kupiga penalti, ambayo ilipanguliwa na kipa Dhaira na mpira kumkuta tena mpigaji, aliyeukwamisha nyavuni.
Kiggi alifunga kwa mpira wa adhabu kutoka upande wa kulia wa Uwanja, umbali wa mita 20, baada ya Abdallah Seseme kuangushwa.    
Kipindi cha pili, Simba walianza kwa kuimarisha kwa kikosi chao wakiwaingiza kwa mpigo, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Jonas Mkude kuchukua nafasi za Mussa Mude, Salim Kinje na Ramadhani Singano ‘Messi’, wakati Bandari walimtoa kipa wao Hassan Hajji na kumuingiza Ahmad Suleiman.
Kwa matokeo hayo, Simba SC imeungana na Tusker ya Kenya kufuzu Nusu Fainali ya michuano hiyo. Tusker ni kinara wa kundi kwa pointi zake saba na Simba imeingia kama mshindi wa pili kwa pointi zake tano.
Wachezaji wa Simba SC walioitwa Stars ni kipa Juma Kaseja, mabeki Amir Maftah na Shomari Kapombe, viungo Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Mrisho Ngasa.
Katika wachezaji wote hao walioitwa Stars, walio kwenye kikosi cha Simba kinachocheza Kombe la Mapinduzi ni Kapombe na Mwinyi Kazimoto pekee. Kaseja, Ngassa, Kiemba ni majeruhi, wakati Amir Maftah imeelezwa ana madai yake anayosubiri alipwe ndipo ajiunge na timu.  

No comments:

Post a Comment